Bunge la Bangladesh lavunjwa baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu
Waandamanaji wanataka kubuniwe serikali ya mpito na mshauri wake mkuu awe Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Muhammad Yunus.
Muhtasari
- Mkasa wa binti kubakwa Tanzania, uchunguzi umefikia hatua nzuri- Msemaji wa polisi
- Uchunguzi wa jinai waanzishwa dhidi ya viongozi wa upinzani Venezuela
- Wapalestina kumi wauawa katika ghasia za Ukingo wa Magharibi
- 'Tumepata Medali zetu za dhahabu kwa njia safi sana' - China
- Kwa nini Kamala Harris alimchagua Tim Walz
- Kamala Harris amchagua Tim Walz kuwa mgombea mwenza wake
- Israel na Hezbollah zafanya mashambulizi ya kujibizana huku mvutano ukizidi kupamba moto
- Hifadhi ya maiti Marekani yatozwa faini ya $950m katika kesi ya miili iliyooza
- Waandamanaji wakamatwa Nigeria kwa kupeperusha bendera ya Urusi
- Bunge la Bangladesh lamevunjwa - Ofisi ya Rais
- Muhammad Yunus: Mpinzani mkuu wa Sheikh Hasina ambaye waandamanaji wanataka awe mshauri mkuu wa serikali Bangladesh
- Maandamano Bangladesh: Tunachokijua kufikia sasa
- Wadukuzi wa Korea Kaskazini wanajaribu kuiba siri za nyuklia na kijeshi, Marekani, Uingereza zasema
- Ukiritimba wa Google katika urambazaji mtandaoni ni kinyume cha sheria- jaji wa Marekani
- Rais Biden akutana na maafisa usalama wa Marekani wakati hofu ya mashambulizi ya Iran ikiongezeka
- Wakenya washinda medali 3 Paris 2024
- Wanajeshi wa Marekani wajeruhiwa katika shambulizi nchini Iraq
- Shangwe nchini Bangladesh baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kukimbia nchi
Moja kwa moja
Lizzy Masinga, Ambia Hirsi & Yusuf Jumah
Mkasa wa binti kubakwa Tanzania, uchunguzi umefikia hatua nzuri- Msemaji wa polisi

Chanzo cha picha, Polisi Tanzania
Maelezo ya picha, Msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania David Misime Maelezo ya sauti, Mkasa wa binti kubakwa Tanzania, uchunguzi umefikia hatua nzuri- Msemaji wa polisi Jeshi la polisi nchini Tanzania limesema uchunguzi kuhusu mkasa wa kubakwa kwa binti mtanzania ulifanywa na kundi la wanaume watano umefikia pazuri na kuwataka wananchi kuwa na subira.
Muda mfupi uliopita Mwandishi wa BBC, Martha Saranga amezungumza na Msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania DavLinkid Misime na kwanza amemuuliza uchunguzi umefikia hatu agani?
Hata hivyo taasisi mbalimbali zimekemea tukio hilo ikiwemo chama cha mawakili tanzania TLS, na tume ya kutetea haki za binadamu wakitaka sheria kali zichukuliwe.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nchini Tanzania Dr Stagomena Tax amenukuliwa na chombo cha habari nchini Tanzania akisema Serikali haitavumilia uvunjaji wa sheria,na atakayebainika kutekeleza ukatili huo atachukuliwa hatua stahiki.
Mwishoni wa wiki iliyopita, video ikimuonesha binti akifanyiwa vitendo vya ukatili na kundi la vijana watano ilisambaa nchini Tanzania na kuzua gumzo na hasira miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii. Sikiliza hapa mahojiano hayo na msemaji wa polisi
Uchunguzi wa jinai waanzishwa dhidi ya viongozi wa upinzani Venezuela

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, María Corina Machado, ambaye alizuiwa kuwania wadhifa huo, ameweza kuunganisha upinzani Mwanasheria mkuu wa Venezuela, mshirika wa karibu wa Rais Nicolás Maduro, ametangaza kuanzisha uchunguzi dhidi ya viongozi wa upinzani María Corina Machado na Edmundo González kwa madai ya "kuchochea uasi".
Viongozi hao wa upinzani hapo awali walitoa wito kwa vikosi vya usalama "kuunga mkono watu" na kupuuza maagizo yoyote ya kukandamiza maandamano dhidi ya serikali.
Mvutano umekuwa ukiongezeka tangu halmashauri ya kusimamia uchaguzi, ambayo inashirikiana kwa karibu na serikali, kumtangaza Bw Maduro kuwa mshindi bila kutoa hesabu za kina za upigaji kura hadharani.
Upinzani umetoa hesabu zake kuthibitisha kuwa Bw González alishinda uchaguzi huo na sio Rais Maduro kama ilivyotangazwa na Tume ya Uchaguzi.
Siku ya Jumapili, gazeti la Washington Post lilisema limekagua zaidi ya karatasi 23,000 za kujumlisha kura zilizokusanywa na upinzani - ambazo ni sawa na 80% ya mashine za kupigia kura kote Venezuela.
Gazeti la The Post lilihitimisha kwamba Bw González "huenda alipata kura zaidi ya mara mbili ya Rais Nicolás Maduro".
Wapalestina kumi wauawa katika ghasia za Ukingo wa Magharibi

Chanzo cha picha, Getty Images
Vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina 10 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Palestina.
Jeshi la Israel linasema lilifanya mashambulizi mawili tofauti ya anga kaskazini mwa eneo hilo likiwalenga wanachama wa makundi yenye silaha.
Kumekuwa na ongezeko la ghasia katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza, vilivyochochewa na shambulio baya la Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba.
Wizara ya afya ya eneo hilo inasema Wapalestina wasiopungua 600 - wanachama wa makundi yenye silaha, wapiganaji na raia - wameuawa katika matukio yanayohusiana na migogoro katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki.
Takriban Waisrael 17, wakiwemo maafisa 12 wa vikosi vya usalama, pia wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Mamlaka ya Palestina Nabil Abu Rudeinah alilaani ghasia za hivi majuzi, pamoja na madai ya mateso na unyanyasaji wa wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israel, kama hatua ya "kuvuka mistari yote ya rangi nyekundu".
Soma pia:
'Tumepata Medali zetu za dhahabu kwa njia safi sana' - Uchina yakashifu mashaka ya kutumia dawa za kusisimua misuli

Chanzo cha picha, Reuters
"Shaka yoyote ni mzaha tu. Mafadhaiko hutufanya tuwe na nguvu zaidi," Qin Haiyang - sehemu ya kikosi cha waogeleaji wanne wa timu ya wanaume ya 4x100m ya Uchina iliyoweka historia baada ya ushindi wao usio na kifani dhidi ya Marekani siku ya Jumatatu anasema.
Kuonekana kwa kauli hiyo ya kukaidi kwa Qin kulikuja mwisho wa wakati ambao umekuwa changamoto kwa Uchina kwenye bwawa.
Baadhi ya waogeleaji mashuhuri nchini - akiwemo Qin na mwenzake Sun Jiajun- wameangaziwa baada ya madai mengi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli, na kufuatiwa na madai tata ya Marekani kwamba Shirika la Kupambana na Dawa za Zilizopigwa marufuku michezoni Duniani (Wada) lilikuwa likificha ushahidi.
Walikuwa miongoni mwa waogeleaji 23 wa Kichina ambao waliripotiwa kupata matokeo chanya ya kutumia dawa hizo katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo.
Na ingawa waogeleaji wa Kichina wamepimwa dawa za kulevya mara mbili zaidi ya mataifa mengine mwaka huu kabla ya kuelekea Paris, matokeo yao yamekabiliwa na shaka.
Mara tu baada ya hafla ya medley siku ya Jumatatu, Adam Peaty wa Timu ya GB alifungua shutuma kwa timu ya Uchina, akisema"hakuna faida ya kushinda ikiwa haujashinda kwa haki".
Kwa nini Kamala Harris alimchagua Tim Walz

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Anthony Zurcher
Mwandishi wa BBC Amerika Kaskazini
Watu wachache walikuwa na Gavana wa Minnesota Tim Walz kwenye orodha zao za awali za makamu wa rais wa Kamala Harris, lakini vyombo vya habari vya Marekani sasa vinaripoti kwamba atakuwa kwenye tiketi ya Democratic.
Mwalimu huyo wa zamani wa shule ya upili na mkufunzi wa kandanda alivutia watu wa chama cha Democratic kwa mtindo wake wa kustaajabisha na uwezo wake wa kupambana na Donald Trump bila kuonekana kuwa mkali sana.
Kumtaja Trump kama na mgombea mwenza wake kama 'watu wa ajabu" likawa neno la chama cha Democratic katika muda wa siku chache - na sasa ni sehemu ya kawaida ya hotuba ya Harris.
Ingawa Minnesota sio mojawapo ya majimbo yenye mapambano makali ya kura , Kambi ya Harris inaweza kutumaini kuwa Walz atawapa njia ya kuvuka mpaka wa katikati ya magharibi katika maeneo kama vile Wisconsin na Michigan, ambayo itasaidia kuamua mshindi wa uchaguzi huu.
Walz pia ana rekodi ya kutunga sheria za ustawi katika jimbo lake huku akiitetea kwa njia ambayo wapiga kura wa wastani na huru wanaweza kuelewa. Katika kazi yake ya awali kama mbunge, aliweza kushinda katika wilaya ambayo ina idadi kubwa ya wapiga kura wa vijijini na wa Republican.
Soma pia:
Habari za hivi punde, Kamala Harris amchagua Tim Walz kuwa mgombea mwenza wake -ripoti
Kamala Harris amemchagua gavana wa Minnesota Tim Walz, kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa rais wa Marekani, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.
Bi Harris na mgombea mwenza wake wanatarajiwa kuanza ziara ya kampeni katika majimbo yanayosadikiwa kuwa na ushindani mkali, mkutano wa kwanza ukipangiwa kufanyika huko Philadelphia baadaye leo.
Kura ya maoni ya hivi punde ya kituo cha CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, inawaonyesha Bi Harris na Trump wakiwa katika kinyang'anyiro kikali kitaifa, huku Mgombea huyo wa chama cha Democratic akiongoza kwa pointi moja dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump.
Maelezo zaidi:
Israel na Hezbollah zafanya mashambulizi ya kujibizana huku mvutano ukizidi kupamba moto

Chanzo cha picha, IDF
Israel inasema imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya kile ilichosema ni "jengo linalofanana kama la kijeshi" linalotumiwa na kundi la waasi la Hezbollah kusini mwa Lebanon.
Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu wanne waliuawa katika shambulio hilo katika mji wa Maifadoun, karibu kilomita 30 kutoka mpaka wa Israel.
Vyanzo vya usalama vililiambia shirika la habari la AFP kwamba watu hao wanne walikuwa wapiganaji wa Hezbollah. Katika jibu dhahiri, kundi hilo lilianzisha mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye miji ya kaskazini mwa Israel, na kuwajeruhi watu wawili.
Inakuja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya Israel na Hezbollah, na Iran ambayo inaunga mkono kundi hilo.
Wiki iliyopita, shambulio la anga la Israel lilimuua kamanda mwandamizi wa Hezbollah Fuad Shukr katika kitongoji cha kusini mwa mji mkuu wa Lebanon Beirut, katika kile maafisa wa Israel walichokiita "kutokomeza kwa kutegema habari za kijasusi".
Maafisa wa Israel wanasema alihusika na shambulio la roketi katika eneo la Milima ya Golan inayokaliwa na Israel mwezi uliopita na kuua watoto na vijana 12. Hezbollah imekanusha kuhusika na shambulio hilo.
Saa chache baada ya Shukr kuuawa, kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh aliuawa katika mji mkuu wa Iran Tehran - Iran ililaumu Israel kwa shambulio hilo .
Hezbollah na Iran zimeapa kulipiza kisasi juu ya vifo hivyo, na hivyo kuzua hofu kwamba mapigano ya kujibizana yanaweza kuchochea mzozo mkubwa zaidi wa kikanda.
Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani, zimewataka raia kuondoka Lebanon haraka iwezekanavyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo alisema Jumanne kwamba alikuwa anafanya kazi kuhakikisha kuwa Hezbollah haisababishi ongezeko kubwa la jibu lake kutokana na kifo cha Shukr.
Shambulio la Israel dhidi ya Maifadoun lilitekelezwa na ndege za kivita, na liliongozwa na mashirika ya kijasusi, Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema katika taarifa iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kujibu, Hezbollah ilifyatua kile ilichokiita "kundi" la ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel, na kuwajeruhi watu wawili katika mji wa kaskazini wa Mazra'a. Lakini chanzo katika kundi hilo kililiambia shirika la habari la Reuters kwamba shambulio hilo halikuwa sehemu ya majibu yake kwa kifo cha Shukr.
Rais wa Marekani Joe Biden alikutana na timu yake ya juu ya usalama wa taifa siku ya Jumatatuhuku wasiwasi wa mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel ukiongezeka.
Hifadhi ya maiti Marekani yatozwa faini ya $950m katika kesi ya miili iliyooza

Chanzo cha picha, CBS
Hifadhi moja ya maiti Marekani ambapo miili 190 iliyoharibika ilipatikana imeagizwa kulipa $950m (£746m) kwa familia za waathiriwa.
Hifadhi hiyo kwa jina Return to Nature, katika mji wa Penrose, Colorado, ilikuwa imewapa jamaa waliokuwa wakiomboleza majivu bandia badala ya mabaki ya wapendwa wao.
Jaji aliamuru malipo hayo katika kesi ya madai, lakini hakuna uwezekano wa kulipwa kwa vile wamiliki wa hifadhi hiyo, Jon na Carie Hallford, walikuwa katika matatizo makubwa ya kifedha.
Wawili hao pia hawakuhudhuria vikao. Bw Hallford yuko kizuizini, huku mkewe akiwa nje kwa dhamana.
"Sitapata hata senti kutoka kwao, kwa hivyo, sijui, inasikitisha kidogo," Crystina Page, ambaye aliajiri hifadhi hiyo ya maiti i kuchoma mabaki ya mtoto wake mnamo 2019, aliiambia Associated Press.
Bi Page, ambaye alibeba kile alichodhani ni majivu ya mwanawe kwa miaka minne kabla ya mwili wake kutambuliwa nyumbani humo , pia alisema kutofika kwa wanandoa hao mahakamani kulikuwa kama 'kofi usoni'
Nigeria: Waandamanaji wakamatwa kwa kupeperusha bendera ya Urusi

Chanzo cha picha, Saadu Labin Gusau
Maelezo ya picha, Polisi wanasema pia wamewakamata mafundi cherehani wanaodaiwa kutengeneza bendera za Urusi Takriban watu 40 wamekamatwa kaskazini mwa Nigeria kwa kupeperusha bendera ya Urusi wakati wa maandamano ya kupinga ongezeko la gharama ya maisha na kile wanachohisi ni "utawala mbaya".
Mkuu wa jeshi Christopher Musa ameonya kuwa ni "kosa la uhaini" kupeperusha bendera za mataifa ya kigeni.
Nigeria imeshuhudia maandamano ya siku sita nchini kote, ambapo takriban watu saba wameuawa na zaidi ya 700 wamekamatwa.
Waandamanaji wamekuwa wakiimba "tuna njaa", huku baadhi yao wakipigwa picha wakipeperusha bendera ya Urusi na kumuunga mkono Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, baadhi ya waandamanaji hawa wameitaka Urusi "kuwaokoa".
Hatua ya kuwakamata waandamanaji inaonekana kama jaribio la kuzuia uungwaji mkono wowote wa Urusi nchini Nigeria ambayo ni mzalishaji mkuu wa mafuta na mshirika mkuu wa madola ya Magharibi.
Nchi kadhaa katika eneo la Afrika Magharibi - ikiwa ni pamoja na jirani wa Nigeria, Niger - zimejitenga na mataifa ya Magharibi na kuelekea Urusi baada ya mapinduzi ya kijeshi ya hivi karibuni.
Serikali za kiraia zinazoungwa mkono na Ufaransa na Marekani zimepoteza umaarufu - wakosoaji walizishutumu kwa kushindwa kukabiliana na ukosefu wa usalama, rushwa na matatizo ya kiuchumi.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu aliingia madarakani Mei 2023 baada ya kushinda uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
Maelezo zaidi:
Bunge la Bangladesh lamevunjwa - Ofisi ya Rais

Chanzo cha picha, Getty Images
Bunge la Bangladesh limevunjwa, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais.
Kulivunja Bunge ilikuwa moja ya masharti yaliyotolewa na waratibu wa maandamano ya wanafunzi, ambao walikuwa wameweka makataa ya saa tisa (09:00 GMT).
Waandamanaji wa wanafunzi wamesema hawatakubali serikali inayoongozwa na jeshi, wakiongeza kuwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Muhammad Yunus amekubali kuwa mshauri mkuu wa serikali ya mpito.
Huku hayo yakijiri Chama cha Huduma ya Polisi ya Bangladesh (BPSA) kimesema kuwa maafisa wake wameanza mgomo.
"Hadi usalama wa kila polisi utakapopatikana, tunatangaza mgomo," Mamlaka hiyo ilisema katika taarifa.
BPSA ambayo inawakilisha maelfu ya maafisa wa polisi kote nchini. Ilisema kuwa zaidi ya vituo 450 vya polisi vilishambuliwa siku ya Jumatatu, katika maandamnao ya kumshinikiza Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu.
Maafisa kadhaa wa polisi pia waliuawa wakati wa maandamano hayo, kulingana na maafisa.
Idhaa ya BBC Bangla tayari ilikuwa imeripoti kuwa hakuna polisi wa trafiki wanaoonekana kwenye barabara nyingi katika mji mkuu wa Dhaka mapema Jumanne, huku wanafunzi wakionekana katika baadhi ya maeneo wakielekeza trafiki.
Soma pia:
Kamala Harris atarajiwa kumtangaza mgombea mwenza wake

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Kamala Harris atafanya kampeni katika miji saba wiki hii, akianza na mkutano wa Philadelphia Jumanne. Makamu wa Rais Kamala Harris anatarajiwa kumtangaza mgombea mwenza wake leo Jumanne, katika hatua itakayohitimisha uvumi wa ni nani atakuwa mgombea mwenza wake wakati Marekani ikielekea kwenye uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba.
Bi Harris aliwahoji washindani kadhaa wakuu huko Washington DC mwishoni mwa juma, wakiwemo Josh Shapiro, Tim Walz na Mark Kelly
Mgombea mwenza atakayemchagua ataungana naye katika ziara ya siku tano ya miji saba wiki hii huku Bi Harris akiendeleza kampeni yake katika majimbo muhimu yanayotarajiwa kushuhudia kinyang'anyiro kikali.
Kura ya maoni ya hivi punde ya kituo cha CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, inawaonyesha Bi Harris na Trump wakiwa katika kinyang'anyiro kikali kitaifa, huku Mgombea huyo mtarajiwa wa chama cha Democratic akiongoza kwa pointi moja dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump.
Maelezo zaidi:
Muhammad Yunus: Mpinzani mkuu wa Sheikh Hasina ambaye waandamanaji wanataka awe mshauri mkuu wa serikali Bangladesh

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Muhammad Yunus, ambaye waandamanaji wanataka ateuliwe kuwa mshauri mkuu wa serikali ya mpito ya Bangladesh, amekuwa akichukuliwa kwa muda mrefu na Sheikh Hasina kama mpinzani wa kisiasa.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 84, anayejulikana kimataifa kama "benki kwa maskini", anasifiwa kwa kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka kwenye umaskini kutokana na matumizi yake ya kwanza ya mikopo midogo midogo.
Prof Yunus na Benki yake ya Grameen walitunukiwa kwa pamoja Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi yao nzuri mwaka wa 2006.
Lakini Bi Hasina alikuwa amemtaja Prof Yunus mara kwa mara kama "mnyonyaji damu" wa maskini na akashutumu Benki yake ya Grameen kwa kutoza viwango vya juu vya riba.
Mwezi Januari, mahakama ya Bangladesh ilimhukumu Prof Yunus kifungo cha miezi sita jela kwa kukiuka sheria za kazi za nchi hiyo, ambazo Prof Yunus amekosoa kuwa hukumu ilichochewa kisiasa.
Unaweza kusoma;
Maandamano Bangladesh: Tunachokijua kufikia sasa

Chanzo cha picha, Reuters
Kuna hali ya sintofahamu miongoni mwa wananchi wengi wa Bangladesh kuhusu kitakachotokea baadaye, siku moja baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kulazimishwa kujiuzulu na kuikimbia nchi kufuatia maandamano makubwa.
Hasina, 76, anaaminika kuwa bado yuko katika nchi jirani ya India, lakini uvumi umeenea kwamba anaweza kuwa anajiandaa kwenda katika nchi nyingine ya kigeni.
Siku ya Jumatatu, mkuu wa jeshi la Bangladesh aliahidi kwamba serikali ya mpito itaundwa hivi karibuni, lakini hakutoa maelezo kuhusu nani anaweza kuiongoza. Viongozi wa wanafunzi wanasema hawatakubali serikali inayoongozwa na jeshi, wakishinikiza mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Muhammad Yunus kuwa mshauri mkuu wa baraza jipya la mawaziri.
Baadhi yao wamemtaka rais wa Bangladesh Mohammed Shahabuddin kulivunja bunge ifikapo saa 15:00 kwa saa za huko leo (09:00 GMT), na wameonya kwamba "watachukua hatua kali" ikiwa matakwa yao hayatatekelezwa.
Endelea kuwa nasi tunapokuletea habari za hivi punde na uchambuzi kutoka Bangladesh.
Wadukuzi wa Korea Kaskazini wanajaribu kuiba siri za nyuklia na kijeshi, Marekani, Uingereza zasema

Chanzo cha picha, Getty Images
Wadukuzi wa Korea Kaskazini wanajaribu kuiba siri za nyuklia na kijeshi kutoka kwa serikali na makampuni binafsi duniani kote, Uingereza, Marekani na Korea Kusini zimeonya.
Wanasema kundi hilo, linalojulikana kwa majina Andariel, Onyx Sleet na DarkSeoul, miongoni mwa mengine linalenga vyombo vya ulinzi, anga, nyuklia na uhandisi ili kupata taarifa za siri, kwa lengo la kuendeleza mipango na malengo ya kijeshi na nyuklia ya Pyongyang.
Kundi hilo limekuwa likitafuta habari katika sekta mbalimbali, kuanzia urutubishaji wa urani hadi mizinga, nyambizi na torpedo na limelenga Uingereza, Marekani, Korea Kusini, Japan, India na nchi nyingine, kwa mujibu wa mwandishi wa usalama wa BBC Gordon Corera.
Iinashukiwa kushambulia vituo vya anga vya Marekani, NASA na makampuni ya ulinzi.
Onyo la hali ya juu kuhusu kundi hili linaonekana kuwa ishara kwamba shughuli yao, ambayo inachanganya ujasusi na faida, inatia wasiwasi mamlaka kwa sababu ya athari zake kwa teknolojia nyeti na maisha ya kila siku.
Marekani inasema kundi hilo linafadhili shughuli zake za ujasusi kupitia operesheni dhidi ya taasisi za afya nchini humo.
Unaweza kusoma;
Ukiritimba wa Google katika utafutaji mtandaoni ni kinyume cha sheria- jaji wa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Jaji wa Marekani ameamua kwamba Google ilikwenda kinyume cha sheria ili kukandamiza washindani wake na kudumisha ukiritimba wa urambazaji mtandaoni na utangazaji unaohusiana.
Uamuzi wa kihistoria wa Jumatatu ni pigo kubwa kwa Alphabet, kampuni mama ya Google, na unaweza kurekebisha jinsi makampuni makubwa ya teknolojia yanavyofanya biashara.
Google ilishtakiwa na wizara ya Haki ya Marekani mwaka 2020 kuhusu udhibiti wake wa takribani 90% ya soko la urambazaji mtandaoni.
Ni mojawapo ya mashtaka kadhaa ambayo yamewasilishwa dhidi ya makampuni makubwa ya teknolojia huku mamlaka ya Marekani ikijaribu kuimarisha ushindani katika sekta hiyo.
Kesi hii wakati fulani imeelezewa kuwa ni tishio kwa Google na mmiliki wake kutokana na utawala wake wa utafutaji na biashara ya utangazaji mtandaoni.
Bado haijafahamika ni adhabu gani Google na Alphabet zitakabiliana nazo kutokana na uamuzi huo.
Faini au masuluhisho mengine yataamuliwa katika kesi ya baadaye.
Rais Biden akutana na maafisa usalama wa Marekani wakati hofu ya mashambulizi ya Iran ikiongezeka

Chanzo cha picha, White House/ X
Rais wa Marekani Joe Biden amekutana na timu yake ya masuala ya usalama wa taifa siku ya Jumatatu huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran dhidi ya Israel.
Bw Biden alisema alikuwa amefahamishwa kuhusu maandalizi ya kuunga mkono Israel iwapo itashambuliwa, huku Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken akisema maafisa walikuwa wakifanya kazi "usiku na mchana" ili kuzuia kuongezeka.
Mvutano uliongezeka wiki iliyopita baada ya mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh, ambapo Iran imeilaumu Israel na kuapa kulipiza kisasi "kikali".
Israel haijadai kuhusika na mauaji hayo.
Nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, pia wamewaambia raia wao kuondoka Lebanon, kukiwa na hofu kuwa Hezbollah inaweza kuchukua hatua yoyote kujibu mashambulizi.
Wakati wa mkutano wa Jumatatu, Bw Biden aliambiwa wakati na asili ya shambulio la Iran bado haijulikani, kulingana na tovuti ya habari ya Marekani ya Axios.
Siku moja kabla, Bw Blinken aliripotiwa kuwaambia viongozi wenzake wa G7 kwamba Iran na Hezbollah zinaweza kushambulia Israel ndani ya saa 24 hadi 48.
Unaweza kusoma;
Wakenya washinda medali 3 Paris 2024

Chanzo cha picha, Getty Images
Beatrice Chebet wa Kenya alishinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki mbio za mita 5,000.
Amekuwa miongoni mwa wanawake mjini Paris baada ya kushinda mbio hizo ambazo zilimfanya bingwa wa mita 1500 Faith Kipyegon kupokonywa medali ya fedha kabla ya kurejeshewa.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 24 alivuka utepe katika dakika 14 na sekunde 28.56 mbele ya Kipyegon aliyechukua nafasi ya pili.
Kipyegon awali alinyang'anywa medali yake ya fedha baada ya kudaiwa kumzuia mwanariadha wa Ethiopia Gudaf Tsegay walipogongana katika kinyanganyiro hicho cha mita 5000.
Hata hivyo, Kipyegon hatimaye alirejeshewa medali hiyo baada ya kulalamika kwa mamlaka.
Wakati huohuo bingwa wa mbio za mita 800 Mkenya Mary Moraa alishinda medali ya shaba katika fainali ya mita 800 kwa wanawake, huku Tsige Duguma wa Ethiopia akishinda fedha nyuma ya Keely Hodgkinson wa Uingereza aliyenyakuwa dhahabu katika mbio hizo.
Wanajeshi wa Marekani wajeruhiwa katika shambulizi nchini Iraq

Chanzo cha picha, Getty Images
Wafanyakazi kadhaa wa Marekani wamejeruhiwa baada ya shambulio la roketi linaloshukiwa kutokea katika kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq, maafisa wa Marekani wamesema.
Shambulio hilo limetokea huku waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akisema kuwa Mashariki ya Kati iko katika wakati mgumu baada ya mauaji ya viongozi wakuu wa Hamas na Hezbollah.
Maafisa waliambia mshirika wa BBC, CBS News kwamba uwanja wa ndege wa Al Asad magharibi mwa Iraq ulishambuliwa na kwamba bado wanatathmini uharibifu uliofanyika.
Bado hawajasema nani alitekeleza shambulio hilo.
Vyanzo vya usalama viliiambia CBS kwamba roketi mbili za Katyusha zilirushwa kwenye kambi hiyo, na kwamba moja ilikuwa imeanguka ndani ya kambi hiyo.
"Tunaweza kuthibitisha kwamba kuna tuhuma za shambulio la roketi leo dhidi ya vikosi vya Marekani na Muungano katika Al Asad, Iraq," alisema msemaji wa Idara ya Ulinzi.
"Dalili za awali zinaonesha kwamba wafanyakazi kadhaa wa Marekani walijeruhiwa.
Wafanyakazi wanafanya tathmini ya uharibifu wa baada ya shambulio, "msemaji huyo aliongeza. Haijulikani ni wafanyikazi wangapi wa Marekani walijeruhiwa.
Afisa mkuu wa jeshi la Marekani alisema hakuna majeraha makubwa, kama kupoteza miguu na mikono, ambayo yameripotiwa wakati huu, na hakuna wahudumu waliouawa.
Rais Joe Biden alifahamishwa kuhusu shambulio hilo, afisa wa Ikulu ya White House alisema.
Katika taarifa yake kwenye ukurasa wa X, Bw Biden alisema yeye na makamu wa rais Kamala Harris walipewa taarifa kuhusu "yanayojiri katika Mashariki ya Kati."
Unaweza kusoma;
Shangwe nchini Bangladesh baada ya Waziri Mkuu kuikimbia nchi

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina amejiuzulu baada ya wiki kadhaa za maandamano mabaya dhidi ya serikali, na kukomesha zaidi ya miongo miwili ya kutawala siasa za nchi hiyo.
Bi Hasina, 76, alikimbia nchi, akiripotiwa kutua India siku ya Jumatatu.
Umati wa watu walioshangilia walijitokeza barabarani kusheherekea taarifa hizo, huku wengine wakivamia ikulu ya waziri mkuu, wakiripotiwa kupora na kuharibu sehemu za makazi yake ya zamani.
Saa chache baada ya Bi Hasina kujiuzulu, Rais Mohammed Shahabuddin aliamuru kuachiliwa kwa waziri mkuu wa zamani Khaleda Zia aliyefungwa jela na wanafunzi wote waliokuwa wamezuiliwa wakati wa maandamano ya hivi karibuni dhidi ya mfumo wa upendeleo wa nafasi za kazi serikalini.
Rais Shahabuddin alisema alikuwa ameongoza mkutano wa wakuu wa jeshi na wawakilishi wa kisiasa.
Alisema serikali ya mpito itaundwa, uchaguzi mpya utaitishwa na amri ya kutotoka nje ya kitaifa kuondolewa.
Mjini Dhaka siku ya Jumatatu, polisi na majengo mengine ya serikali yalishambuliwa na kuchomwa moto.
Waandamanaji walijaribu kubomoa sanamu ya kiongozi wa uhuru Sheikh Mujibur Rahman, baba yake Bi Hasina.
Vikosi vya jeshi na polisi vilisambazwa katika jiji lote. Huduma ya simu za mkononi iliripotiwa kukatika kwa saa kadhaa kabla ya kurejeshwa.
Siku ya Jumatatu, waandamanaji walionekana wakibeba samani kutoka kwenye makazi ya waziri mkuu.
Makumi waliripotiwa kuuawa siku ya Jumatatu, ingawa idadi kamili bado haijafahamika. Shirika la habari la AFP liliripoti idadi ya waliofariki kuwa 66, ingawa shirika la habari la Dhaka Tribune lilisema kuwa watu 135 wameuawa.
Unaweza kusoma;
