Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Afghanistan: Je, Taliban ni kundi la aina gani ?
Kundi la Taliban liliondolewa madarakani nchini Afghanistan na vikosi vilivyoongozwa na Marekani mwaka 2001 lakini taratibu kundi hilo likaanza kujiimarisha tangu wakati huo na sasa hivi limeiteka upya Afghanistan
Lakini je Taliban ni kina nani?
Taliban lina maanisha wanafunzi katika lugha ya Kipashto na lilianza kuchipuka mapema miaka ya 1990 kaskazini mwa Pakistan kufuatia kuondoka kwa wanajeshi wa Umoja wa Usovieti nchini Afghanistan.
Inaaminika kwamba vuguvugu la Pushtun kwanza lilianza kujitokeza katika mikutano ya kidini ambayo mara nyingi ilikuwa inasimamiwa kifedha na Saudi Arabia - ambalo lilikuwa linahubiri msimamo mkali wa Waislamu wa Sunni.
Ahadi iliyotolewa na Taliban - katika maeneo ya Pashtun zilikuwa ni pamoja na kuleta amani na usalama na kuanzisha sheria kali za Kiislamu maarufu kama Sharia watakapoingia madarakani.
Kuanzia kusini magharibi mwa Afghanistan, Taliban kwa haraka sana walianza kuwa na ushawishi.
Septemba 1995 walikalia eneo la Herat linalopakana na Iran na mwaka mmoja baadaye likateka mji mkuu wa Afghan, Kabul, na kutimua utawala wa Rais Burhanuddin Rabbani - mmoja wa waanzilishi wa Afghan mujahideen uliokuwa unapinga utawala wa Usovieti.
Kufikia mwaka 1998, Taliban ilikuwa inadhibiti karibu asilimia 90 ya nchi ya Afghanistan.
Raia wa Afghan waliokuwa na wasiwasi na utawala wa mujahideen na mapigano baada ya kuondoka kwa wanajeshi wa muungano wa Usovieti, walikaribisha utawala wa Taliban hasa kwasababu ya kufanikiwa kukabiliana na ufisadi, ukosefu wa sheria na kutengeneza barabara katika maeneo waliokuwa wanadhibiti kwa ajili ya maendeleo ya kibiashara.
Lakini pia Taliban ilianzisha na kuunga mkono adhabu zinazoendana na dini ya Kiislamu - kama vile hukumu ya mauaji hadharani kwa walioshitakiwa kwa mauaji au uzinifu na kukatwa mikono kwa waliopatikana na hatia ya kutekeleza wizi. Wanaume walitakiwa kukuza kidevu huku wanawake wakitakiwa kuvaa burka- vazi linalofunika uso.
Taliban walipiga marufuku televisheni, muziki na sinema na kukataza wasichana wenye umri wa miaka 10 na zaidi kwenda mashuleni. Walishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa tamaduni. Mfano mmoja ni mwaka 2001 pale Taliban walipoendelea na ubomozi wa masanamu maarufu ya Bamiyan katikati mwa Afghanistan, licha ya kusababisha hasira kimataifa.
Pakistan ilikataa mara kadhaa kwamba inashirikiana Taliban lakini kilichojitokeza ni kwamba raia wengi wa Afghan ambao awali walijiunga na vuguvugu hilo walikuwa wamepata mafunzo ya dini ya Kiislamu yaani walienda madrasa huko Pakistan.
Pia Pakistan ilikuwa moja ya nchi tatu pamoja na Saudi Arabia na Nchi ya Falme za Kiarabu (UAE) kutambua kundi la Taliban walipokuwa madarakani nchini Afghanistan. Pia ilikuwa ya mwisho kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na kundi hilo.
Wakati fulani, Taliban walitishia kukosesha Pakistan uthabiti katika maeneo waliokuwa wanayadhibiti ya kaskazini magharibi.
Moja ya shambulizi lililoshutumiwa vikai kimataifa ni lile lililotokea Oktoba 2012, pale walipompiga risasi msichana wa shule Malala Youzafzai alipokuwa anarejea nyumbani katika mji wa Mingora.
Na uvamizi mbaya zaidi wa kijeshi ukatokea miaka miwili baadaye kufuatia mauaji ya halaiki katika shule ya Peshawar na kupunguza ushawishi wa kundi hilo.
Na hadi kufikia sasa watu watatu mashuhuri wa Taliban huko Pakistan wameuliwa na Marekani kwa mashambulizi ya anga mwaka 2013 akiwemo kiongozi mkuu, Hakimullah Mehsud.