Makao makuu ya Jeshi Sudan huko al-Fashir, yatekwa na wanamgambo

Video iliyochapishwa na kundi la wanamgambo la RSF imeonyesha wanajeshi wake wakishangilia mbele ya bango la Kambi ya Jeshi ya Sixth Infantry, ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan katika eneo la Darfur, magharibi mwa nchi hiyo.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Herminie aapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Shelisheli

    A

    Chanzo cha picha, SNN

    Dk. Mathew Antonio Patrick Herminie ameapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Shelisheli katika hafla iliyofanyika jioni ya leo katika uwanja wa Stad Linite, Roche Caïman.

    Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa serikali, mabalozi, wageni mashuhuri pamoja na wananchi.

    Dk. Herminie, ambaye ni kiongozi wa chama cha United Seychelles, alishinda uchaguzi wa urais uliomalizika hivi karibuni baada ya kumbwaga Rais aliyekuwa madarakani, Wavel Ramkalawan, katika duru ya pili ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa. Alipata asilimia 52.7 ya kura, huku Bw. Ramkalawan akipata asilimia 47.3.

    Uchaguzi huo uliingia raundi ya pili baada ya wagombea wote wawili kushindwa kupata zaidi ya nusu ya kura katika duru ya kwanza.

    Ushindi wa Dk. Herminie unaashiria kurudi madarakani kwa chama cha United Seychelles baada ya miaka mitano ya kuwa upinzani. Chama hicho kiliongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1977 hadi 2020.

    Dk. Herminie, ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa kati ya mwaka 2007 na 2016, ameanza rasmi muhula wake kwa kuahidi kukuza haki za kijamii na kulinda mazingira tete ya taifa hilo la visiwa. Pia ametangaza kuwa serikali yake itasitisha ujenzi wa hoteli ya kifahari inayofadhiliwa na Qatar kwenye kisiwa chenye umuhimu mkubwa wa ikolojia.

    Shelisheli, inayojulikana kwa fukwe zake safi na msimamo wake wa maendeleo endelevu, inaendelea kuwa moja ya vituo vinavyoongoza duniani vya utalii wa kifahari na wa kimazingira. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Shelisheli pia ni taifa tajiri zaidi barani Afrika kwa kipato cha mtu mmoja mmoja (per capita).

  2. Vikosi vya RSF vyatangaza kuteka makao makuu ya jeshi mjini al-Fashir, Sudan

    S

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kundi la wanamgambo Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan, limesema Jumapili kuwa limefanikiwa kuteka makao makuu ya jeshi la Sudan katika mji wa al-Fashir, ngome ya mwisho ya jeshi hilo katika eneo la Darfur, magharibi mwa nchi hiyo.

    Video iliyochapishwa na RSF imeonyesha wanajeshi wake wakishangilia mbele ya bango la Kambi ya Jeshi ya Sixth Infantry. Shirika la habari la Reuters limeweza kuthibitisha eneo hilo, lakini halikuweza kuthibitisha tarehe ya tukio hilo. Jeshi la Sudan halijatoa tamko lolote kuhusu hali yake ya sasa katika eneo hilo.

    Kutekwa kwa al-Fashir kunachukuliwa kama ushindi mkubwa wa kisiasa kwa RSF, kwani kunaweza kuharakisha mgawanyiko wa kivitendo wa nchi hiyo. Hatua hiyo inaweza kuiwezesha RSF kuimarisha udhibiti wake katika eneo pana la Darfur, ambalo imekuwa ikilitumia kama kitovu cha serikali mbadala iliyoanzishwa mapema majira ya kiangazi mwaka huu.

    Hata hivyo, wanaharakati wameonya kwa muda mrefu kuwa kutekwa kwa mji huo na RSF kunaweza kusababisha mashambulizi ya kikabila, kama ilivyotokea baada ya kundi hilo kutwaa kambi ya wakimbizi ya Zamzam kusini mwa mji huo.

    RSF imekuwa ikiuzingira mji wa al-Fashir, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini kwa muda wa miezi 18, ikipambana na jeshi la serikali, wapiganaji wa zamani na wanamgambo wa eneo hilo.

    Katika kipindi hicho, RSF imetuhumiwa kushambulia raia kwa kutumia ndege zisizo na rubani na mashambulizi ya mizinga mara kwa mara, hatuailiyosababisha njaa kali miongoni mwa wakazi wapatao 250,000 waliobaki magharibi mwa mji huo.

    Reuters imeripoti kuwa haikuweza kuwasiliana na wakazi wa al-Fashir, ambao hutegemea vifaa vya Starlink kwa mawasiliano kutokana na kukosekana kwa huduma za simu za kawaida kwa muda mrefu.

    Wiki iliyopita, RSF ilidai kuwa ilikuwa inawawezesha raia na wapiganaji waliokubali kujisalimisha kuondoka mjini al-Fashir. Hata hivyo, waliotoroka wameeleza kwamba walikumbana na vitendo vya uporaji, ubakaji na mauaji vilivyofanywa na wanajeshi wa RSF njiani.

    Ujumbe maalum wa Umoja wa Mataifa ulioundwa kuchunguza mzozo huo ulisema mwezi uliopita kwamba RSF wamehusika na makosa kadhaa ya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa harakati za kuuzingira mji wa al-Fashir. Jeshi la Sudan pia limetajwa kufanya makosa ya kivita katika mapigano hayo.

  3. Cameroon yakamata vinara wa upinzani 30 siku moja kabla ya matokeo ya urais kutangazwa

    ar

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mamlaka nchini Cameroon imewakamatwa takriban wanasiasa na wanaharakati 30 wanaohusishwa na mgombea wa urais wa upinzani Issa Tchiroma Bakary, timu yake ya kampeni imesema Jumapili, hali inayoongeza mvutano kuelekea kutangazwa kwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 12.

    Miongoni mwa waliokamatwa ni Anicet Ekane, kiongozi wa chama cha MANIDEM, na Djeukam Tchameni, mwanaharakati mashuhuri wa harakati ya Union for Change, ambao wote waliunga mkono azma ya Tchiroma kugombea urais.

    Kukamatwa kwao kunatokea wakati kukiwa na makabiliano yanayoongezeka kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa Tchiroma katika taifa hilo la Afrika ya Kati linalozalisha kakao na mafuta. Tchiroma ametoa wito wa kufanyika kwa maandamano ya kitaifa Jumapili mchana.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cameroon, Paul Atanga Nji, alithibitisha katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumamosi kuwa baadhi ya watu wamekamatwa kuhusiana na kile alichokiita “harakati za uasi,” ingawa hakutaja majina wala idadi kamili ya waliotiwa mbaroni.

    “Wito wa maandamano unaotolewa na baadhi ya wanasiasa wanaotawaliwa na tamaa ya madaraka bila shaka unaunda mazingira ya mgogoro wa kiusalama na kuchochea utekelezaji wa mpango wa uasi,” alisema Nji.

    Katika chapisho kwenye ukurasa wa Facebook wa kampeni yake Jumapili, Tchiroma alikanusha tuhuma za kupanga uasi na kudai kuwa baadhi ya maofisa wa serikali walijaribu kufanya mazungumzo ya siri na baadhi ya waliokamatwa kabla ya kuwatia mbaroni.

    “Mliwatafuta mjadiliane nao, sasa mnasema ni magaidi? Walipokataa mapendekezo yenu ndiyo mnawakamata?” aliandika Tchiroma.

    Tchiroma, ambaye ni waziri wa zamani na aliwahi kuwa mshirika wa Rais Paul Biya, amejitangaza mshindi wa uchaguzi huo na amesisitiza kuwa hatakubali matokeo yoyote tofauti.

    Maandamano yamezuka katika miji kadhaa wiki iliyopita baada ya vyombo vya habari vya ndani kuripoti matokeo ya awali yanayoonyesha kuwa Biya yuko mbioni kutangazwa mshindi.

    Biya, mwenye umri wa miaka 92, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1982 na ni rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani aliye madarakani kwa sasa, anaweza kuendelea kutawala kwa miaka mingine saba iwapo Baraza la Katiba litamtangaza mshindi Jumatatu.

  4. Vilabu vikubwa vya soka vya Sudan kucheza ligi Rwanda

    Al Hilal

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vilabu vitatu vya soka vya Sudan vitaruhusiwa kushiriki ligi ya Rwanda msimu huu, ili viendelee kucheza huku migogoro ya ndani nchini mwao ikiendelea kuzuia shughuli za kawaida za michezo.

    Sudan imekumbwa na mgogoro kati ya jeshi na Rapid Support Forces tangu Aprili 2023, ambapo zaidi ya watu 150,000 wameripotiwa kuuawa na takriban milioni 12 wamekimbia makazi yao, hali inayosababisha mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.

    Watu waliokimbia wakati mgogoro ulipoibuka walianza kurejea mwaka huu baada ya jeshi la Sudan kuchukua tena mji mkuu Khartoum, lakini vilabu viwili vya mjini humo vitaendelea na kucheza nje kwa sababu miundombinu yao imeharibiwa vibaya.

    Msimu uliopita, Al Hilal na Al Merrikh waliruhusiwa kucheza ligi nchini Mauritania, upande mwingine wa bara, ili kuendeleza shughuli za klabu.

    Sasa, pamoja na Al Ahli Wad Madani, vilabu hivi vimepewa ruhusa ya kujiunga na ligi ya Rwanda msimu huu, Shirikisho la Soka la Rwanda (Rwanda Football Association), limesema.

    Mnamo Julai, Al Hilal na Al Merrikh, ambao kati yao wamezoa mataji yote isipokuwa manne tangu ligi ya Sudan ilipoanzishwa mwaka 1965, waliruhusiwa kucheza mashindano madogo ya ndani ili kuamua ni nani atakayeshiriki mashindano ya klabu barani Afrika msimu wa 2025-26.

    Mashindano hayo ya timu nane yalifanyika mbali na mzozo katika eneo la Ad-Damer, umbali wa kilomita 430 kutoka Khartoum, na Atbara, kilomita 320 kaskazini mwa mji mkuu, huku Al Hilal na Al Merrikh wakipata nafasi kuwakilisha Afrika, na Al Ahli Wad Madani kumaliza nafasi ya tatu.

    Al Hilal imejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kuifunga timu ya Police ya Kenya jumla ya mabao 4-1. Katika mechi ya “nyumbani” ya raundi ya pili waliibuka na ushindi wa 3-1 siku ya Ijumaa, mechi iliyochezwa Benghazi, Libya.

    Libya pia imetumika kama makazi ya timu ya taifa ya Sudan, ambayo itashiriki Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Morocco mwishoni mwa mwaka huu licha ya kutocheza mechi za nyumbani tangu Machi 2023.

  5. Tanzania kukumbwa na mvua kubwa ya siku 3 kuanzia leo

    A

    Chanzo cha picha, TMA

    Tanzania inatarajia kupata mvua kubwa zitakazodumu kwa kipindi cha siku tatu kwenye ukanda wake wa Pwani, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini humo (TMA). Taarifa ya mvuo hizo iliyochapichwa na Mwanananchi mvua jizo zinatarajiwa kunyesha kuanzia tarehe 26 hadi 28 Oktoba.

    Mikoa iliyoainishwa kukumbwa na hatari ya mvua kubwa ni Mtwara, Lindi, Pwani na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

    Taarifa hiyo inasema mvua hizo zinaweza kuambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa pwani, kutokana na msukumo wa kimbunga kinachoitwa Tropical Storm Chenge kinachozidi kusogea Magharibi mwa Bahari ya Hindi.

    Mamlaka hiyo ya Hali ya Hewa inasema inaendelea kufuatilia maendeleo ya kimbunga na mvua hizo.

    Hata hivyo, baadhi ya wataalam wa hali ya hewa wanasema kuwa kiwango cha mvua kinategemea mabadiliko ya haraka ya mfumo wa hali ya hewa, na kuhimiza wananchi kufuatilia taarifa rasmi mara kwa mara kupitia vyombo vya habari na tovuti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuchukua tahadhari.

  6. Maelfu waandamana Tunisia kupinga janga la uchafuzi wa mazingira

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelfu ya raia wa Tunisia waliandamana katika mji mkuu, Tunis, siku ya Jumamosi kupinga janga kubwa la mazingira linalosababishwa na uchafuzi kutoka kiwanda cha kemikali cha serikali kilichoko mjini Gabes, huku maandamano hayo yakienea kutoka kusini hadi maeneo mengine ya nchi.

    Maandamano haya ni sehemu ya mlolongo wa upinzani unaoonyesha kuongezeka kwa hasira za wananchi kuhusu jinsi serikali inavyoshughulikia tatizo la uchafuzi wa mazingira na kuzorota kwa huduma za kijamii. Hali hii imekuwa changamoto kubwa zaidi kwa Rais Kais Saied tangu alipochukua madaraka yote mwaka 2021.

    Wakazi wa Gabes wameripoti ongezeko la magonjwa ya kupumua, mifupa (osteoporosis), na saratani, ambayo wanasema yanasababishwa na gesi zenye sumu kutoka viwanda vya shirika la kemikali la serikali, vinavyotupa maelfu ya tani za taka baharini kila siku.

    Wimbi jipya la maandamano Gabes lilichochewa mapema mwezi huu baada ya makumi ya wanafunzi wa shule kuathiriwa na gesi zenye sumu kutoka kiwandani kinachozalisha kemikali na mbolea. Wakati wa maandamano mjini Tunis, waandamanaji walibeba mabango na kuimba kauli mbiu za kuunga mkono wakazi wa Gabes, wakilaani hatua za serikali kuwa “za ukandamizaji”. Serikali ilisema imewakamata watu waliokuwa wakihusishwa na vurugu.

  7. “Nimeshinda Uchaguzi, siogopi kutupwa jela” – Kiongozi wa upinzani Cameroon, Bakary

    d

    Kiongozi wa upinzani nchini Cameroon, Issa Tchiroma Bakary, ambaye amejitangaza mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 12 Oktoba, ameiambia BBC kwamba hatakubali kura kuibiwa, huku matokeo rasmi yakitarajiwa kutangazwa kesho Jumatatu.

    Bakary amesema timu yake imekusanya matokeo kutoka vituo mbalimbali vya kupigia kura na kwamba “hakuna shaka kabisa” kuhusu ushindi wake. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 76, aliwahi kuwa waziri serikalini kabla ya kujitenga na Rais Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92, ambaye anatafuta muhula mwingine baada ya kuwa madarakani kwa miaka 43.

    Chama tawala kimepinga madai ya ushindi wa Bakary, kikiyaita kuwa ni kinyume cha sheria kwa sababu ni Baraza la Katiba pekee ndilo lenye mamlaka ya kutangaza matokeo rasmi.

    Katika mahojiano nyumbani kwake mjini Garoua, kaskazini mwa Cameroon, Bakary alisema amewahimiza wafuasi wake kulinda kura zao. “Hatutakubali kura zao kuibiwa na mtu yeyote,” alisema akiwa amevalia joho jeupe lenye mapambo ya dhahabu.

    Waziri huyo wa zamani alisema hana wasiwasi kuhusu kukamatwa au kufungwa gerezani. “Lakini najua tayari nimeshinda uchaguzi wa urais,” alisisitiza. “Hakuna shaka, wala kivuli cha shaka. Ushindi wangu haupingiki.”

    Akihoji uwezo wa Biya, rais mzee zaidi duniani kwa sasa, kuendelea kushikilia wadhifa huo, Bakary alisema chama tawala CPDM “kimebanwa ukutani” na hakiwezi kukubali ukweli wa kura. Alitoa changamoto kwao kuthibitisha kama anachosema si kweli.

    Bakary alitetea uamuzi wake wa kujitangaza mshindi, akisema sheria “haizuii kufanya hivyo.” Awali, alisema ameshinda uchaguzi huo kwa takribani asilimia 55 ya kura, akitaja takwimu zilizokusanywa kutoka asilimia 80 ya wapiga kura wote nchini.

  8. Kamala Harris kuwania tena urais Marekani

    s

    Makamu wa rais wa zamani wa Marekani, Kamala Harris, ameiambia BBC kwamba bado hajamaliza safari yake ya kisiasa, akidokeza kuwa anaweza kuwania tena urais.

    Kauli yake inakuja wakati chama cha Democrat kikiendelea kutafuta majibu baada ya ushindi mkubwa wa Donald Trump wa chama cha Republican mwaka mmoja uliopita. Lawama nyingi zimeelekezwa kwa rais wa zamani Joe Biden kwa kutojiondoa mapema kabla ya uchaguzi.

    Wapo pia wanaohoji kama Harris angeweza kuendesha kampeni bora zaidi na kutoa ujumbe ulio wazi kuhusu suala kuu lililokuwa likiwahusu Wamarekani:Uchumi.

    Katika mahojiano hayo na BBC, Harris alifichua uwezekano wa kugombea tena urais, akisema kwamba anawaamini wajukuu wake wadogo wataona rais mwanamke “katika maisha yao, bila shaka.”

    Alipoulizwa kama huyo rais mwanamke anaweza kuwa yeye, Harris alijibu kwa maneno, “inawezeka”, akithibitisha kwamba anafikiria uwezekano wa kuwania tena wadhifa huo. Alisema bado hajafanya uamuzi rasmi, lakini akaweka wazi kwamba bado anaona ana nafasi ya kuendelea kwenye siasa.

    “Bado sijamaliza,” alisema Harris. “Maisha yangu yote yamekuwa ya utumishi kwa jamii na hiyo ipo ndani yangu.”

    Alipoulizwa kuhusu tafiti za maoni ya wapiga kura zinazomweka nyuma katika kinyang’anyiro cha kupata tiketi ya chama cha Democrat, hata nyuma ya mwigizaji wa Hollywood, Dwayne ‘The Rock’ Johnson, Harris alisema hajawahi kuamini kura za maoni. “Kama ningesikiliza kura za maoni, nisingewahi kugombea ofisi yangu ya kwanza, wala ya pili na hakika nisingekuwa nimekaa hapa leo.”

  9. Trump ashuhudia utiaji saini makubaliano ya amani kati ya Cambodia na Thailand

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesimamia rasmi utiaji saini wa makubaliano ya amani kati ya Thailand na Cambodia, yaliyofanyika leo, yakihitimisha mzozo wa mpaka uliosababisha mapigano makubwa mwezi Julai.

    Waziri Mkuu wa Thailand Anutin Charnvirakul na Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Manet wameweka sahihi kwenye makubaliano hayo ya pamoja mbele ya Rais Trump, ambaye alihusishwa moja kwa moja katika mazungumzo hayo ya upatanishi.

    Akizungumza mara baada ya tukio hilo, Trump alisema kulikuwa na “simu nyingi sana kati yetu wanne” kufuatia “umwagaji damu” uliotokea kati ya Thailand na Cambodia mapema mwaka huu. Aliongeza kwa maneno yake, “tulifanikiwa kuyasitisha mapigano hayo.”

    Mzozo huo ulianzia mwezi Julai katika eneo la mpakani, ambapo vikosi vya nchi hizo mbili vilirushiana risasi na mabomu karibu na eneo la Chong An Ma upande wa Thailand na An Seh upande wa Cambodia. Hali hiyo ilisababisha vifo na uharibifu, na kuibua wasiwasi wa kimataifa.

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kupitia makubaliano haya, pande zote zimekubaliana kusitisha uhasama, kuanzisha kamati ya pamoja ya mpaka, na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na usalama. Trump ameyataja makubaliano hayo kama “ushindi mkubwa wa diplomasia na amani.”

    Waziri Mkuu Hun Manet amepongeza juhudi za Marekani, akisema “makubaliano haya ni mwanzo mpya wa uhusiano wa kirafiki kati ya Cambodia na Thailand,” huku Waziri Mkuu Anutin akisema nchi yake “iko tayari kufungua ukurasa mpya wa amani na maendeleo ya pamoja.”