'Nilimpoteza mwanangu vitani, lakini nikamuokoa mtoto mwingine'

    • Author, Anne Soy
    • Nafasi, Naibu Mhariri wa Afrika
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Alawia Babiker Ahmed,19, alipoteza ujauzito alipokuwa akikimbia vita vikali ambavyo vimeathiri vibaya eneo la Darfur magharibi mwa Sudan.

"Nilikuwa natembea huku navuja damu," aliiambia BBC, kabla ya kuongeza kwamba aliwaona watu ambao "walikuwa katika hali mbaya zaidi" akisimulia dhiki aliyokumbana nayo katika safari yake ya siku tatu aliyotembea kwa miguu kwa takriban kilomita 70 (maili 45) kutoka mji uliozingirwa wa el-Fasher hadi mji mdogo wa Tawila.

Katika harakati ya kukwepa mashambubulizi ya anga na wanamgambo baada ya kupoteza ujauzito wake, Alawia anasema yeye na familia yake walimuoana mtoto mdogo akimlilia mama yake ambaye alikuwa amefariki kando ya barabara.

Alawia anasema alimbeba mtoto na kuondoka naye: "Tuliufunika mwili wa mama yake na kuendelea na safari."

Sudan imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa tangu kuzuka kwa mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya waasi RSF mwezi Aprili 2023, na kusababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu na kuwalazimu watu milioni 12 kuyakimbia makazi yao.

Darfur imekuwa ngome kuu wa mapigano, huku RSF ikidhibiti sehemu kubwa ya eneo hilo - isipokuwa jiji la el-Fasher ambalo limesalia mikononi mwa jeshi na washirika wake.

El-Fasher imekuwa chini ya mashambulizi makali wakati RSF inajaribu kuiteka. Mwezi Aprili ilitangaza mipango ya kuunda serikali sambamba na ile iliyoanzishwa na jeshi, na kuzusha hofu kwamba inaweza kusababisha mgawanyiko wa Sudan.

Alawia alisema wakati mashambulizi yalipozidi mwezi uliopita, yeye na familia yake walilazimika kukimbia na kutembea hadi Tawila, magharibi mwa El-Fasher.

Kaka yake, Marwan Mohamed Adam, 21, aliiambia BBC kwamba alivamiwa njiani na magenge washirika wa RSF - ikiwa ni pamoja na "kupigwa shingoni, mkononi na mguuni" na kuibiwa vitu vichache alivyokuwa amebeba.

Marwan aliongeza kuwa alinusurika tu kwa sababu alidanganya magenge kuhusu alikotoka.

Alisema washambuliaji hao waliwachukua na kuwaua vijana ambao walibaini kuwa walikuwa wa el-Fasher, hivyo alipohojiwa alidai kuwa anatokea Shaqra, kituo cha mapumziko cha kuelekea Tawila.

"Unahisi uwoga, unahisi kuwa tayari umekufa,'' anasema.

Mwanamke mwingine, Khadija Ismail Ali, aliiambia BBC kuwa " miili ilikuwa imetapakaa kila mahali mitaani".

Alisema Jamaa zake 11 waliuawa wakati wa shambulizi la El-Fasher, na watoto watatu walikufa wakati wa safari yao ya siku nne kutoka mjini kwenda Tawila.

"Watoto walikufa kutokana na kiu njiani," Khadija alisema.

Kijiji chao cha el-Tarkuniya, kilishambuliwa Septemba iliyopita na wanamgambo washirika wa RSF, ambao waliiba mavuno yao.

Walikimbilia kwenye kambi ya wakimbizi ya Zamzam iliyokumbwa na njaa, na hali ilipozidi kuzorota wahamia El-Fasher na sasa wako Tawila.

Shirika la misaada ya kimatibabu Alima lilisema watu wenye silaha walinyakua ardhi na mashamba ya baadhi ya familia baada ya kushambulia vijiji vyao.

Utapiamlo mkali, hasa miongoni mwa watoto wanaowasilia Tawila, umefikia kiwango cha kutisha, iliongeza.

Alawia alisema dada yake alidondosha chakula kidogo walichokuwa wamebeba wakati wakikimbia mashambulizi ya anga na makombora waliyokumbana nayo baada ya kupita Shaqra.

"Ilikuwa ni maharagwe na chumvi kidogo na tulikuwa tumebeba ili kuwapikia watoto," alisema.

Waliendelea kutembea bila chakula wala maji hadi wakakutana na mwanamke aliyewaambia wangeweza kupata maji katika kijiji jirani.

Familia hiyo ilianza safari ya kuelekea kijijini baada ya saa sita usiku, lakini hawakujua kwamba walikuwa wakitembea katika eneo lililodhibitiwa na wapiganaji wa RSF.

"Tuliwasalimia, lakini hawatukujibu. Walituambia tukae chini na wakaanza kupekua vitu vyetu," Alawia alikumbuka.

Wapiganaji hao walichukua dola 33 ambazo ambazo familia ilikuwa nayo, pamoja na nguo na viatu walivyokuwa wamebeba.

"Viatu vyangu havikuwa vizuri, lakini walivichukua," Alawia alisema.

Aliongeza kuwa wapiganaji wa RSF walikataa kuwapa maji, kwa hivyo waliendelea na safari hadi walipofika kijiji cha el-Koweim. Huko, walipa kisima kilichokuwa kikilindwa na wapiganaji wa RSF.

"Tuliomba maji angalau wampe mtoto yatima waliyekuwa naye, lakini walikataa," Alawia alisema, akiongeza kuwa walijaribu hata kumtumia mtoto mwenyewe kuomba maji kisimani, lakini wanaume hao walimchapa na kumfukuza.

Licha ya kulemewa na kiu na uchovu, familia hiyo iliendelea na safari hadi ikafika Tawila, ambako Alawia anasema alizimia akakimbizwa hospitali.

Aliruhusiwa kuondoka hospitalini hapo baada ya kupata matibabu. Marwan pia alitibiwa majeraha aliyopata baada ya kuvamiwa na kupigwa.

Alawia anasema walijaribu kuwatafuta jamaa za mtoto waliyemuokoa, na baada ya kumpata mmoja wao wakamkabidhi.

Alawia na familia yake sasa wanaishi mjini Tawila, baada ya kukaribiswa na familia moja.

"Maisha sio mabaya, tunamshukuru Mungu, lakini tuna wasiwasi kuhusu hatima yao ya siku zijazo," Alawia aliambia BBC.

Marwan alisema anataka kwenda nje ya nchi ili aendelee na masomo yake na kuanza maisha mapya.

Hili ni jambo ambalo mamilioni ya Wasudan wamefanya, kwani maisha yao yamesambaratishwa na vita ambavyo havionyeshi dalili ya kuisha.

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi