Je, Kamala Harris ana uwezo na sifa za kumshinda Trump?

Chanzo cha picha, Getty Images
Chini ya saa 24 baada ya Joe Biden kutangaza kuwa anaachana na azma ya kugombea urais kwa muhula wa pili, sasa njia ya Makamu wa Rais Kamala Harris kupata uteuzi wa urais kupitia chama cha Democratic iko wazi.
Kupata uteuzi linaweza kuwa jambo rahisi. Changamoto kubwa zaidi - ni kumshinda mgombea mteule wa Republican, Donald Trump mwezi Novemba.
Kulingana na kura za maoni za hivi karibuni, Bi Harris yuko nyuma ya Trump kwa asilimia ndogo tu – kama ilivyokuwa kwa Biden kabla ya tangazo lake la kihistoria.
Wanasiasa wakubwa wa chama chake wanamuunga mkono Harris, kama vile Spika wa zamani wa Bunge, Nancy Pelosi – mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa.
Fursa ya makamu wa rais dhidi ya Trump, ni kuvutia wapiga kura wa msimamo wa kati katika majimbo yanayobadilika-badilika na kuongeza ushawishi katika ngome za Democratic.
Uimara wa Harris kwa Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa timu ya kampeni ya Harris, makamu wa rais alichangisha zaidi ya dola za kimarekani milioni 80, katika michango mipya ndani ya saa 24 tangu tangazo la Biden la kujiondoa.
Kiasi kikubwa zaidi cha pesa kuchangishwa siku moja na mgombea yeyote katika mzunguko wa uchaguzi huu.
Kiasi hicho ni pamoja na karibu milioni 100 anayoirithi kutoka katika hazina ya ufadhili ya Biden-Harris, hazina inayompa msingi imara wa kifedha kwa kampeni zijazo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Harris, ikiwa atakuwa mteule, ataondoa mojawapo ya mashambulizi makubwa ya Republican dhidi ya mpinzani wao; umri wake.
Makamu wa rais, ana umri wa miaka 59, atakuwa mgombea mwenye nguvu na anayeweza kutoa hoja thabiti kwa chama chake. Anaweza pia kuugeuza umri wa Trump miaka 78 dhidi yake, kwani atakuwa mtu mzee zaidi kugombea urais.
Harris pia anaweza kupata uungwaji mkono kutoka kwa wapiga kura weusi, kura za maoni zinaonyesha walikuwa wakiachana na Biden katika miezi ya hivi karibuni.
Ikiwa anaweza kupata uungwaji mkono na hao na kuungwa mkono na jamii nyingine za wachache na wapiga kura vijana – (muungano wa ushindi wa Barack Obama 2008 na 2012).
Hayo yanaweza kumsaidia kupata uungwaji mkono dhidi ya Trump katika majimbo machache ambayo yataamua uchaguzi wa mwaka huu.
Kazi yake kama mwendesha mashtaka pia inaweza kumwongezea sifa. Alifanya kazi nzuri ya utekelezaji sheria kabla ya uteuzi wa makamu wa rais 2019. Na hilo linaweza kumsaidia katika kampeni dhidi ya Trump.
Makamu wa rais pia amekuwa mpiga kampeni mkuu kuhusu haki ya uavyaji mimba, jambo ambalo limethibitika kuwa mojawapo ya masuala yenye nguvu zaidi kwa chama cha Democratic katika chaguzi za hivi karibuni.
Udhaifu wa Harris

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika utawala wa Biden, alipewa jukumu la kushughulikia mzozo wa wahamiaji kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.
Hatua zilizoshindwa na taarifa zenye makosa - ikiwa ni pamoja na mahojiano ya Juni 2021 na mtangazaji wa NBC News, Lester Holt - yaliharibu msimamo wake na kufungua mashambulizi ya wahafidhina.
"Uhamiaji ni eneo dhaifu kwa Wana-demokratic. Hili ni suala muhimu sana kwa wapiga kura wanaoishi katika vitongoji hivyo. Wanaamini mfumo wetu wa uhamiaji haujasimamiwa ipasavyo,” anasema Mbunge wa zamani wa Democratic kutoka New York, Steve Israel.
Kampeni za Trump pia zitajaribu kubadilisha historia yake akiwa mwendesha mashtaka - kwa kuangazia rekodi zake na kushambulia maamuzi yake ya zamani kama mwendesha mashtaka.
Mbio zake za kuwa mgombea wa urais wa Democratic 2020 zilishindwa. Aliongoza vyema mapema, lakini mseto wa mahojiano yasiyoeleweka, ukosefu wa maono yenye ufafanuzi wa wazi na kampeni iliyosimamiwa vibaya, yalimfanya aache mbio hizo hata kabla ya mchujo ya awali.
Labda fursa kubwa kwa Harris ni kwamba, yeye sio rais aliye madarakani. Anaweza kujitenga na baadhi ya sera zisizopendwa za Biden.
Tarajia juhudi kubwa za Warepublican kumpaka matope Harris, kwamba ni hatari kuwa rais.
Harris amepiga hatua kubwa katika siasa za Marekani - sasa lazima aonyeshe kuwa anaweza kushindana.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












