'Nilimwambia binti yangu kuwa simu ya baba imeharibika kwa hivyo hawezi kutupigia'

Wanida, her husband Anucha and their daughter as a baby

Chanzo cha picha, Wanida Maarsa

Maelezo ya picha, Wanida katika nyakati za furaha zaidi na mumewe Anucha wakati binti yao alipokuwa mdogo

Zaidi ya watu 240 wanashikiliwa mateka na Hamas katika Ukanda wa Gaza huku raia wa Thailand wakiaminika kuwa kundi kubwa la wageni .

Takriban raia 25,000 wa Thai walikuwa wakifanya kazi nchini Israeli wakati wa shambulio la Oktoba 7, wengi wao wakiwa katika sekta ya kilimo.

Bangkok imethibitisha kuwa wafanyikazi 24 wa Thailand walitekwa nyara, 34 waliuawa na 19 kujeruhiwa.

Hata hivyo, serikali ya Thailand haijathibitisha rasmi kwamba Anucha Angkaew, 28, ni mateka huko Gaza, ingawa mkewe aliona picha yake ya Hamas mtandaoni.

Anatoka sehemu maskini ya kaskazini-mashariki mwa Thailand na amekuwa akifanya kazi nchini Israel kwa miaka miwili.

"Maisha yetu yamekuwa bora tangu Art alipoenda Israel," mkewe Wanida Maarsa aliambia BBC kupitia simu, akimuita mume kwa jina lake la utani.

Anasema aliweza kutuma $1,400 (£1,130) nyumbani kila mwezi na alikuwa amelipa deni lilihusiana na gharama zake za kusafiri .

"Nilikuwa na wasiwasi mwanzoni lakini wafanyakazi wengi ambao wamekuwa wakifanya kazi katika shamba moja kwa miaka mingi walisema kwamba hakuna mfanyakazi wa Thailand aliyefariki kutokana na mashambulizi," anaongeza.

Anucha Angkaew

Chanzo cha picha, Wanida Maarsa

Maelezo ya picha, Anucha alikuwa akituma nyumbani $1,400 kwa mwezi kutoka Israel hadi alipotekwa nyara
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Haya yote yalibadilika tarehe 7 Oktoba na sasa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu kutekwa nyara kwake.

Wanida hajasema lolote kwa binti yao mwenye umri wa miaka saba.

"Anaendelea kuuliza lini baba atatupigia simu, nilimwambia kuwa simu ya baba imeharibika hivyo hawezi kutupigia," anasema Wanida.

Mara ya mwisho alizungumza na mumewe jioni ya tarehe 6 Oktoba. Alikuwa amechoka baada ya wiki ndefu kwenye shamba la parachichi. Kisha akamtumia ujumbe siku ya Jumamosi.

"Hakusoma ujumbe huo wala kunipigia simu kama kawaida. Niligundua kilichompata asubuhi nilipoona picha yake kwenye mitandao ya kijamii," anasema.

Mfanyakazi mwenzake amemwambia Wanida kwamba Anucha alimtumia ujumbe na kumwambia ajifiche kwenye chumba cha wageni kulala mashambulizi yakiendelea.

Katika mazungumzo yao ya mwisho, Wanida alituma picha za binti yao kwa mumewe. Sasa binti yake anatumia simu ya mkononi ya Wanida kuchukua klipu za video zake na kujaribu kumtumia baba yake.

'Sitamwambia chochote. Nataka kusubiri hadi nijue kwamba atarudi au la."

Ron Sherman (left) and father Alex Sherman (centre)

Chanzo cha picha, Alex Sherman

Maelezo ya picha, Alex Sherman (katikati) anatumai mwanawe Ron (kushoto) anaweza kunusurika kama mateka huko Gaza na kurudi nyumbani

Familia ya Sherman ya uraia wa Israel na Argentina ilisikia shambulio la Hamas likitokea kwa wakati halisi.

Ron, mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka 19, alikuwa akihudumia muda wake katika jeshi kwenye kivuko cha mpaka cha Erez. Saa 0630 za ndani tarehe 7 Oktoba, Alex alijibu simu ya mtoto wake.

"Nasikia milio ya risasi, watu wakipiga mayowe kwa Kiarabu... nadhani kuna magaidi humu ndani," Alex anasema mwanawe alimwambia.

Kwa kuhofia sauti yake ingefichua alipokuwa , Ron kisha akaanza kuwatumia ujumbe wazazi wake kutoka kwenye makao ya kituo cha kijeshi alikokuwa amejificha.

Huu ndio ujumbe wa mwisho ambao Ron alituma: "Tayari wako mlangoni, huu ndio mwisho, nakupenda sana."

Ron ni mmoja wa Waajentina 15 wanaoshikiliwa mateka huko Gaza.

Ron Sherman

Chanzo cha picha, Alex Sherman

Maelezo ya picha, Ron Sherman ni shabiki mkubwa wa Lionel Messi

"Mwanangu alifanya kazi ya kawaida kwenye kivuko cha mpaka ambapo bidhaa huvushwa ," Alex Sherman, babake Ron, aliambia BBC.

"Hakuwa mpiganaji wa nyanjani kwa sababu alikuwa na pumu. Alikuwa na matatizo ya mapafu na alitumia kipulizi."

Baada ya ujumbe wa mwisho, wazazi wake walikuwa katika mshtuko.

"Tulitazamana tukiwa na huzuni. Mke wangu alidhani amekufa na nilitumai wamemchukua akiwa hai," anasema Alex kutoka nyumbani kwao Lehavim kusini mwa Israel.

Saa nne au tano baadaye, video iliibuka kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wanamgambo wa Hamas wakimteka nyara Ron.

“Kwetu sisi hiyo video ilikuwa zawadi kwa sababu tuliona mtoto wetu yuko hai na nadhani watamuweka hai ili wafanye mazungumzo,” anasema Alex.

"Kuna wakati ndani yake (video)unaona wale wavulana watatu waliotekwa nyara. Ron ndiye yuko katikati, hakuna shaka. Mwanangu alikuwa na sura ya hofu, sijawahi kumuona hivyo."

Alex Sherman anafikiri mashambulizi ya ardhini ya jeshi la Israel huko Gaza yanaweza kusaidia kumuokoa mwanawe.

"Hamas itajadiliana tu chini ya shinikizo kubwa," anasema.

Ingawa mwezi umepita na Hamas inasema baadhi ya mateka, ikiwa ni pamoja na raia wa kigeni, wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel, Alex ananing'inia katika hali hiyo ngumu.

"Natumai ananisikiliza na anajua kuwa tunafanya kila kitu kinachoweza kufanywa ili kumrudisha nyumbani," anasema Alex. "Siwezi hata kuingia chumbani kwake. Natamani nimkumbatie tena."

Joshua Loitu Mollel and Clemence Felix Mtenga

Chanzo cha picha, MASHAV Israel

Maelezo ya picha, Joshua Loitu Mollel na Clemence Felix Mtenga (kulia) kutoka Tanzania wanashikiliwa Gaza

Wanafunzi wawili kutoka Tanzania pia wanazuiliwa mateka huko Gaza. Clemence Felix Mtenga, 22, ni mmoja wao. Yeye ni mtaalamu wa kilimo na alikuwa akifanya kazi kwenye kibbutz karibu na mpaka wa Gaza.

"Familia ina wasiwasi sana kwa sababu yeye ni mdogo wetu na alikwenda Israel hivi majuzi," dadake Christina Mtenga hivi majuzi aliambia redio ya BBC Swahili.

"Ujumbe kwa Clemence ni kwamba anapaswa kuwa jasiri, ajue tunampenda na kumuombea usiku na mchana, tukitumai kuwa atarejea hivi karibuni."

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah