Uchaguzi wa Tanzania 2020: Maalim Seif kuweka rekodi ya kugombea urais au atawapa mtihani CUF?

Katibu Mkuu wa chama cha CUF Maalim Seif Sharrif Hamad
Maelezo ya picha, Ndani ya chama cha CUF makundi yote mawili ya Maalim Seif (Pichani) na Profesa Lipumba yanachukuliwa kuwa na nguvu za aina yake,
    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

CHAMA cha Wananchi (CUF) bado kipo kwenye mgogoro wa kisiasa ambao umeibua makundi mawili ya Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharrif Hamad na Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba, lakini kinakabiliwa na jukumu zito kila linapotajwa jina la Maalim Seif Sharrif Hamad.

Mgogoro wa sasa unaingia katika awamu nyingine ambapo wanachama na wafuasi wamegawanyika katika pande hizo mbili, huku wakiwa katikati ya giza nene kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 visiwani Zanzibar na Tanzania Bara.

Matokeo ya mgogoro huo yameonekana pia baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, chini ya Jaji Dk. Benhajj Masoud mnamo mwezi Februari 18 mwaka huu kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) wa kambi ya Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati hatua hiyo ya Mahakama ikivunja sehemu ya nguvu za kambi ya Lipumba, bado upo mwendelezo wa mgogoro ndani ya chama hicho, ambapo uamuzi wa kesi ya msingi ya kupinga uhalali wa uenyekiti wa Lipumba bado haujatolewa.

Tukiacha suala la hukumu ya Mahakama, ndani ya chama cha CUF makundi yote mawili ya Maalim Seif na Profesa Lipumba yanachukuliwa kuwa na nguvu za aina yake, hali ambayo imekuwa ikikiteteresha chama hicho kadiri ya siku zinavyokwenda.

Mgogoro: kukimbiwa na wanasiasa

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tundu Lisu ni mmoja wa wanasiasa wenye nguvu na ushawishi walio tayari kupambana na upande wowote, licha ya kuibuka kwa vita vya kisiasandani ya chama cha CUF

Bila kujali sababu zozote za nje walizotoa kukihama chama hiki, lakini ukweli unabaki kuwa kimekimbiwa na baadhi ya makada na viongozi wake, ambao wamekwenda kutafuta fursa za kisiasa ndani ya chama tawala cha CCM.

Miongoni mwa waliokihama chama hicho ni Julius Mtatiro (aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad), Maulid Mtulia (aliyekuwa mbunge wa chama hicho katika jimbo la Kinondoni), Abdallah Mtolea (aliyekuwa Mbunge wake wa chama hicho katika jimbo la Temeke), na Zuberi Kuchauka (aliyekuwa Mbunge wa chama hicho katika jimbo la Liwale mkoani Lindi).

Athari nyingine ya mgogoro huo ni wabunge 8 wa viti maalumu wa CUF na madiwani wawili wamepoteza nafasi zao kutokana na msuguano baina ya kambi hizo mbili zinazohasimiana.

Swali kuu hapa ni kwamba, katika mazingira haya, Maalim Seif anaweza kukinusuru chama cha CUF au kinahitaji kizazi kingine cha uongozi ili kukipaisha zaidi kisiasa?

Nguvu na ushawishi wa Maalim Seif

Katibu mkuu huyo amekuwa na nguvu ya kisiasa visiwani Zanzibar, wakati Lipumba anaonekana kuteka nguvu ya kisiasa ya chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara. Maalim ana nguvu kisiasa na ushawishi mkubwa katika pande hizo, ndiyo maana baadhi ya wanasiasa wanaendelea kumpigania na kuonyesha imani kubwa waliyonayo kwake.

Julius Mtatiro (aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad)

Chanzo cha picha, AZANIA POST

Maelezo ya picha, Miongoni mwa waliokihama chama cha CUF ni Julius Mtatiro (aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF kambi ya Maalim Seif Sharif Hamad)

Nguvu na ushawishi wa Maalim Seif kisiasa visiwani zilichochea mabadiliko ya kikatiba ili kujenga mshikamano kati ya chama tawala na wapinzani, ambapo kulitengenezwa nafasi ya makamu wa kwanza wa rais (ambaye anatakiwa kutoka chama cha upinzani). Ingawa nafasi hiyo hivi sasa iko wazi, baada ya mgogoro wa kisiasa ulioibuka pindi CUF iliposusia kurudiwa kwa uchaguzi baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Katika chaguzi mbalimbali za mwaka 1995, 2000, 2005,2010, na 2015 zinaonyesha kuwa kiongozi huyo ni hazina ndani ya chama hicho, hasa pale anavyojizolea kura kila uchaguzi.

Vilevile nguvu za Maalim zinaonekana kwenye uongozi ndani ya chama. CUF hakijawahi kuwa na Katibu mkuu mwingine tangu kilipoanzishwa mnamo mwaka 1992. Jambo hilo kisiasa linaleta changamoto kwao kumpata kiongozi wa aina hiyo. Matokeo ya kutokuwapo katibu mwingine kumetengeneza dhana kuwa, Visiwani na Bara kuwa, CUF ni Maalim na Maalim ni CUF.

Licha ya kuibuka kwa vita vya kisiasa na mtazamo hasi dhidi ya chama hicho, bado kina hazina ya wanasiasa wenye nguvu na ushawishi walio tayari kupambana dhidi ya upande wowote.

Bunge la Tanzania
Maelezo ya picha, Chama cha CUF ni cha pili cha upinzani kwa kuwa na wawakilishi wengi bungeni

Wanasiasa waliomo ndani ya chama hicho ni kama vile Ali Saleh, Ismail Jussa Ladhu, Juma Duni Haji, na Mansoor Yusuf Himid kwa kuwataja wachache.

Ataweka rekodi ya kugombea urais?

Jina la Maalim Seif Sharrif Hamad lina rekodi ya kipekee katika uchaguzi mkuu. Kiongozi huyo amegombea urais wa Zanzibar katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Maalim Seif ni mwanasiasa aliyegombea urais wa Zanzibar mara nyingi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini Tanzania. Hadi sasa amegombea urais wa Zanzibar mara 5, na iwapo mwaka 2020 atapitishwa itakuwa ni mara ya 6.

Safari ya Maalim Seif kugombea urais ilianza mwaka 1995 alipopambana na mgombea wa CCM, Salmin Amour. Kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) matokeo ya urais mwaka 1995, Salmin Amour alishinda kwa asilimia 50.24 dhidi ya 49.76 alizopata Maalim Seif. Hata hivyo, CUF ilitangaza kutoutambua ushindi huo.

Mwaka 2000, Seif aliingia ulingoni kupambana na Amani Abeid Karume, mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume. Kwa mara nyingine, matokeo ya ZEC yalionyesha Seif aliangushwa baada ya kujikusanyia asilimia 32.96 ya kura dhidi ya asilimia 67.04 alizopata Amani Karume. Uchaguzi wa mwaka 2000, alipata asilimia chache (32.96%).

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko katika chaguzi hizo ambapo baadhi ya waangalizi walisema haukukidhi vigezo vya kidemokrasia kutokana na wagombea kutoka vyama vya upinzani kutishwa na vyombo vya dola.

Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola walisema uchaguzi huo ulitawaliwa kwa kile walichokiita 'uchafu mwingi'.

Vidonda vya uchaguzi wa mwaka 2000 vilijitokeza zaidi mwaka 2001, ambapo baadhi ya wafuasi wa CUF walipoteza maisha baada ya kushambuliwa na vyombo vya dola. Maandamano ya Januari 27, 2001, yalichangia kusainiwa kwa makubaliano ya pili ya amani baina ya pande mbili za CUF na CCM ili kuleta utulivu visiwani Zanzibar.

Uchaguzi wa mwaka 2005, CUF walimteua Maalim Seif kupambana tena na Amani Abeid Karume wa CCM. Uchaguzi huo ulipokamilika, ZEC ilimtangaza Amani Abeid Karume kuwa mshindi baada kujikusanyia asilimia 53.18, huku Seif Hamad akijipatia asilimia 46.07 ya kura zote.

Hata hivyo waangalizi wa kimataifa kwa mara nyingine, walisema kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki. Taarifa ya waangalizi wa Jumuiya ya Madola walisema palikuwa na kasoro nyingi na uhaba wa uhuru miongoni mwa wapigakura na wagombea. CUF ilipinga matokeo hayo.

Maalim Seif alirudi tena kwenye kinyang'anyiro cha mwaka 2010 akiwakilisha CUF dhidi ya Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM. Baada ya uchaguzi wa Oktoba 31, 2010, ZEC ilimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar kwa kupata asilimia 50.1 dhidi ya 49.1 za Seif.

Viongozi wa CCM

Chanzo cha picha, IKULU/TANZANIA

Maelezo ya picha, Chama cha CUF kimeshindwa na chama tawala cha CCM kwenye urchaguzi wa urais mara kadhaa

Kutokana na makubaliano ya vyama hivyo kumaliza mgogoro wa muda mrefu visiwani humo, Maalim Seif alitakiwa kuwa sehemu ya serikali ambapo aliteuliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, huku Balozi Seif Ali Iddi akiwa makamu wa pili wa Rais.

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2015 yalifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Mwenyekiti wake Jecha Salum Jecha. ZEC ilitangaza pia uchaguzi wa marudio utafanywa Machi 20, mwaka uliofuata.

Licha ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, Maalim Seif aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mnamo Oktoba, 2015 na kusema yeye ndiye mshindi wa kiti cha urais Zanzibar na alikataa kushiriki uchaguzi wowote wa marudio.

Mtihani mikononi mwa CUF-Zanzibar

Katika kuhitimisha mapito yote ya Maalim Seif kisiasa utaona nguvu zake za kisiasa zimeleta matunda ndani ya chama hicho na ustawi wa kisiasa Zanzibar. Mchakato wa marekebisho ya mifumo ya utawala imekuwa sehemu ya mabadiliko yaliyochangiwa na Maalim Seif.

Ndio maana, kila uchaguzi unapowadia, matokeo rasmi yanayonyesha imani ya wafuasi na wanachama wa CUF bado iko kwa Maalim Seif. Wanaonekana kuamini kuwa kiongozi huyo kuwa na uwezo wa kuongoza Zanzibar. Kwa hiyo matumaini na mategemeo hayo ndiyo chanzo cha Maalim Seif kuwa jabali la kisiasa visiwani Zanzibar hadi leo.

Hata hivyo, changamoto waliyonayo CUF kwa sasa ni kufanya uamuzi wa kumteua tena Maalim Seif agombee urais au wamtupe na kumgeukia mwanasiasa mwingine?

Hili si jambo dogo, ni muhimu kwa mustakabali wa chama na uwekezaji uliofanywa na wanasiasa mbalimbali ndani na nje ya chama.

Je, wanasiasa na wanachama wa CUF wataendelea kumtegemea Maalim Seif au watakuja na sura mpya ya kujenga chama chao kwenye uchaguzi ujao? Chama hicho kitamudu kuvuka dhoruba kubwa la mgogoro unaoendelea kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020?

Muda utaongea.