Aliyekuwa mwanadiplomasia wa Marekani ahukumiwa kifungo cha maisha kwa unyanyasaji Burkina Faso
Raia mmoja wa Marekani amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwanyanyasa kingono wasichana wawili wa kike wakati akifanya kazi katika ubalozi wa Marekani nchini Burkina Faso.
Idara ya Sheria ya Marekani ilisema Fode Sitafa Mara mwenye umri wa miaka 41, kutoka Maryland, alihukumiwa siku ya Jumatano kufuatia kesi ya wiki mbili mnamo mwezi Oktoba 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya shirikisho ya jimbo hilo.
Baraza la mahakama lilimpata na hatia ya makosa manne ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto mdogo, pamoja na kujaribu kulazimisha na kumshawishi mtoto mdogo na kujaribu kuzuia haki kupatikana.
Mashtaka yaliwasilishwa kama sehemu ya Mradi wa ‘Safe Childhood,’ mpango wa kitaifa uliozinduliwa na Idara ya Sheria mwaka wa 2006 ili kupambana na unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Waendesha mashtaka walisema makosa hayo yalifanyika mwaka 2022 na 2023 huko Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso, ambapo Mara alikuwa ameajiriwa na ubalozi wa Marekani.
Kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, unyanyasaji huo ulitokea katika nyumba iliyokodishwa kwa wanadiplomasia huyo wa Marekani.
Kwa sababu jengo hilo lilitengwa kwa matumizi rasmi, iliangukia chini ya mamlaka ya Marekani, na hivyo kuruhusu mamlaka ya Marekani kushtaki kesi hiyo.
Ripoti zinasema waathiriwa hao wawili, ambao walikuwa na umri wa miaka 13 na 15 wakati unyanyasaji ulipoanza, na alitoka katika mazingira magumu. Waendesha mashtaka walisema Mara alitumia vibaya mazingira yao kwa muda wa takriban mwaka mmoja.A
"Uhalifu wake ulikuwa kitu kibaya. Ingawa hakuna hukumu ambayo ingeweza kuondoa madhara aliyosababisha, uamuzi wa leo unaonyesha kwamba wale wanaowanyanyasa watoto - ndani au nje ya nchi - watakabiliwa vilivyo na mfumo wa sheria Marekani," alisema Naibu Mwanasheria Mkuu A Tysen Duva.
Alitumia ugonjwa unaohatarisha maisha wa mama wa wasichana huyo kama fursa ya kudai ngono, akiwaambia hangeweza kuwasaidia bila kupokea kitu kama malipo, ilisema Ofisi ya Masuala ya Umma.
Mara alikuwa amewapa wasichana hao simu ili aweze kuwapigia wakati mkewe ameenda kazini, iliongeza.
Pia alihukumiwa kwa kutuma jumbe chafu za ngono kwa mmoja wa wasichana na kujaribu kumshawishi mfanyakazi wa ndani kuwapotosha wachunguzi.
Kesi hiyo ilichunguzwa na mamlaka ya Marekani kwa usaidizi kutoka Burkina Faso.
Pia unaweza kusoma: