Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Sisi sio tishio kwa usalama wa Marekani': Raia wa Afghanistan
- Author, Mallory Moench na Flora Drury
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ahmad amekuwa akijificha nchini Afghanistan kwa miaka kadhaa.
Mfanyakazi huyo wa zamani wa jeshi la Afghanistan anaishi kwa hofu ya kupatikana na Taliban, ambayo iliingia madarakani mwaka 2021 wakati vikosi vya Marekani vilipojiondoa katika taifa hilo la Asia ya Kati.
Kutokana na hilo, Ahmad hawezi kupata kazi wala huduma za matibabu na amekuwa akitegemea misaada kutoka kwa wahisani na marafiki walio nje ya nchi kujikimu kimaisha. Mwanawe wa kiume aliye na umri wa miaka 12, hawezi kuenda shule.
Wakinipata, Ahmad ''wataniangamiza'' anasema, akiashiria Taliban.
Matumaini yake yalikuwa mpango wa Marekani wa kuwapokea wakimbizi wanaokabiliwa na hali kama yake nchini Marekani, na alikuwa amesalia hatua ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kukamilisha mpango huo - kabla ya mchakato mzima wa uhamiaji kusitishwa na utawala wa Trump
Bado, alikuwa na matumaini. Lakini matumaini hayo yalididimia Alhamisi wiki iliyopita alipoamkia taarifa za Rais Marekani Donald kutoa agizo mpya ya kuwapiga marufuku watu walio na pasipoti za Afghanistan kuingia nchini humo, akitaja vitisho vya usalama wa taifa
"Mimi sio tishio kwa usalama wa Marekani," Ahmad aliiambia BBC.
BBC haitaji jina lake halisi ili kulinda usalama wake.
"Tulikuwa Marafiki wa Marekani," alisema.
Marufuku ya usafiri ya Trump iliyoanza kutekelezwa Jumatatu, inawazuia raia wa Afghanistan na mataifa mengine 11, zikiwemo saba kutoka barani Afrika kuingia Marekani. Nchi zingine saba pia zimewekewa vikwazo vya muda.
Kulingana na Marufuku hiyo, Afghanistan ilijumuishwa kwa sababu Taliban inachukuliwa na serikali ya Marekani na nchi hiyo haina "mamlaka kuu yenye uwezo au ushirikiano wa kutoa pasipoti au hati za kiraia", au "hatua zinazofaa za uchunguzi na ukaguzi". Pia inabainisha kiwango cha juu kiasi cha watu ambao wanaishi nchini humo licha ya muda wa viza zao kukamilika.
Utawala wa Trump, hata hivyo, hivi karibuni uliondoa hadhi ya muda ya ulinzi kwa zaidi ya Waafghani 9,000 wanaoishi Marekani, ikisema kuwa tathmini yake ilionyesha hali ya usalama na kiuchumi nchini Afghanistan imeimarika.
Lakini wale wanaoishi Afghanistan wanakabiliwa na msururu wa vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Taliban kulingana na tafsiri yake kali ya Sharia ya dini ya Kiislamu..
Zile zinawaathiri wanawake - ni pamoja na kufinika nywele kwa lazima kuvaa hijab), vikwazo vya usafiri na masomo kwa wasichana walio na umri wa zaidi ya miaka 12 - hatua ambayo ni "ubaguzi wa kijinsia", kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Taliban inasema inaheshimu haki za wanawake kulingana na Sharia na utamaduni wa Afghanistan.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2023 iligundua kuwa kulikuwa na visa vya kuaminika kwamba mamia ya maafisa wa zamani wa serikali na wanajeshi wameuawa tangu kundi hilo liliporejea madarakani mwaka 2021, licha ya msamaha wa jumla. Taliban imesema hapo awali Waafghanistan wote wanaweza "kuishi nchini bila hofu yoyote" - na wale walio nje ya nchi wanapaswa kurejea kusaidia kujenga upya nchi.
"Kuna msamaha wa jumla," Mohammad Suhail Shaheen, balozi wa Taliban nchini Qatar, aliiambia BBC mapema mwaka huu. "Usalama wa umeimarishwa kote nchini Afghanistan. Kila raia na anaweza kufika sehmu yoyote ya nchi bila vikwazo vyovyote au matatizo yoyote."
Marufuku ya Trumpinatoa msamaha kwa kundi maalum la wahamiaji - ikiwa ni pamoja na Waafghanistan ambao walifanya kazi moja kwa moja na jeshi la Marekani kabla ya Taliban kurejea madarakani mwaka 2021.
Lakini Ahmad, ambaye maombi yake ya kupata makazi mapya yaliungwa mkono na mwanachama wa zamani wa huduma ya Marekani, hastahili kupata Viza Maalum ya Wahamiaji (SIV) kwa sababu hakufanya kazi moja kwa moja Marekani.
Na sio yeye pekee anayejipata katika hali hiyo.
Takriban raia 200,000 wa Afghanistan wamepatiwa makazi mapya tangu jeshi la Marekani lilipojiondoa nchini humo, lakini bado kuna maelfu zaidi wanaosubiri hatima yao kuamuliwa.
Baadhi yao wamekimbilia nchi jirani ya Pakistan ili kusubiri uamuzi kufanywa kuhusu maombi yao.
Samira, ambaye alizungumza na BBC Idhaa ya Afghanistan, kwa sasa yuko Pakistan- ambayo imekuwa ikiwafukuza maelfu ya raia wa Afghanistan katika miezi ya hivi karibuni.
"Kurejea Afghanistan sio chaguo kwetu - itakuwa changamoto kubwa," alisema. "Watoto wetu tayari wamepoteza miaka ya elimu, na hatuna matumaini ya kurudi salama."
Zaidi ya familia 8,300 wa raia wa Marekani wako tayari kwa mahojiano nchini Afghanistan, huku wengine zaidi ya 11,400 wakisubiri kuunganishwa tena na familia zao, kulingana na data ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliyochapishwa na AfghanEvac.
Mojo, ambaye aliomba kutambuliwa kwa jina lake la utani, ni mmoja wa Waafghanistan 200,000 ambao tayari wamefika Marekani, kwa sababu alifanya kazi moja kwa moja na jeshi la Marekani. Sasa ni raia wa Marekani.
Dada yake, hata hivyo, bado yuko nchini Afghanistan ambako yeye na mumewe "wanaishi kisiri huku wakiwindwa kama wanyama," anasema. Wanabadilisha anwani na jiji wanaloishi kila baada ya miezi michache kwa usalama wao.
Walikamilisha ukaguzi wa matibabu kwa ajili ya kupata hifadhi nchini Marekani, lakini kama wale wengine waliozungumza na BBC, hatima yao haijulikani mchakato ulipositishwa mwezi Januari.
Agizo hili la hivi punde limemfanya Mojo, ambaye anaishi Houston, Texas, na jamaa zake wengine familia kupoteza "matumaini kabisa".
Marufuku hiyo pia inawaathiri Waafghanistan ambao wanajaribu kuingia Marekani kwa ajili ya kupata makazi mapya.
Zarifa Ghafari anasoma katika Chuo Kikuu cha Cornell katika jimbo la New York, lakini kwa sasa yuko Ujerumani kwa majira ya kiangazi na mtoto wake mdogo.
Alisema alianza harakati za kurejea Marekani siku ya Alhamisi ili kuendelea na masomo yake, kabla ya kuanza kwa marufuku ya kusafiri siku ya Jumatatu.
Kupigwa marufuku kumemweka chini ya "shinikizo kubwa" na kumfanya ajihisi "mdhaifu sana", mwanasiasa huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 30 aliambia BBC.
Kinachofanya hali kuwa mbaya zaidi, alisema, ni kwamba alilazimika kurudi Ujerumani kila baada ya miezi michache ili kudumisha hali yake ya ukaaji huko pia. Akielezea hali yake kama "hatari", alisema alikuwa na wasiwasi kuhusu jinsi angeweza kufanya safari zake za kawaida kwenda Ujerumani wakati marufuku ya kusafiri ilipoanza.
Shawn VanDiver, wa AfghanEvac, alisema marufuku hiyo ilivunja ahadi ya Marekani kwa Waafghanistan katika kipindi cha miaka 20 waliyokuwa nchini humo.
"Sera hii inawaadhibu watu waliotoroka Taliban, walihatarisha maisha yao kusaidia demokrasia, tayari wamehakikiwa, waliambiwa na serikali ya Marekani wasubiri," aliandika kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii X.
"Hawa sio tisho. Ni washirika wetu - na wanaachwa nyuma."