Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Pakistan iko 'vitani' na Afghanistan - Waziri wa ulinzi
Mashambulizi hayo yalitokea baada ya Taliban wa Afghanistan kutangaza shambulio kubwa dhidi ya vituo vya kijeshi vya Pakistan karibu na mpaka Alhamisi usiku.
Muhtasari
- Aliyekuwa mwanadiplomasia wa Marekani ahukumiwa kifungo cha maisha kwa unyanyasaji Burkina Faso
- Pakistan iko 'vitani' na Afghanistan - Waziri wa ulinzi
- Bill Clinton kutoa ushahidi kwa Bunge kuhusu Epstein
- Waghana takriban 55 wameuawa katika vita vya Urusi na Ukraine, Waziri amesema
- Mlipuko katika mgahawa Kazakhstan waua watu saba
- Pakistan yazuia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika miji muhimu - Waziri wa Habari
- Wairan wengi wanakabiliwa na adhabu ya kifo kwa maandamano - Mkuu wa haki za binadamu wa UN
- Afghanistan na Pakistan lazima zifuate sheria za kimataifa - UN
- Iran yajitolea kupatanisha Pakistan na Afghanistan
- China yataka Pakistan na Afghanistan kumaliza mzozo kupitia mazungumzo
- Taliban wa Afghanistan wadai kuwaua askari 50 wa Pakistan
- Africa CDC yaonya kuhusu usalama wa takwimu katika mikataba ya afya kati ya Afrika na Marekani
- Epstein alijaribu kununua jumba la kifahari huko Morocco siku chache kabla ya kukamatwa kwake 2019
- Ukraine: Zaidi ya waafrika 1,700 wanapigana kwa niaba ya Urusi
- China yawaondoa maafisa tisa wa kijeshi kabla ya mkutano muhimu wa kisiasa
- 'Tulidhani ni tetemeko la ardhi, kisha tukasikia mlipuko mkubwa' - mkazi wa Kabul
- Wizara ya sheria Marekani yashutumiwa kuficha faili za Epstein zinazohusiana na Trump
- Maafisa 10 wa FBI walioshiriki katika uchunguza dhidi ya Trump wafutwa kazi
- Raia wa Marekani ni miongoni mwa waliopigwa risasi na kuuawa katika boti Cuba
- Hillary Clinton asema hakujua kuhusu uhalifu wa Epstein
- Pakistan yaishambulia Afghanistan
- Mazungumzo kati ya Marekani na Iran yamalizika kwa maendeleo makubwa
Moja kwa moja
Rashid Abdallah & Asha Juma
Aliyekuwa mwanadiplomasia wa Marekani ahukumiwa kifungo cha maisha kwa unyanyasaji Burkina Faso
Raia mmoja wa Marekani amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwanyanyasa kingono wasichana wawili wa kike wakati akifanya kazi katika ubalozi wa Marekani nchini Burkina Faso.
Idara ya Sheria ya Marekani ilisema Fode Sitafa Mara mwenye umri wa miaka 41, kutoka Maryland, alihukumiwa siku ya Jumatano kufuatia kesi ya wiki mbili mnamo mwezi Oktoba 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya shirikisho ya jimbo hilo.
Baraza la mahakama lilimpata na hatia ya makosa manne ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto mdogo, pamoja na kujaribu kulazimisha na kumshawishi mtoto mdogo na kujaribu kuzuia haki kupatikana.
Mashtaka yaliwasilishwa kama sehemu ya Mradi wa ‘Safe Childhood,’ mpango wa kitaifa uliozinduliwa na Idara ya Sheria mwaka wa 2006 ili kupambana na unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Waendesha mashtaka walisema makosa hayo yalifanyika mwaka 2022 na 2023 huko Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso, ambapo Mara alikuwa ameajiriwa na ubalozi wa Marekani.
Kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, unyanyasaji huo ulitokea katika nyumba iliyokodishwa kwa wanadiplomasia huyo wa Marekani.
Kwa sababu jengo hilo lilitengwa kwa matumizi rasmi, iliangukia chini ya mamlaka ya Marekani, na hivyo kuruhusu mamlaka ya Marekani kushtaki kesi hiyo.
Ripoti zinasema waathiriwa hao wawili, ambao walikuwa na umri wa miaka 13 na 15 wakati unyanyasaji ulipoanza, na alitoka katika mazingira magumu. Waendesha mashtaka walisema Mara alitumia vibaya mazingira yao kwa muda wa takriban mwaka mmoja.A
"Uhalifu wake ulikuwa kitu kibaya. Ingawa hakuna hukumu ambayo ingeweza kuondoa madhara aliyosababisha, uamuzi wa leo unaonyesha kwamba wale wanaowanyanyasa watoto - ndani au nje ya nchi - watakabiliwa vilivyo na mfumo wa sheria Marekani," alisema Naibu Mwanasheria Mkuu A Tysen Duva.
Alitumia ugonjwa unaohatarisha maisha wa mama wa wasichana huyo kama fursa ya kudai ngono, akiwaambia hangeweza kuwasaidia bila kupokea kitu kama malipo, ilisema Ofisi ya Masuala ya Umma.
Mara alikuwa amewapa wasichana hao simu ili aweze kuwapigia wakati mkewe ameenda kazini, iliongeza.
Pia alihukumiwa kwa kutuma jumbe chafu za ngono kwa mmoja wa wasichana na kujaribu kumshawishi mfanyakazi wa ndani kuwapotosha wachunguzi.
Kesi hiyo ilichunguzwa na mamlaka ya Marekani kwa usaidizi kutoka Burkina Faso.
Pia unaweza kusoma:
Pakistan iko 'vitani' na Afghanistan - Waziri wa ulinzi
Waziri wa ulinzi wa Pakistan amesema nchi hiyo iko katika "vita vya wazi" na Afghanistan, baada ya kuanzisha mashambulizi ya anga huko Kabul kama sehemu ya wimbi la mashambulizi kote nchini humo.
"Uvumilivu wetu sasa umekwisha," alisema Khawaja Muhammad Asif kufuatia mashambulizi hayo.
Mashambulizi hayo yalitokea baada ya Taliban wa Afghanistan kutangaza shambulio kubwa dhidi ya vituo vya kijeshi vya Pakistan karibu na mpaka Alhamisi usiku.
Mashambulizi ya hivi karibuni yanafuatia miezi kadhaa ya mapigano kati ya mataifa hayo mawili jirani, licha ya kukubaliana kusitisha mapigano mpango ambao ulikuwa dhaifu mnamo mwezi Oktoba.
Mazungumzo ya mwaka jana yalishindwa kufikia makubaliano mapana kukomesha kabisa uhasama, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa kutochukulia mazungumzo hayo kwa uzito mkubwa.
Soma zaidi:
Bill Clinton kutoa ushahidi wa kibinafsi kwa Bunge kuhusu Epstein
Rais wa zamani Bill Clinton anatarajiwa kutoa Ushahidi siku ya Ijumaa faraghani, kwa jopo la bunge kuhusu uhusiano wake na marehemu Jeffrey Epstein, mhalifu wa kingono.
Ushahidi wa Clinton, uliopangwa kufanyika saa tano asubuhi ET (16:00 GMT), unafuata ule wa mkewe, Katibu wa zamani wa Mambo ya Nje Hillary Clinton, ambaye aliiambia Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Bunge la Wawakilishi siku ya Alhamisi kwamba hakumbuki kukutana na Epstein na hakuwa na chochote cha kushirikisha kuhusu sakata ya uhalifu wa kingono ya Epstein.
Bill Clinton alisafiri kwa ndege ya Epstein mara kadhaa mwanzoni mwa miaka ya 2000 baada ya kuondoka madarakani, na sehemu ya mamilioni ya nyaraka zilizotolewa na Idara ya Sheria zinajumuisha picha zake akiwa na wanawake ambao nyuso zao zimefutwa. Amekana kufanya makosa na ameelezea kujutia uhusiano wake na Epstein.
Mwenyekiti wa jopo la Republican, Mwakilishi James Comer wa Kentucky, anasema Bill Clinton na mkewe hawashutumiwi kwa makosa lakini lazima wajibu maswali kuhusu uhusiano wao na Epstein katika shirika lao la hisani.
Walikubali kutoa ushahidi karibu na makazi yao makuu ya Chappaqua, New York, baada ya Baraza la Bunge la Wawakilishi kutishia kuwachukulia hatua kwa kukataa kutoa ushirikiano. Baadhi ya Wademocrats waliunga mkono hatua hiyo.
Soma zaidi:
Waghana takriban 55 wameuawa katika vita vya Urusi na Ukraine, Waziri asema
Takriban Waghana 55 wameuawa wakipigana vitani nchini Ukraine, huku wengine wawili wakishikiliwa kama wafungwa wa kivita, waziri wa mambo ya nje wa Ghana amesema.
Katika safari yake kwenda Kyiv, Samuel Okudzeto Ablakwa alisema kwamba takriban Waghana 272 wanaaminika kushawishiwa kuingia katika mzozo huo tangu 2022, akirejelea mamlaka ya Ukraine.
Ablakwa alielezea takwimu hizo kama "zinazohuzunisha na kutisha," akisema Ghana "haiwezi kufumbia macho takwimu hizi za kuvunja moyo".
Hakusema ni upande gani ambao Waghana walikuwa wakipigana lakini waziri wa mambo ya nje wa Ukraine alisema Jumatano kwamba zaidi ya watu 1,700 kutoka nchi 36 barani Afrika wamesajiliwa kupigania Urusi.
Waghana 55 ndio idadi kubwa zaidi ya majeruhi kutoka nchi moja ya Afrika kuthibitishwa rasmi katika vita vya Ukraine na Urusi.
Vyombo vya habari vya ndani nchini Cameroon vimeripoti kwamba raia wake 94 wamekufa katika mzozo huo, lakini mamlaka hazijatoa maoni yoyote kuhusu takwimu hizi.
Waafrika Kusini wawili na takriban Mkenya mmoja wamefariki katika mzozo huo.
Ablakawa alisema takwimu za majeruhi "sio tu idadi, zinawakilisha maisha ya binadamu, matumaini ya familia nyingi za Ghana na taifa letu".
Alisema serikali ya Ghana imejitolea "kufuatilia na kusambaratisha mipango yote ya usafirishaji watu kwa njia haramu" pamoja na kuanzisha kampeni kali za uhamasishaji umma ili kuzuia vijana wa nchi hiyo kuingizwa kwenye mzozo huo.
"Hii si vita yetu na hatuwezi kuruhusu vijana wetu kuwa ngao za kibinadamu kwa wengine," aliongeza.
Siku ya Alhamisi, raia wa Kenya alishtakiwa kwa tuhuma za kuwashawishi vijana wa kiume kwenda Urusi na ajira za kazi, lakini wakaishia kupigana nchini Ukraine. Festus Arasa Omwamba alikana mashtaka hayo.
Jumla ya Wakenya 1,000 wamesajiliwa kupigania Urusi katika vita vyake vya miaka minne dhidi ya Ukraine, ilisema ripoti kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi ya Kenya (NIS), iliyotolewa wiki iliyopita.
Ubalozi wa Urusi nchini Kenya umekanusha madai kwamba ulihusika katika kuwasajili watu kupigana vitani.
Hata hivyo, ilisema kwamba sheria ya Urusi iliwaruhusu raia wa kigeni waliopo nchini humo kisheria kujiunga na jeshi kwa hiari.
Siku ya Jumatano, waziri wa mambo ya nje wa Ghana alimhimiza Rais Volodymyr Zelensky kuwaachilia huru wafungwa wawili wa kivita wa Ghana waliokamatwa wakipigania Urusi.
"Wao ni waathiriwa wa udanganyifu, taarifa za uongo, taarifa potofu, na mitandao ya biashara haramu ya wahalifu," alisema.
Aliishukuru Ukraine kwa kuhakikisha sheria za kimataifa zinaheshimiwa katika kuwashughulikia wafungwa.
"Tumepokea ripoti kwamba wako katika afya njema," alisema. "Hawajateswa. Hawajatendewa ukatili tangu walipokamatwa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiga alisema pande zote mbili zilijadili "kwa uwazi" kuhusu uwezekano wa kuwarudisha wafungwa hao Ghana.
Soma zaidi:
Pakistan yazuia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika miji muhimu - Waziri wa Habari
Waziri wa Habari wa Pakistani Atta Tarar ameandika kwenye Twitter kwamba Pakistan imezuia majaribio ya Taliban wa Afghanistan ya kurusha ndege ndogo zisizo na rubani kushambulia maeneo yao lengwa huko Abbottabad, Swabi na Nowshera.
"Mifumo ya Kupambana na Ndege Zisizo na Rubani imedondosha ndege zote zisizo na rubani. Hakuna aliyepoteza maisha," ujumbe wake wa Twitter uliongeza.
Abbottabad ni mji wa kijeshi wenye chuo cha kijeshi cha Jeshi la Pakistani.
Kauli ya Tarar inakuja baada ya msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Taliban, Zabihullah Mujahid, kudai kuwa ameanzisha "mashambulizi ya anga" kulenga kambi ya kijeshi karibu na Faizabad huko Islamabad, kambi ya kijeshi huko Nowshera, maeneo ya kijeshi huko Jamrud, na maeneo mengine huko Abbottabad.
Taarifa ya Taliban iliongeza kuwa "operesheni ya angani ilitekelezwa kwa mafanikio, ikilenga kambi muhimu za kijeshi za Pakistani, vituo vya kutoa amri, na vifaa vya kimkakati. Mashambulizi hayo yalifanywa kujibu mashambulizi ya angani yaliyofanywa jana usiku na vikosi vya Pakistani huko Kabul, Kandahar na Paktia.
Afghanistan yasema ilitumia ndege zisizo na rubani kushambulia Pakistan
Awali, Wizara ya ulinzi na msemaji wa serikali wa Afghanistan walisema kuwa "wamefanikiwa kufanya" mashambulizi ya angani kwa kutumia ndege zisizo na rubani kushambulia maeneo ya kijeshi nchini Pakistan.
Mashambulizi ya Pakistan katika majengo ya serikali yapitisha ujumbe mzito - Mtaalam
Wakati huohuo, mashambulizi ya Pakistan ya safari hii yamelenga vituo vya serikali vya Taliban badala ya maeneo ya kigaidi nchini Afghanistan, Michael Kugelman, mjumbe mwandamizi wa Asia Kusini katika Baraza la Atlantiki, aliambia kipindi cha Newsday cha BBC.
Hii ina maana kwamba "sasa inalenga utawala wenyewe", alisema.
Pakistan inadai kwamba Taliban wa Afghanistan wanawahifadhi magaidi ili kufanya mashambulizi dhidi ya Pakistan. Ingawa kumekuwa na hatua za kidiplomasia zilizochukuliwa ili kupunguza mvutano huo, hazijaleta suluhisho la kudumu.
Wakati huo huo kauli mbiu kutoka kwa Taliban zinaonyesha kuwa imejitolea "kufanya mashambulizi yasiyokoma" upande wa mpaka wa Pakistan, alisema, akiongeza kuwa hii ilikuwa "hatari" na inaweza kusababisha mzozo huo kutanuka.
Soma zaidi:
Katika Picha: Kadinali Pengo aagwa Dar es Salaam Tanzania
Waumini wa Kanisa Katoliki, jamaa na waombolezaji kwa jumla wanahudhuria misa ya kuuaga mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salaam Tanzania.
Marehemu Kardinali Pengo atazikwa huko Pugu Jumamosi Februari 28, 2026.
Melezo zaidi:
Mlipuko katika mgahawa Kazakhstan waua watu saba
Mlipuko na moto katika mgahawa umewaua watu wasiopungua saba na kuwajeruhi 19 katika mji wa kaskazini mwa Kazakhstan wa Shchuchinsk, mamlaka za mitaa zilisema siku ya Ijumaa.
Msichana wa miaka 16 alikuwa miongoni mwa waliofariki, huku wengine wapatao 13 wakiwa bado hospitalini, waliongeza katika chapisho kwenye Instagram, lakini hawakutoa maelezo zaidi.
Wairan wengi wanakabiliwa na adhabu ya kifo kwa maandamano - Mkuu wa haki za binadamu wa UN
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk siku ya Ijumaa ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa matumizi ya adhabu ya kifo nchini Iran, akionya kwamba watu wengi zaidi wako hatarini kunyongwa baada ya hukumu ya kwanza ya kifo inayohusishwa na maandamano makubwa ya Januari kutolewa wiki hii.
"Nimeshtushwa na ripoti kwamba takriban watu wanane, wakiwemo watoto wawili, wamehukumiwa kifo kutokana na maandamano hayo," Turk alisema katika hotuba yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, akiongeza kuwa watu wengine 30 walionekana kuwa katika hatari ya kuhukumiwa kifungo hicho.
Mahakama ya mapinduzi mjini Tehran ilitoa hukumu ya kifo kwa mwanamume mmoja wa Iran anayetuhumiwa kwa "uadui dhidi ya Mungu" ambayo ikithibitishwa itakuwa hukumu ya kwanza kama hiyo inayohusishwa na maandamano makubwa ya mwezi Januari, chanzo kilicho karibu na familia ya mwanamume huyo kilisema.
Makundi ya haki za binadamu yanasema maelfu ya watu waliuawa katika msako mkali dhidi ya maandamano hayo, machafuko mabaya zaidi ya ndani nchini Iran tangu enzi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979. Wakati wa machafuko hayo, Rais wa Marekani Donald Trump aliionya Tehran kwamba anaweza kuagiza hatua za kijeshi ikiwa itatekeleza mauaji.
"Nina wasiwasi sana kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa jeshi la kikanda na athari zake kwa raia, na natumai sauti ya mantiki itashinda," Turk alisema katika hotuba hiyo hiyo.
Oman ambayo ni mpatanishi ilisema mazungumzo mjini Geneva siku ya Alhamisi kati ya Marekani na Iran yalipiga hatua kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran, lakini hakukuwa na dalili yoyote ya mafanikio ambayo yangeweza kuzuia mashambulizi ya Marekani huku kukiwa na ongezeko kubwa la kijeshi.
Soma zaidi:
Afghanistan na Pakistan lazima zifuate sheria za kimataifa - UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, pamoja na Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, wameeleza msimamo wao kuhusu hali ya hivi karibuni ya mvutano na mapigano kati ya Pakistan na Afghanistan.
Guterres amezihimiza nchi hizo mbili kuzingatia kikamilifu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, hususan sheria za kimataifa za haki za binadamu.
Kwa upande wake, Volker Turk ametoa wito kwa Afghanistan na Pakistan kufanya mazungumzo ya pamoja ili kutatua matatizo yaliyotokana na mapigano ya mpakani na mashambulizi mabaya ya anga yaliyoleta vifo.
Inafaa kufahamika kuwa Pakistan imedai kwamba baada ya mashambulizi “yasiyochokozwa” kutoka kwa Taliban wa Afghanistan, ililenga vituo vya ulinzi vya Taliban katika miji ya Kabul, Paktia na Kandahar, na kuua wanachama 133 wa utawala wa Taliban wa Afghanistan pamoja na kuwajeruhi zaidi ya 200.
Hata hivyo, BBC haijaweza kuthibitisha madai hayo kwa njia huru.
Soma pia:
Iran yajitolea kupatanisha Pakistan na Afghanistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa Iran iko tayari kuwezesha mazungumzo kati ya Pakistan na Afghanistan.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X, alisema: “Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao ni mwezi wa kujizuia na kuimarisha mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu, inafaa Afghanistan na Pakistan kushughulikia na kutatua tofauti zao za sasa kwa kuzingatia ujirani mwema na kupitia mazungumzo.”
Alisema Iran iko tayari kutoa kila aina ya msaada ili kuwezesha mazungumzo kati ya nchi hizo mbili na kuimarisha uelewano pamoja na ushirikiano.
Iran tayari ilikuwa imewahi kujitolea kupatanisha nchi hizo mbili hapo awali wakati mvutano wa mpakani ulipokuwa unaongezeka.
Soma Zaidi:
China yataka Pakistan na Afghanistan kumaliza mzozo kupitia mazungumzo
China imezitaka Afghanistan na Pakistan kutatua mgogoro wao kwa njia ya mazungumzo, ikisema kumaliza uhasama ni kwa maslahi ya wananchi wa nchi zote mbili.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema inaeleza “wasiwasi mkubwa” kuhusu kuongezeka kwa mvutano katika mpaka wa Afghanistan na Pakistan, na kuzipa wito nchi hizo “kutatua tofauti na migogoro yao kupitia mazungumzo na majadiliano.”
Wizara hiyo iliongeza kuwa China “inafanya juhudi za upatanishi kwa kutumia rasilimali zake yenyewe katika mgogoro huo, na iko tayari kuchukua jukumu la kujenga katika kupunguza mvutano na kuboresha uhusiano wa pande mbili.”
“Kama jirani na rafiki, China ina wasiwasi mkubwa kuhusu mvutano huu na inasikitishwa na vifo vilivyotokea katika mzozo huu. Ongezeko lolote la hali ya taharuki litaleta madhara na hasara kwa pande zote,” alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa kumaliza mapigano ni “kwa maslahi ya msingi ya nchi zote mbili na wananchi wake, na kutasaidia kudumisha amani na utulivu katika eneo hilo.”
Soma Zaidi:
Taliban wa Afghanistan wadai kuwaua askari 50 wa Pakistan
Mamlaka ya Taliban nchini Afghanistan imesema kuwa imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya vituo vya mpaka vya Pakistan mashariki na kusini-mashariki mwa nchi hiyo.
Msemaji wa serikali ya Taliban, Zabiullah Mujahid, aliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kwamba vikosi vya Afghanistan viliharibu vituo 19 vya mpaka vya Pakistan na kuwakamata wanajeshi kadhaa wa Pakistan.
Aidha, alidai kuwa zaidi ya wanajeshi 50 wa Pakistan waliuawa.
Hata hivyo, hakuna uthibitisho huru uliotolewa kuthibitisha takwimu hizo.
Kwa upande wake, Pakistan imedai kuwa imeharibu vituo 27 vya mpaka vinavyomilikiwa na Taliban wa Afghanistan, na kusema kuwa imewasababishia hasara kubwa wanamgambo wa Taliban.
Pia unaweza kusoma:
Africa CDC yaonya kuhusu usalama wa takwimu katika mikataba ya afya kati ya Afrika na Marekani
Kuna masuala makubwa katika makubaliano ambayo Marekani inafanya na nchi za Afrika kuhusu namna ufadhili wake wa kimataifa wa afya utakavyotekelezwa kuanzia sasa, amesema Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) Alhamisi.
“Kuna wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi ya takwimu na kuhusu ushirikishwaji wa vimelea vya magonjwa,” alisema Mkurugenzi Mkuu Jean Kaseya katika mkutano na wanahabari uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Jumatano, Zimbabwe ilijiondoa katika mazungumzo na Marekani kuhusu makubaliano yenye thamani ya dola milioni 367 kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ikieleza wasiwasi kuhusu usalama wa taarifa nyeti na kudai kuwa makubaliano hayo hayakuwa ya usawa. Serikali ya Zambia nayo ilisema imepinga kipengele fulani katika makubaliano yake.
Makubaliano hayo ni sehemu ya mfululizo wa mikataba ya nchi mbili inayobadili namna utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unavyotoa mabilioni ya dola za ufadhili wa afya duniani. Hatua hizo zinafuatia kuvunjwa kwa shirika la misaada la Marekani mwaka jana, kupunguzwa kwa ufadhili na mikataba duniani kote, pamoja na ahadi ya kuweka “Marekani Kwanza” katika mkakati wake wa afya ya kimataifa.
Hata hivyo, Kaseya alisema taasisi hiyo imekuwa ikiunga mkono nchi wanachama pale zinapoomba msaada, na itaendelea kutoa ushauri iwapo zitahitaji kujadiliana upya na Marekani, pamoja na kuzisaidia kutekeleza makubaliano yoyote zitakayokubaliana nayo.
“Niliambia nchi zangu zote, mnaungwa mkono kikamilifu na Africa CDC. Hata kama mnataka kutathmini upya mikataba na Marekani… mkihitaji Africa CDC iwepo, tutakuwepo,” alisema.
Kwa mujibu wa ubalozi wa Marekani, tayari nchi 16 za Afrika zimesaini mikataba kama hiyo yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 18.3.
Pia unaweza kusoma:
Epstein alijaribu kununua jumba la kifahari huko Morocco siku chache kabla ya kukamatwa kwake 2019
Jeffrey Epstein alijaribu kununua jumba la mamilioni ya dola huko Morocco siku moja kabla ya kukamatwa kwake mnamo 2019, kulingana na hati zilizotolewa na Idara ya Sheria ya Marekani mwezi uliopita.
Epstein alitaka kumiliki Bin Ennakhil tangu 2011, lakini mizozo na muuzaji kuhusu bei na mpangilio wa ununuzi iliendelea kwa miaka kadhaa.
Jumba la kifahari katika kitongoji cha kifahari cha Palmeraie cha Marrakech limefafanuliwa kuwa kazi bora ya usanifu, iliyojengwa na mafundi 1,300 na kuangazia nakshi na vinyago vya kupendeza.
Epstein alitia saini uhamisho wa kielektroniki wa $14.95m (£11m) tarehe 5 Julai 2019, siku moja kabla ya kukamatwa kwake, kufuatia makubaliano ya kununua kampuni ya kigeni iliyomiliki mali hiyo kwa €18m (£13.3m).
Kulingana na hati zilizotolewa, uhamisho huo ulikuwa shughuli kuu ya mwisho ya kifedha ya Epstein katika kipindi hicho kabla ya kukamatwa kwake na mamlaka ya Marekani kwa mashtaka ya biashara ya ngono aliporejea New York.
Siku tatu baada ya kukamatwa, mhasibu wa Epstein Richard Kahn alighairi uhamisho wa kielektroniki na ununuzi wa jumba hilo la kifahari haukukamilika .
Pia unaweza kusoma:
Ukraine: Zaidi ya waafrika 1,700 wanapigana kwa niaba ya Urusi
Zaidi ya Waafrika 1,700 wanapigana upande wa Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, alisema Jumatano, akiongeza kuwa Moscow inatumia udanganyifu kuwashawishi kujiunga na mapigano hayo.
Akizungumza pamoja na mwenzake wa Ghana, Sybiha alisema mazungumzo yanaendelea na serikali mbalimbali barani Afrika ili kuzuia raia wao kuhadaiwa katika mipango hiyo. Ghana itakuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka ujao.
“Tunaona wazi kuwa Urusi inajaribu kuwahadaa raia wa Afrika kuingia katika vita vya maangamizi,” Sybiha aliambia mkutano na wanahabari. “Kwa mujibu wa takwimu zetu, kwa sasa kuna zaidi ya raia 1,780 kutoka bara la Afrika wanaopigana katika jeshi la Urusi.”
Aliongeza kuwa wapiganaji hao wanatoka katika nchi 36 tofauti za Afrika.
Mamlaka za Urusi zimekanusha madai ya kuwaajiri kinyume cha sheria raia wa Afrika kujiunga na majeshi yake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, alisema wengi wa Waafrika wanaopigana kwa niaba ya Urusi ni waathiriwa waliotapeliwa, wakihadaiwa kupitia mtandao wa siri (dark web) kwa ahadi za ajira za kawaida.
“Hawana historia ya kiusalama. Hawana uzoefu wa kijeshi. Hawajapata mafunzo,” alisema Ablakwa. “Walishawishiwa na kudanganywa, kisha wakawekwa mstari wa mbele vitani.”
Ablakwa alionesha mshikamano wake na Ukraine na akatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili kumaliza vita hivyo, ambavyo vilitimiza miaka minne tangu kuanza kwake Jumanne. Alisema atamwomba Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, kuwaachilia huru raia wawili wa Ghana waliotekwa wakiwa wanapigana upande wa Urusi.
Aidha, Ablakwa alisema Ghana itahamasisha kampeni za uelimishaji wa umma kuhusu mitandao ya usafirishaji haramu wa watu inayowadanganya Waafrika kujiunga na majeshi ya Urusi, wakati wa uongozi wake katika Umoja wa Afrika.
Soma Pia:
China yawaondoa maafisa tisa wa kijeshi kabla ya mkutano muhimu wa kisiasa
China imewaondoa maafisa 19, wakiwemo tisa kutoka jeshini, kwenye orodha ya wabunge wake kabla ya mkutano wake mkubwa zaidi wa kila mwaka wa kisiasa wiki ijayo.
Uondoaji huo ulitangazwa na chombo kikuu cha kutunga sheria nchini humo, Kamati ya Kudumu ya Bunge la Wananchi (NPC).
Hakuna sababu rasmi ya kuondolewa kwao imetolewa, lakini inakuja wiki chache tu baada ya Rais Xi Jinping kumuondoa Zhang Youxia, jenerali wake wa ngazi ya juu na pia mmoja wa washirika wake wa karibu wa kijeshi, kutoka kwa jukumu lake.
Tangu aingie madarakani, Xi amezindua mawimbi ya misukumo ya kupinga ufisadi, akiita ufisadi "tishio kubwa" kwa Chama cha Kikomunisti.
Hatahivyo, wakosoaji wengine wanasema imekuwa ikitumika kama zana ya kuwasafisha wapinzani wa kisiasa Kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari vya serikali, walioondolewa ni pamoja na Li Qiaoming, kamanda wa Jeshi la Ukombozi la Wananchi (PLA) Ground Force na Shen Jinlong, kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la PLA.
Pia katika orodha hiyo walikuwemo maafisa wengine kadhaa wa kijeshi na maafisa kadhaa wa mkoa akiwemo Sun Shaochong, mkuu wa zamani wa chama katika eneo la Inner Mongolia.
Hatua hiyo inakuja wiki chache tu baada ya Zhang kuondolewa kwenye wadhifa wake, baada ya kushutumiwa kwa "ukiukaji mkubwa wa nidhamu na sheria"
Soma Zaidi:
Habari za hivi punde, 'Tulidhani ni tetemeko la ardhi, kisha tukasikia mlipuko mkubwa' - mkazi wa Kabul
Mkazi wa Dashti Barchi katika Wilaya ya 6 ya Kabul, ambayo iko karibu na eneo lililoripotiwa kulengwa na shambulio la anga la Pakistani la jana usiku, alisema kuwa nyumba yake ilitikisika sana kutokana na mlipuko uliosababishwa na mojawapo ya mashambulizi.
"Kwanza, tulifikiri kuwa ni tetemeko la ardhi, kwa sababu kulikuwa na tetemeko la ardhi huko Kabul siku chache zilizopita," alisema.
"Kisha tukasikia mlipuko mkubwa." Mkazi huyo, ambaye jina lake halijatajwa kwa sababu za usalama, aliongeza kuwa watu wa Dashti Barchi walikimbilia nje na kukesha usiku kucha.
"Hakuna mtu aliyelala baada ya hapo. Kila mtu aliogopa." Alisema kuwa ndege zilionekana zikiruka juu ya Kabul muda mfupi baada ya mlipuko huo.
"Tulipoona ndege zikiwa juu, tuligundua kuwa ni ndege za Pakistani." Eneo lililolengwa lilikuwa takriban kilomita 4 hadi 5 kutoka nyumbani kwake, alisema.
“Mke wangu na wazazi wangu waliogopa sana, sote tulikuwa macho usiku kucha.
Wizara ya sheria Marekani yashutumiwa kuficha faili za Epstein zinazohusiana na Trump
Afisa wa ngazi ya juu wa chama cha Democratic katika kamati ya bunge inayomchunguza Jeffrey Epstein ameishutumu wizara ya sheria ya Marekani kwa kuficha faili zenye madai ya unyanyasaji wa kingono kwa mtoto mdogo yaliyotolewa dhidi ya Rais Donald Trump.
Robert Garcia, ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi, amesema yeye binafsi aliziona hati zenye madai hayo ambazo hazijawekwa wazi.
Kujibu, wizara ya sheria imesema "HAKUNA kilichofutwa", ikiongeza kuwa hati zilizuiliwa ikiwa "zilikuwa nakala rudufu au sehemu ya uchunguzi unaoendelea."
Trump amekataa kufanya makosa yoyote kuhusiana na kesi ya Epstein
Wizara ya sheria pia imesema hapo awali kwamba baadhi ya faili hizo zina "madai yasiyo ya kweli na ya kutia chunvi dhidi ya Rais Trump".
Epstein, mhalifu wa ngono alikuwa rafiki wa Trump kwa miaka kadhaa. Baadaye walitofautiana - jambo ambalo lilitokea mwanzoni mwa miaka ya 2000, kulingana na Trump, miaka miwili kabla ya Epstein kukamatwa kwa mara ya kwanza.
Idara ya sheria imetoa mamilioni ya faili zinazoonyesha uchunguzi dhidi ya Epstein.
Baadhi ya faili zilitiwa wino, na maafisa wamekiri kwamba faili zingine hazikutolewa kabisa.
Garcia amesema faili alizoziona "zinaweka wazi" kwamba mwanamke mmoja "alitoa madai " dhidi ya Trump ambayo "hayajaonyeshwa" katika rekodi ambazo zimetolewa hadharani na wizara hiyo.
Siku ya Alhamisi, Garcia alisema yeye na wanachama wa chama chake watafanya kazi katika siku chache zijazo kudai faili zilizobaki ambazo hazijatolewa ili zitolewe, ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na madai ya mwanamke huyo dhidi ya Trump.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X, wizara hiyo imesema itapitia upya kujua kama kuna faili zozote zimefichwa isivyofaa.
Mwakilishi wa Republican wa Kentucky, James Comer, mwenyekiti wa Kamati ya Uangalizi ya Baraza la Wawakilishi, alisema Alhamisi wabunge bado wanachunguza shutuma kwamba idara ya sheria imeficha faili zinazomhusu Trump.
Maafisa 10 wa FBI walioshiriki katika uchunguza dhidi ya Trump wafutwa kazi
FBI imewafukuza kazi takriban maafisa 10, ambao wote walishiriki katika uchunguzi kuhusu jinsi Donald Trump alivyoshughulikia nyaraka za siri baada ya muhula wake wa kwanza.
Kusitishwa kwao kazi Jumatano, kumethibitishwa na CBS, na kulitangazwa muda mfupi baada ya mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, kuiambia Reuters kwamba maafisa hao wa shirikisho walimchunguza alipokuwa raia wakati wa uchunguzi wa hati hizo.
Patel hakutoa ushahidi wowote wa makosa yaliyofanywa na wafanyakazi wa FBI waliofukuzwa kazi.
Baada ya Trump kuondoka Ikulu ya White House mwaka 2021, Wakili Maalum Jack Smith aliongoza uchunguzi dhidi ya Trump ambaye sasa ni Rais. Kesi moja ililenga kujua ikiwa Trump alijaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020.
Nyingine ilihusisha hati za siri ambazo Trump alizipeleka katika makazi yake ya Mar-a-Lago huko Florida na juhudi zake za kuzuia Wizara ya Sheria ya Marekani kuzipata.
Wafanyakazi wa FBI waliofutwa kazi Jumatano wote walishiriki katika kesi juu ya hati za siri.
Trump na washirika wake wawili walishtakiwa mwaka 2023, kufuatia uchunguzi wa Smith kuhusu hati hizo.
2024, jaji wa shirikisho huko Florida alifuta kesi dhidi ya Trump, baada ya kugundua kuwa Smith aliteuliwa kinyume cha sheria.
Mwaka huu, mahakama ya rufaa ya shirikisho huko Georgia ilifuta kesi dhidi ya washtakiwa wawili wa mwisho kwa ombi la wizara ya sheria ya Trump.
Tangu Trump aliporejea Ikulu ya White House mwezi Januari, wizara ya sheria na FBI wamewafukuza kazi wafanyakazi walioshiriki katika uchunguzi dhidi yake.
Wizara ya sheria pia imefungua mashtaka dhidi ya mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey, ambaye Trump alimfukuza kazi wakati wa muhula wake wa kwanza mwaka 2017, na Mwanasheria Mkuu wa New York Letitia James, ambaye aliongoza kesi dhidi ya Trump.