Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu kombora jipya la Ukraine lenye uwezo wa kubeba tani ya vilipuzi, likitishia jeshi ya Urusi
Kabla ya kuondoka kwa Rais Volodymyr Zelensky kuelekea Washington, Ukraine imezindua rasmi kombora lake jipya la masafa marefu lijulikanalo kama Flamingo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, kombora hilo lina uwezo wa kusafiri umbali wa hadi kilomita 3,000 na kubeba mzigo wa vilipuzi wa hadi tani moja.
Iwapo taarifa hizi zitathibitishwa na uzalishaji wa wingi utaanza, basi Flamingo linaweza kuwa changamoto kubwa kwa sekta ya kijeshi ya Urusi.
Hasa, linaweza kuwa tishio kwa maeneo ya Urusi ya Ulaya na hata maeneo ya mbali zaidi kutoka Ukraine.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Denys Shmyhal, alieleza siku ya Jumatatu kwamba taifa hilo sasa linamiliki silaha ya masafa marefu yenye nguvu kubwa.
Hata hivyo, alibainisha kuwa maelezo ya kina kuhusu kombora hilo yatatolewa "wakati ufaao".
Katika tarehe hiyo hiyo, 18 Agosti, gazeti la Zerkalo Nedeli lilichapisha video ya majaribio yaliyofanyika miezi michache iliyopita.
Kwa mujibu wa waandishi, video hiyo inaonyesha uzinduzi wa kombora la aina hiyo hiyo ya Flamingo.
Kombora lenye utambulisho mpya
Jioni ya Jumapili, mpiga picha wa shirika la habari la Associated Press, Yefrem Lukatsky, alichapisha picha ya awali isiyojulikana ya kombora la Flamingo.
Picha hiyo inaonesha makombora mawili ya aina ya cruise yakiwa yamepakiwa kwenye trela maalum za usafirishaji.
Kwa mujibu wa mwanahabari Lukatsky, makombora hayo yana uwezo wa kuruka zaidi ya kilomita 3,000 na yanazalishwa kwa wingi na kampuni ya Ukraine iitwayo Fire Point.
Tovuti ya kijeshi ya Fire Point pia imeeleza kuwa tayari inazalisha ndege zisizo na rubani za mashambulizi aina ya FP-1, zenye uwezo wa kufika hadi kilomita 1,600.
Hadi sasa, ni ndege ya VB140 pekee iliyowahi kutajwa iliyotengenezwa mahsusi kuharibu droni za adui.
Ujerumani ilikuwa imeahidi kufadhili uzalishaji wake.
Hata hivyo, hii ndiyo mara ya kwanza kwa taarifa kuhusu kombora hili la cruise kuwekwa wazi kwa umma.
Inaaminika kuwa kutangazwa kwa taarifa hizi kumefanyika kwa ridhaa ya kampuni ya utengenezaji na uongozi wa kijeshi na kisiasa wa Ukraine jambo lenye uzito hasa ikizingatiwa kuwa Rais Zelensky anafanya mazungumzo muhimu na Donald Trump pamoja na viongozi wa Ulaya kuhusu mustakabali wa vita dhidi ya Urusi.
Lukatsky alibainisha kuwa picha hiyo ya kombora ilipigwa tarehe 14 Agosti, katika eneo lisilojulikana nchini Ukraine.
Muonekano wa kombora hilo mpya umeibua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao wamelilinganisha na kombora la Kijerumani V-1 kutoka Vita ya Pili ya Dunia au ndege isiyo na rubani ya Kisovieti aina ya Tu-1.
Hata hivyo, wachambuzi wengine wa kijeshi wanaamini kuwa linaweza kuwa toleo la Ukraine la kombora la FP-5, lililobuniwa na kampuni ya Milanion Group, inayofanya kazi katika Falme za Kiarabu na Uingereza.
FP-5 na sifa zake za kiufundi
Milanion Group ni kampuni inayozalisha silaha na ndege zisizo na rubani, na imekuwa ikishirikiana na Ukraine tangu mwaka 2021.
Katika mwaka huo, kampuni ya Ukraine ya magari ya kivita ilinunua gari la kijeshi la roboti aina ya AGEMA UGV 8×8 kutoka kwao.
