DRC: Rais Tshisekedi aapa kuwafungua wafungwa wote wa kisiasa

rais wa DRC Felix Tchisekedi
Maelezo ya picha, Iwapo rais Felix Tchisekedi atawaachilia kweli au kutowaachilia wafungwa wa kisiasa kitakuwa ni kipimo cha mamlaka aliyonayo ya kisiasa nchini mwake

Rais mpya wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Felix Tshisekedi, amesema kuwa anataka kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa wakiwemo watu wote waliofungwa wakati wa maandamano yaliyofanyika kabla ya uchaguzi wa mkuu wa mwezi wa Disemba mwaka jana.

Bwana Tshisekedi alikuwa mgombea wa upinzani katika uchaguzi uliibua mgawanyiko na shutuma kwamba kulikuwa na wizi wa kura ili kuwazuwia wakosoaji wa rais Joseph Kabila kuingia madarakani.

Katika hotuba yake aliyoitoa katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa rais wa Kongo , Felix Tshisekedi, amesema ''Nitamuomba waziri wa sheria kuwa kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa waliowekwa gerezani kwa ajili ya maoni yao''.

rais Felix Tchisekedi akiwa pamoja na rais Joseph kabila
Maelezo ya picha, Rais felix Tchisekedi (kulia) akiwa pamoja na mtangulizi wake Joseph kabila

Mwandishi wa BBC anasema miongoni mwa wafungwa haoni huenda ni wafuasi wake''.

Bwana Tshisekedi aligombea kama kiongozi wa upinzani katika uchaguzi uliokuwa na utata wa Disemba mwaka jana baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila kung'atuka madarakani.

Hata hivyo Mahakama ya katiba DR Congo ndiyo iliyomuidhinisha rasmi Felix Tshisekedi kuwa rais wa nchi hiyo, na ilikataa ombi la rufaa iliowasilishwa na Martin Fayulu.

Moja ya magereza nchini Kongo lililoteketezwa na wafungwa waliotoroka wakiwemo wafungwa wa kisiasa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Baadhi ya Magereza nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yanaripotiwa kujaa kupita kiasi wafungwa wa kisiasa ambao mara kwa mara wamekuwa wakiteketeza moto magereza na kutoroka

Wito wa Bwana Tshisekediwa kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa unaonekana kama pigo kwa mtangulizi wake.

Ikiwa wataachiliwa huru kweli au la , itakuwa ni kipimo cha mamlaka aliyonayo Bwana Felix Tshisekedi nchini humo.