Waasi wa M23 wasema rais wa zamani Joseph Kabila amewasili mjini Goma

Waasi wa M23 wanaopigana mashariki mwa DRC wanasema rais wa zamani Joseph Kabila amewasili katika mji mkuu Goma

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Jeshi la Uganda lamshutumu balozi wa Ujerumani kwa 'shughuli za uasi'

    Jenerali Muhoozi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Uganda limetangaza kusitisha ushirikiano wote wa kijeshi na Ujerumani baada ya kumshutumu balozi wake, Mathias Schauer, kwa kujihusisha na "shughuli za uasi" na kuwa "hastahili kabisa" kuwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

    Uamuzi wake unaashiria kuzorota kwa kasi kwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

    Akikana shutuma hizo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani alizitaja kuwa "upuuzi na zisizo na uhalali wowote", shirika la habari la Reuters linaripoti.

    Shambulizi hilo lisilo la kawaida dhidi ya Schauer lilikuja baada ya kuripotiwa kuzusha wasiwasi kuhusu mkuu wa jeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa rais, katika mkutano uliofanyika wiki jana.

    Katika ukurasa wa X hivi karibuni, jenerali huyo alitishia kumkata kichwa kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine.

    Jenerali Kainerugaba pia alijigamba kuhusu kumtesa mlinzi wa Wine baada ya kumzuia. Mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa muda mrefu yamekuwa yakishutumu serikali ya Uganda kwa kulenga upinzani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

    Wine anatarajiwa kuchuana na Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa takribani miongo minne, katika uchaguzi utakaofanyika mwaka ujao.

    Wakosoaji wa Museveni wanadai kuwa serikali inaongozwa na nasaba ya familia, mke wake, Janet Museveni ni waziri wa elimu, na kaka yake, Jenerali Salim Saleh, ndiye mratibu mkuu wa programu ya serikali inayojulikana kama Operesheni Wealth Creation.

    Jenerali Saleh alifanya mkutano wa faragha na wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya (EU) wiki iliyopita, ambapo Schauer - balozi wa Ujerumani nchini Uganda tangu 2020 - aliibua wasiwasi kuhusu ujumbe wa kutatanisha wa mkuu wa jeshi, na "uharibifu wa sifa" iliyokuwa ikisababisha Uganda, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

    Maelezo zaidi:

  3. Urusi: Kuna hisia nyingi kupita kiasi wakati huu muhimu

    Putin

    Chanzo cha picha, AFP

    Katika mkutano wa leo wa Kremlin, nilimuuliza msemaji wa Vladimir Putin, Dmitry Peskov, jinsi alivyokuwa na wasiwasi na ukosoaji wa Donald Trump kwa rais wa Urusi, pamoja na maoni yake kwamba Putin alikuwa "mwendawazimu" na mashambulio yake yanayoendelea dhidi ya Ukraine.

    Peskov alijibu: "Bila shaka, kuanza kwa mchakato wa mazungumzo, ambayo upande wa Marekani ulifanya juhudi kubwa, ni mafanikio muhimu sana na tunawashukuru sana Wamarekani na binafsi kwa Rais Trump kwa msaada wao katika kuandaa na kuanzisha mchakato huu wa mazungumzo.

    "Ni mafanikio muhimu sana. Bila shaka, wakati huo huo huu ni wakati muhimu sana ambao umeunganishwa na mchanganyiko wa hisia wa kila mtu anayehusika.

    "Tunafuatilia kwa makini athari zote. Hata hivyo, Rais Putin anachukua maamuzi hayo ambayo ni muhimu kwa usalama wa nchi yetu."Sote tulishuhudia jinsi utawala wa Kyiv ulivyotishia viongozi wa kigeni kabla hawajafika Moscow kuadhimisha Siku ya Ushindi. Kila mtu alisikia vitisho hivi vya utawala wa Kyiv. ''

    "Na viongozi wengi waliokuwa hapa walishuhudia majaribio ya utawala wa Kyiv kushambulia eneo la Urusi kwa ndege zisizo na rubani, miji mikubwa, hata mji mkuu, usiku wa kuamkia siku hiyo muhimu.Majaribio haya yanaendelea. Tunalazimika kuchukua hatua na Rais Putin anafanya kile kinachohitajika ili kuhakikisha usalama wa Urusi."

    Unaweza kusoma;

  4. Waasi wa M23 wasema rais wa zamani Joseph Kabila amewasili mjini Goma

    Kabila

    Chanzo cha picha, Joseph Kabila PR

    Waasi wa M23 wanaopigana mashariki mwa DRC wanasema rais wa zamani Joseph Kabila amewasili katika mji mkuu Goma, akitokea uhamishoni.

    Serikali mjini Kinshasa imemshutumu Bw Kabila kwa kuhusishwa na kundi linaloungwa mkono na Rwanda, M23. Wiki iliyopita, Seneti iliondoa kinga yake dhidi ya kushtakiwa ili aweze kushtakiwa kwa uhaini, Mhariri wetu wa kanda ya Afrika, Will Ross, anaripoti.

    Joseph Kabila yuko katika mazingira magumu kwa sasa kwa kuwa hana tena kinga ya kushtakiwa.

    Wiki iliyopita Bw Kabila alisema kipaumbele chake kikuu ni kuondoa kile alichokiita udikteta. Kwa hiyo inawezekana kwamba mtu ambaye kwa muda mrefu anaonekana kuwa karibu na Rwanda anajiunga na waasi wa Kigali wanaoungwa mkono na M23 kama sehemu ya harakati za kujaribu kumpindua rais Felix Tshisekedi.

    Kuna hatari ambayo inaweza kusababisha mvutano mpana wa mzozo katika nchi jirani kwa pande zinazopingana.

    Unaweza kusoma;

  5. Mwanafunzi wa China asema chuo kikuu kilimfanya 'kuvua suruali' ili kuthibitisha kuwa alikuwa hedhi

    Vyuo vikuu vya China hushutumiwa kwa kile wakosoaji wanaona kama majaribio ya kudhibiti wanafunzi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chuo kimoja mjini Beijing kimejikuta kikiwa katikati ya ghadhabu ya umma baada ya kudaiwa kumtaka mwanafunzi athibitishe kuwa alikuwa kwenye kipindi chake cha hedhi ili kupata likizo ya ugonjwa.

    Video ya mtandaoni, iliyorekodiwa ndani ya kile kinachoonekana kama kliniki na kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii mwezi huu, inamuonesha mwanamke akimuuliza mwanamke mzee: "Je, kila msichana mwenye hedhi lazima avue suruali yake na kukuonesha kabla ya kupata ruhusa ya likizo ya ugonjwa?" "Kimsingi ndiyo," mwanamke mzee anajibu.

    "Hii ni sheria ya shule." Vyombo vya habari vya ndani vilibainisha eneo la video hiyo kama kliniki katika chuo kikuu cha chuo kikuu cha Gengdan Institute, ambacho baadaye kilisema katika taarifa kwamba wafanyakazi wake "wamefuata itifaki".

    Lakini watumiaji wa mitandao ya kijamii wameichukulia hatua hiyo kama uingiliaji mkubwa wa faragha.

    Katika taarifa yake ya tarehe 16 Mei, Taasisi ya Gengdan iliripotiwa ikisema video za tukio hilo zinazosambaa mtandaoni "zimepotoshwa", na kwamba taasisi hiyo ina haki ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale "walioeneza kwa nia mbaya video zisizo za kweli".

    Taarifa hiyo pia ilisema kuwa wafanyakazi walifuata utaratibu ufaao wakati wa mkutano, kama vile "kuanzisha kazi ya kliniki baada ya kupata kibali cha mwanafunzi", na hawakutumia zana au kufanya uchunguzi wa mwili.

  6. Msaidizi wa Zelensky asema Urusi 'inakwamisha' mazungumzo ya kusitisha mapigano

    Yermak

    Chanzo cha picha, Reuters

    Msaidizi mkuu wa rais wa Ukraine ameitaka Urusi kuharakisha juhudi za kufikia usitishaji mapigano na kuishutumu Moscow kwa "kukwama" kwa majadiliano.

    "Kwa sasa, Moscow inazuia hata mjadala wa mapendekezo, haitoi maelezo mahususi, inapoteza muda tu. Njia pekee ya kuifanya Moscow iende kwa kasi ni kupitia vikwazo na silaha," Andriy Yermak anasema katika chapisho kwenye X.

    Wiki iliyopita, Trump na Putin walikuwa na mazungumzo kwa njia ya simu kwa saa mbili kujadili makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopendekezwa na Marekani.

    Trump alisema anaamini wito huo umekwenda "vizuri sana", na kuongeza kuwa Urusi na Ukraine "zitaanza mara moja" mazungumzo ya kusitisha mapigano na "kukomesha vita".

    Ukraine imekubali hadharani kusitisha mapigano kwa siku 30.

    Putin amesema tu Urusi itafanya kazi na Ukraine kuunda "mkataba" kuhusu "amani inayowezekana ya siku zijazo".

    Unaweza kusoma;

  7. Watu 54 wauawa katika mashambulizi ya Israel mjini Gaza - ripoti

    Msichana amesimama kwenye magofu ya jengo la shule katika Jiji la Gaza ambalo lilikumbwa na shambulio la anga

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Msichana amesimama kwenye magofu ya jengo la shule katika Jiji la Gaza ambalo lilikumbwa na shambulio la anga

    Takribani Wapelestina 54 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya anga ya Israeli usiku wa kuamkia leo, ikiwa ni pamoja na shambulizi dhidi ya shule ambayo inahifadhi wakimbizi katikati mwa Gaza, wakurugenzi wawili wa hospitali wameiambia BBC.

    Shule ya Fahmi Al-Jargwi iliyopo mjini Gaza imekuwa makazi ya mamia ya familia zilizofurushwa kutoka mji wa Beit Lahia, kwa sasa inakabiliwa na mashambulizi makali ya Israeli.

    Msemaji wa Kikosi cha Ulinzi wa Raia wa Gaza kinachoendeshwa na Hamas alisema miili 20, ikiwa ni pamoja na ya watoto, ilipatikana - mingi ilichomwa vibaya, baada ya moto kuteketeza madarasa mawili yaliyogeuzwa kuwa makazi.

    Jeshi la Israel (IDF) lilisema lililenga "kituo na udhibiti wa Hamas na Islamic Jihad".

    IDF ilisema eneo hilo lilikuwa linatumiwa "na magaidi kupanga... mashambulizi dhidi ya raia wa Israel na wanajeshi wa IDF", na kuishuutumu Hamas kwa kutumia "wakazi wa Gaza kama ngao".

    Moto ulikuwa kila mahali. Niliona miili iliyoungua ikiwa imelala chini," Rami Rafiq, mkazi anayeishi karibu na shule hiyo, alisema katika mahojiano na BBC kwa njia ya simu. "Mwanangu alizimia alipoona tukio hilo la kutisha."

    Kanda za video zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha moto mkubwa ukiteketeza sehemu za shule, zikiwa na picha za waathiriwa walioungua vibaya, wakiwemo watoto, na walionusurika wakiuguza majeraha mabaya.

    Soma pia:

  8. Ndege ya Japan yatua kwa dharura baada ya mtu mmoja kujaribu kufungua mlango

    Polisi walisema mtu huyo alizuiliwa na abiria wengine na wafanyakazi wa ndege

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ndege ya Japan iliyokuwa ikitoka Tokyo kuelekea Texas ililazimika kutua kwa dharura baada ya abiria kujaribu kufungua moja ya milango yake wakati wa safari hiyo.

    Ndege nambari 114 ya Nippon Airways (ANA) ilielekezwa Seattle saa chache baada ya kupaa siku ya Jumamosi "kutokana na abiria mkorofi", shirika hilo la ndege lilisema.

    Polisi wa Seattle waliambia vyombo vya habari kuwa walikuwa wamearifiwa kuhusu mtu ambaye "alijaribu kufungua milango ya kutokea wakati wa safari ya ndege".

    Mwanaume huyo, ambaye hakutambuliwa, alikuwa "na shida ya kiafya" na ilibidi azuiliwe na abiria wengine na wafanyakazi wa ndege, polisi walisema.

    Baadaye alipelekwa hospitali. Haijabainika iwapo atakabiliwa na mashtaka yoyote.

    "Usalama wa abiria na wafanyakazi wetu ndio kipaumbele chetu kikuu na tunapongeza juhudi za watekelezaji sheria wa eneo hilo kwa msaada wao," ANA ilisema katika taarifa.

    Wakati ndege ilikuwa ikingoja kwenye lami ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Seattle-Tacoma, mtu wa pili aliondolewa kwenye ndege kwa "tabia mbaya", mamlaka ilisema.

    Data ya safari ya ndege inaonesha kwamba ndege hiyo ilifika mahali ilipo, George Bush Intercontinental Airport huko Houston, Jumamosi mwendo wa 12:40 saa za ndani (17:40 GMT), saa nne baada ya muda wake uliopangwa kuwasili.

    Hili ni tukio la hivi karibuni zaidi katika msururu wa matukio kama haya.

    Mnamo Aprili, ndege ya Jetstar kutoka Bali, Indonesia ililazimika kugeuka wakati wa safari yake kuelekea Melbourne, Australia, baada ya abiria vilevile kujaribu kufungua mlango wa ndege angani.

    Novemba mwaka jana, mwanaume aliyejaribu kufungua mlango wa ndege wakati wa safari ya ndege ya American Airlines alizuiliwa na kufungwa na abiria wenzake kwa mkanda.

    Na mnamo Novemba 2023, abiria tisa wa ndege ya Asiana Airlines walipelekwa hospitalini wakiwa na matatizo ya kupumua baada ya mtu kufanikiwa kufungua mlango wa dharura wa ndege kabla ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Korea Kusini.

    Unaweza kusoma;

  9. Marekani yamkamata mtu kwa madai ya kujaribu kulipua ubalozi wake huko Israel

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Raia wa nchi mbili za Marekani na Ujerumani alikamatwa Jumapili kwa madai ya kujaribu kulipua ubalozi wa Marekani huko Tel Aviv, Israel, kulingana na wizara ya sheria.

    Maafisa walisema walimkamata Joseph Neumayer, 28, katika uwanja wa ndege wa John F Kennedy mjini New York.

    Alikuwa amerejeshwa na mamlaka ya Israel baada ya kupatikana na vifaa vya vilipuzi kwenye mkoba karibu na ubalozi huo.

    Bw Neumeyer alifikishwa mahakamani Jumapili na anazuiliwa gerezani, wizara hiyo ilisema.

    "Mshtakiwa huyu anashtakiwa kwa kupanga shambulio baya lililolenga ubalozi wetu nchini Israel, likitishia vifo kwa Wamarekani, na maisha ya Rais Trump," Mwanasheria Mkuu wa Serikali Pamela Bondi alisema.

  10. India iko katika hali ya tahadhari baada ya meli iliyobeba shehena hatari kuzama

    .

    Chanzo cha picha, Indian Coast Guard/Twitter

    Mamlaka katika jimbo la Kerala kusini mwa India wametoa tahadhari baada ya meli iliyokuwa imebeba mafuta na shehena ya hatari kuvuja na kuzama katika ufuo wa jimbo hilo katika bahari ya Arabia.

    Mwagikaji huo ulitokea katika meli yenye bendera ya Liberia ambayo ilipinduka karibu na jiji la Kochi siku ya Jumapili.

    Ukanda wa pwani una wingi wa viumbe hai na pia ni kivutio muhimu cha watalii.

    Wafanyakazi wote 24 waliokuwemo kwenye meli hiyo wameokolewa lakini baadhi ya makontena 640 ya meli hiyo yameripotiwa kuwa yakielea ufukweni na hivyo kusababisha yahamishwe.

    Mamlaka inahofia kuwa mafuta, fyueli na vitu vingine vyenye madhara ambavyo vimevuja kutoka kwa meli na shehena yake vinaweza kuhatarisha afya ya wakaazi na viumbe vya baharini.

    Soma zaidi:

  11. Maelfu wamkumbuka George Floyd kwenye maadhimisho ya kifo chake

    .

    Chanzo cha picha, TWITTER/RUTH RICHARDSON

    Maelfu wanamkumbuka George Floyd katika kumbukumbu ya miaka mitano tangu alipofariki dunia aliyeuawa na polisi.

    Mauaji ya Floyd, mwanamume mweusi huko Minneapolis yalisababisha maandamano nchini Marekani kupinga ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi.

    Siku ya Jumapili, familia ya Floyd ilikusanyika katika mji wao wa Houston karibu na kaburi la Floyd kwa ibada iliyoongozwa na Kasisi Al Sharpton, huku Minneapolis.

    Hata hivyo, kile ambacho wengi walikisifu kama "juhudi" ya kitaifa kukabiliana na ubaguzi wa rangi baada ya kifo cha Floyd, inaonekana kufifia wakati wa utawala wa Rais Donald Trump kwa kurudisha nyuma mageuzi ya polisi huko Minneapolis na miji mingine.

    Soma zaidi:

  12. Korea Kaskazini yamkamata afisa mkuu kwa kushindwa kuzindua meli ya kivita

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Korea Kaskazini imemkamata afisa wa nne kutokana na kushindwa kuzinduliwa kwa meli mpya ya kivita jambo ambalo limemkasirisha kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un.

    Ri Hyong-son, naibu mkurugenzi wa Idara ya viwanda vya silaha wa Chama tawala, "alihusika kwa kiasi kikubwa kwa matokeo hayo", shirika la habari la serikali KCNA lilisema Jumatatu.

    Meli hiyo ilikuwa imeharibika sehemu yake ya ndani, katika kile Kim alichoeleza kama "kitendo cha uhalifu" ambacho "kiliharibu sana heshima na sifa ya [nchi]" hiyo.

    Chombo hicho kinarekebishwa chini ya mwongozo wa kikundi cha wataalam, KCNA alisema.

  13. 'Hali ni mbaya' - BBC yaangazia mtoto aliyeachwa njaa Gaza

    .

    Hakuna msisimko wowote hata wakati unapozungumza na raia. Watoto wanapata shida kutazama. Ni nini kinachoweza kumshangaza mtoto anayeishi kati ya wafu, wanaokufa, wanaongojea kufa? Huku njaa ikiwamaliza.

    Wanasubiri kwenye foleni ama kupata mgao mdogo au wakose kabisa.

    Wamemzoea mpigapicha anayefanyakazi kwa ajili ya BBC.

    Anashuhudia njaa wanayopitia, kufa kwao, na kufunikwa taratibu kwa miili yao - au vipande vya miili yao - katika sanda nyeupe ambazo zinaandikwa majina yao, kama yanajulikana.

    Kwa miezi 19 ya vita, na sasa chini ya mashambulizi mapya ya Israel, mpigapicha huyu wa eneo - ambaye jina lake tumelificha kwa sababu ya usalama wake - amesikiliza kilio cha uchungu cha manusura katika ua wa hospitali.

    Alimtafuta Siwar Ashour, msichana wa miezi mitano ambaye sura yake imedhoofika na kilio cha uchovu katika hospitali ya Nasser huko Khan Younis kimekuathiri sana.

    Alikuwa na uzani wa zaidi kidogo tu ya kilo 2. Mtoto wa kike wa miezi mitano anayepaswa kuwa na kilo 6 au zaidi.

    Siwar ameruhusiwa kurejea nyumbani.

    .

    Siwar ni mtulivu, anajihisi salama na uwepo wa wanawake wawili. Hawezi kunyonya maziwa ya kawaida kwa sababu ya tatizo la mzio. Chini ya hali ya vita na zuio la Israeli kwa misaada inayowasili, kuna uhaba mkubwa wa maziwa.

    Najwa, mamake Siwar, 23, anaeleza kuwa hali ya mtoto wake iliimarika kidogo alipokuwa hospitalini, lakini sasa imeanza tena kuzorota kwa sababu ya ukosefu wa maziwa.

    Nzi hujaa mbele ya uso wa Siwar. "Hali ni mbaya sana," anasema Najwa, "wadudu wanamjia, lazima nimfunike na kitambaa ili wasimguse".

    Siwar ameishi na sauti ya vita tangu Novemba mwaka jana alipozaliwa. Milio ya risasi na ndege zisizo na rubani za Israel zinazunguka juu ya anga. Sauti ya vifaru, ndege za kivita, na roketi ni kubwa sana na ziko karibu nasi. Siwar anaposikia sauti hizi, anashtuka na kuanza kulia."

    Soma zaidi:

  14. Mashambulizi ya Israel huko Gaza yaua watu 24 - madaktari

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Takriban Wapalestina 24 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya anga ya Israel usiku kucha, ikiwa ni pamoja na shambulizi dhidi ya shule ambayo ni makazi kwa familia zilizohamishwa katikati mwa Gaza, kulingana na madaktari na maafisa wa ulinzi wa raia.

    Shambulizi hilo lililenga shule ya Fahmi Al-Jargawi katika Jiji la Gaza, ambayo imekuwa ikihifadhi mamia ya watu waliokimbia makazi yao kaskazini wa Beit Lahia, ambao kwa sasa unashuhudia mashambulizi makali kutoka kwa jeshi la Israel.

    Msemaji wa shirika la Ulinzi wa Raia wa Gaza linaloendeshwa na Hamas alisema miili 20, ikiwa ni pamoja na watoto, iliokolewa shuleni humo - wengi wao wakiwa wameungua vibaya - baada ya moto kuteketeza vyumba viwili vya madarasa.

    Wanajeshi wa Israel wametafutwa ili kutoa maoni yao.

    "Moto ulikuwa kila mahali. Niliona miili iliyoungua ikiwa imelala chini," alisema Rami Rafiq, mkazi anayeishi mkabala na shule hiyo, kupitia simu na BBC. "Mwanangu alizimia alipoona tukio hilo la kutisha."

    Kanda za video zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha moto mkubwa ukiteketeza sehemu za shule, zikiwa na picha za waathiriwa walioungua vibaya, wakiwemo watoto, na walionusurika wakiuguza majeraha mabaya.

    Ripoti za ndani zilisema miongoni mwa waliofariki ni Mohammad Al-Kasih, mkuu wa uchunguzi wa polisi wa Hamas kaskazini mwa Gaza, pamoja na mke wake na watoto.

    Muda mfupi kabla ya shambulizi la shule, shambulio lingine la anga la Israeli lilishuhudiwa katika nyumba moja iliyopo katikati mwa jiji la Gaza, na kuua watu wanne zaidi, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas ilisema.

    Mashambulizi hayo mawili ni sehemu ya mashambulizi makubwa ya Israel ambayo yameongezeka katika sehemu ya kaskazini ya eneo hilo kwa muda wa wiki moja iliyopita.

    Soma zaidi:

  15. Trump amwita Putin 'mwendawazimu' baada ya shambulio kubwa la Urusi huko Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema "hajafurahishwa" na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, kufuatia shambulio kubwa zaidi la anga dhidi ya Ukraine.

    Katika hali ambao ni nadra sana kutokea, Trump alisema: "Ni kitu gani kilichomtokea? Anaua watu wengi sana." Baadaye alimwita Putin "mwendawazimu".

    Awali, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema "ukimya" wa Marekani juu ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi ndio unaompa kiburi Putin, akitoa "shinikizo" - ikiwa ni pamoja na vikwazo vikali - dhidi ya Urusi.

    Takriban watu 12 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa nchini Ukraine usiku wa kuamkia Jumapili baada ya Urusi kufanya shambulizi la ndege zisizo na rubani na makombora 367 - idadi kubwa zaidi katika usiku mmoja tangu Putin alipoanzisha uvamizi nchini humo mnamo 2022.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini New Jersey siku ya Jumapili, Trump alisema: "Nimemfahamu Putin kwa muda mrefu, nilishirikiana naye kila wakati, lakini anatuma makombora mijini na kuua watu, na sifurahii hata kidogo."

    Alipoulizwa iwapo anafikiria kuongeza vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi, Trump alijibu: "Kabisa." Rais wa Marekani ametishia mara kwa mara kufanya hivyo kabla - lakini bado hajaweka vikwazo vyovyote dhidi ya Moscow.

    Muda mfupi baadaye, Trump aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa Truth Social kwamba Putin "amekuwa mwendawazimu kabisa".

    "Nimekuwa nikisema kwamba anataka Ukraine yote, sio kipande tu, na labda hiyo inathibitisha kuwa kweli, lakini ikiwa atafanya hivyo, itasababisha kuanguka kwa Urusi!"

    Lakini Trump hakumsaza hata Zelensky, alimtolea maneno makali na kusema kuwa "haifanyii nchi yake vizuri kwa jinsi anavyozungumza".

    "Kila kitu kutoka kinywani mwake kinasababisha matatizo, sifurahii, na itakuwa bora ikiwa ataacha" Trump aliandika kuhusu Zelensky.

    Soma zaidi:

  16. Bila shaka hujambo, karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja