Mzozo wa Msumbiji: Jeshi lasema limemkamata kiongozi wa kundi la jihadi raia wa Tanzania

Chanzo cha picha, AFP
Vikosi vya jeshi la Msumbiji vinasema kuwa vimemkamata kiongozi wa kijihadi, raia wa Tanzania, katika wilaya ya Nangade kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 39, anayejulikana kama Ali, alikamatwa pamoja na wanamgambo wengine wa Kiislamu sita wenye uhusiano na kundi la Islamic State, maafisa wa kijeshi wameeleza.
Amesema alikuwa mmoja wa viongozi wa wanamgambo ambao kazi yao ilikuwa kuajiri wapiganaji na kutekeleza mashambulizi ya moja kwa moja.
Kukamatwa kwake kunakuja huku kukiwa na hali mbaya ya usalama katika wilaya hiyo, na mfululizo wa mashambulizi ya wanajihadi katika siku za hivi karibuni.
Unaweza pia kusoma
Katika kipindi cha takribani wiki mbili, waasi hao wameshambulia vijiji saba vya Nangade, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.
Shambulio la hivi karibuni lilitokea katika kijiji cha Limualamuala siku ya Jumamosi na kusababisha vifo vya watu sita waliokuwa wakihudhuria sherehe za kufundwa.
Serikali ya Tanzania bado haijazungumza lolote kuhusu taarifa hizo.












