Yafahamu baadhi ya mashambulizi makubwa yaliyoshuhudiwa na Iran katika miaka ya hivi karibuni

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Shambulizi la mapema mwaka huu la kundi la Islamic State liliua makumi ya watu karibu na kaburi la Qassem Soleimani
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kundi la Hamas limesema kuwa mkuu wa ofisi yake ya kisiasa, Ismail Haniyeh, aliuawa katika shambulio la angani la Israel lililomlenga katika mji mkuu wa Iran, Tehran.

Kwa mujibu wa habari kutoka Tehran, kiongozi huyo wa Hamas aliuawa alfajiri ya Jumatano.

Haniyeh alikuwa akishiriki katika sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.

Israel na Hamas wamekuwa wakipigana katika Ukanda wa Gaza tangu wapiganaji hao walipoanzisha mashambulizi dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana .

Wakati maafisa wa Iran wakiishutumu Israel au Marekani kwa kuhusika na baadhi ya matukio hayo, makundi ya Kiislamu yamedai kuhusika na mengine.

Pia unaweza kusoma

Je, Iran imeshuhudia mashambulizi gani katika miaka ya hivi karibuni?

  • Mwezi Novemba 2011, mlipuko katika handaki la kuhifadhi silaha la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Irani nje kidogo ya Tehran uliua watu 36, akiwemo Jenerali Hassan Moghadam, mkuu wa mipango kikosi hicho. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran, mlipuko huo ulitokana na operesheni ya Marekani na Israel kulenga mpango wa nyuklia wa Iran.
  • Mnamo Oktoba 2013, kundi la upinzani la Sunni la Iran liitwalo Jaish al-Adl lilidai kuhusika na mauaji ya walinzi 14 wa mpaka wa Iran karibu na mpaka na Pakistan. Jaish al-Adl, shirika lisilojulikana sana, lilisema shambulio dhidi ya walinzi wa mpakani lilikuwa ni kulipiza kisasi madai ya "mauaji" ya Iran nchini Syria na "vitendo vikali" vya Wasunni nchini Iran.
  • Mwezi Aprili 2015, kundi lenye silaha ambalo halijatambuliwa liliwaua wanajeshi wanane wa Iran kwenye mpaka na Pakistan, maafisa wa Iran walisema. Tukio hilo lilitokea katika mkoa wa mpaka wa Sistan-Polchestan, maafisa walisema.
  • Ali Asghar Mirshekari, naibu gavana, alinukuliwa akisema kuwa washambuliaji walirusha makombora yaliyokuwa yakishikiliwa kwa mkono wakati wa makabiliano na walinzi wa mpaka. Aliongeza kuwa washambuliaji walikimbia na kurudi Pakistan.
  • Mwezi Juni 2017, takriban watu 12 waliuawa na 42 kujeruhiwa katika mashambulizi pacha kwenye Majlis (bunge) na kaburi la Ayatollah Khomeini huko Tehran. Mashambulizi yote mawili yalitekelezwa na watu wenye silaha na washambuliaji wa kujitoa mhanga. Mwanamke mmoja alijilipua kwa mkanda uliokuwa na kilipuzi ndani ya eneo la kaburi hilo, na mshambuliaji mwingine aliuawa na polisi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani. Kundi la Islamic State lilidai kuhusika na mashambulizi yote mawili.
  • Mwezi Septemba 2018, takriban watu 30 waliuawa na kadhaa kujeruhiwa katika shambulio kwenye gwaride la kijeshi katika mji wa kusini-magharibi mwa Iran wa Ahvaz, kulingana na shirika rasmi la habari la Iran. Waziri wa mambo ya nje wa Iran wakati huo, Mohammad Javad Zarif, alilaumu "utawala wa kigeni" unaoungwa mkono na Marekani kwa shambulio hilo, lakini kundi la Islamic State baadaye lilidai kuhusika na shambulio la Ahvaz. Shambulio hilo lilitokea katika Siku kuu ya Jeshi la Kitaifa la Iran, ambayo ni kumbukumbu ya Baghdad kutangaza vita dhidi ya Tehran (1980-1988) mwezi Septemba 22.
  • Mwezi Februari 2019, shambulio la bomu liliwalenga wanajeshi wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran katika mkoa wa Chestan-Baluchestan, sawa na maadhimisho ya miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu, na kuua watu 27. Iran ilishutumu baadhi ya nchi zenye utajiri wa mafuta katika eneo hilo (bila kutaja zipi) kwa kuhusika na shambulio hilo. Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema wakati huo kwamba "mizizi mikuu ya ugaidi katika eneo hili ni Marekani, Israel, na baadhi ya nchi za eneo la mafuta zinazotoa msaada wa kifedha kwa magaidi," kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran (IRNA).
  • Mwezi Novemba 2020, mwanasayansi mashuhuri wa nyuklia wa Irani Mohsen Fakhrizadeh aliuawa karibu na Tehran katika shambulio la msafara wake. Fakhrizadeh, mmoja wa wanasayansi mashuhuri wa Iran katika uwanja wake, alikuwa rasmi mkuu wa idara ya utafiti na maendeleo ya Wizara ya Ulinzi, na Iran imeishutumu Israel kwa kuhusika na kifo chake.
  • Mwezi Aprili 2021, mlipuko ulitokea katika kituo cha nyuklia cha Natanz, na kukizima kwa muda. Iran ilimtambua mshukiwa wa shambulio hilo ambaye alikuwa ametoroka nchini, lakini ikashutumu Israel kwa kupanga shambulio hilo.
  • Mwezi Oktoba 2022, shambulio kwenye kaburi la Shah Cheragh huko Shiraz, lililodaiwa na ISIS, liliwaua watu 13.
  • Mnamo Agosti 2023, mtu mmoja aliuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika kile ambacho vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa ni shambulio la "kigaidi" kwenye kaburi moja katika mji wa Shiraz. Shirika rasmi la habari la IRNA liliripoti wakati huo kwamba mtu mwenye silaha alijaribu kuingia kwenye hekalu la Shah Cheragh na kuwafyatulia risasi wageni kabla ya kutengwa.
  • Mwezi Desemba 2023, polisi 11 na wafanyikazi wa jeshi waliuawa katika shambulio kwenye kituo cha polisi katika mji wa kusini mashariki mwa Irani wa Rask. Televisheni ya serikali ilishutumu kundi linalotaka kujitenga la Jaish-e Adl kwa kuhusika na shambulio hilo.
  • Januari iliyopita, makumi ya watu waliuawa katika milipuko miwili ya bomu karibu na kaburi la Jenerali wa Iran, Qassem Soleimani, katika kumbukumbu ya mwaka wa nne wa kuuawa kwake na Marekani, na kundi la Islamic State lilidai kuhusika na shambulio hilo.
pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah