Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mazungumzo ya simu ya Trump yana thamani sawa kwa Ukraine na Urusi?
Na Yusuph Mazimu
Tangu kuanza kwa vita vya sasa vya Ukraine mwaka 2022, juhudi mbalimbali za kidiplomasia zimefanyika kutafuta amani ya kudumu. Umoja wa Ulaya, Umoja wa mataifa umekuwa mstari wa mbele. Hivi karibuni Donald Trump, rais wa Marekani amekuwa mstari wa mbele zaidi akijinasibu kuwa ndiye mwenye funguo na suluhisho la mzozo wa Ukraine.
Mazungumzo ya simu kati ya Donald Trump na viongozi wa Urusi na Ukraine yameibua mjadala kuhusu nafasi yake katika mchakato wa amani.
Trump alizungumza na Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa masaa mawili na siku moja baadae akazungumza na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kwa lisaa moja, akijaribu kupatanisha makubaliano ya kusitisha mashambulizi na kuangazia uwekezaji katika miundombinu ya nishati ya Ukraine.
Lakini, je, mazungumzo haya yana thamani sawa kwa pande zote mbili? Na ni hatua gani zimepigwa hadi sasa katika juhudi za kumaliza mgogoro huu?
Alichozungumza na Putin kwa saa mbili
Katika mazungumzo yake na Vladimir Putin, Trump alifanikisha makubaliano ya kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine kwa siku 30. Hatua hii ilionekana kama juhudi ya kupunguza madhara ya vita kwa raia wa kawaida na kuhakikisha Ukraine inaendelea kuwa na umeme na huduma za msingi.
Hata hivyo, swali kubwa lililojitokeza ni kama Urusi ingeheshimu makubaliano hayo. Historia ya vita vya Ukraine imeonyesha kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano mara nyingi huja na ukiukwaji wake ndani ya muda mfupi. Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mashambulizi bado yanaendelea, huku pande zote zikilaumiana kwa uvunjaji wa makubaliano hayo.
Kwa kuzingatia baadhi ya vichwa vya habari nchini Urusi , Moscow inaamini kwamba mazungumzo ya hivi punde kwa njia ya simu kati ya Rais Putin na Trump yalikwenda vizuri - kwa hakika kwa Ikulu ya Kremlin.
"Simu iliyoweka rekodi ya Putin-Trump," inasema Komsomolskaya Pravda. Tovuti ya gazeti hilo inaongeza: "Kwa jinsi mambo yalivyo Russia imepata ushindi wa kidiplomasia hapa." Wengi wanaona simu ya Trump ilikuwa na thamani kubwa zaidi Urusi.
Kwa nini wengine nchini Urusi wanadai "ushindi" baada ya simu hii iliyochukua saa mbili?
Labda kwa sababu, hadi mwisho wa mazungumzo hayo, Vladimir Putin hakuwa ameshinikizwa kufanya makubaliano yoyote makubwa kwa Ukraine au Marekani. Kinyume chake, alikataa wazo la Rais Trump la usitishaji mapigano wa siku 30 bila masharti.
Badala ya kuishinikiza Moscow kwa kuiweka tishio vya vikwazo na adhabu kali zaidi, ili kuifanya Urusi kusaini mpango wake, serikali ya Marekani ilijibu kwa kumsifu kiongozi wa Kremlin.
"Tulikuwa na simu nzuri," Donald Trump aliambia Fox News.
"Ningempongeza Rais Putin kwa yote aliyofanya leo kupitia simu hiyo na kusogeza nchi yake karibu na makubaliano ya mwisho ya amani," alisema mjumbe wa Trump Steve Witkoff.
Alichozungumza na Zelensky kwa lisaa moja
Trump pia alizungumza na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky siku moja baada ya kuzungumza na Putin, akijadili uwezekano wa Marekani kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya Ukraine, hasa katika mitambo ya nyuklia. Hili lilionekana kama njia mbadala ya kulinda miundombinu ya Ukraine kwa kuiimarisha badala ya kutegemea makubaliano yasiyo na uhakika na Urusi.
Rais wa Marekani Donald Trump ameita mazungumza yake ya simu yalikuwa "mazuri sana". Yalikuwa mazungumzo yaliyochukua saa moja.
Zelensky alisema baadaye kwamba anaamini kwamba "amani ya kudumu inaweza kupatikana mwaka huu" chini ya uongozi wa Trump.
Pia walijadili uwezekano wa umiliki wa Marekani wa mtambo wa kuzalisha umeme wa Zaporizhzhia unaoshikiliwa na Urusi, Zelensky alisema.
Hali ya kupendeza ya mazungumzo hayo ni tofauti kabisa na ziara ya Zelensky katika Ikulu ya Marekani mwezi uliopita, ambapo viongozi hao wawili - pamoja na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, walihusika katika majibizano na malumbano.
Kwa Zelensky na Ukraine kwa ujumla, thamani ya mazungumzo haya inaweza kuwa tofauti na ile ya Urusi. Wakati Urusi inaweza kuona fursa ya kupunguza shinikizo la kimataifa kwa kujionyesha kama mshiriki wa mazungumzo ya amani, Ukraine inaweza kuwa makini zaidi, ikitilia shaka nia halisi ya Urusi. Kwao, msaada wa kiuchumi na uwekezaji unaweza kuwa muhimu zaidi kuliko makubaliano yasiyo na uhakika ya kusitisha mapigano.
Changamoto zinazokumba juhudi za kusaka amani
Licha ya juhudi hizi za Trump, changamoto kadhaa zinaendelea kuzuia upatikanaji wa amani ya kudumu
Uaminifu wa Urusi: Katika historia ya vita hivi, Urusi imekuwa na rekodi ya kutotekeleza makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano. Je, mkataba wa siku 30 utaheshimiwa haa kama ni kusitisha kushambulia miundombinu ya nishati?
Kuendelea kwa mashambulizi kuendelea: Ripoti zinaonyesha kuwa licha ya makubaliano haya na juhudi zinazoendelea, mashambulizi bado yanaendelea, huku Urusi na Ukraine zikilaumiana kwa ukiukaji wa mkataba huo na hata mikataba mingi iliyowahi mkufikiwa huko nyuma kabla ya vita ya sasa.
Nia ya Marekani na Trump: Ingawa Trump ameonyesha nia ya kushiriki katika juhudi za amani, kuna mjadala kuhusu maslahi ya Marekani katika mgogoro huu na iwapo Trump anatumia juhudi hizi kama sehemu ya ajenda yake ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2024. Au ajenda ya kuinufaisha zaidi Marekani na madini na nishati iliyopo Ukraine.
Msimamo wa Zelensky: Rais wa Ukraine anasisitiza kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana bila Urusi kuondoa wanajeshi wake kutoka kwa maeneo inayoyadhibiti, jambo ambalo bado halionekani kuwa kwenye ajenda ya mazungumzo haya. Mazungumzo yameegemea masuala mengine zaidi, kuliko kusitisha vita na kuondoa wanajeshi wa Urusi kwenye ardhi ya Ukraine. Wanajeshi hao kuendelea kuwepo Ukraine ni kuendelea kuchochea mapgano zaidi.
Je, mazungumzo haya yanazaa matunda?
Kwa sasa, haijulikani ikiwa juhudi za Trump na simu zake kama zitaleta matokeo ya muda mrefu au ni hatua ya muda mfupi tu. Wakati Urusi inaweza kuona mazungumzo haya kama fursa ya kujinasua kwenye shinikizo la kimataifa, Ukraine inatafuta suluhisho la kweli na la kudumu. Katika mzozo huu yenyewe ndiyo mathirika zaidi, ikishambuliwa, watu wake wakiuawa na miundo mbinu yake ikiharibiwa vibaya.
Pengine kuna mwanga wa juhudi zilizochukuliwa mpaka sasa hata za pande hizi kukubali kuzungumza kwa lengo la kutafuta suluhu. Kukubali tu kuzungumza ni ishara tosha nia na dhamira zao, hofu ni kwamba nia na dhamira hizo zitakuwa kwenye muelekeo mmoja?
Hadi sasa, bado kuna ukosefu wa hakikisho kwamba Urusi itaheshimu makubaliano haya ya sasa, na kama historia inavyotuonyesha, mazungumzo ya kidiplomasia mara nyingi huambatana na ukiukwaji wa makubaliano.
Kwa hivyo, swali kuu linabaki: Je, simu za Trump zinaweza kuwa na uzito sawa kwa Ukraine na Urusi, au ni mkakati mwingine wa kisiasa bila suluhisho la kweli?