Vifaa hivyo vilitumika baadaye na kikosi maalum cha Kraken katika uwanja wa mapambano kwa shughuli za usafirishaji wa risasi na uokoaji.
Pia, inafahamika kuwa tawi la kampuni hiyo nchini Uingereza, Milanion NTGS, kwa sasa linaiuzia Ukraine mizinga ya kujisukuma ya Alakran ya milimita 120, inayowekwa juu ya magari ya kivita aina ya VAMTAC.
Katika maonesho ya kijeshi ya IDEX-2025 yaliyofanyika Februari mwaka huu, Milanion Group iliwasilisha kwa mara ya kwanza kombora lake jipya la FP-5 mbele ya umma.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, FP-5 lina uwezo wa:
- Kusafiri umbali wa hadi kilomita 3,000
- Kupaa hadi urefu wa kilomita 5
- Kuweka kasi ya kati ya kilomita 850–900 kwa saa
- Kufikia kasi ya juu ya kilomita 950 kwa saa
- Kubaki angani kwa hadi saa 4
Maelezo ya kampuni:
"FP-5 ni kombora linalorushwa kutoka ardhini, likiwa sehemu ya mfumo wa ndege zisizo na rubani. Linabeba mzigo wa hadi kilo 1,000 na hutumika kulenga mabomu yaliyotegwa ardhini kwa kutumia uratibu wa ramani.
Kombora hili linaweza kutumika mchana na usiku, hata katika mazingira yenye vikwazo vya mawasiliano ya redio."
Taarifa kutoka Army Recognition, tovuti ya kijeshi ya Ubelgiji, zinaeleza kuwa kifurushi cha FP-5 kinajumuisha injini ya mafuta imara, kituo cha udhibiti ardhini, vifaa vya usafirishaji, mfumo wa kurushia, na vipuri.
Urushaji wa kombora hili unachukua kati ya dakika 20 hadi 40.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa Defense Express ya Ukraine, muda huo mrefu wa uzinduzi ni matokeo ya mkakati wa kupunguza gharama za utengenezaji:
"FP-5 limeundwa kuwa rahisi kadiri iwezekanavyo. Mabawa yake hayaikunji, na halihitaji kontena maalum kwa ajili ya kurushwa. Hilo linasaidia kupunguza gharama na kuongeza kasi ya uzalishaji."
Ukilinganisha na makombora mengine Flamingo linachukua muda mwingi zaidi kurushwa.
Silaha inayotishia sekta ya kijeshi ya Urusi
Ingawa haijathibitishwa iwapo Ukraine inaweza kuzalisha makombora ya Flamingo takribani 50 kwa mwezi, uwezo wa kutengeneza hata 10 hadi 15 kwa mwezi ni mkubwa hasa ikiwa kila kombora linaweza kubeba hadi tani moja ya vilipuzi.
Kwa masafa ya kilomita 3,000, Ukraine inaweza kushambulia sio tu maeneo ya mpaka, bali pia mikoa ya mbali kama Urals na Tatarstan.
Kwa mfano:
Umbali kati ya Kyiv na Moscow ni kilomita 750
Kutoka Kharkiv hadi Yelabuga (Tatarstan) – takriban kilomita 1,400
Kutoka Kharkiv hadi kiwanda cha "Kupol" kilichoko Izhevsk – takribani kilomita 1,300.
Droni zinaweza kulenga maeneo haya, lakini hazina nguvu sawa na Flamingo ambalo lina uwezo mkubwa wa uharibifu.
Swali kuu sasa ni: Je, mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi inaweza kudhibiti kombora la aina hii?
Kwa kuwa kombora lina urefu wa mabawa wa mita 6 na uzito wa tani 6, ni vigumu kwa Urusi kuweka ulinzi madhubuti wa anga katika kila eneo muhimu kutokana na ukubwa wake.
"Hili ni kombora rahisi.
Halihitaji mifumo tata ya uongozaji kama Storm Shadow au SCALP.
Lengo lake ni moja kuharibu sekta ya kijeshi ya Urusi," anasema Pavel Narozhny, mzalendo wa kijeshi kutoka taasisi ya Reactive Mail.
Akaongeza:
"Tunaweza bado kulenga viwanda vyao kwa kutumia droni za bei nafuu. Hazina kasi kubwa, lakini zinaweza kufika."
Ikiwa makombora kama haya yangerushwa mara kadhaa kwa mwezi, Urusi haingeweza kulinda kikamilifu vifaa vyake muhimu.
Je, Flamingo ni bora kuliko Tomahawk?
Mwakilishi wa Fire Point alidai kuwa Flamingo ni bora zaidi ya kombora la Marekani la Tomahawk:
"Kwanza, Tomahawk ni teknolojia ya zamani. Pili, sifa zake za kiufundi ni duni ukilinganisha na Flamingo. Tatu, ni mara tano zaidi kwa gharama bila hata kujumlisha gharama za usafirishaji."
Aliongeza kuwa makombora hayo hayawezi tena kuitwa mfano wa majaribio; yameingia katika uzalishaji wa mfululizo na yote yanatengenezwa ndani ya Ukraine.
Swali kuu linabaki: jinsi Flamingo litakuwa na ufanisi katika hali halisi ya mapigano dhidi ya mifumo yenye nguvu ya ulinzi wa anga ya Urusi.
Hoja ya kisiasa inayopaswa kuchukuliwa kwa umakini
Pavel Aksenov, mwandishi wa kijeshi wa idhaa ya BBC Urusi anasema:
Tangazo la jaribio jipya la kombora ni muhimu kisiasa kabla ya mazungumzo muhimu. Hii inaweza kuwa hoja moja kwa Volodymyr Zelensky: Ukraine haijitetei tu, pia ina uwezo wa kutoa pigo kubwa.
Ingawa vyombo vya habari vya Ukraine vinaripoti kwamba kombora hilo limejaribiwa katika hali ya mapigano, kuna habari kidogo juu ya uwezo wake.
Hakuna anayejua kama inaweza kuruka kilomita 3,000 na kichwa cha kilo 1,000.
Lakini hii inapaswa kuchukuliwa kwa uzito.
Kwanza, ikiwa kweli inaruka, shambulizi kama hilo linaweza kusababisha uharibifu mkubwa.
Kwa sababu mlipuko wa kilo 1,000 ni karibu mara mbili ya kombora la Caliber au Tomahawk.
Pili, kwa kuzingatia picha, kombora hili ni silaha rahisi ya kupambana.
Kombora mara nyingi huongozwa na satelaiti, rubani, na moduli ya GSM, kawaida kadi ya simu ya Urusi.
Huenda haina mfumo wa mwongozo wa gharama na wa kisasa ambao ungeiruhusu kupiga kwa usahihi wa mita chache.
Lakini ikiwa lengo ni kiwanda, usahihi huo hauhitajiki.
Kombora kama hilo linaonekana kubwa kwenye chombo kitumiwacho na marubani kuonyesha vitu kwenye skrini kiitwacho rada.
Ikiwa na injini ya ndege na muundo wa chuma, inaweza kuonekana kama ndege kwenye rada.
Inaweza kupigwa chini na mfumo wowote wa kombora la kuzuia ndege.
Lakini ikiwa kombora hilo litaruka umbali wa kilomita 3,000, basi mifumo ya ulinzi wa anga itahitaji kuwa katika hali ya kusubiri kila wakati ili kulinda kila kiwanda kikubwa au kituo muhimu.
Na gharama ya kombora hili inaweza kuwa chini ya makombora mawili ya kukinga ndege yaliyotumika kulidungua.
Ukraine ni nchi inayounda injini za ndege.
Kwa mfano, P95-300 ilijengwa kwenye kiwanda cha Motor-Sich.
Haijulikani ikiwa kuna hifadhi yoyote ya injini kama hizo, lakini Ukraine ina wataalamu ambao wanaweza kuunda silaha kama hizo.
Ukraine ni nchi ambayo pia inatengeza ndege.
Sasa msururu wa utengenezaji umesimama, lakini kuna wahandisi wa anga.
Kwa hiyo, habari zinazoonekana kuwa za kisiasa haziwezi kupuuzwa.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid