Biashara haramu ya mbao kwenda China inavyofadhili uasi Msumbiji

as

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano huko Cabo Delgado
    • Author, Angela Henshall
    • Nafasi, BBC

Usafirishaji wa mbao, unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 23 kwa mwaka, kutoka misitu ya kale ya Msumbiji hadi China unasaidia kufadhili waasi wa itikadi kali za Kiislamu pamoja na mtandao mkubwa wa uhalifu kaskazini mwa nchi hiyo.

Biashara hii haramu ya miti ya inahusishwa na wanamgambo wa Msumbiji wenye mafungamano na kundi la Islamic State katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado, kulingana na taarifa ambayo BBC imeipata kutoka Shirika la Uchunguzi wa Mazingira (EIA).

Miti migumu ya kitropiki inapendwa sana kutengenezea samani za kifahari nchini China. Misitu ya Msumbuji inalindwa chini ya mkataba wa kimataifa, ikimaanisha kuwa miti hiyo hukatwa kwa biashara ndogo tu ambayo haitishii uhai wa misitu.

Hata hivyo, uchunguzi wa siri wa miaka minne wa EIA katika nchi zote mbili umebaini kuwa kuna usimamizi mbovu wa makubaliano ya misitu, ukataji miti haramu na ufisadi miongoni mwa maafisa wa bandari na kufanya biashara hiyo kupanuka bila kudhibitiwa katika maeneo yanayokadhibitiwa na waasi.

Ufichuzi huo unakuja wakati kumezuka upya mapigano kaskazini mwa Msumbiji. Siku ya Ijumaa, waasi wasiopungua 100 walifanya shambulio kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitatu kwenye mji wa Macomia, ambalo hatimaye lilizimwa na jeshi.

"Eneo la shambulio hilo linathibitisha kwamba uasi umesogea kusini zaidi kutokana na kuongezeka kwa wanajeshi kaskazini mwa nchi hiyo. Pia waasi wamepata fedha za kutosha kuajiri katika jimbo jirani la Nampula kusini zaidi," kulingana na mchambuzi wa kutoka Msumbiji, Joe Hanlon.

Pia unaweza kusoma

Uchunguzi na Ripoti

we

Chanzo cha picha, Environmental Investigation Agency

Maelezo ya picha, Picha hii iliyotolewa na EIA inaonyesha magogo ambayo hayajachakatwa katika bandari ya Shaghai

Ripoti ya serikali ya Msumbiji iliyochapishwa mapema mwaka huu na kuonekana na BBC - Ripoti ya Kitaifa ya Tathmini kuhusu Fedha za Ugaidi - inasema waasi wa al-Shebab wamechukua fursa ya biashara haramu ya mbao "kuchochea na kufadhili ghasia."

Ripoti inasema ushiriki wa waasi hao katika "usafirishaji haramu wa mazao ya msituni, ikiwa ni pamoja na mbao, na rasilimali nyingine za msituni unachangia kiwango cha juu sana cha kukusanya fedha kwa kundi la waasi. Ilikadiria mapato yake kutokana na shughuli hizi yalifikia dola milioni 1.9 kwa mwezi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kutokana na changamoto ya kulifikia eneo la Cabo Delgado imekuwa vigumu kubaini ni kwa kiwango gani waasi hao wanajihusisha na biashara ya mbao, lakini zipo ripoti za makampuni kulipa ada ya ulinzi ya 10% kwa vikundi vya waasi ili yafanye ukataji haramu wa mbao katika maeneo ya misitu.

Misitu yenye miti ya thamani – ina makubaliano. Mtu yeyote anayetaka kukata katika maeneo haya lazima alipe ada kwa mamlaka. Utaratibu huu kwa kawaida hukupa leseni kutoka mamlaka.

Lakini vyanzo vya biashara ambavyo havikutaka kutajwa vinakadiria kuwa 30% ya mbao zilizokatwa huko Cabo Delgado huenda zimetoka katika misitu inayokaliwa na waasi.

Inaafikiriwa kuwa kuna maeneo kadhaa maarufu yenye misitu huko Cabo Delgado ambapo ukataji miti na uuzaji wa mbao hufanyika: Nairoto; Muidumbe, Mueda, na Napai, katika jimbo jirani la Nampula.

Wakati mamlaka ya China imefanya kuwa ni kinyume cha sheria kukata miti katika nchi yake, idadi kubwa ya mbao zinaendelea kuagizwa kutoka nje.

Mwaka jana Msumbiji ilikuwa muuzaji mkuu kwa bara la Afrika wa mbao za hongmu kwenda China, ikiuza zaidi ya tani 20,000 zenye thamani ya dola milioni 11.7, kulingana na Trade Data Monitor, kampuni ya kibiashara inayofuatilia biashara ya kimataifa.

Imeshinda nchi nyingine kama Senegal, Nigeria na Madagaska kwani aina za mbao za rosewood zimeisha, au sheria zinazopiga marufuku usafirishaji nje zimetekelezwa kwa usimamizi mkali zaidi.

Kama sehemu ya uchunguzi wake wa siri, EIA ilifuatilia shehena kubwa ya mbao kutoka Msumbiji. Kati ya Oktoba 2023 na Machi 2024, wachunguzi walifuatilia takriban kontena 300 za mbao kutoka bandari ya Beira hadi China.

Mbao ngumu za Pau preto ambazo zinapatikana kaskazini mwa Msumbiji na nchini Tanzania, zimeorodheshwa kama aina ya miti ambayo iko hatarini kwa mujibu wa Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN).

Makontena haya 300 yalikuwa yakisafirisha tani 10,000 za mbao. Trader inakadiria thamani ya kila kontena kuwa karibu dola 60,000, na kuweka thamani ya jumla ya usafirishaji kuwa karibu dola milioni 18.

Picha za siri za EIA zilizoonekana na BBC zinaonyesha shehena hii pia ilikuwa na mbao ambazo hazijasafishwa. Hii inavunja sheria ya Msumbiji yenyewe ya 2017 ya kutouza nje mbao zozote ambazo hazijachakatwa. Makontena hayo pia yalikuwa na mbao zilizochakatwa.

Myororo wa usafirishaji

n
Maelezo ya picha, Mbao husafirishwa maelfu ya maili hadi Shanghai

Kwa kawaida miti inapokatwa na huchukuliwa kusafishwa katika viwanda vya mbao karibu na Montepuez, mji mkubwa huko Cabo Delgado. Kisha huhamishwa kutoka viwanda vya Montepuez kwa malori hadi bandari za Pemba au Beira.

Katika bandari hizi mizigo inapaswa kukaguliwa na mamlaka ya Msumbiji na kupokea kibali au leseni ya kuuza nje. Lakini EIA inasema taarifa mara nyingi huripotiwa vibaya au haziwekwi kabisa katika makaratasi ya forodha.

Mbao zinazosafirishwa kati ya Msumbiji na China mara nyingi hubebwa na meli za makampuni ya Maersk na CMA-CGM, kulingana na uchunguzi wa EIA.

Msemaji kutoka Maersk alisema katika taarifa yake kwa BBC, "imejitolea kupambana na biashara haramu ya misituni na haitakubali ikiwa itajua biashara iliyo kinyume na mamlaka za Msumbuji au kinyume cha sheria. Tunaomba wateja wetu watangaze kwa usahihi mizigo yao na tunategemea mamlaka ya forodha kuthibitisha biashara hiyo na vyeti.”

Taarifa hiyo ilieleza, ni jambo la kawaida katika usafirishaji kwa wateja kupakia na kufunga makontena yao kabla ya kuyakabidhi kwa wasafirishaji.

Msemaji wa CMA-CGM alisema inasafirisha bidhaa za wateja kwa kufuata kanuni za ndani na kimataifa na "haihusiki na haina njia ya kudhibiti asili ya bidhaa ambazo zote husafirishwa kwenye makontena yaliyofungwa."

Msemaji huyo pia alisema kuwa "CMA-CGM haisafirishi mbao ambazo hazijachakatwa, na imeanzisha sheria inayokataza kusafirisha mbao ambazo hazijachakatwa kuondoka Msumbiji."

BBC yasaka majibu

xc

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Jeshi la Msumbiji limepata uungwaji mkono kutoka mataifa mengine ya Afrika ikiwemo Rwanda katika kupambana na waasi hao

BBC ilimuuliza mwakilishi wa Msumbiji, Cornelio Miguel, ambaye anafanya kazi katika Maeneo ya Hifadhi, ikiwa uchunguzi hufanyika kuhusu mbao za pau preto. Hakutoa maoni.

BBC iliwasiliana na baadhi ya makampuni ya biashara ya China yaliyotajwa katika ripoti ya EIA, lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa tayari kutoa maoni yake iwapo yanapokea mbao kutoka Msumbiji.

Shughuli za waasi katika jimbo hilo zimesababisha mzozo mkubwa zaidi barani Afrika, huku zaidi ya watu milioni moja wakilazimika kuyahama makazi yao.

Waasi hao huwalenga raia, kufanya mauaji, kukata vichwa, ubakaji na utekaji nyara. Nyumba na vijiji vimeshambuliwa kwa mabomu na kuchomwa moto.

Vurugu hizo zimevuruga sehemu kubwa ya Cabo Delgado kwa takriban muongo mmoja na kusababisha serikali kutegemea wanajeshi wa kigeni kapiga doria jimbo hilo.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi