Biden amuunga mkono Kamala Harris kuwa mgombea urais wa Democratic

"Leo nataka kutoa usaidizi wangu kamili na uidhinishaji kwa Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu'

Muhtasari

  • Kifundo cha nywele za mwanzilishi wa fani ya uuguzi chauzwa kwa pauni 3,500
  • Mahakama ya Bangladesh yafutilia mbali nafasi nyingi za kazi baada ya machafuko
  • Mwanasiasa wa upinzani Kenya, Raila Odinga awataka vijana kufanya mazungumzo na serikali
  • Donald Trump ameuambia mkutano kuwa 'alipigwa risasi kuitetea demokrasia'
  • Israel yawashambulia waasi wa Houthi nchini Yemen baada ya ndege isiyo na rubani kupiga Tel Aviv

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Yusuf Jumah ; Mhariri: Athuman Mtulya

  1. Kwaheri

    Tunakomea hapo kwa leo.Tukutane kesho Jumatatu alfajiri kwa habari na matukio zaidi kutoka barani afrika na kote duniani.Alamsiki

  2. Bill Clinton na mkewe Hillary wamuunga mkono Harris

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bill Clinton, rais wa zamani wa Marekani, na mkewe Hillary Clinton, ambaye alishindana na Trump mwaka 2016, wamemuunga mkono Kamala Harris kuwa mgombeaji wa chama cha Democratic

    Katika taarifa iliyotumwa kwenye X, wanasema watafanya "chochote wawezacho kumuunga mkono".

    "Sasa ni wakati wa kumuunga mkono Kamala Harris na kupigana kwa kila kitu tulicho nacho ili kumchagua," wanaongeza.

    Wanandoa hao wakuu wa siasa za Amerika huchukua sauti ya pingamizi dhidi ya Trump.

    "Tumepitia misukosuko mingi, lakini hakuna kitu ambacho kimetufanya kuwa na wasiwasi zaidi kwa nchi yetu kuliko tishio linaloletwa na muhula wa pili wa Trump," wanasema.

    "Ameahidi kuwa dikteta siku ya kwanza, na uamuzi wa hivi majuzi wa Mahakama yake ya Juu ya Utumishi utamtia moyo zaidi kuvunja Katiba."

  3. Tutashinda - Harris

    TH

    Chanzo cha picha, EPA

    Tumesikia hivi punde kutoka kwa Makamu wa Rais Kamala Harris, ambaye ameungwa mkono na Biden kuchukua uteuzi wachama cha Democratic katika uchaguzi wa urais mnamo Novemba.

    Anaandika: "Nitafanya kila niwezalo kuunganisha Chama cha Kidemokrasia-na kuunganisha taifa letu-ili kumshinda Donald Trump na ajenda yake kali ya Project 2025."

    “Tuna siku 107 kabla ya siku ya uchaguzi. Pamoja, tutapigana. Na kwa pamoja tutashinda."

    Harris asema ni 'taadhima' kuungwa mkono na Biden

    Zaidi sasa kutoka kwa Kamala Harris, ambaye ametoa taarifa baada ya kujua kwamba Joe Biden amehitimisha azma yake ya kuchaguliwa tena na kumuidhinisha kuwa mgombeaji wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Novemba.

    Anamshukuru Biden kwa "uongozi wake wa ajabu" na "miongo kadhaa ya huduma kwa nchi yetu".

    Akisimulia jinsi alivyokutana na rais, anaendelea kuandika juu ya "uaminifu na uadilifu... upendo wake kwa nchi yetu na watu wa Amerika".

    Anaelezea uamuzi wake wa kusitisha ombi lake la kuchaguliwa tena kama "tendo la kujitolea na la kizalendo" na anasema "amepata taadhima" ya kuidhinishwa na Biden.

  4. Obama amsifu mmoja wa 'marais wenye athari kubwa' wa Marekani

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    "Joe Biden amekuwa mmoja wa marais wa Marekani wenye atahri kubwa, na vile vile rafiki mpendwa na mshirika wangu," anaandika Barack Obama kwenye X.

    "Leo, pia tumekumbushwa - tena - kwamba yeye ni mzalendo wa hali ya juu," Obama anaendelea kusema .

    Obama alimteua Biden kama naibu wake wakati akiwa madarakani. Lakini katika kipindi cha hivi majuzi cha shinikizo kwa Biden, inasemekana alijiunga na Wanademokrasia wengine wakuu kumtaka kuzingatia msimamo wake.

    Obama hajatangaza waziwazi kumuunga mkono Harris

    Kauli ya Rais wa zamani Barack Obama inatoa pongezi kwa Rais Joe Biden, ambaye alihudumu kwa uaminifu kama makamu wake wa rais kwa miaka minane.

    Lakini jambo moja linaonekana wazi: haungi mkono Kamala Harris. Badala yake, anasema: "Nina imani ya ajabu kwamba viongozi wa chama chetu wataweza kuunda mchakato ambao mteule bora ataibuka." Biden hakukubali. kumuunga mkono Harris katika taarifa yake ya kwanza, lakini alifanya hivyo saa moja baadaye katika chapisho kwenye X.

  5. Hali ilivyo nje ya Ikulu ya Marekani

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bernd Debusmann JrAkiripoti kutoka Ikulu ya Marekani

    Nimefika hivi punde katika Ikulu ya White House ambako, licha ya habari hizo nzito , tukio hilo ni la kawaida la kile ambacho mtu anaweza kupata Jumapili yoyote.

    Makundi makubwa ya watalii - baadhi ya Wamarekani , wengine wa kigeni - wanazunguka nje. Wengi wanaonekana kutojua kilichotokea.

    "Wow," mzee mmoja kutoka Texas aliniambia katika mshangao mkubwa . "Siwezi kuamini kwamba alifanya hivyo."

    Wachache, hata hivyo, walikuja mara moja kama walivyosikia. Moja kwa moja mbele ya Ikulu ya White House, mwanamume na mwanamke wote wameshikilia mabango yaliyochorwa kwa haraka.

    Ya mwanamke inasma "Asante Joe", wakati ya mwanaume imeandikwa "Kwaheri Joe". Anasema hatampigia kura Trump, lakini anafurahi kwamba Biden anamaliza kampeni yake.

    Nilipokuwa nikiondoka, mwanamume mwenye ndevu aliyevalia kofia ya "Trump 2024" alimsogelea mwanamke huyo, akiwashutumu Wanademokrasia kwa "kuwapuuza wapiga kura wao wenyewe" kwa kumshinikiza Biden ajiuzulu.

    "Naweza kusema ninachotaka," alimjibu kwa hasira. "Niko hapa kumshukuru."

  6. Biden atamatisha kampeni yake: Nini kimetokea

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Katika dakika 90 zilizopita, Rais Joe Biden ametangaza kuwa anamaliza kampeni yake ya kuchaguliwa tena katika Ikulu ya White House.

    Inafuatia wiki za shinikizo kutoka ndani ya chama chake, zlizochochewa na matokeo yake katika mdahalo ulioyumba dhidi ya Donald Trump mwishoni mwa Juni.

    • Alisema uamuzi wake ni "kwa maslahi ya chama changu na nchi" na kwamba imekuwa heshima kubwa zaidi maishani mwake kuhudumu kama rais wa Marekani.
    • Biden alisema atamaliza muda uliosalia wa muhula wake katika Ikulu ya White House na ameidhinisha Makamu wa Rais Kamala Harris kuchukua nafasi ya kwanza ya mgombea urais wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa Novemba.
    • Wapinzani wake wa kisiasa, akiwemo Spika wa Bunge Mike Johnson, wamemtaka ajiuzulu mara moja. Mpinzani wa Biden , Donald Trump, anasema Mdemocrat huyo "hafai kuhudumu"
    • Lakini Biden amepokea pongezi kutoka kwa watu mashuhuri ndani ya chama chake, kama vile Gavana wa California Gavin Newsom, na zaidi - kama vile muigizaji wa Star Wars Mark Hamill, ambaye alisema "alirudisha uaminifu, utu na uadilifu" kwa White House baada ya Trump.
  7. Biden mmoja wa marais wenye athari kubwa katika historia, asema Newsom

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Joe Biden "ataingia katika historia kama mmoja wa marais wenye athari na wasio na ubinafsi," anasema Gavana wa California Gavin Newsom.

    Akiandika kwenye X, anasema Mdemocrat mwenzake huyo "amepigana kwa bidii kwa watu wanaofanya kazi na kutoa matokeo ya kushangaza kwa Wamarekani wote".

    Newsom ni mojawapo ya majina ambayo yametolewa kama mrithi anayetarajiwa wa Biden. Unaweza kusoma juu yake na wengine hapa

  8. Jinsi Biden alivyoporomoka kisiasa chini ya mwezi mmoja

    Juni 27 Mjadala wa Urais ambapo majibu ya Biden mara nyingi hayakuwa na mashiko yaliwaacha wengi wakijiuliza juu ya kufaa kwake kusalia katika ofisi ya raisi.

    28 Juni Biden alitaraji kuwatoa wate staka kwa hotuba ya kampeni jimboni North Carolina ambapo alisema: "Sizungumzi vizuri kama nilivyokuwa nikizungumza awali. Sifanyi mjadala kama nilivyokuwa nikifanya. Lakini najua ninachojua: najua jinsi ya kusema ukweli.

    Tarehe 2 Julai Lloyd Doggett ndiye Mwakilishi wa kwanza kutoka chama cha Democratic kumtaka Biden ajiuzulu - na baadaye aliungwa mkono na wengine kutoa wito huo

    5 Julai Katika mahojiano na George Stephanopolous wa running ya ABC, Biden anasema ni “Mwenyezi Mungu” pekee ndiye anayeweza kumshawishi asigombee urais na hatafanya mtihani wa kutahmini hali yake ya ufahamu.

    8 Julai Baada ya wikendi ya kutokubaliana ndani ya chama, Biden anaeleza kupitia kipindi cha habari Morning Joe "Siendi popote" na anawatumia wafuasi wa chama chale barua ndefu ya kuomba umoja.

    10 Julai Spika wa zamani wa Bunge Nancy Pelosi anakiambia kipindi cha Morning Joe "ni juu ya rais kuamua kama atagombea,"akiweka wazi kuwa suala hilo halijatatuliwa. George Clooney amble ni mwigizaji maarufu na mfadhili wa chama cha Democratic anamtaka Biden ajiuzulu, huku Peter Welch anakuwa seneta wa kwanza wa Democratic kumtaka ajiondoe.

    11 Julai Mwishoni mwa mkutano wa kilele wa Nato huko Washington,Biden anamwita Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kama "Rais Putin" na Makamu wa Rais Harris kama Trump.

    Tarehe 13 Julai Presha ya kisiasa inaondoka kwa muda mfupi kutoka kwa Biden wakati Trump anapigwa risasi sikioni katika jaribio la kumuua.

    Tarehe 17 Jula Biden alipimwa na kukutwa na Covid na kusitisha kampeni ili kujitenga.Mwanademokrasia mkuu Adam Schiff anatoa wito kwa Biden "kupitisha mwenge."Wabunge wengine wanachukua msemo huo.

    18 Julai Kipande cha picha ya video kinasambaa kwa Biden akisahau jina la Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin katika mahojiano ambapo pia anasema angeacha kuwania urais ikiwa "hali ya kiafya itaibuka." Ripoti zilizovuja za viongozi wa bunge wakizungumza kuhusu kuondoka kwenye kinyang'anyiro hicho huku Obama akisema ana nafasi ndogo ya kushinda.

    Julai 19 Biden anatangaza kuwa atarejea kwenye kampeni wiki ijayo. Idadi ya Wanademokrasia wa Bunge wanaodai kujiondoa kwake imefikia 30 na wafadhili wakuu kuongeza joto.

    Tarehe 20 Julai Trump awashutumu Wanademokrasia kwa kutojua mteule wao ni nani.

    Leo katika taarifa,Biden anajiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais. Anaidhinisha Makamu wa Rais Kamala Harris kuchukua nafasi ya kwanza ya tikiti ya chama hicho

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

  9. Maafisa wa chama cha Democratic wafanya mkutano wa dharura

    Mkutano wa dharura wa maafisa wakuu wa Kamati ya Kitaifa ya chama cha Democratic (DNC) unaendelea sasa hivi, mshirika wetu wa Marekani CBS inaripoti.

  10. Biden lazima ajiuzulu sasa, asema Spika wa Bunge

    Majibu yanaendelea kufurika - ikiwa ni pamoja na kutoka kwa Spika wa Bunge, Mike Johnson.

    "Ikiwa Joe Biden hafai kugombea urais, hafai kuhudumu kama rais," mwanachama huyo wa Republican anaandika kwenye X.

    "Lazima ajiuzulu mara moja," Johnson anaongeza, akiendelea kusema kwamba siku ya kupiga kura katika uchaguzi wa Marekani, 5 Novemba, "haiwezi kufika hivi karibuni".

  11. Biden kusalia kama rais hadi uchaguzi wa Novemba

    Mengi zaidi i kutoka kwa taarifa ya Biden sasa.

    Anasema ingawa anajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, hajiuzulu kama rais wa Marekani na atasalia Ikulu ya Marekani kwa miezi sita ya mwisho ya muhula wake.

    "Ninaamini ni kwa manufaa yangu kwa chama changu na nchi kwa mimi kujiuzulu na kuzingatia tu kutimiza wajibu wangu kama rais kwa muda uliosalia wa muhula wangu," anaandika.

    Kama ukumbusho, uchaguzi wa rais wa Marekani ni tarehe 5 Novemba - mshindi anahudumu kwa miaka minne.

  12. Biden hana uwezo wa kuwa rais, Trump asema

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Katika dakika chache zilizopita, Donald Trump ametoa maoni kuhusu uamuzi wa Joe Biden kujiondoa, akichapisha kwenye jukwaa lake Truth Social: "Joe Biden aliyepotoshwa hakufaa kugombea urais, na kwa hakika hafai kuhudumu na hakuwahi kamwe!"

    "Alipata nafasi ya Urais tu kwa uwongo, Habari za Uongo.....

    "Wale wote waliokuwa karibu naye, ikiwa ni pamoja na Daktari wake na Vyombo vya Habari, walijua kwamba hakuwa na uwezo wa kuwa Rais, na hakuweza," anaandika.

    "Tutateseka sana kwa sababu ya urais wake, lakini tutarekebisha uharibifu aliofanya haraka sana. TUIFANYE MAREKANI KUWA KUBWA TENA!"

  13. Biden ameitanguliza nchi kwanza - Schumer

    Kiongozi wa Wengi katika Seneti ya Democrat Chuck Schumer anasema leo inaonyesha Rais Joe Biden ni "mzalendo wa kweli na Mmarekani mkuu".

    Katika chapisho kwenye X, anasema: "Joe Biden amekuwa sio tu rais na kiongozi mkuu bali ni binadamu wa ajabu sana.

    "Uamuzi wake bila shaka haukuwa rahisi, lakini alitanguliza nchi yake, chama chake na mustakabali wetu mbele."

  14. Taarifa kamili: Uidhinishaji wa Biden wa Kamala Harris

    Kuna taarifa ya Biden juu ya Harris , ambayo aliichapisha kwenye X muda mfupi uliopita:

    Wanademokrasia wenzangu, nimeamua kutokubali kuteuliwa na kuelekeza nguvu zangu zote katika majukumu yangu ya Urais kwa muda wote uliosalia.

    Uamuzi wangu wa kwanza kama mteule wa chama mnamo 2020 ulikuwa kumchagua Kamala Harris kama Makamu wangu wa Rais.

    Na umekuwa uamuzi bora zaidi ambao nimefanya.

    Leo nataka kutoa uungwaji mkono na uidhinishaji wangu kamili kwa Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu. Wanademokrasia - ni wakati wa kuungana na kumshinda Trump.

    Hebu tufanye hili

  15. Habari za hivi punde, Biden amuidhinisha Kamala Harris

    th

    Chanzo cha picha, EPA

    Joe Biden ametangaza hivi punde kwamba anamuidhinisha Kamala Harris kuwa mteule wa chama cha Democratic kwa kinyang'anyiro cha urais wa Marekani 2024, katika chapisho kwenye X.

    "Leo nataka kutoa usaidizi wangu kamili na uidhinishaji kwa Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu. Democrats - ni wakati wa kushirikiana na kumshinda Trump. Hebu tufanye hivi," anaandika kwenye X.

  16. Rais Ruto asema “yatosha” hatokubali maandamano tena Kenya

    Rais wa Kenya William Ruto

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Kenya William Ruto amesema kwamba hatokubali tena ,”kushurutishwa na maandamano” akitaja kwamba “yametosha.”

    Rais Ruto aliyekuwa akihutubia wananchi katika kaunti ya Bomet, alikohudhuria ibada ya jumapili katika kanisa la Africa Gospel Church, amesema kwamba vijana walimtaka kufutilia mbali mswada wa fedha, hatua aliyokubaliana nayo na vile vile kufanya mabadiliko serikalini kama walivyotaka.

    “ Kuendelea mbele tutalilinda taifa. Tutalinda maisha na mali. Tutawazuiwa wauaji, na waporaji mali. Tutazuia uvunjaji wa sheria kwa sababu Kenya ni taifa lilaoheshimu demokrasia.” Alisema Rais Ruto mapema leo.

    Matamshi yake yanatolewa siku chache baada ya vijana kumtaja kama mtu ambaye si mkweli pindi tu alipotangaza nusu ya baraza lake jipya la mawaziri ambapo amewarejesha mawaziri sita waliohudumu katika baraza lake la kwanza lililodonolewa kazini Alhamisi Julai 18.

    Vijana waliokerwa na orodha hiyo wametangaza maandamano ambayo wamesema yatalenga maeneo muhimu ikiwemo Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jommo Kenyatta . Awali alitangaza kuandamana katikati mwa jiji la Nairobi na kukusanyika katika bustani la Uhuru hadi kufikia idadi ya watu milioni tano kabla ya kuelekea Ikulu ya Rais lakini hilo halikufanyika Alhamisi Julai 25 ambapo taifa lilisalia kushuhudia utulivu japo polisi walikuwa mwengi katika miji mikuu.

    Huku akisema kwamba changamoto zinzaoikumba taifa yanapaswa kutatuliwa kupitia njia za Kidemokrasia, Rais Ruto ametoa onyo kwa wale wanaopanga maandamano ya vijana kwamba: “Munataka tumalize hii kitu, na tusimamishe hii vita? Na tusimamishe maandamano ya maafa? Na maandamano ya kuharibu mali ya watu? Nitasimamisha hali hiyo.” Alisema RAis Ruto.

    Awali Rais Ruto aliishutumu shirika moja lisilo la kiserikali kutoka Marekani na kutaja kwamba linafadhili kupanga maandamano, hali ambayo shirika hilo imekanusha.

    Mapema wiki jana wizara ya mambo ya kigeni Kenya iliiandikia barua Wakfu wa Ford kuitaka kueleza shughuli zake , ambapo ikaijibu kwa barua na kusema kwamba kamwe haihusiki na mipango yanayoonekana kuwa kinyume na sheria na maadili yake ya kutetea haki.

    “Enough is Enough! Si imetosha hii maneno? Walisema tusipitishe mswada wa fedha, Mimi nimewacha Finance Bill. Nikawaita wakasema hawtaki kuja kuzungumza, tukajadiliana kwa X Space wakatoroka huko hawakuweko. Wakaniambia wanataka mazungumzo, nikaitisha mazungumzo, wamekataa. Wanaedndelea kusema hawana sura, wala kabila, mimi nimewambia sasa my friends, Nimewapa nafasi kila mmoja kujieleza , lakini haiwezi kuendelea hivi,”

    Mapema jumapili hii, kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliwataka vijana kubuni kikundi kitakachojadiliana na serikali kwa pamoja na wadau wengine nchini Kenya ili kuoata suluhu kwa matatizo yanayowakumba.

    Unaweza kusoma;

  17. Waandaaji wa maandamano Uganda 'wanacheza na moto', Rais Museveni asema

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa madarakani tangu 1986

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewaonya watakaoandamana nchini humo kwamba watakuwa “ wanacheza na moto” ikiwa wataendelaa na mipango yao ya kufanya maandamano dhidi ya ufisadi hadi bungeni siku ya Jumanne Julai 23.

    Vijana nchini Uganda wamekuwa wakiandaa maandamano kwenye mitandao ya kijamii wakitaka ufisadi kumalizwa serikalini.

    Wameshawishika na maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika katika nchi jirani ya Kenya, ambapo vijana wenzao wamekuwa wakiandaa maandamano ambayo yalimlazimu Rais William Ruto kusitisha mipango ya kuongeza kodi.

    Katika taarifa iliyopeperushwa kwenye runinga nchini Uganda, Rais Museveni aliwaonya waandaaji kwamba mpango wao wa kufanya maandamano hautakubalika wala kustahmiliwa.

    “Tuko mbioni tukijaribu kuzalisha mali…Nanyi mnataka kutusumbua. mnacheza na moto kwa sababu hatutakubali mtusumbue,” alisema.

    Bwana Museveni amelaumiwa na wakosoaji wake kwa kuingoza Uganda kiimla, tangu kuchukua mamlaka mwaka 1986, lakini wafuasi wake wamempongeza kwa kudumisha amani katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

    Rais huyo pia amewashutumu wanaopanga maandamano hayo kuwa “wanashirikiana na mashirika na watu kutoka mataifa ya kigeni” kuleta vurugu nchini Uganda. Ila hakueleza zaidi kuhusu madai hayo.

    Polisi nchini humo, hapo awali walikuwa wametangaza kwamba walikata kutoa idhini kwa watu waliotaka kuandamana hadi nje ya majengo ya bunge siku ya Jumanne.

    Mmoja wa viongozi wa maandamano hayo aliambia kituo cha Habari cha AFP kwamba wataendelea na mpango wao.

    “Hatuhitaji idhini ili kufanya maandamano ya amani. Ni haki tuliopatiwa kwenye katiba,” Louez Opolez alinukuliwa akisema.

    Serikali za Marekani na Uingereza zimeweka vikwazo dhidi ya Spika wa bunge la taifa la Uganda Anita Annet Amiong mapema mwaka huu baada yay yeye kudaiwa na kushtumiwa kuhusika katika ufisadi.

    Among alikanusha kuhusika na uvunjaji wa sheria.

    Vikwazo hivyo vinazuia kusafiri hadi Uingereza na Marekani. Uingereza pia, imesema kwamba itaweka vikwazo vya umiliki wa mali dhidi yake. Amekanusha kuhusika katika kuvunja sheria.

    Uingereza aidha imeweka vikwazo vya aina hiyo dhidi ya maafisa wawili serikalini- mawaziri ambao walifutwa kazi na Rais Museveni baada ya wao kukabiliwa na mashataka ya ufisadi.

    Mary Goretti Kitutu na Agnes Nandutu wameshtakiwa mahakani kuhusiana na kashfa inayohusisha maelfu ya mabati ya kujengea nyumba ambayo ilitarajiwa kupeanwa kwa jamii maskini katiak eneo la kaskazini mashariki la Karamoja.

    Wote wamekanusha mashtaka hayo.

  18. Marekani yaponea chupuchupu kupata kipigo cha Sudani Kusini katika mechi ya maandalizi ya Olimpiki

    LeBron James alifikisha pointi 23 na kusaidia USA kutoka na ushindi mwembamba

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani ilirejea kifua mbele baada ya kuwa nyuma na alama 16 kuzuia kushindwa na Sudan Kusini kwa alama 101 – 100.

    Katika mechi ya maandalizi ya mashindano ya Olimpiki iliyochezwa jijini London, Sudan kusini iliidhibiti vikali Marekani iwapo Marekani ingeshindwa ingekuwa hali ambayo haijawahi kutokea katika historia ya taifa hilo.

    Sudan Kusini iliongoza kwa vikapu 58-42 kuingia robo ya pili ya michuano hiyo, kabla ya kuongoza kwa alama 14 wakati wa mapumziko, katika mechi ya kujiandaa kwa Olimpiki iliyochezwa katika uwanja wa O2 Arena.

    Marekani ilirejea katika robo ya tatu ikiwa kifua mbele kwa vikapu 16-0 , na kuwa na alama tano juu ya Sudan Kusini, lakini wapinzani wao walirejea kileleni kwa pointi moja kukiwa kumesalia sekundi 20 ili robo hiyo ikamilike.

    Marekani ilijikakamua na kupata ushindi muhimu kwa alama moja kukiwa kumesalia sekunde nane huku Sudan Kusini ikishindwa kurejea na kujipatia ushindi ambao ungekuwa wa kihistoria.

    Marekani inalenga kujipatia dhahabu ya tano mtawalia katika mchezo wa mpira wa kikapu kwenye mashindano ya Olimpiki huku Sudan kusini ambayo imeorodheshwa nambari 33 ulimwenguni ikishiriki katika mashindano yake ya kwanza ya Olimpiki.

    Timu ya wanaume ya Marakenai ina wachezaji 12 wanaoshiriki kwenye ligi kuu ya marekani NBA baadhi yao wakiwa wachezaji nyota kwenye ligi hiyo. Sudan Kusini ina wachezaji 4 pekee ambao wanacheza kwenye ligi hiyo.

  19. Kifundo cha nywele za mwanzilishi wa fani ya uuguzi chauzwa kwa pauni 3,500

    Kifundo cha nywele za Florence Nightingale

    Chanzo cha picha, TENNANTS AUCTIONEERS

    Kifungu cha nywele cha Florence Nightingale kimeuzwa kwa bei ya zaidi ya pauni 3,500 katika mnada uliofanyika North Yorkshire.

    Nywele hizo, ambazo zimethibitishwa kuwa za Nightingale ambaye alikuwa mwanzilishi wa taaluma ya uuguzi katika karne ya 19, zilitarajiwa kuuzwa kati ya pauni elfu mbili na pauni elfu tatu.

    ZIliuzwa kwa pamoja na Saini yake ambayo ilikuwa imeandikwa kwenye karatasi ndogo.

    Kampuni yam nada Tennants auctioneers, imesema kwamba bidhaa zinazouzwa katika mnada wa Leyburn zilikuwa zinamilikiwa na dada yake Nightingale.

    Florence Nightingale alifahamika kama ‘ mwanamke mwenye taa ya mwanga’ wakati wa vita vya Crimea

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jody Beighton, mhusika wa minada na mwenye kukagua ubora wa bidhaaa ameeleza kifungu hicho cha nywele kuwa kitu nadra sana.

    Nightingale, anatajwa kama mwanzilishi wa fani ya uuguzi. Ali alifahamika kama ‘ mwanamke mwenye taa ya mwanga’ wakati wa vita vya Crimea.

    Vita hivyo vilizuka mnamo 1853. Uingereza, Ufaransa, Uturuki na Sardinia ziliungana kukabiliana na Urusi.

    Nightingale aliombwa kuwaleta pamoja wauguzi 38 ambao wangewasaidia madaktari kuwahudumia wanajeshi katika hospitali ya kijeshi nchini Uturuki.

    Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa wanawake kukubaliwa kuhudumu katika jeshi.

    Baada ya wao kuwasili huko, Nightingale aliipanga timu yake kuwajibikia majukumu ya usafi wa hospitali na kuhakisha kwamba wanajeshi waliangaliwa vyema.

    Alibuni chuo cha wauguzi cha Nightingale katika hospitali ya St, Thomas mjini London mnamo 1860.

    Tasisi hiyo ilikuwa ya kwanza ya aina yake ambayo ilitoa mafunzo kwa wauguzi ambao walitumwa kote Uingereza kuhudumu.

    Alifariki mnamo 1910 akiwa mwenye umri wa miaka 90.

  20. Mahakama ya Bangladesh yafutilia mbali nafasi nyingi za kazi baada ya machafuko

    Wanawake

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mahakama ya juu nchini Bangaldesh imetupilia mbali mfumo wa serikali ya nchi hiyo uliotenga kiasi fulani cha ajira serikalini kwa familia za waliopogania uhuru wa nchi hiyo, jambo ambalo limechangia maandamano makali yaliyoongozwa na vijana nchini humo.

    Kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo ya juu kimetupilia mbali amri ya mahakama ya chini ambayo mapema mwezi jana ilirejesha mpango huo ambao ulionekana kuwazuia wengine kupata ajira na kusababisha maandamano ambapo watu mia moja wamefariki.

    Mwanasheria Mkuu AM Amin Uddin amewaleleza wanahabari nchini humo kwama mahakama ya juu zaidi imesema kwamba amri ya mahakama kuu ya awali ilikuwa sio halali.

    Aidha amesema pia, ‘ asilimia tano ya kazi zilizopo katika utumisha wa umma yatasalia kuwafaa Watoto wa waliopigania uhuru wa taifa hilo, huku asilimia mbili ikiwandea wengine wote.’

    Serikali ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina ilikuwa imeondoa mpango huo mnamo 2018 lakini mahakama kuu nchini humo ikairejesha mwezi jana, hali iliyozusha maandamano kila siku tangu kutolewa.