Al Hilal: Mabingwa wa Sudan wanaocheza kuwaondolea raia mawazo ya vita

Al Hilal walicheza mechi zao zote za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa nchini Tanzania

Chanzo cha picha, AL HILAL SPORTS CLUB

Takriban mwaka mmoja baada ya kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, klabu yenye mafanikio makubwa zaidi ya soka nchini humo, Al Hilal, inasema inaendelea kucheza ili kutoa " bughudha" kwa watu nchini Sudan.

Mzozo huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 14,000 na kuwalazimu milioni nane kuyakimbia makazi yao na Umoja wa Mataifa umeonya kuwa huenda ukasababisha mzozo mkubwa zaidi wa chakula duniani.

Michuano ya taifa ilikatizwa lakini mabingwa hao wa Sudan walipata mwanya wa kuendelea na shughuli zao uwanjani kwa kufikia makubaliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kucheza na timu zake kuanzia Agosti.

"Tunacheza wakati huu wa mzozo ili kundoka fikra za watu wetu kutoka kwenye vita," Dk Hassan Ali, katibu mkuu wa Al Hilal, aliiambia BBC Sport Africa.

“Wengi wa mashabiki wa soka nchini Sudan wakati mwingine hawana lolote hata katika nyakati za kawaida, walichonacho ni ushindi wa Al Hilal ambao unawafanya wawe na furaha na familia zao.

"Ni jukumu la kimaadili. Sio kucheza ili kushinda alama au vikombe. Hapana, tunacheza kwa ajili ya wafuasi wetu ili kuweka ari yao."

Klabu hii ya takribani karne moja, inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, ilituma maombi kwa mashirikisho mengine kadhaa barani kote na kupokea majibu chanya kutoka Uganda na Libya kabla ya kufanya makubaliano na Tanzania.

"Tulipendelea Tanzania kwa sababu mpira wa miguu huko ni wa maendeleo na wenye ushindani, na tungependa kujiandaa vyema kwa mashindano yajayo katika ngazi ya Afrika," aliongeza Dk Ali.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuifahamu Tanzania pia kulichangia, kwani Tanzania ndiyo iliyokuwa tegemeo la klabu hiyo wakati wa kampeni za Ligi ya Mabingwa msimu huu ambazo zilimalizika kwa kuondolewa katika hatua ya makundi.

Msemaji wa TFF , nchini Tanzania, Clifford Mario Ndimbo aliambia BBC kwamba vilabu vyote kwenye ligi vinaunga mkono kujumuishwa kwa Al Hilal, lakini mechi zao zitahesabiwa kuwa za kirafiki.

Kucheza nchini Tanzania kunaweza pia kuisaidia Al Hilal kuepuka kuhama kwa wachezaji wengi kabla ya ushiriki wao katika mashindano ya bara msimu ujao.

Klabu hiyo yenye maskani yake Omdurman kwa sasa ina takribani wachezaji kumi wa kigeni katika kikosi chake.

"Nadhani itawasaidia Al Hilal kuwabakisha wachezaji wao na Florent Ibenge, kocha ambaye anajulikana katika bara zima na ana jukumu kubwa katika kile wanachojaribu kufanya," mchambuzi wa soka wa Sudan Abdul Musa alisema. katika BBC Sport Africa.

"Wanahitaji aina fulani ya ushindani ambao wanaweza kuwa tayari kushindana katika ngazi ya bara. Ikiwa hutacheza ligi, ni vigumu."

Kuhamishwa kwa sababu ya vita

Uwanja wa Al Hilal, uliokuwa miongoni mwa viwanja bora zaidi nchini, sasa uko katika hali mbaya baada ya takriban mwaka mzima wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Chanzo cha picha, AL HILAL SPORTS CLUB

Uamuzi wa Al Hilal kuhamia ng'ambo ni hali ambayo Wasudani wengi wamekabiliana nao, na kulazimika kuyahama makazi yao tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Aprili mwaka jana.

"Vita daima huwa na athari mbaya," Dk Ali alisema.

"Tuko uhamishoni na wachezaji wanacheza katika hali ngumu sana, hali ya vita mbali na familia zao.

"Katika ngazi ya uongozi, hatuwezi kuonana ana kwa ana. Wajumbe wa bodi wametawanyika sehemu mbalimbali za dunia.

Lini soka ya kulipwa itarejea Sudan bado haijafahamika, huku makundi ya kijeshi yakiendelea kupigania udhibiti wa nchi.

Lakini hata kama vita vitakwisha sasa, Al Hilal haitaweza kutumia uwanja wake wa kisasa uliokarabatiwa mwaka wa 2018.

Klabu hiyo inasema itagharimu takribani pauni milioni 3.2 (dola milioni 4) kukarabati uharibifu wa uwanja wake wa Omdurman, uliopewa jina la utani la "Blue Jewel", ambao uliporwa.

"Kabla ya vita, tuliagiza vifaa vipya vya taa vya kisasa. Vifaa hivi vyote vilivyoagizwa kutoka Uhispania viliibwa," alilalamika Dkt Ali.

"Nyasi zinahitaji kukarabatiwa. Ofisi zetu, vitu hivyo vyote, viliharibiwa vibaya."

Mufilisi

Wapinzani wa Al Hilal na Omdurman Al Merreikh walikutana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika 2022.

Chanzo cha picha, Getty Images

Al Merreikh, klabu kongwe zaidi ya Sudan, pia inatafuta makao mapya.

Klabu hiyo imepokea majibu chanya kutoka kwa Tanzania, Libya, Uganda, Kenya na Ghana, lakini BBC Sport Africa inaelewa kuwa watatua Tanzania kama wapinzani wao Al Hilal.

Wakati vilabu viwili vikubwa nchini humo vikiwa na mbinu za kujinasua kutoka katika mzozo huo na kuendelea kucheza, klabu nyingi za soka za Sudan zimelazimika kuachana na wachezaji wao tangu michuano hiyo ilipomalizika.

"Takriban vilabu vingine 15 vimekoma kabisa kufanya kazi," Musa alisema.

"Hawana uwezo wa kuendelea kulipa mishahara yao. Bila mapato hali ni ngumu sana, hivyo wachezaji wengi sasa wako huru."

Matokeo yake, wachezaji wengi wanatafuta nafasi kwingine.

Kuhama, "suluhisho la pekee"

Wanajeshi wa Sudan

Chanzo cha picha, DANY ABI KHALIL / BBC

Ingawa mishahara Afrika Kaskazini ni ya chini kuliko ile ya wachezaji wa Sudan walio nyumbani, mshambuliaji huyo ana nia ya kuendelea kufanya kazi licha ya dhiki ya kisaikolojia anayohisi akijaribu kuangazia kazi yake huku usalama wa familia yake ukiwa hauna uhakika katika nchi yake.

"Mchezaji yeyote ambaye yuko Libya ataenda kwenye mazoezi au mechi na kumalizia siku yake kutazama habari kutoka Sudan," Mano aliiambia BBC Sport Africa.

“Wachezaji wanahitaji faraja ya kisaikolojia ili wawe wabunifu, kuna msaada lakini lazima tuwepo ili familia zetu zile.

"Hatupati mapato sawa na yale ya Sudan, lakini ndiyo suluhu pekee. Tuna fursa ya kujiuza na kurudi kwenye soka kama tulivyokuwa Sudan."

Kwa sasa, Wasudani wanajaribu kujinusuru na vita.

Wakati bunduki zitakimya, Musa anaamini kwamba urejesho wa soka ya kitaifa utachukua muda.

"Vita viliturudisha nyuma kwa muda mrefu," alisema.

“Wachezaji wengi wameondoka, hivyo timu zitalazimika kusajili tena ili kuweza kushindana.

"Kazi nyingi itahitajika, lakini jambo kuu ni kukomesha vita."