Kwa nini mvutano unaongezeka kwenye mpaka kati ya Belarus na Poland?

Chanzo cha picha, Getty Images
Poland inatuma wanajeshi 10,000 zaidi katika mpaka wake na Belarus, kufuatia madai ya kuvamiwa na helikopta za kijeshi za Belarus.
Serikali ya Poland inaeleza kuwa hii ni hatua ya ulinzi dhidi ya mamluki wa kundi la Wagner la Kirusi, ambao wameweka ngome Belarus na sasa wanaelekea mpakani.
Lakini je ni tukio gani la hivi punde kwenye mpaka kati ya Poland na Belarus?
Serikali ya Poland inadai kuwa mnamo Agosti 1, helikopta mbili za kijeshi za Belarus ziliruka katika mwinuko wa karibu kilomita mbili kutoka eneo lake, katika eneo la Bialowieza.
Vikosi vya jeshi la Belarus wakati huo vilikuwa vikifanya mazoezi katika eneo la mpaka.
Serikali ya Belarusi ilisema "hapakuwa na ukiukwaji wa mpaka wa helikopta za Mi-8 na Mi-24", ikataja mashitaka hayo kuwa "hadithi ya vikongwe".
Wakazi wa Bielowieza walichapisha picha kwenye mitandao ya kijamii za helikopta aina ya Mi-8 na Mi-24 yenye nembo za Belarus, ambazo walisema ziliruka juu ya mji huo.
BBC ililinganisha nambari za mfululizo za helikopta na zile zilizoonekana katika uwanja wa karibu wa ndege wa Machulishchi mnamo 2018.
Uvamizi huu wa kijeshi unakuja baada ya maelfu ya wahamiaji kwenda Poland kutoka Belarus.
Poland inadai kuwa tangu 2021, Belarus imekuwa ikiwahimiza watu kutoka Mashariki ya Kati na Afrika kusafiri hadi Belarus na kuvuka mpaka kinyume cha sheria.

Chanzo cha picha, Getty images
Ingawa kuna vivuko vichache kuliko miaka miwili iliyopita, walinzi wa mpaka wa Poland wanasema wahamiaji 19,000 wamejaribu kuvuka mpaka tangu kuanza kwa mwaka huu, ikilinganishwa na 16,000 mwaka jana.
Serikali ya Poland imeuita mkakati wa Belarus, vita vya mseto”.
Je, mamluki wa Wagner wa Kirusi wanajiandaa kuingia Poland?
Baada ya kushindwa kwa maasi mwezi Juni mwaka jana na mamluki kutoka Kundi la Wagner la Urusi, baadhi ya wanajeshi wake walihamia Belarus.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Wanaomba kwenda magharibi... kuchukua safari ya Warszawa Lakini bila shaka ninawaweka katikati ya Belarus, kama tulivyokubaliana," alitania Rais wa Belarus Alexander Lukashenko, wakati wa mazungumzo na Vladimir Putin. .
Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki alisema kundi la wapiganaji 100 wa Wagner walikuwa wakielekea Grodno, mji ulioko kaskazini magharibi mwa Belarus unaopakana na Poland. Hali ni "hatari zaidi", anasema.
Wapiganaji wa Belarus Wagner wanaweza kuingia Poland wakijifanya kama wahamiaji, wanaweza pia kujifanya kama walinzi wa mpaka wa Belarus na kuwasaidia wahamiaji wengine haramu kuvuka, kulingana na Mateusz Morawiecki.
Kwa nini eneo hili la mpakani ni muhimu sana?
Wizara ya Ulinzi ya Belarus ilisema kuwa wanajeshi wa Wagner wapo katika kambi ya Brestsky kusini mwa nchi hiyo, takriban kilomita 10 kutoka mpaka wa Poland, na walikuwa wakitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Belarus.
"Kama mamluki, wanajeshi hawa wanaweza kusababisha machafuko ya mpaka, ambayo Urusi na Belarus hazingeweza kuwajibika moja kwa moja," alisema Barbara Yoxon, mhadhiri mkuu wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Lancaster.
Mpaka kati ya Poland na Lithuania ni mstari unaoitwa Pengo la Suwalki.
Ukanda huu wa kilomita 95 wa ardhi pia hutumika kama kiunganishi kati ya Belarus na eneo la Urusi lililoimarishwa sana kiulinzi la Kaliningrad.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wachambuzi wengi wa masuala ya kijeshi wanaona pengo la Suwalki kama kigezo kinachowezekana kusababisha mzozo kati ya mataifa ya NATO na Urusi.
Hofu ni kwamba ikiwa Urusi na Belarus zitatumia nguvu za kijeshi kuzuia ukiukaji huu, zinaweza kuitenganisha Jamhuri za Baltic (Lithuania, Latvia na Estonia) na washirika wao wa NATO wa Ulaya.
"Hii ni hatua nyembamba sana, anaelezea Bw. Yoxon. Urusi na Belarus zinaweza kuizuia kwa urahisi NATO kutuma vikosi vya ulinzi kuyalinda mataifa ya Baltic."
Uvamizi huu unaodaiwa unaonyesha kuwa Urusi inakusudia kuzishambulia Jamhuri za Baltic, kulingana na idadi ndogo ya wachambuzi wa kijeshi.
Hata hivyo, Profesa Malcolm Chalmers wa Shirika la Huduma za Kifalme la Umoja wa Mataifa anaamini kuwa hili ni zoezi la Urusi. "Hili kwa kiasi fulani ni zoezi la Urusi na Belarus kujaribu maji na kuona jinsi NATO inaweza kujibu, au kutojibu, kwa uvamizi katika eneo lake," Chalmers alielezea.
Urusi na Belarus zimetia saini mikataba kadhaa ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni. Belarus imeruhusu wanajeshi wa Urusi kuivamia Ukraine kutoka kwenye mpaka wake na kuiruhusu Urusi kuweka makombora ya kinyuklia kwenye ardhi yake.

Chanzo cha picha, VOENTV/WIZARA YA ULINZI YA BELARUS KUPITIA REUTERS
Anais Marin, wa chama cha wataalam wa masuala ya kimataifa Chatham House, anaamini kwamba uvamizi unaodaiwa huenda ni wazo la Urusi, "kuhakikisha kwamba Belarus inasalia kuwa adui wa Poland na NATO, na mshirika mkubwa wa Moscow".
Poland inafanya nini kukabiliana na mvutano wa mpaka?
Wizara ya Ulinzi ya Poland inasema inatuma wanajeshi 10,000 zaidi kwenye mpaka na Belarus. Inabainisha kuwa 4,000 kati yao watasaidia moja kwa moja walinzi wa mpaka na kwamba 6,000 watawekwa kwenye hifadhi.
Mnamo Julai, serikali ilituma wanajeshi 1,000 zaidi kwenye mpaka ili kulinda dhidi ya uvamizi unaowezekana wa wapiganaji wa Wagner.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadokeza kuwa wanasiasa wa Poland wanaweza kutia chumvi vitisho kutoka kwa Wagner na Belarus kwa sababu wanakabiliana na uchaguzi hivi karibuni na wanataka kuonyesha kuwa wao ni wakali katika masuala ya usalama.















