Chama tawala cha Msumbiji chashinda kwa kishindo katika uchaguzi uliozozaniwa

Chama tawala cha Msumbiji, Frelimo, kimeshinda uchaguzi uliogubikwa na mgawanyiko, ghasia, na hivyo kurefusha muda wa miaka 49 madarakani wa chama hicho katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, tume ya uchaguzi imetangaza.

Muhtasari

  • Chama tawala cha Msumbiji chashinda kwa kishindo katika uchaguzi uliozozaniwa
  • "Tumekuwa tukikutana kunywa bia kila Alhamisi kwa miaka 56"
  • Politico: Takriban nchi saba zinapinga kujiunga kwa Ukraine na muunngano wa NATO
  • DRC: Tshisekedi asema katiba ni 'dhaifu' inahitaji kufanyiwa marekebisho
  • Ndege zisizokuwa na rubani 40 kati ya 50 za Urusi zadunguliwa Ukraine - Jeshi la Anga la Ukraine
  • Viongozi wa Jumuiya ya Madola kuikaidi Uingereza kuhusu malipo ya utumwa
  • Tumbiri kumi na mbili wamekufa katika mbuga ya wanyama Hong Kong
  • IMF yaonya dunia kuepuka vita vya kibiashara duniani
  • Uturuki yashambulia maeneo ya PKK baada ya shambulio baya karibu na Ankara
  • Wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Ukraine watazidisha mzozo, Lukashenko aiambia BBC
  • Nyota wa Tarzan Ron Ely afariki dunia akiwa na umri wa miaka 86
  • Afisa wa Lebanon asema watu 19 wameuawa katika shambulio la Israeli dhidi ya nyumba ya familia moja
  • Wanajeshi wa IDF wanapaswa kukataa maagizo ambayo yanaweza kuwa uhalifu wa kivita, waziri wa zamani wa Israel
  • Takriban watu watano wauawa katika shambulizi dhidi ya kampuni ya usafiri wa anga Uturuki

Moja kwa moja

Na Asha Juma na Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya mubashara kwa leo tukutane tena hapo kesho majaaliwa.

  2. Chama tawala cha Msumbiji chashinda kwa kishindo katika uchaguzi uliozozaniwa

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Daniel Chapo atakuwa rais wa kwanza wa Msumbiji aliyezaliwa baada ya uhuru mwaka 1975

    Chama tawala cha Msumbiji, Frelimo, kimeshinda uchaguzi uliogubikwa na mgawanyiko , ghasia, na hivyo kurefusha muda wa miaka 49 madarakani wa chama hicho katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, tume ya uchaguzi imetangaza.

    Daniel Chapo, mgombea urais wa Frelimo ambaye hajulikani kwa kiasi fulani ambaye ameonekana kuwa wakala wa mabadiliko, atachukua nafasi ya Filipe Nyusi, ambaye amehudumu kwa mihula miwili.

    Akiwa na umri wa miaka 47, Chapo, ambaye alipata 71% ya kura, atakuwa rais wa kwanza kuzaliwa baada ya uhuru wa Msumbiji mwaka 1975. Mpinzani wake wa karibu, Venancio Mondlane alipata 20% ya kura.

    Uchaguzi huo umekumbwa na madai ya wizi wa kura na mauaji ya wafuasi wa upinzani, na hivyo kusababisha maandamano kote nchini humo.

    Rais wa Zombabwe Emerson Mnangagwa, ambaye pia amekumbwa na madai ya udanganyifu katika uchaguzi kwa miaka mingi, amempongeza Chapo kwa "ushindi wake mkubwa", hata kabla ya matokeo kutangazwa.

    Kundi la zamani la waasi la Renamo, ambalo hapo awali lilikuwa chama kikuu cha upinzani, lilishika nafasi ya tatu.

    Tume ya uchaguzi inasema asilimia 43 ya wapiga kura ambao ni zaidi ya milioni 17 walijisajiri kushiriki katika uchaguzi huo.

    Unaweza pia kusoma:

  3. Zaidi ya vijana 150 wa Kisomali waliokuwa katika magereza ya Libya warejeshwa Somalia

    g

    Chanzo cha picha, SNTV

    Zaidi ya vijana mia moja wa Kisomali wamekaribishwa leo katika uwanja wa ndege wa Adan Adde mjini Mogadishu baada ya kuachiliwa walioachiliwa kutoka kwenye magereza nchini Libya.

    Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Habari, Petroli, Usalama, Mkuu wa Jeshi la Polisi na muwakilishi wa Ofisi ya Rais ya JFS inayoshughulikia masuala ya Uhamiaji na Haki za watoto kwa pamoja waliwakaribisha vijana hao waliorejeshwa nchini.

    Jumla ya vijana 164 wamefungwa katika jela za nchi hiyo kwa muda walipokuwa wakijaribu kuvuka Libya kuelekea nchi za Ulaya.

    Vijana 109 kati ya yao walirejeshwa mjini Mogadishu, huku watu wengine 55 wakipelekwa katika Uwanja wa ndege wa Hargeisa.

    Serikali ya Somalia imefanya jitihada za kuwarudisha vijana hao walioteseka kwa muda mrefu katika magereza ya Libya. Walikuwa mikononi mwa vikundi vya waasi, na sasa wamefanikiwa kuwarudisha katika nchi yao ya asili, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya serikali ya Somalia.

    “Wallahi hatuwezi kuongelea matatizo tuliyopitia, utalia tukiongelea miaka 3 tuliyokuwa peke yetu, kwenye kambi nilipochukuliwa dola zangu elfu 15, tulikuwa tunapelekwa kwenye kambi nyingine. na huko walikuwa wanachukua elfu 8 kutoka kwetu, katika kambi nyingine tulikuwa tukiwalipa 5,000, kambi hizo ni za wakimbizi,” anasema Abdirisaaq mmoja wa vijana hao kwa hisia.

    Saeed Osman, mmoja wa vijana walioachiliwa kutoka Mogadishu leo, alizuiliwa nchini Libya kwa mwaka mmoja na nusu, na alikabiliwa na matatizo mengi kama alivyosema.

    Saeed aliwaonya vijana wa Kisomali dhidi ya uhamiaji, hasa kuhatarisha maisha yao nchini Libya, ambayo alisema ni "kuzimu".

  4. "Tumekuwa tukikutana kunywa bia kila Alhamisi kwa miaka 56"

    g
    Maelezo ya picha, Tangu 1968, marafiki karibu hawakukosa safari ya kila wiki ya kwenda kwenye baa

    Kundi la marafiki - Paul Gaines, Bill Munden, Ken King, Peter Thirwall, Brian Ayres na Dick Cotton - wamekusanyika karibu na meza wakiwa na glasi za pombe aina ya Stones na Guinness kwenye kona tulivu ya baa ya White Swan Alhamisi jioni. Haya yamekuwa maisha yao kwa zaidi ya miongo mitano.

    Hakuna hata mmoja wao anayeweza kuwaza kwenda mahali pengine popote - kwa sababu wamekuwa wakikusanyika pamoja kunywa bia kila siku ya Alhamisi kwa miaka 56 iliyopita.

    Wanaume hao, ambao sasa wana umri wa miaka themanini, wanasema ni mara chache sana hawakukutana, ni mara 24 tu hawakuweza kukutana tangu 1968 kunywa pamoja.

    "Kuna nyakati ambapo tumekuwa tukikutana kila Alhamisi kwa mwaka mmoja, miaka miwili au mitatu mfululizo," anaongeza Dick "Inavutia sana."

    g

    Chanzo cha picha, Bill Munden

    Maelezo ya picha, Katika miaka ya 1970 na 1980, utambazaji wa baa na wake ukawa jambo la kawaida

    Safari za kwenda kwenye baa hiyo zilianzishwa na wanafunzi wa wakati huo Ken na Paul, ambao walicheza gofu kwa muda wao wa ziada na kisha kwenda kuchukua lita moja ya bia.

    Tabia hii haraka ikageuka kuwa mila isiyoweza kuvunjika, na Ken anatania kwamba mtu yeyote anayethubutu kukosa kikao cha baa bila sababu lazima angejieleza kwa maandishi.

    Idadi ya kikundi ilibadilika kwa miaka - wakati mwingine marafiki, wenzake na majirani walijiunga nao.

    Unaweza pia kusoma:

  5. Politico: Takriban nchi saba zinapinga kujiunga kwa Ukraine na muungano wa NATO

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban nchi saba - Marekani, Ujerumani, Hungary, Slovakia, Ubelgiji, Slovenia na Uhispania - hazina haraka ya kuialika Ukraine katika muungano wa NATO, Gazeti la Politico laandika.

    Balozi wa Marekani katika Muungano wa NATO Julianne Smith alisema katika mahojiano na gazeti hilo kwamba muungano huo bado hauko tayari kuipatia uanachama Ukraine.

    Volodymyr Zelensky mwenyewe alisema kuwa Ujerumani ina wasiwasi juu ya utayari wa Kyiv kujiunga na NATO. Wakati huo huo, vyanzo vya Politico vinasisitiza kuwa Berlin na Washington hazijaondoa uwezekano kwamba Ukraine inaweza kuwa mwanachama wa muungano huo wakati fulani.

    Nchi nyingine mbili za NATO, Hungary na Slovakia, sasa zinatawaliwa na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia zikipinga maoni ya kuunga mkono utawala wa Kremlin.

    Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban mara kwa mara amezuia mipango ya Umoja wa Ulaya ya kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

    Hata hivyo, kama vyanzo vya Washington na NATO ambavyo havikutaka kufichuliwa kwa majina yao katika mazungumzo na Politico vinavyosema, nchi nyingine pia hazina uhakika juu ya utayari wa Ukraine kujiunga na muungano huo.

    "Nchi kama Ubelgiji, Slovenia, na Uhispania zinajificha nyuma ya Marekani na Ujerumani. Wana wasiwasi," gazeti hilo linanukuu chanzo hicho kikisema.

    Chanzo kingine kimeiambia Politico kwamba nchi "zinaiunga mkono [Ukraine kujiunga na NATO] kwa maneno tu , lakini mara tu itakapokuwa katika hali ya halisi ," wataanza kuzungumza hadharani zaidi dhidi ya wazo hilo.

    Uanachama wa NATO ni moja ya vipengele vikuu vya mpango wa ushindi wa Rais Zelensky, ambao aliuwasilisha wiki iliyopita.

    Vita vya Ukraine: soma zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  6. DRC: Tshisekedi asema katiba ni 'dhaifu' inahitaji kufanyiwa marekebisho

    g

    Chanzo cha picha, Présidence RDC/ X

    Tshisekedi alisema idadi ya mihula ya urais haitabadilishwa, lakini wapinzani wake wanasema ana nia ya kuwania muhula wa tatu.

    Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, anasema kuwa katiba ya nchi hiyo inapaswa kurekebishwa kwa sababu ina "udhaifu" fulani.

    Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Tshisekedi kuzungumza hadharani kuhusu suala hilo lenye utata, baada ya chama chake cha UDPS kuanzisha kampeni mwezi huu ya kurekebisha katiba.

    Katika hotuba yake kwa lugha ya Lingala, Rais Tshisekedi alisema kuwa katiba inapaswa kurekebishwa kulingana na "hali halisi ya Kongo".

    Tshisekedi alisema kuwa "hatua hii haitaathiri idadi ya mihula katika uchaguzi wa rais" lakini wapinzani wake wanasema kuwa ni njia ya kujaribu kufanya kampeni kwa ajili ya muhula wa tatu.

    Wanamtaka aachie madaraka wakati muhula wake wa pili alioapishwa Januari (1) mwaka huu utakapomalizika.

    Wakati wa ziara yake siku ya Jumatano katika mji wa Kisangani katika jimbo la Tshopo, kaskazini-mashariki mwa nchi, Tshisekedi alisema kuwa katiba inapaswa kurekebishwa.

    Miongoni mwa sababu alizozitoa, Tshisekedi alisema kulikuwa na ucheleweshaji wa kuanzisha taasisi baada ya uchaguzi wa hivi karibuni, na kwamba kuna udhaifu katika mamlaka ya wakuu wa mikoa.

    Unaweza pia kusoma:

  7. Ndege zisizokuwa na rubani 40 kati ya 50 za Urusi zadunguliwa Ukraine - Jeshi la Anga la Ukraine

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanajeshi wa Urusi wameshambulia Ukraine kwa kutumia ndege zisizo na rubani 50 usiku wa Alhamisi. Walifanikiwa kuzidungua droni 40 kati yake, kulingana na ripoti ya jeshi la anga la Ukraine.

    Ukraine inasema mikoa ya Odessa, Nikolaev, Dnepropetrovsk, Vinnytsia, Zhytomyr, Khmelnytsky, Cherkasy, Kirovograd, Kiev, Poltava na Chernihiv ndiyo iliyolengwa katika mashambuzi hayo.

    Makombora mawili zaidi ya anga yanayoongozwa yaliyorushwa ndani ya Ukraine, lakini hayakuweza kufikia malengo yake, vikosi vya jeshi la Ukraine vimesema.

    Vita vya Ukraine: soma zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  8. Viongozi wa Jumuiya ya Madola kuikaidi Uingereza kuhusu malipo ya utumwa

    h

    Chanzo cha picha, PA Media

    Waziri Mkuu Sir Keir Starmer alisema wiki hii kwamba anataka kujadili changamoto za sasa na viongozi wa Jumuiya ya Madola, hasa mabadiliko ya hali ya hewa, badala ya siku zilizopita.

    Wakuu wa serikali za Jumuiya ya Madola wanajiandaa kuikaidi Uingereza na kukubaliana kuhusu mipango ya kuchunguza haki ya malipo ya biashara ya utumwa iliyovuka Bahari ya Atlantiki, BBC imebaini.

    Ofisi ya waziri mkuu Downing Street inasisitiza kuwa suala hilo haliko katika ajenda ya mkutano wa kilele wa nchi 56 za Jumuiya ya Madola, ambao utaanza katika kisiwa cha Samoa katika kisiwa cha Pasifiki siku ya Ijumaa.

    Lakini vyanzo vya kidiplomasia vimesema maafisa walikuwa wakijadili makubaliano ya kufanya utafiti zaidi na kuanza "mazungumzo ya maana" kuhusu suala ambalo linaweza kuiacha Uingereza ikidaiwa mabilioni ya pauni za fidia.

    Haki ya urejeshaji wa utumwa inaweza kuja kwa njia nyingi, ikiwa ni pamoja na fidia ya fedha, msamaha wa deni, kuomba msamaha rasmi, programu za elimu, ujenzi wa makumbusho, msaada wa kiuchumi, na usaidizi wa afya ya umma.

    Uingereza haikutaka lugha yoyote katika tamko kuhusu haki ya upatanishi, lakini kwa sasa inabidi ikubali itajumuisha aya tatu kamili zinazoelezea msimamo wa Jumuiya ya Madola.

    Maafisa kutoka Caricom, chombo kinachowakilisha nchi za Carribean wametaka kupanua suala hili ili lijumuishe sio biashara ya watumwa tu katika Atlantiki bali pia Pasifiki.

    Tamko la rasimu linasema nchi nyingi wanachama "zinashiriki uzoefu wa kawaida wa kihistoria kuhusiana na biashara hii ya kuchukiza, na kunyang'anywa mali kwa watu wa asili".

  9. Tumbili kumi na wawili wafa katika mbuga ya wanyama Hong Kong

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tumbili wa kumi na wawili wamekufa katika mbuga ya wanyama ya Hong Kong, huku uchunguzi ukiendelea kubaini kama aliapata maambukizi ya bakteria ambayo yaliwaua tumbiri wengine 11 katika siku 10 zilizopita.

    Tumbili huyo alikuwa ametengwa tangu tarehe 13 Oktoba wakati vifo vinane vya kwanza vilikuwa tayari vimeripotiwa.

    Uchunguzi wa maiti umepata idadi kubwa ya bakteria wanaosababisha sepsis (hali mbaya ambayo mwili hujibu vibaya kwa maambukizi) ambao huenda walitoka kwenye udongo uliochafuliwa karibu na zuio la nyani, mamlaka ilisema.

    Wafanyikazi waliokuwa wakichimba udongo karibu na vizimba kuliaminika kuwa na udongo uliochafuliwa kupitia viatu vyao.

  10. IMF yaonya dunia kuepuka vita vya kibiashara

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Uchumi wa dunia unaweza kudorora kwa ukubwa wa uchumi wa pamoja wa Ufaransa na Ujerumani, ikiwa kutakuwa na vita vya kibiashara kati ya mataifa makubwa yenye uchumi mkubwa duniani, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeiambia BBC.

    Hili linawadia wakati wasiwasi ukiongezeka kabla ya uwezekano wa kuchaguliwa tena kwa Donald Trump.

    Trump anasema ana mpango wa kuanzisha ushuru wa jumla au ushuru wa hadi 20% kwa bidhaa zote zinazoingia Marekani, wakati Umoja wa Ulaya tayari unapanga kulipiza kisasi ikiwa Washington itaendelea na ushuru huo mpya.

    Wiki iliyopita, Trump alisema "ushuru ndilo neno zuri zaidi katika kamusi", na mawaziri wa fedha katika soko la kimataifa sasa wanaanza kulichukulia kwa uzito matarajio ya yeye kuanza kutekeleza mawazo hayo.

    Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF Gita Gopinath alisema Shirika hilo bado haliwezi kutathmini maelezo mahususi ya mipango ya biashara ya Trump, lakini linafikiria kwamba "ikiwa kuna utenganishaji na utumiaji wa kiwango kikubwa wa ushuru, unaweza kuishia na hasara kwa Pato la Taifa la karibu hadi 7%.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Uturuki yashambulia maeneo ya PKK baada ya shambulio baya karibu na Ankara

    .

    Chanzo cha picha, AP

    Serikali ya Uturuki imesema jeshi lake lilishambulia maeneo ya Iraq na Syria yenye uhusiano na kundi la wanamgambo wa Kikurdi PKK, baada ya kulilaumu kwa shambulizi karibu na Ankara na kuua takriban watu watano.

    Video mbalimbali za shambulio la mapema Jumatano zinaonyesha watu wasiopungua wawili wakifyatua risasi karibu na lango lakampuni ya safari za Angani ya Uturuki (TAI), ambayo iko umbali wa kilomita 40 nje ya mji mkuu.

    Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo, ambapo watu 22 walijeruhiwa.

    "Jumla ya malengo 32 ya magaidi yaliharibiwa" katika shambulio la kulipiza kisasi, wizara ya ulinzi ya Uturuki ilisema katika taarifa.

    Rais Recep Tayyip Erdogan alitaja shambulio hilo dhidi ya TAI kuwa "baya" kwenye chapisho kwenye X.

    Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya alisema kuwa washambuliaji wawili, mwanamke na mwanamume, "waliuawa", na kuongeza kuwa shambulio hilo lina uwezekano mkubwa kuwa limehusisha PKK.

    Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) kimepigwa marufuku kama shirika la kigaidi nchini Uturuki, Marekani na Uingereza, na kimekuwa kikipigana dhidi ya taifa la Uturuki tangu miaka ya 1980 kwa ajili ya haki zaidi kwa Wakurdi walio wachache nchini humo.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Ukraine watazidisha mzozo, Lukashenko aiambia BBC

    .

    Hakuna viongozi wengi duniani ambao wamekuwa madarakani kwa miaka 30.

    Alexander Lukashenko wa Belarus ameshutumiwa kwa kuiba uchaguzi, kukandamiza upinzani na kusambaratisha demokrasia.

    Uingereza, EU na Marekani hazimtambui kama rais halali wa Belarus.

    Kuna jambo lingine unapaswa kujua kumhusu: kama kuna kiongozi yeyote anayemfahamu Vladimir Putin kwa nje, ni Lukasjenko. Wanaume hao wawili wamefahamiana kwa miaka mingi na hukutana mara kwa mara.

    Alexander Lukashenko alikutana na BBC pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Brics wa nchi zinazoibukia kiuchumi. Anataka Belarus kuwa mwanachama.

    Nilimwomba atoe maoni yake kuhusu madai kwamba Korea Kaskazini ilituma wanajeshi kupigana pamoja na Urusi nchini Ukraine.

    "Upuuzi," Lukashenko alijibu. "Kwa jinsi ninavyomjua tabia yake Putin hawezi kamwe kujaribu kushawishi nchi nyingine kujihusisha na jeshi lake katika operesheni maalum ya Urusi nchini Ukraine."

    "Na ikiwa ripoti zimethibitishwa?" niliuliza.

    "Ingekuwa hatua kuelekea kuongezeka kwa mzozo ikiwa vikosi vya jeshi vya nchi yoyote, hata Belarusi, vingekuwa vitani," alijibu Alexander Lukashenko.

    Soma zaidi:

  13. Nyota wa Tarzan Ron Ely afariki dunia akiwa na umri wa miaka 86

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Muigizaji wa Marekani Ron Ely, anayejulikana sana kwa kuigiza nafasi ya Tarzan katika kipindi cha televisheni cha miaka ya 1960 chenye jina sawa na hilo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86.

    "Ulimwengu umepoteza mmoja wa wanaume wakuu ambao umewahi kuwafahamu - na nimempoteza baba yangu. " binti wa mwigizaji huyo, Kirsten Casale Ely, alisema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Instagram.

    Mwanzoni kabisa, kipindi cha Tarzan kilipeperushwa hewani na mtandao wa televisheni wa NBC kuanzia mwaka 1966 hadi 1968, ambapo mwigizaji huyo alivunjika mifupa kadhaa na kuripotiwa kushambuliwa na wanyama wakati akifanya shughuli zake.

    Baada ya kustaafu kuigiza mnamo 2001, Ely alikua mwandishi na kuchapisha riwaya.

    Ely alirejea kwa muda mfupi kuigiza filamu moja ya televisheni, Expecting Amish, mwaka wa 2014, ambapo aliigiza kama mzee wa Kiamishi.

    Katika miaka ya 1980, alionekana katika vipindi vingine vya runinga vikiwemo vya ucheshi vya cruise ship-based, The Love Boat, na vile vile Wonder Woman akiwa na nyota Lynda Carter.

    Alizaliwa huko Texas mnamo 1938, Ely aliendelea walioana na mchumba wake wa shule ya upili mnamo 1959, kabla ya kutalikiana miaka miwili baadaye.

    Alijulikana pia kwa kuandaa shindano la urembo la Miss America mapema miaka ya 1980, ambapo alikutana na mkewe Valerie na kujaaliwa watoto watatu.

    Ely alifariki nyumbani kwake huko Los Alamos huko Santa Barbara, California mnamo 29 Septemba.

  14. Afisa wa Lebanon asema watu 19 wameuawa katika shambulio la Israeli dhidi ya nyumba ya familia moja

    .

    Chanzo cha picha, Tefffahtacom/Facebook

    Takriban watu 19, wakiwemo wanawake sita na watoto watano, waliuawa katika shambulizi la Israel kwenye nyumba moja kusini mwa Lebanon siku ya Jumanne, afisa wa eneo hilo amesema.

    Suad Hammoud aliambia BBC kwamba waliofariki ni pamoja na mkuu wa shule wa zamani Ahmed Ezzedine na vizazi vitatu vya familia yake, ambao wote waliishi katika jengo la ghorofa tatu katika kijiji cha Teffahta.

    Imamu wa kijiji hicho, Sheikh Abdo Abo Rayya, aliuawa alipokuwa akitembea karibu na nyumba hiyo wakati wa shambulizi hilo pamoja na wapita njia wawili, aliongeza.

    Jeshi la Israel bado halijazungumzia tukio hilo, lakini mara kwa mara limesema linachukua hatua za kupunguza madhara kwa raia.

    Imefanya maelfu ya mashambulizi ya angani kote Lebanon katika muda wa wiki nne zilizopita, ikilenga kile ilichosema ni watendaji wa kundi la Hezbollah, miundombinu na silaha.

    Soma zaidi:

  15. Wanajeshi wa IDF wanapaswa kukataa maagizo ambayo yanaweza kuwa uhalifu wa kivita, waziri wa zamani wa usalama wa Israel aiambia BBC

    .

    Wanajeshi wa IDF wanapaswa kukataa maagizo ambayo yanaweza kuwa uhalifu wa kivita, waziri wa zamani wa usalama wa Israel aiambia BBC

    Akiwa mtu ambaye aliwahi kuwatumikia mawaziri wakuu wanne wa Israel na alikuwa naibu mkuu wa Baraza la Usalama la Taifa la nchi hiyo, uamuzi wa Eran Etzion uliaminiwa katika ngazi za juu zaidi za serikali.

    Mkosoaji wa muda mrefu wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, yeye pia ni mtu ambaye miaka yake ya utumishi wa umma ilimletea heshima kubwa.

    Lakini sasa Bw Etzion, mwanajeshi wa zamani, anaonya kwamba - Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) - linaweza kuwa linafanya uhalifu wa kivita kaskazini mwa Gaza.

    Na anapendekeza kwamba maafisa na wanajeshi wanapaswa kukataa amri zisizo halali.

    "Wanapaswa kukataa. Ikiwa mwanajeshi au afisa anatarajiwa kufanya jambo ambalo linaweza kushukiwa kuwa uhalifu wa kivita, lazima wakatae. Ndivyo ningefanya kama ningekuwa mimi. Hivyo ndivyo ninavyofikiri mwanajeshi yeyote wa Israel anafaa kufanya,” aliambia BBC.

    Tumeketi kwenye ushoroba wa nyumba yake huko Shoresh katikati mwa Israel.

    Jua limechomoza vizuri kabisa. Mtaa wenye utulivu ambapo baadhi ya wajenzi wanaboresha nyumba.

    Chini ya maili 40 barabarani ni kitongoji cha Gaza cha Jabalia.

    Wakati mimi na Bw Etzion tunazungumza, madaktari na wafanyakazi wa matibabu katika Hospitali ya Kiindonesia huko Jabalia wanapaza sauti wakituma ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa wakiomba msaada.

    Soma zaidi:

  16. Takriban watu watano wauawa katika shambulizi dhidi ya kampuni ya usafiri wa anga Uturuki

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Takriban watu watano wameuawa na wengine 22 kujeruhiwa katika shambulio lililotokea kwenye makao makuu ya kampuni ya usafiri wa anga karibu na mji mkuu wa Uturuki Ankara, mamlaka imethibitisha.

    Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya alisema kuwa washambuliaji wawili, mwanamke na mwanamume, "hawajaunga mkono upande wowote", na kuongeza kuwa shambulio hilo lina uwezekano mkubwa lilihusisha waasi wa Kikurdi wa PKK.

    Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.

    Wizara ya ulinzi ya Uturuki ilitangaza jana Jumatano kwamba mashambulizi ya anga yameanzishwa katika maeneo ya waasi wa Kikurdi kaskazini mwa Iraq na kaskazini mwa Syria.

    Video mbalimbali za shambulio la mapema Jumatano zinaonyesha watu wasiopungua wawili wakifyatua risasi karibu na kampuni ya usafiri wa anga ya Uturuki, ambayo iko umbali wa kilomita 40 nje ya mji mkuu.

    Makamu wa Rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz alisema wanne kati ya waathiriwa walikuwa wafanyikazi wa kituo hicho huku wa tano akiwa dereva wa teksi.

    Vyombo vya habari vya eneo hapo awali viliripoti kwamba washambuliaji walimuua dereva wa teksi kabla ya kuchukua gari lake kutekeleza shambulio hilo.

    Mlipuko huo ulifanyika wakati wa mabadiliko ya zamu, na wafanyikazi walilazimika kuelekezwa kwenye makazi, walisema.

    Yerlikaya pia alithibitisha kuwa wanajeshi saba wa kikosi maalum walikuwa miongoni mwa 22 waliojeruhiwa katika shambulio hilo.

    Kundi la PKK limepigwa marufuku kama shirika la kigaidi nchini Uturuki, Marekani na Uingereza, na limekuwa likipigana dhidi ya taifa la Uturuki tangu miaka ya 1980 kwa ajili ya kupata haki zaidi kwa Wakurdi walio wachache nchini humo.

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 24/10/2024