Kesi ya Derek Chauvin: George Floyd 'alifariki dunia taratibu' wakati amekamatwa na polisi

George Floyd, alikuwa baba ya msichana wa miaka sita

Chanzo cha picha, TWITTER/RUTH RICHARDSON

Maelezo ya picha, George Floyd, alikuwa baba ya msichana wa miaka sita

Mtu mmoja aliyeshuhudia dakika za mwisho za maisha ya George Floyd ameelezea kilichotokea katika siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa kesi ya Derek Chauvin, polisi mzungu anayeshutumiwa kwa kumuua Bwana Floyd mwanaume mweusi.

Donald Williams III, shahidi wa mwendesha mashitaka, amesema Bwana Floyd alikuwa "alifariki dunia taratibu" kipindi cha dakika tisa za mwisho pale Bwana Chauvin alipopiga goti juu ya mgongo wake na shingoni.

Wakili wa Bwana Chauvin alimtetea mteja wake akisema kitendo cha utumiaji nguvu cha mteja wake "sio cha kuridhisha lakini kulikuwa na ulazima wa kufanya hivyo".

Kesi hiyo inaonekana na wengi kama nyakati muhimu katika kukabiliana na suala la ubaguzi wa rangi nchini Marekani.

Katika tukio hilo lililotokea Mei 2020 - Bwana Chauvin alinaswa kwenye ukanda wa video akiwa amepiga goti juu ya shingo ya Bwana Floyd, mwanamume mweusi, katika mji wa Minneapolis - na kuchochea maandamano Marekani na dunia kote kupinga ukatili unaotekelezwa na polisi pamoja na ubaguzi wa rangi.

Bwana Chauvin, 45, ambaye alifutwa kazi na idara ya polisi, amekanusha makosa yanayomkabili ya mauaji na kuua bila kukusudia ambayo adhabu yake inaweza kuwa kifungo gerezani cha hadi miaka 40.

Maafisa wengine waliokuwepo wakati hilo linatoke ni - Tou Thao, J Alexander Keung na Thomas Lane - watafikishwa mahakamani baadaye mwaka huu.

Kitu gani kilichosemwa siku ya kwanza ya kusikizwa kwa kesi hiyo?

Donald Williams, mjasiriamali, 33, amesema alikuwa anataka kuingia katika mgahawa mmoja uliopo Minneapolis, Minnesota, aliposhuhudia kukamatwa kwa Bwana Floyd Mei 25, 2020.

The George Floyd Square is seen the day before open statements in the trial of former police officer Derek Chauvin, who is facing murder charges in the death of George Floyd, in Minneapolis, Minnesota, on 28 March 2021

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kuuawa kwa George Floyd kumesababisha maandamano Marekani na kote dunia dhidi ya ukatili na ubaguzi wa rangi.

Alisema aliamua kutoingia mgahawani kwasababu baada ya hapo "alikosa nguvu" na badala yake akaanza mazungumzo na maafisa wa polisi na kuwataka kuangalia mapigo ya moyo wake.

Ameiambia mahakama alimuona Bwana Floyd akifariki dunia taratibu hadi dakika ya mwisho ya uhai wake.

"Alifariki dunia akitapatapa kama samaki anavyokufa akiwa mfukoni," alisema. "Taratibu macho yake yakageuka na kuanza kubadilika kuelekea nyuma ya kichwa chake" hadi "akawa amefariki kabisa, hana tena maisha ndani yake".

Mwanzoni mwa kesi hiyo, waendesha mashitaka walianza kwa kuonesha ukanda wa video ya dakika 9, iliyochukuliwa na mmoja wa waliokuwa wanashuhudia tukio hilo, ambayo ina muonesha Bwana Chauvin akipiga goti juu ya mgongo na shingo ya Bwana Floyd, 46.

Mwendesha mashitaka Jerry Blackwell aliiambia mahakama kuwa Bwana Floyd alisema mara 27 kwamba hawezi kupumua.

Ukanda huo ulithibitisha kuwa Bwana Chauvin "alikuwa anafanya kitu hatari... bila kufikiria athari zake katika mwili wa George Floyd," Bwana Blackwell amesema.

Wakili upande wa utetezi Eric Nelson, katika ufunguzi wa taarifa yake, alisema kuwa ushahidi uliopo "ni zaidi ya dakika 9 na sekunde 29" zinazojitokeza kwenye video hiyo.

Alisema kuwa ushahidi huo unaonesha Bwana Floyd "alifariki kwa tatizo lenye kuhusishwa na moyo ambalo kitaaluma linasababishwa na shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa moyo, utumiaji wa methamphetamine na kusambaa kwa homoni ya adrenalini mwilini mwake".

Mahakama pia imesikiliza ushahidi kutoka kwa polisi wa kitengo cha 911, Jena Scurry, ambaye alipeleka polisi katika nagahawa kulikotokea tukio hilo baada George Floyd kuripotiwa kwa kutumia pesa feki ya dola 20 kulipia bili yake.

People gather during a demonstration outside the Hennepin County Government Center on March 29, 2021 in Minneapolis

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu waliandamana katika eneo la Minneapolis

Mahakama pia ilisikiliza ushahidi kutoka kwa waliochukua video hiyo, Alisha Oyler, ambaye amekuwa akifanyakazi katika duka lililo karibu.

Kabla ya kuanza kwa kesi hiyo, Familia ya Bwana Floyd, mawakili wa haki za kiraia na wanaharakati walipiga goti nje ya mahakama katika kipindi ambacho Bwana Chauvin alipiga goti lake juu ya shingo ya Bwana Floyd.

Yapi zaidi tunayofahamu kuhusu kesi hiyo?

Washiriki 15 waliokuwa mahakamani kusikiliza kesi hiyo - wanawake 9 na wanaume 6 - walichaguliwa; 9 ni wazungu na sita ni weusi au wenye asili mbili.

Derek Chauvin

Chanzo cha picha, DARNELLA FRAZIER

Maelezo ya picha, Derek Chauvin polisi mzungu anayeshutumiwa kwa kumuua George Floyd mwanamume mweusi baada ya kumuwekea goti juu ya shingo yake
1px transparent line

Hakimu mmoja - ambaye alikuwa kama wa akiba iwapo mmoja kati ya waliochaguliwa ataondoka kabla ya kesi kuanza kusikilizwa - aliondolewa Jumatatu na kesi hiyo ikaanza kusikilizwa na mahakimu 12 huku wawili wakiwa wa akiba.

Wataendelea kutowatambulisha au kutoonekana wakati kesi hiyo inaendelea kwenye televisheni, ambayo inatarajiwa kuendelea kwa wiki nne.

Mahakama hiyo iliyopo katikati mwa Minneapolis imezungushiwa uzio vizuri, imewekewa vizuizi vilivyojengwa kwa zege na sengenge.

Kwanini kesi hii inachukuliwa kwa uzito mkubwa?

Ukanda wa video unamuonesha Derek Chauvin akipiga goti juu ya shingo ya George Floyd mnamo mwezi Mei mwaka jana ilitazamwa dunia nzima.

Kwa wengi, kifo cha Floyd akiwa katika kituo cha polisi kilidhihirisha wazi unyama unaotekelezwa na polisi - hasa dhidi ya watu weusi na kusababisha maandamano kote dunia yaliyopinga ubaguzi wa rangi.

Hata hivyo, licha ya tukio hilo kusababisha hasira kote dunia, sio la kwanza wala la mwisho.

Marekani, polisi huwa ni nadra sana kwa polisi kupatikana na hatia na kuchukuliwa hatua kama walikuwa kazini.

Uamuzi katika kesi hii unafuatiliwa ulimwengine kote na utakuwa ishara ya vile mfumo wa sheria Marekani unavyofanya kazi hasa kwa kesi za mauaji yaliyotokea wakati polisi akiwa kazini.