Hofu ya vifo vingi yaibuka tetemeko kubwa likizikumba Myanmar, China na Thailand

Myanmar imetangazwa hali ya hatari katika mikoa yake mikubwa ya Sagaing, Mandalay, Magway, Bago, Easter Shan state na Naypyidaw

Muhtasari

Moja kwa moja

Na lizzy Masinga & Dinah Gahamanyi & Mr.Seif

  1. Habari za hivi punde, Watui 144 wamefariki na 732 kujeruhiwa nchini Myanmar - kiongozi wa kijeshi

    Takriban watu 144 wamekufa na 732 kujeruhiwa kufikia sasa nchini Myanmar, kufuatia tetemeko la ardhi lililopiga katikati mwa nchi hiyo.

    Timu ya BBC Burma inasema takwimu hizi zinatoka kwa kiongozi wa kijeshi wa Myanmar Min Aung Hlaing, ambaye anasema takwimu hizo zinatarajiwa kuongezeka.

    Akifafanua idadi hiyo mpya, kiongozi huyo wa kijeshi anasema watu 96 wamekufa huko Nai Pyi Taw, 18 huko Saigaing na 30 huko Mandalay.

    Kuhusu waliojeruhiwa, 132 kati ya hawa wanatoka Nay Pyi Taw na 300 wanatoka Sagaing, na idadi bado inatathminiwa katika maeneo mengine - takwimu za kijeshi zinasema.

    Nchini Thailand, kama tulivyoripoti, watu watatu wamefariki kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa.

  2. Video: Tazama wakati jumba la kidini lilipoanguka kufuatia tetemeko la ardhi Myanmar

    Maelezo ya video, Moment pagoda collapses in Myanmar after earthquake

    Jengo linalotumika kwa masuala ya kidini nchini Myanmar maarufu pagoda laanguka kufuatia tetemeko la ardhi.

    Sehemu ya juu ya Shwe Sar Yan Pagoda ya Myanmar, kusini-mashariki mwa Mandalay, imeporomoka kufuatia tetemeko kubwa la ardhi.

    Walioshuhudia wanasikika wakipiga kelele huku sehemu ya jengo hilo ikianguka chini.

    Tetemeko hilo kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 lilikumba eneo la kati la Myanmar, huku Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani likibainisha kuwa kitovu hicho kilikuwa kilomita 16 kaskazini-magharibi mwa mji wa Sagaing.

  3. Tetemeko la ardhi Myanmar: Tunachojua kufikia sasa

    .

    Chanzo cha picha, BBC Burmese Service

    Tetemeko kubwa la ardhi limepiga katikati mwa Myanmar.Tetemeko hilo la ukubwa wa 7.7 lilisikika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Thailand na kusini-magharibi mwa Uchina.Mamia wanahofiwa kufariki, ingawa ni vigumu kupata habari sahihi.

    Tetemeko la ardhi lilipiga wapi?

    Kitovu cha tetemeko la ardhi kilikuwa kilomita 16 kaskazini-magharibi mwa mji wa Sagaing nchini Myanmar, katika kina cha kilomita 10 (maili 16), Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani (USGS) lilisema.Huu ni karibu na mji wa Mandalay, mji wa pili kwa ukubwa nchini Myanmar wenye wakazi wapatao milioni 1.5, na takriban kilomita 100 kaskazini mwa mji mkuu wa Nay Pyi Taw.

    Ni maeneo gani yaliathiriwa?

    Nchini Myanmar, kuna ripoti za barabara kuharibiwa katika mji mkuu pamoja na uharibifu wa majengo kote nchini.Mitetemeko mikali pia ilisikika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Thailand na kusini-magharibi mwa Uchina.

    Iilikuwa baya kiasi gani?

    Huenda ikachukua muda kabla ya takwimu rasmi za majeruhi kujulikana, lakini mjumbe wa timu ya uokoaji iliyoko Mandalay ameambia BBC kwamba idadi ya waliofariki huko "angalau ni mamia".

    Je, hili inalinganishwaje na matetemeko mengine makubwa ya ardhi?

    Tarehe 26 Disemba 2004, mojawapo ya matetemeko makubwa zaidi kuwahi kurekodiwa yalipiga pwani ya Indonesia, na kusababisha tsunami ambayo ilisomba jamii nzima karibu na Bahari ya Hindi.Tetemeko hilo la kipimo cha 9.1 liliua takriban watu 228,000.

  4. Putin apendekeza kuanzishwa kwa serikali inayoongozwa na Umoja wa Mataifa nchini Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Putin

    Vladimir Putin amependekeza kuwa Ukraine inapaswa kuwekwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Mataifa kwa muda ili kuchagua kile alichokiita serikali yenye uwezo zaidi.

    Ni jaribio la hivi punde la rais wa Urusi kupinga uhalali wa serikali ya Kyiv. Ukraine ilimshutumu Putin kwa kupendekeza mawazo "ya kichaa" ili kuchelewesha harakati zaidi kuelekea makubaliano ya amani - ambayo yanaungwa mkono na Rais wa Marekani Donald Trump.

    Ikulu ya White House ilisisitiza kuwa utawala wa Ukraine utaamuliwa na katiba na watu wake.

    Matamshi ya Putin yanakuja wakati Marekani ikitaka kusuluhisha usitishaji mapigano katika vita kamili na Ukraine, ambavyo sasa vimeendelea kwa mwaka wa nne.

    Siku ya Jumanne, Ikulu ya White House ilisema pande hizo mbili ziliweka makubaliano madogo katika Bahari Nyeusi.

    Lakini Urusi iliweka mbele orodha ya masharti ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vya nchi za Magharibi, na kusababisha wasiwasi kwamba Moscow ilikuwa inajaribu kuzuia hatua zozote za kusitisha mapigano.

    Akizungumza na wanamaji wa nyambizi inayotumia nguvu za nyuklia katika mji wa Murmansk kaskazini mwa Urusi, Putin alisema utawala wa muda chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa unaweza kujadiliwa "na Marekani, na nchi za Ulaya, na bila shaka na washirika wetu na marafiki".

    “Hii itakuwa ni kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa kidemokrasia, kuweka madarakani serikali yenye uwezo inayoaminika na wananchi na kisha kuanza mazungumzo ya makubaliano ya amani na kusaini hati halali,” aliongeza.

    Moscow inasema mamlaka ya sasa ya Ukraine sio halali kwani Rais Volodymyr Zelensky amesalia madarakani hadi mwisho wa muhula wake na kwa hivyo sio mshirika halali wa mazungumzo.

    Lakini Zelensky amesalia kwa sababu uchaguzi umesitishwa, kisheria .

    Itakuwa vigumu sana kufanya uchaguzi halali huku zaidi ya raia milioni tano wa Ukraine wakihama makazi yao ng'ambo huku mamia kwa maelfu wakiipigania nchi yao katika mstari wa mbele .

  5. Video: Tazama wakati jengo refu la ghorofa lilipoanguka Bankok

    Maelezo ya video, Tetemeko la ardhi la Myanmar: Wakati jumba refu la ghorofa lilipoanguka Bangkok

    Wafanyikazi wanahofiwa kukwama kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa kubwa linaloendelea kujengwa katika mji mkuu wa Thailand.

    Tetemeko lenye ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter lilipiga nchi jirani ya Myanmar siku ya Ijumaa katika kina cha kilomita 10, na kufuatiwa na mtetemeko mkubwa baadaye, kulingana na Utafiti wa Jiolojia ya Marekani.

    Wafanyakazi wanaweza kuonekana wakikimbia eneo la tukio katika kitongoji cha Chatuchak.

    Kwingineko jijini, umati wa watu ulikimbilia barabarani kwa hofu huku majengo yakiyumba na maji yakitiririka kutoka kwenye vidimbwi vya paa.

  6. Watu Milioni 28 wanakabiliwa na njaa nchini DRC - UN

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watu milioni ishirini na nane wanakabiliwa na njaa kali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni rekodi kwa nchi hiyo, inayochochewa na mzozo unaozidi kati ya serikali na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki, Umoja wa Mataifa ulisema Alhamisi.

    Mgogoro wa muda mrefu wa kibinadamu nchini Kongo umechochewa na mzozo huo, huku watu milioni 2.5 zaidi wakikabiliwa na njaa tangu kutokea kwa ghasia za hivi majuzi mwezi Disemba, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilisema katika taarifa ya pamoja.

    Kati ya milioni 28 nchini Kongo, milioni 3.9 wanakabiliwa na viwango vya juu vya dharura vya njaa. Nchi hiyo ina idadi ya watu zaidi ya milioni 100, hivyo robo ya wananchi wanakabiliwa na njaa Kubwa.

    Mapigano kati ya serikali na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda yameongezeka tangu kuanza kwa mwaka hadi kuwa mzozo mkubwa zaidi mashariki mwa Kongo katika miongo kadhaa na kusababisha maelfu ya yatu kuyahama makazi yao.

    "Hali ya sasa ni mbaya kwa idadi ya watu, kwani mavuno hamna, bei ya chakula inapanda, mamilioni ya watu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na wanazidi kuathirika," Athman Mravili, mwakilishi wa muda wa FAO nchini Kongo.

    Zaidi ya watu milioni 10 ya wale wanaokabiliwa na njaa kali wako mashariki mwa Kongo, ambayo imekumbwa na ukosefu wa usalama karibu mara kwa mara tangu vita vya baada ya mauaji ya kimbari ya 1994 yaliyosababisha vifo vya mamilioni ya watu na kusababisha makumi ya vikundi vya wanamgambo.

    Kwingineko nchini, mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya franc ya Kongo kumefanya iwe vigumu kwa wengi kupata chakula cha kutosha, ilisema taarifa hiyo.

  7. Hofu ya vifo vingi yaibuka Myanmar ikikumbwa na tetemeko kubwa

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tetemeko kubwa la ardhi la kipimo cha 7.7 limepiga katikati mwa Myanmar, Utafiti wa Jiolojia wa Marekani unasema.

    Tetemeko hilo limetokea kilomita 16 (maili 10) kaskazini-magharibi mwa jiji la Sagaing kwa kina cha kilomita 10, USGS inaongeza.

    Wafanyakazi 43 wa ujenzi hawajulikani walipo baada ya jengo la ghorofa kubwa ambalo halijakamilika kuporomoka mamia ya maili huko Bangkok.

    Kuna ripoti za barabara kuharibika katika mji mkuu wa Myanmar Naypyidaw, huku mitetemeko mikali ikisikika kwingineko nchini Thailand na kusini-magharibi mwa China.

    Myanmar imekuwa katika msukosuko wa kisiasa tangu jeshi la kijeshi kunyakua mamlaka katika mapinduzi ya 2021. Kupata habari imekuwa ngumu.

    Jeshi la kijeshi ambalo lilitawala Myanmar tangu mapinduzi ya mwaka 2021 limetangaza hali ya hatari katika mikoa ya Sagaing, Mandalay, Magway, Bago, Easter Shan state na Naypyidaw, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.

  8. Rais wa Zimbabwe anayekabiliwa na upinzani mkali amteua mkuu mpya wa jeshi

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Rais wa Zimbabwe anayekabiliwa na upinzani mkali amteua mkuu mpya wa jeshi

    Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amemteua mkuu mpya wa jeshi kabla ya maandamano yaliyopangwa siku ya Jumatatu, yaliyoitishwa na kundi la wapiganaji wa vita wanaotaka kumshinikiza rais kujiuzulu.

    Meja jenerali wa zamani, Emmanuel Matutu, anachukua nafasi hiyo mara moja.

    Rais Mnangagwa amekabiliwa na wito kutoka kwa wafuasi wake wa zamani kujiuzulu kutokana na usimamizi mbaya na ufisadi.

    Mapema wiki hii Mnangagwa alimstaafisha ghafla mkuu wake wa jeshi na kumteua kuwa waziri wa michezo na sanaa na utamaduni.

    Ingawa haijabainika ni kiasi gani cha uungaji mkono wa umma kwa maveterani hao kupitia maandamano yao yaliyopangwa, waziri wa usalama amewaonya Wazimbabwe dhidi ya kushiriki katika maandamano hayo.

    Polisi wametangaza marufuku ya siku nne kuzunguka mji mkuu kwa kubeba silaha au zana zozote zinazoweza kutumika kusababisha vurugu

  9. Watu sita wafariki baada ya manowari ya watalii kuzama katika Bahari ya Shamu

    h

    Chanzo cha picha, David McArthur MBE/Reuters

    Watalii sita wa Urusi wamefariki dunia baada ya manowari ya watalii kuzama katika Bahari ya shamu karibu na mji wa Hurghada nchini Misri.

    Watu wengine 39 waliokolewa baada ya meli hiyo, Sindbad kuzama mwendo wa saa 10:00 kwa saa za huko (08:00 GMT), maafisa wanasema. Tisa wanasemekana kujeruhiwa huku wanne wakiwa katika hali mbaya.

    Wawili kati ya waliofariki ni watoto, shirika la habari la Urusi la Tass linaripoti, likimnukuu afisa mmoja wa Urusi.

    Mamlaka bado inaendelea na uchunguzi na hadi sasa haijajulikana ni nini kilisababisha tukio hilo.

    Hili ni tukio la pili kuhusisha meli ya kitalii katika Bahari ya Shamu katika miezi ya hivi karibuni. Mnamo Novemba, mashua ilipinduka karibu na Marsa Allam, ambayo ilisababisha watu 11 kutoweka, ikidhaniwa wamekufa.

    Sindbad imekuwa ikifanya kazi kama manowari ya kitalii kwa miaka kadhaa.

    Sindbad Submarines, kampuni inayoendesha safari hizo, inasema vyombo vyake huchukua abiria katika safari ya kuchunguza miamba ya matumbawe karibu na ufuo wa Hurghada.

    Gavana wa Bahari ya Shamu, Amr Hanafy, alisema abiria 45 kwenye Sindbad wanatoka Urusi, India, Norway na Sweden. Wafanyakazi watano wa Misri pia walikuwa ndani ya chombo hicho.

    Bw. Hanafy alisema sita waliofariki wote walikuwa Warusi, lakini taarifa kamili za waathiriwa bado hazijatolewa.

    Uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea, lakini Chama cha Waendeshaji watalii wa Urusi kilinukuu kwenye chapisho la Telegram kwamba manowari hiyo iligonga mwamba na hatimaye kupoteza msukumo ikiwa kwenye kina cha mita 20 (futi 65).

  10. Wamiliki wa baa wakamatwa kwa kuwanyanyasa kingono wanawake 41 nchini Ubelgij

    Pombe

    Chanzo cha picha, PA Media

    Wasimamizi watatu wa baa nchini Ubelgiji ni miongoni mwa wanaume watano ambao wamekamatwa kuhusiana na uchunguzi wa vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kingono kwa makumi ya wanawake, polisi wa eneo hilo wamesema.

    Waendesha mashtaka walisema washukiwa hao walihusishwa na unywaji pombe wa waathiriwa wa kike 41 kuanzia Desemba 2021 hadi Desemba 2024.

    Washukiwa hao watatu waliendesha biashara katika mji wa kaskazini-magharibi wa Kortrijk ambapo vitendo vya kuweka vilevi kwenye vinywaji vilifanyika. Wachunguzi wanasema wanaamini walijadiliana kuhusu mashambulizi hayo.

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma ilisema kwa jumla wanaume watano walikamatwa Jumatano na Alhamisi.

    Wanaume wawili waliokamatwa walifika mbele ya hakimu siku ya Alhamisi, waendesha mashtaka walisema.

    Wanaume wengine wawili bado wanahojiwa na wapelelezi huku mtu wa tano akiachiliwa baada ya kuhojiwa.

    Wanaume hao wanashukiwa kwa ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na usimamizi haramu wa vitu vyenye madhara, ofisi ya mwendesha mashtaka ilisema.

    Maafisa wanaamini kuwa dawa zilichanganywa katika vinywaji vya wanawake hao, ikiwa ni pamoja na ketamine, dawa ya ganzi inayotumika kwa ajili ya kujiburudisha kwa sababu ya athari zake za hallucinogenic.

  11. Jeshi la Israel latangaza kuyazuia makombora mawili yaliyorushwa kutoka Yemen

    g

    Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

    Jeshi la Israel lilitangaza kuwa jeshi lake la anga lilizuia makombora mawili yaliyorushwa kutoka Yemen siku ya Alhamisi kabla ya kuingia kwenye anga ya Israel.

    Ving'ora vya mashambulizi ya anga vilisikika mjini Jerusalem, Tel Aviv na maeneo mengine ya Israel ya kati kufuatia kurushwa kwa roketi kutoka Yemen.

    Milipuko mikubwa ilisikika huko Yerusalemu baada ya ving'ora kulia.

    Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha vipande vya roketi vikianguka katika mji wa Adh Dhahiriya, karibu na Hebron, kusini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Shirika la utangazaji la Israel limeripoti kuwa mfumo wa ulinzi wa makombora wa Marekani wa THAAD ulishiriki katika kuzuia makombora yaliyorushwa kutoka Yemen kuelekea Israel.

    televisheni ya Israel, channel 12, iliripoti kuwa maagizo yalitolewa kwa ndege iliyopangwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion ili kugeuza safari yake kuelekea Larnaca, Cyprus, sanjari na kuzuiwa kwa kombora.

    Kwa upande wao, Wahouthi walisema walilenga uwanja wa ndege wa Ben Gurion na kambi ya kijeshi katikati mwa Israel kwa makombora mawili.

    Televisheni ya Al Masirah yenye uhusiano na Waouthi iliripoti kwamba makombora mawili yaliyotumika ni kombora la balistiki la "Dhu al-Fiqar" na kombora la "Palestine 2" la hypersonic.

    Kituo hicho kiliongeza kuwa Wahouthi pia walilenga meli za kivita za "maadui" katika Bahari Nyekundu, ikiwa ni pamoja na meli ya kubeba ndege za Marekani Truman.

    Waasi wa Kihouthi wanarusha makombora kuelekea Israel kutoka Yemen, kwa kile wanachodai ni "kuiunga mkono Gaza."

    Huku Israel ikirejelea operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza takriban siku 10 zilizopita, kasi ya kurusha roketi kutoka Yemen imeongezeka, huku jeshi la Israel ikiripotiwa kuzuia makombora sita katika kipindi cha wiki iliyopita.

    Unaweza pia kusoma:

  12. Watoto milioni moja wanaweza kufariki iwapo Marekani itapunguza ufadhili, shirika la misaada linaonya

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Muungano wa Gavi unasema kuwa watoto milioni 500 wanahitaji kuchanjwa kote duniani

    Shirika la afya duniani limeonya kuwa watoto milioni moja wanaweza kufa kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika iwapo Marekani itasitisha msaada wake wa kifedha.

    Dk Sania Nishtar - mkuu wa Gavi, muungano ambao hununua chanjo muhimu kwa nchi zinazoendelea - aliiambia BBC kuwa kupunguzwa kwa ufadhili wa Marekani kutakuwa na "athari mbaya kwa usalama wa afya duniani".

    Hii inafuatia ripoti katika gazeti la New York Times kwamba utawala wa Trump unaazimia kusitisha ufadhili kwa Gavi - Marekani ni wafadhili wa tatu kwa ukubwa wa muungano huo.

    Gavi haikuwa imepokea taarifa ya kusimamishwa kazi kutoka kwa Marekani lakini imekuwa "ikishirikiana na White House na Congress" kupata $300m (£230m) kwa shughuli zake mwaka wa 2025, na ufadhili wa muda mrefu, Dk Nishtar alisema.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Marekani ilibatilisha visa takriban 300 za wanafunzi wa kigeni -Marco Rubio asema

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema kuwa Marekani imefuta visa vya wanafunzi 300 wa kigeni kama sehemu ya juhudi za Rais Donald Trump za kuwabana waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina katika vyuo vikuu.

    "Labda zaidi ya 300 kwa wakati huu," alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ziara yake Guyana. "Tunafanya hivyo kila siku, kila ninapompata mmoja wa hawa vichaa."

    Rubio aliulizwa kuthibitisha ni visa ngapi za wanafunzi ambazo utawala ulikuwa umebatilisha katika hatua yake ya kukabiliana na matamshi katika vyuo vikuu yanayoonekana kuwa ni ya chuki dhidi ya Israel.

    Matamshi hayo yanafuatia maafisa wa uhamiaji kumzuilia mwanafunzi wa shahada ya udaktari wa Kituruki anayesoma Chuo Kikuu cha Tufts - kukamatwa ambako waziri huyo alikutetetea.

    Unaweza pia kusoma:

  14. Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ikiwa leo ni Ijumaa tarehe 28.03.2025 tukikuletea habari za kikanda na kimataifa