‘Nilimuitia mwanangu kifo’

Chanzo cha picha, Maryam Musa
Na Buhari Muhammad
BBC News, Abuja
Maandamano ya kupinga ugumu wa maisha na njaa nchini Nigeria yaliyoanza Agosti 1 yamesababisha maafa watu kadhaa na mmoja wao alikuwa Usman Ismail Muhammad mwenye umri wa miaka 21.
Mama yake alikuwa amesisitiza ajiunge naye kwa maandamano katika jimbo la Kano, kaskazini magharibi mwa Nigeria. Lakini aliuawa kwa kupigwa risasi siku hiyo hiyo.
Familia yao ya watu 20 ilikuwa inatatizika kuishi na kama mtoto wa kwanza wa kiume, majukumu mengi yalikuwa mabegani mwa Usman. Familia ilijumuisha wake watatu wa baba yake, ambaye wakati mmoja alikuwa mwenyekiti wa chama cha siasa katika ngazi ya serikali ya mtaa.
Ingawa Usman alikuwa amepanga kujiunga na maandamano, mama yake alipokuwa akitoka nyumbani Alhamisi asubuhi, hakuwa tayari. Lakini aliendelea kumpigia simu, kwani kupinga ndiyo njia pekee ya kueleza kusikitishwa kwao na uchumi unaozidi kuwa mbaya.
"Nilimwita mwanangu kwenye uwanja wa maandamano, nisichojua ni kwamba nilikuwa nikimwitia kifo chake," Maryam, mama yake, aliiambia BBC. Aliendelea kupiga simu ili kuhakikisha kuwa ameondoka nyumbani na kujiunga naye kwenye maandamano ya #EndBadGovernance.

Chanzo cha picha, MARYAM MUSA
Siku moja kabla, "Alitoa moja ya viatu vyake, suruali ya jeans ya bluu na shati nyeupe," kwa maandalizi ya maandamano, alisema. Siku ya maandamano, walipaswa kujiunga na msafara wa waandamanaji wengine waliokuwa wakielekea katika jumba la serikali ya jimbo la Kano.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Huko, walitarajia kuwasilisha malalamiko yao kwa gavana wa jimbo, au yeyote ambaye angejitokeza kuwasikiliza. Kulingana naye, muda si mrefu walifika, walikuwa wamesimama nje ya nyumba ya serikali pamoja na waandamanaji wengine wakati maafisa wa usalama walipoanza kurusha vitoa machozi.
Hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kumuona Usman.
“Kulikuwa na moshi wa vitoa machozi na risasi zikaanza, kusikika niliogopa sana hivyo tukakimbia,” alisema Maryam ambaye alisaidiwa kufika nyumbani kwa pikipiki. Kabla habari hizo hazijamfikia, alihisi mtoto wake amekufa katika janga alilolikimbia.
“Tangu wakati ufyatuaji risasi ulipotokea, nilikuwa na maumivu moyoni. Na nilijua tu kwamba kuna jambo baya limetokea, "alisema.
Katika mazungumzo yake ya mwisho na Usman kabla ya maandamano, alimweleza siri kuhusu jinsi maisha yalivyokuwa magumu kwa familia na jinsi zililivyopita siku nne bila kupika chakula.
"Alinihakikishia kwamba shida zetu zitakuwa jambo la zamani punde tu atakapokuwa mfanyakazi wa afya," Maryam anakumbuka. Lakini Usman hawezi tena kutimiza ahadi zake kwake.
Usman alikuwa amesomea Stashahada ya uuguzi katika shule ya uuguzi ya Jimbo hilo, lakini hakuweza kupata kazi katika sekta ya afya, mama yake alimtafutia kazi kazi ya kuuza vitambaa sokoni na kaka yake.
Katika miaka miwili akifanya kazi na mjomba wake, Usman alikuwa akipata mshahara wa kila mwezi wa N45,000 (dola 30), nusu yake ililenga kutoa chakula kwa familia. Kulingana na Maryam, pia aliwasaidia ndugu zake kwa kuwalipia karo ya shule.
Siku ya Jumatano - siku ya maandamano - wakati mshahara wake ulipolipwa, alilipa baadhi ya deni ambalo familia hiyo ilidaiwa kutokana na kununua chakula. Salio la mshahara wake lilikuwa mfukoni alipopigwa risasi na kuuawa. Lakini mwili wake ulipoletwa, pesa zote hazikuwepo, mama yake alisema.
Walipouchunguza mwili wake, alikuwa amepigwa risasi sehemu mbili: mgongoni na begani mwake.
"Kifo chake kitakuwa kovu katika moyo wangu milele," Maryam alisema, "Tunataka haki kwake kutoka kwa serikali".
Siku ya Jumapili, Rais wa Nigeria Bola Tinubu, katika hotuba ya televisheni, alikiri kutokea kwa maafa katika maeneo mbalimbali ya nchi kufuatia maandamano hayo. Lakini jeshi la polisi nchini limesita kukiri kupoteza maisha, hasa kutokana na risasi zilizopigwa na maafisa wake.
Wakati BBC ilipowasiliana na Abdullahi Haruna Kiyawa, msemaji wa polisi wa jimbo la Kano, ili kutoa maoni yake kuhusu mauaji ya Usman, alisema operesheni hiyo ilifanywa kwa pamoja na vyombo vingine vya usalama. Alisema jambo hilo lilifanya iwe vigumu kwake kubainisha ni nani hasa alihusika na mauaji ya kijana huyo.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












