Zaidi ya vijana 100 watekwa nyara katika mashambulizi Msumbiji
Watu wenye silaha wamewateka nyara zaidi ya vijana 100 kutoka kijiji cha Naulala katika Mkoa wa Niassa kaskazini mwa Msumbiji, Shirika la Habari la Lusa limeripoti.
Moja kwa moja
DRC yageuza kauli kuhusu uwepo wa jeshi la Uganda nchini humo

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mashambumbulio ya ADF/IS yamekuwa ya mara kwa mara tangu Machi 2020 Jeshi la Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo limethibitisha kuwa linafanya operesheni ya pamoja na kikosi maalum cha Uganda dhidi ya kikundi cha waasi.
Kuthibitishwa kwa taarifa hii kunakuja siku moja tu baada ya Msemaji wa jeshi la Congo kukanusha uwepo wa vikosi vya Uganda katika nchi hiyo.
Kubadilika kwa msimamo wa DRC kumekosolewa na umma.
Msemaji wa DRC Patrick Muyaya alisema opresheni ziliafikiwa baada ya tathmini.
Jumanne Uganda ilisema kuwa inashiriki operesheni dhidi ya waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), ambao wana uhusiano na kikundi cha Islamic State. ADF kimekuwa kikilaumiwa kwa mashambulio ya kujitoa muhanga katika mji mkuu wa Uganda -Kampala yaliyowauwa watu wanne.Uganda ilisema kuwa ilifanya mashambulio ya anga kwenye ngome za ADF na jeshi la Congo lilisema operesheni ya pamoja inalenga kurejesha maeneo yanayoshikiliwa na waasi hao
ADF huendesha harakati zake katika nchi hizo mbili.
Unaweza pia kusoma:
- Rais wa Uganda Yoweri Museveni awataka waasi wa ADF kujisalimisha
- Namna ambavyo waasi wa Uganda walikuwa washirika wa IS nchini DRC
- ADF: Lifahamu kundi la waasi kutoka Uganda linaloshirikiana na Islamic State
Tamasha la Koffi Olomide kufanyika Rwanda, licha ya kilio cha wanaharakati

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Muimbaji Koffi Olomide akiwa katika tamasha lad'Anoumabo (Femua) mjini Abidjan, mu Septemba 2021 Kampuni iliyoandaa tamasha la muziki la mwanamuziki wa DRC Koffi Olomide mjini Kigali imesema kuwa haina muda wa kuzungumzia kuhusu mashitaka yanayomkabili mwanamuziki huyo, na badala yake inaahidi kuwa kutakuwa na onyesho’’tamu ‘’ Jumamosi ijayo.
Bado kuna watu wengi wanaoendelea kupinga tamasha la muziki la Koffi Olomide kufanyika mjini Kigali kufuatia kupatikana na hatia ya unyanyasaji dhidi ya wanawake .
Bruce Intore, mkuu wa kampuni iliyoandaa tamasha hilo- Intore Entertainment, amefafanua "suala hilo litatatuliwa na ngazi husika ikiwa ni pamoja na mahakama ".

Chanzo cha picha, Koffi Olomide
Bw Bruce Intore amesema "tunaheshimu mawazo na haki za watu wenye wenye maoni tofauti kumuhusu msanii huyu."
Watu wapatao 1200 tayari wamekwisha saini la kutaka tamasha la Koffi olomide analotarajia kulifanya mjini Kigali lisitishwe.
Mwezi Desemba, mahakama ya Paris itatoa uamuzi wa rufaa juu ya mashitaka ya unyanyasaji wa kingono uliodaiwa kutekelezwa na nyota huyo dhidi ya wanenguaji wake wa zamani. Alipatikana na hatia hapo awali, lakini amekuwa akikanusha madai ya wachezaji wake wanne wa zamani.
Wiki iliyopita mwanaharakati wa hai za wanawake nchini Rwanda Juliette Karitanyi, aliiambia BBC kuwa: "Kumruhusu [Koffi Olomide] kufanya tamasha hapa, ni sawa na kuwapuuza wale aliowanyanyasha.
Unaweza pia kusoma zaidi:
- Wanaharakati wa haki za wanawake Rwanda wasitisha tamasha la Koffi Olomide
- Koffi Olomide: Tutarajie nini kwenye kesi ya unyanyasaji wa kingono, ubakaji inayomkabili?
- Koffi Olomidé: Nyota wa muziki Congo ahukumiwa Ufaransa kwa kupatikana na hatia ya ubakaji wa mtoto wa miaka 15
Msako wa afisa feki wa polisi aliyeiba mbwa na zawadi za Krismasi

Chanzo cha picha, KWA HISANI YA FAMILIA
Maelezo ya picha, Mbwa mwenye miezi miwili Mmarekani XL anayeitwa 'Money' aliibiwa Polisi wa manispaa nchini Uingereza wawasaka wanaume wawili waliojifanya kuwa maafisa polisi na kumingia kwa lazima ndani ya nyumba, na kumnyanyasa mwanamke na kumuiba mbwa wake.
Walidai kuwa walikuwa wakifanya msako wa madawa ya kulevya walipovamia nyumba hiyo iliyopo eneo la Putney kusini magharibi mwa London, Jumatatu.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 30 alinyanyaswa na kumuacha akipewa matibabu hospitalini.
Wanaume hao waliingia ndani ya nyumba na kuiba mbwa, zawadi za Krismasi na pesa. Polisi ilisema.
Waziri wa mambo ya nje wa China awasili Ethiopia

Chanzo cha picha, MFA ETHIOPIA
Waziri wa mambo ya nje wa China amewasili katika mji kuu wa Ethiopia Addis Ababa kwa ziara rasmi nchini humo huku nchi za magharibi zikiwasihi raia wake kuondoka katika nchi hiyo iliyopo kwenye upembe wa Afrika kufuatia mzozo wa kivita unaoendelea kuongezeka kaskazini mwa nchi.
Naibu waziri mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen amempokea waziri wa mambo ya nje wa Uchina katika uwanja wa ndege.
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Wakati Waziri mkuu Abiy Ahmed akiwa hayupo, akiwa kwenye eneo la vita kuongoza mapambano dhidi ya waasi wa Tigray People's Liberation Front (TPLF), Bw Wang anatarajia kufanya mazungumzo na Bw Demeke.
Awali China ilielezea msimamo wake wa kuto "ingilia "masuala ya ndani ya Ethiopia huku vikosi vya nchi hiyo vikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa Marekani na mataifa ya Muungano wa ulaya kuhusu mzozo katika eneo la kaskazini mwa nchi na mzozo wa kibinadamu unaoendelea kuwa mbaya zaidi.
Unaweza pia kusoma:
- Waziri Mkuu wa Ethiopia aonekana akiwa na sare za kijeshi
- Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed awataka raia kuwasaidia wanajeshi kupigana vita dhidi ya waasi wa TPLF Tigray
- Mgogoro wa Ethiopia wa Tigray: Jinsi TPLF ilivyolizidi maarifa jeshi la Ethiopia
Zaidi ya vijana 100 watekwa nyara katika mashambulizi Msumbiji

Watu wenye silaha wamewateka nyara zaidi ya vijana 100 kutoka kijiji cha Naulala katika Mkoa wa Niassa kaskazini mwa Msumbiji, Shirika la Habari la Lusa limeripoti.
Niassa inapakana na Cabo Delgado, ambayo imekuwa ikikabiliana na waasi wa jihadi tangu Oktoba 2017.
"Kundi la watu wenye silaha limewateka nyara vijana 100 na kuchoma makazi na vibanda katika kijiji cha Naulala, Mkoa wa Niassa, kaskazini mwa Msumbiji," Lusa limeripoti, likinukuu vyanzo vya Msumbiji.
Vyombo vya habari vya Msumbiji hapo awali viliripoti msururu wa mashambulizi kwenye mpaka wa Cabo Delgado na Niassa ambapo takriban maafisa watano wa polisi waliuawa.
Ripoti zilisema kuwa jamii zinazoishi katika wilaya za Mecula na Merrupa za Niassa zililazimika kukimbia baada ya wanamgambo wa Kiislamu kukimbia operesheni za jeshi huko Cabo Delgado kuanza kufanya kazi katika wilaya hizo.
Mwezi Oktoba, Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika nchini Msumbiji (SAMIM) ulionya juu ya hatari ya shughuli za wanamgambo kuenea katika majimbo ya Niassa na Nampula.
unaweza pia kusoma:
- Kwanini ni vigumu kukabiliana na kundi la IS Msumbiji?
- Cabo Delgado: Uhusiano uliopo kati ya mali asili,uasi na mapigano nchini Msumbiji
- Mzozo wa Msumbiji: Wanajeshi wa Rwanda waongoza vita dhidi ya wapiganaji Msumbiji
Miili 9 zaidi yapatikana baada ya tukio la kuzama kwa boti Nigeria
Maafisa wa Nigeria wamethibitisha kuwa miili tisa zaidi ya mkasa wa ajali ya boti ya Jumanne imepatikana Jumatano asubuhi.
Hii inafanya idadi ya waliofariki kufikia 29 kufikia sasa.
Shughuli ya utafutaji na uokoaji inaendelea ikihusisha polisi, zima moto na wanachama wa Kikosi cha Usalama na Ulinzi wa Raia wa Nigeria pamoja na waliojitolea.
Polisi katika eneo hilo wameiambia BBC kwamba idadi ya manusura waliookolewa kufikia sasa bado ni saba.
Manusura wa ajali ya boti walikuwa wengi wanafunzi wa shule ya Kiislamu - wenye umri wa kati ya miaka sita na 12 - waliokuwa wakisafiri kwenda kwenye sherehe za kidini katika mji wa Bagwai.
Watu 29 wafariki baada ya boti iliyokuwa na wanafunzi kuzama nchini Nigeria

Chanzo cha picha, AFP
Boti iliyokuwa imebeba zaidi ya watu 50 imezama majini katika jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria.
Polisi wanasema miili 29 imepatikana na watu saba kuokolewa kufikia sasa kufuatia ajali hiyo iliyotokea Jumanne jioni.
Maafisa na wakaazi waliambia BBC kwamba boti hiyo ilikuwa imebeba makumi ya watu kutoka kijiji cha Badau kuelekea mji wa Bagwai, ambapo walipaswa kuhudhuria sherehe za kidini ya Kiislamu.
Wengi wa wahasiriwa walikuwa wanafunzi.
Msemaji wa polisi katika jimbo la Kano anasema operesheni ya kuwasaka na kuwaokoa watu inaendelea. Waliookolewa kufikia sasa wamepelekwa hospitali kwa matibabu.
Bado haijabainika ni nini kilisababisha mashua hiyo kupinduka majini.
Nchini Nigeria, ajali kama hizo mara nyingi hulaumiwa kutokana na upakiaji kupita kiasi na utunzaji duni wa boti pamoja na ukosefu wa udhibiti mzuri na mamlaka.
Takriban wasichana saba walikufa maji wakati mashua ilipopinduka katika jimbo jirani la Jigawa wiki mbili zilizopita.
Mnamo Mei, zaidi ya watu 100 walikufa katika jimbo la Kebbi katika ajali kama hiyo.
WHO yawataka walio katika hatari kuahirisha safari ikiwa hawajachanjwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirika la Afya Duniani limesema watu ambao hawana afya njema au walio kwenye hatari ya kupata maambukizi wanapaswa kuahirisha kusafiri ikiwa hawajachanjwa kabisa.
Katika ushauri wake wa hivi punde, wakala wa Umoja wa Mataifa amejumuisha watu walio na umri wa zaidi ya miaka 60 na wale walio na maradhi kama vile ugonjwa wa moyo, saratani na kisukari.
Taarifa ya awali ya WHO ilishauri dhidi ya safari zote za watu wa kundi hili.
Toleo lililosahihishwa lilibainisha kuwa ni wale tu walio hatarini zaidi na ambao hawajachanjwa kikamilifu ndio wanaopaswa kuahirisha safari.
Hii inaambatana na ushauri wa awali wa WHO wa kusafiri wakati wa janga hili, na unakuja huku kukiwa na wasiwasi kuhusu aina mpya ya Omicron.
WHO pia ilirejelea msimamo wake kwamba marufuku ya kusafiri kwa hakuzuii kuenea kwa virusi hivyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema "ana wasiwasi mkubwa" kuhusu kutengwa kwa eneo la kusini mwa Afrika, akiongeza kuwa "watu wa Afrika hawawezi kulaumiwa kwa kiwango cha chini cha chanjo kinachopatikana".
Hapo awali, mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema bado kuna maswali mengi kuhusu Omicron, ikiwa ni pamoja na maambukizi yake, ukali wa ugonjwa unaoweza kuchochea, na ufanisi wa vipimo na chanjo.
Unaweza pia kusoma:
- Kirusi Kipya cha Covid-19: Aina ya mpya ya kirusi yatajwa kuwa ni 'ya kutia hofu' na kuitwa Omicron
- Afrika Kusini imesema 'imeadhibiwa' kwa kugundua virusi vipya vya corona aina ya Omicron
Jeshi la DRC, Uganda kufanya operesheni dhidi ya ADF

Chanzo cha picha, AFP
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limethibitisha operesheni ya pamoja na kikosi maalum cha Uganda dhidi ya kundi la wapiganaji la ADF karibu na eneo la mpaka wa nchi zote mbili.
Taarifa ya jeshi Jumanne usiku ilisema vitengo maalum vya majeshi mawili "sasa vinaendelea kuwinda na kulinda maeneo ya ADF yaliyopigwa leo asubuhi".
Mizinga mikubwa ilisikika Jumanne katika maeneo ya Watalinga na Kichanga, mwandishi wa habari anayeishi katika mji wa karibu wa Beni aliambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu.
Operesheni hizo za pamoja "zilikubaliwa baada ya kutathminiwa", msemaji wa serikali ya DR Congo Patrick Muyaya aliandika kwenye ukurasa wa Twitter Jumanne usiku.
Matamshi ya Bw Muyaya yalizua hasira kubwa siku ya Jumatatu alipokuwa akiwaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kwamba "hakukuwa na wanajeshi wa Uganda nchini DR Congo".
“Aibu ya taifa...msemaji wa serikali anayesema uongo hadharani,” mmoja alimjibu.
"Na wewe Muyaya, unawaona wapumbavu Wacongo, jana ulikana kwamba wanajeshi wa Uganda wako DRC, na ona [unachosema] leo",
Mwingine aliandika. Mwezi Juni, rais wa DR Congo Felix Tshisekedi na Yoweri Museveni wa Uganda walikutana katika mpaka wa nchi mbili wa Mpondwe ambapo walikubaliana juu ya ushirikiano wa kupigana na ADF, lakini kwa namna gani na lini haikutangazwa.
Zimbabwe yarejesha masharti ya kupambana na Covid 19 ikiwemo zuio la kutotoka nje

Chanzo cha picha, Getty Images
Zimbabwe imerejesha marufuku ya kutotoka nje na karantini za lazima kwa wasafiri wote huku kukiwa na ongezeko la visa vya Covid ili kuzuia kuenea kwa aina mpya ya kirusi cha Omicron.
Nchi hiyo imerekodi zaidi ya visa 130,000 vya Covid na takriban vifo 4,700 tangu janga hilo lianze mapema mwaka jana.
Mamlaka ya Zimbabwe iliimarisha masharti ya Covid ikitaja ukosefu wa uwajibikaji upande wa umma na wanaamini kuwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi msimu wa sikukuu unapokaribia.
Pia kuna hofu ya wimbi la nne.
Rais Emmerson Mnangagwa alipitisha tena amri ya kutotoka nje kutoka saa tatu usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi saa za huko
Wasafiri wote wa kimataifa watahitajika kupimwa wanapowasili na kuwekwa karantini katika kituo kilichoteuliwa na serikali kwa gharama zao wenyewe.
Biashara zote zitahitajika kufungwa saa moja usiku.
Masharti hayo ni pigo kwa sekta ya utalii, ambayo ilitarajia msimu wa kawaida wa sikukuu.
Hatua hizo zitatathminiwa baada ya wiki mbili.
Mwanafunzi awaua watatu na kujeruhi wanane Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Wanafunzi watatu wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa akiwemo mwalimu mmoja katika shambulizi la risasi katika shule ya sekondari katika jimbo la Michigan nchini Marekani.
Maafisa wanasema mvulana wa miaka 16 na wasichana wawili wa miaka 14 na 17 walikufa.Polisi wanadai mshukiwa, mwanafunzi wa shule hiyo, alitumia bunduki ambayo baba yake alinunua siku zilizopita.
Wanafunzi wameelezea kujificha chini ya madawati wakati wa shambulio hilo. Wengine walikuwa wamesalia nyumbani Jumanne kwa sababu ya wasiwasi wa usalama.
Polisi walipokea simu za dharura kutoka kwa shule ya sekondari katika mji wa Oxford, takriban maili 40 (65km) kutoka Detroit.Ndani ya dakika chache, maafisa walikuwa wamepokea simu 100 kwa namba 911, Afisa Msaidizi wa Kaunti ya Oakland Mike McCabe aliwaambia waandishi wa habari.
Maafisa wanasema mshukiwa, mvulana mwenye umri wa miaka 15, alijisalimisha dakika tano baada ya polisi kuitwa.
Hakuna risasi iliyofyatuliwa wakati wa kukamatwa, na kijana huyo hakujeruhiwa, Bw McCabe alisema, akiongeza kwamba mvulana huyo alikuwa darasani kabla ya ufyatuaji risasi kuanza. Mkuu wa polisi wa kaunti ya Oakland, Mike Bouchard, alisema maafisa wake walimdungua mpiga risasi akiwa bado na risasi saba kwenye bunduki.
Xiomara Castro: Honduras kupata rais wa kwanza mwanamke

Chanzo cha picha, Reuters
Honduras inatarajiwa kumchagua rais wake wa kwanza mwanamke, Xiomara Castro, baada ya chama tawala kukubali kushindwa.
Bi Castro, mgombea wa chama cha mrengo wa kushoto cha Libre (Free) Party, ana uongozi wa awali wa karibu asilimia 20 dhidi ya mpinzani wake.
Ushindi wake utamaliza utawala wa miaka 12 wa chama cha mrengo wa kulia cha National Party, ambacho kimekumbwa na kashfa na tuhuma za ufisadi.
Bi Castro atachukua nafasi ya Rais aliyeleta mgawanyiko Juan Orlando Hernández.
Amekuwa akikabiliwa na tuhuma za uhusiano na biashara ya dawa za kulevya baada ya kaka yake Antonio kufungwa jela kwa ulanguzi nchini Marekani.
Bi Castro ameahidi "kuiondoa Honduras kutoka kwenye shimo" la "udikteta wa mihadarati na ufisadi".
Mumewe, Manuel Zelaya, alitawala nchi hiyo kuanzia mwaka 2006 hadi 2009, alipotimuliwa madarakani kwa mapinduzi.
Aligombea wadhifa huo mara mbili hapo awali katika miaka iliyofuatia kuondolewa kwake mamlakani.
Kura bado zinahesabiwa na baraza la uchaguzi bado halijatangaza mshindi rasmi.
Hata hivyo kukubali kushindwa kwa chama tawala kulikuja siku mbili baada ya Bi Castro kuongoza katika matokeo ya awali.
Mpinzani wake mkuu Nasry Asfura alisema kwenye matangazo ya runinga ya ndani kwamba alikuwa amemtembelea Bi Castro na familia yake.
"Sasa nataka kusema hadharani kwamba ninampongeza kwa ushindi wake na kama rais mteule," Bw Asfura alisema, na kuongeza: "Natamani Mungu amwangazie na kumwongoza ili utawala wake utufanyie mema sisi sote wa Honduras. ".
Mwandishi wa Marekani amuomba msamaha mwanamume aliyefungwa kimakosa kwa ‘kumbaka’

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwandishi raia wa Marekani Alice Sebold ameomba msamaha kwa kuhusika kwake na kufungwa kimakosa mwanamume aliyeondolewa mashtaka wiki iliyopita kwa kumbaka mwaka 1981.
Kwenye kitabu chake Lucky, alieleza kubakwa na kisha kuwaambia polisi kuwa alimuona mwanamume mweusi barabarani ambaye aliamini kuwa ndiye alimshambulia.
Anthony Broadwater alikamatwa na kuhukumiwa na kukaa gerezani miaka 16.
Taarifa kutoka kwa Bw Broadwater, iliyotolewa na mawakili wake ilisema ametulia kwamba Bi Sebold ameomba msamaha.
Katika taarifa ya Bi Sebold ya kuomba msamaha, alisema, “samahani, kwanza kabisa kwa kuwa yale maisha ungeishi yaliibwa kinyume na haki kutoka kwako, na ninajua kuwa hakuna msamaha unaweza kubadilisha kile kilikufanyikia”.
Alielezea kwa undani jinsi alivyoshambuliwa akiwa na umri wa miaka 18 na mwanafunzi wa chuo cha Syracuse mjini New York.
Miezi kadhaa baadaye alisema alimuona mwanamume mweusi barabarani ambaye alidhani kuwa ndiye alimshambulia na kuwajulisha polisi.
Kisha polisi akamkamtaa Bw Broadwater ambaye yaripotiwa alikuwa eneo hilo wakati huo.
Baada ya kukamatwa, Bi Sebold alishindwa kumchagua katika safu ya polisis, na kuchagua mwanamume mwingine.
Lakini Bw Broadwater hata hivyo akafunguliwa mashtaka na kuhukumiwa.
Baada ya kuachiliwa kutoka gerezani mwaka 1998, Bw Broadwater alibaki kwenye sajili ya wahalifu wa ngono.
Aliachiliwa huru tarehe 22 Novemba baada ya kesi yake kuangaliwa upya na kupatikana kuwa alihukumiwa kwa ushudi kidogo na ambao sasa umepotoshwa.
Aliposikia habari hizo aliliambia shirika la AP kwamba alikuwa analia machozi ya furaha na ya unafuu.
Bi Sebold alisema katika taarifa yake kuwa alitumia siku nane za mwisho akijaribu kuelewa jinsi hii liliweza kutokea
“Pia nilisumbuliwa na ukweli kuwa mbakaji wangu hawezi kuja kujulikana na huenda aliendelea kuwabaka wanawake wengine na kwamba haweza kutumikia kifungo jela kama vile Bw Broadwater,” aliongeza.
Kitabu cha Lucky kiliuza nakala milioni moja na ndicho kulizundua taaluma ya uandishi ya Bi Sebold.
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hivi leo tarehe 1 Disemba 2021
