Unajua kwanini abiria wa safari za ndege huzuiwa kubeba 'power bank'?

Power bank

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Chanzo cha moto kwenye ndege ya Airbus A321 nchini Korea Kusini kimebainika.

Mamlaka za eneo hilo zilisema moto huo ulisababishwa na 'power bank'.

Ndege ya abiria ya Air Busan ilishika moto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Gimhae nchini Korea Kusini Januari 28, 2025. Watu watatu walijeruhiwa kidogo.

Wizara ya Uchukuzi ya Korea Kusini ilisema mnamo Machi 14 kwamba uchunguzi ulibaini kuwa power bank iliharibika na kusababisha ndege hiyo kushika moto.

Power bank ilikuwa kwenye eneo la kuhifadhia juu ya kiti cha abiria, ambapo moto huo ulizuka kwa mara ya kwanza.

Wadadisi wanasema kuwa kifaa hicho kilionesha dalili za moto, lakini haijulikani ni kwa nini betri ya power bank hiyo iliharibika.

Jambo kuu ni kwamba hii ni ripoti ya uchunguzi wa muda mfupi tu. Ripoti ya mwisho ya uchunguzi kuhusu ndege hiyo bado haijatolewa.

Ilipigwa marufuku tangu 2016

Mashirika ya ndege duniani kote yamepiga marufuku power bank kubebwa kwenye mizigo inayoingia (vitu unavyokabidhi kabla ya kupanda ndege) kwa miaka mingi kwa sababu za kiusalama.

Power bank zina betri ya lithiamu-ioni.

Betri hizi zina uwezo wa kuzalisha joto kubwa na zinaweza kusababisha mshtuko wa umeme ikiwa kuna kasoro yoyote ndani yake.

Kulingana na ushauri uliotolewa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga, tangu 2016, abiria wamepigwa marufuku kubeba betri zozote za lithiamu-ion kwenye mizigo iliyokaguliwa kwenye ndege.

Kufuatia moto kwenye ndege ya Airbus nchini Korea Kusini, Air Busan imeanza kuchukua hatua kali za kiusalama, na kutangaza kuwa abiria hawataruhusiwa tena kubeba power bank kwenye mizigo yao ya mkononi.

Kampuni hiyo ilisema kuwa hatua hii imechukuliwa kutokana na kuongezeka kwa matukio ya power bank kupata joto.

Uchunguzi wa muda kuhusu chanzo cha ajali ya ndege nchini Korea Kusini umegundua kuwa power bank ndiyo iliyosababisha moto kwenye ndege hiyo.

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati huo huo, China Airlines na Thai Airlines pia zinatekeleza sheria kama hiyo.

Scoot, shirika la ndege la gharama nafuu la Singapore Airlines, litapiga marufuku matumizi na kuzichaji power bank kwenye safari za ndege kuanzia tarehe 1 Aprili.

Mnamo Februari 28, serikali ya Korea Kusini ilitangaza kwamba abiria wanaopanda ndege za ndani wanapaswa kukaa na betri zao na chaja, badala ya kuzihifadhi kwenye masanduku ya juu ndani ya ndege.

Kumekuwa na matukio ya moto kwenye meli yaliyosababishwa na betri za lithiamu hapo awali.

Mnamo Machi 2017, headphones za mwanamke zililipuka kwenye ndege kutoka Melbourne, Australia, hadi Beijing.

Hii ilisababisha jeraha usoni mwake. Mwanamke huyo alizinduka baada ya kusikia headphone zake zikilipuka na mara moja akazivua na kuzitupa chini.

Baada ya ajali hiyo, ilibainika kuwa ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu katika betri ya lithium-ion.

Hapo awali, safari ya ndege huko Sydney ilisitishwa baada ya moshi kuonekana kutoka eneo la mizigo.

Baadaye iligundulika kuwa betri ya lithiamu-ioni iliyohifadhiwa kwenye mizigo ilikuwa imepata moto.

Betri za lithiamu-ion zina uwezo wa kutoa joto kali.

Chanzo cha picha, Getty Images

Jumuiya ya Huduma za Mazingira ya Uingereza ilisema katika ripoti ya 2022 kwamba zaidi ya matukio 700 ya moto huripotiwa kila mwaka katika sehemu za kutupa taka.

Matukio mengi haya husababishwa na betri za lithiamu zilizotupwa.

Betri za lithiamu-ion zinaweza kulipuka ikiwa zimeharibiwa au kuvunjika. Betri hizi hazitumiwi tu katika power bank, bali pia katika miswaki ya betri, vinyago, simu za mkononi na kompyuta mpakato.