Israel itajibu baada ya Hamas kutoa mabaki ya miili ya mateka yasio sahihi - Netanyahu

Hamas inadai inajitahidi kupata na kutambua mabaki yote, lakini inakosa vifaa vinavyohitajika kutokana na uharibifu mkubwa katika Gaza.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Mariam Mjahid

  1. Serikali ya kijeshi ya Madagascar yateua Baraza la Mawaziri wengi wakiwa raia

    G

    Chanzo cha picha, Randrianian/X

    Serikali ya Madagascar inayoongozwa na wanajeshi, ambayo ilipata madaraka mwanzoni mwa mwezi huu, imetangaza baraza la mawaziri siku ya Jumanne lililojumuisha mawaziri wengi raia, ikiwemo baadhi ya wapinzani wakuu wa rais aliyefukuzwa, Andry Rajoelina.

    Uteuzi huu unaashiria hatua muhimu katika mzozo wa kisiasa wa Madagascar, huku wanajeshi wakiimarisha madaraka yake.

    Kwa mujibu wa serikali ya mpito ya sasa imesema itashughulikia changamoto za kiuchumi na mgawanyiko wa kisiasa.

    Wanajeshi walifanya mapinduzi mwanzoni mwa mwezi huu baada ya Rajoelina kukimbia kutoka kisiwa cha Bahari ya Hindi kufuatia wiki za maandamano yaliyoongozwa na vijana.

    Kanali Michael Randrianirina alichukua wadhifa wa rais wa muda mfupi siku chache baadaye.

    Hadi sasa, hakujakuwa na maandamano ya kupinga uteuzi wa baraza la mawaziri.

    Soma pia:

  2. Tunaamini kuwa suala la Bahari ya Shamu ni la kisheria, kihistoria na kiuchumi - Abiy Ahmed

    h

    Chanzo cha picha, Abiy Ahmed /FB

    Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amewaomba viongozi wakuu wa dunia ikijumuisha Marekani, China, Urusi, na Umoja wa Ulaya kusaidia juhudi za Uhabeshi za kupata upatikanaji wa Bahari Nyekundu, akieleza kuwa suala hilo ni la lazima na la kimsingi kwa taifa hilo.

    Akizungumza na wabunge siku ya Jumanne, Bw. Abiy alisisitiza kuwa Uhabeshi inapendelea mazungumzo ya amani na tayari imeomba ushiriki wa kimataifa ili kusaidia kupata suluhisho la kidiplomasia.

    Aidha, alihoji kisheria mchakato wa kihistoria uliosababisha Ethiopia kuwa bila bandari kufuatia uhuru wa Eritrea mwaka 1993.

    Kabla ya hapo, Ethiopia ilikuwa na upatikanaji wa Bahari Nyekundu kupitia bandari kama Assab, ambayo baadaye ilijumuishwa Eritrea baada ya kujitenga.

    Tangu wakati huo, Ethiopia imekuwa ikitegemea kwa kiasi kikubwa bandari za jirani yake mdogo Mashariki, Djibouti, kwa karibu zote za bidhaa zake zinazoingizwa na kusafirishwa nje ya taifa hilo.

    Matamshi ya hivi karibuni ya Bw. Abiy yamezua mvutano na Eritrea, ambayo inaona mapendekezo yoyote ya kuangalia upya hali ya ardhi kama tishio.

    Kama sehemu ya juhudi zake za kupata upatikanaji wa baharini, Uhabeshi ilisaini makubaliano ya awali na Somaliland mwanzoni mwa mwaka huu.

    Mkataba huo, uliokusudiwa kuanzisha uwepo wa jeshi la majini na upatikanaji wa bandari, ulionekana na Somalia kama kitendo cha ukatili, kwani inachukulia Somaliland kama sehemu ya eneo lake la kiasili.

    Makubaliano hayo yalisababisha mvutano wa kikanda na kuibua hofu ya kutokuwa na utulivu katika Pembe ya Afrika.

    Ingawa makubaliano bado hayajafutwa rasmi, hatma yake bado haijulikani.

    Mvutano unaoendelea kati ya Addis Ababa na Asmara umeibua hofu kuwa vita vipya vinaweza kuibuka kati ya nchi jirani hizi mbili.

    Soma pia:

  3. Ni kipi kinachoendelea Sudan baada ya RSF kudhibiti el Fasher

    Mamia kwa maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mamia kwa maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea

    Watafiti nchini Marekani wanasema wamepata ushahidi wa mauaji ya halaiki, baada ya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kuudhibiti mji wa el-Fasher kutoka kwa jeshi la Sudan.

    Maabara ya Utafiti wa Kibinadamu katika Chuo Kikuu cha Yale inasema picha za satelaiti zinaonyesha makundi ya kile kinachoonekana kuwa miili ya binadamu karibu na magari ya RSF na ukuta unaozunguka jiji hilo.

    Watafiti hao wanasema kuwa picha hizo pia zinathibitisha kuwa RSF imekamata nyadhifa zote za jeshi.

    Pia wameona ushahidi wa shughuli za nyumba hadi nyumba na vizuizi vipya vya barabarani kote jijini.

    Ripoti ya Yale inaonya kwamba mtindo wa ghasia unaonekana kulengwa kikabila sawa na ukatili mkubwa uliorekodiwa hapo awali katika maeneo mengine ya Darfur tangu mzozo huo uanze Aprili 2023.

    Pia inasema maendeleo ya RSF, pamoja na upatikanaji wa kibinadamu wenye vikwazo, "huongeza hatari ya uhalifu dhidi ya ubinadamu au hata mauaji ya kimbari".

    Wakati huo huo, familia za waathiriwa wa Sudan zimezungumza na idhaa ya BBC.

    "Tumeshuhudia jamaa zetu wengi wakiuawa," mwanamume mmoja ambaye alipoteza mawasiliano na wanafamilia huko El-Fasher aliambia Idhaa ya BBC.

    Anasema walikusanywa sehemu moja na kuuawa kufuatia kutekwa kwa jiji hilo.

    Mawasiliano "yamekatika kabisa" katika Jimbo la Darfur Kaskazini, mkazi huyo anasema, kwa hivyo hajui nini kimetokea kwa wanafamilia ambao bado wako hai.

    Soma pia:

  4. ChatGPT yatoa takwimu kuhusu watumiaji wanaoonyesha dalili za mawazo ya kujitoa uhai

    gg

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kampuni ya OpenAI imechapisha takwimu mpya zinazokadiria idadi ya watumiaji wa ChatGPT wanaoonyesha dalili zinazoweza kuashiria dharura za kiafya ya akili, ikiwamo wazimu, kurukwa na akili na mawazo ya kujitoa uhai.

    OpenAI imesema kuwa takriban asilimia 0.07 ya watumiaji wake hai katika kipindi cha wiki moja walionyesha dalili hizo, na kuongeza kuwa mfumo wake wa akili bandia (AI) umewekwa ili kutambua na kutoa majibu kwa mazungumzo nyeti yanayohusiana na hali hizi.

    Ingawa kampuni inasisitiza kuwa matukio haya ni nadra sana, wakosoaji wameonyesha wasiwasi kuwa hata asilimia ndogo inaweza kumaanisha mamia ya maelfu ya watu kutokana na idadi kubwa ya watumiaji wa ChatGPT, ambao hivi karibuni walifikia milioni 800 wa watumiaji hai kwa wiki, kama alivyosema Mkurugenzi Mtendaji Sam Altman.

    Ili kukabiliana na changamoto hii, OpenAI imeanzisha mtandao wa wataalamu wa afya ya akili na teknolojia kutoka duniani kote ili kutoa ushauri wa kitaalamu.

    Katika tukio jingine lililotokea Agosti mwaka huu, mtu aliyeshutumiwa kwa mauaji na kujiua katika eneo la Greenwich, Connecticut, alitoa rekodi za masaa ya mazungumzo yake na ChatGPT, ambayo yanaonekana kuwa chanzo cha kuongezeka kwa mawazo potofu aliyokuwa nayo.

    Profesa Robin Feldman, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sheria na Ubunifu wa AI katika Chuo Kikuu cha California, anasema, “Watumiaji wengi wanakumbwa na kurukwa na akili inayohusiana na matumizi ya AI kutokana na chatbots kuunda udanganyifu thabiti wa uhalisia.”

    Anasisitiza kuwa OpenAI inastahili sifa kwa uwazi wake na juhudi za kupambana na tatizo hili, lakini pia anabainisha kuwa “hata onyo la kina linaweza kutolewa, mtu aliye katika hatari ya kiafya ya akili huenda asiweze kulizingatia.”

    Soma pia:

  5. Netanyahu asema Israel itajibu baada ya Hamas kuwakabidhi miili ambayo sio ya mateka wao

    h

    Chanzo cha picha, EPA

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametangaza kuwa Israel itachukua hatua baada ya Hamas kutoa mabaki ya binadamu ambayo hayakuwa ya yoyote ya wafungwa 13 wa Israeli waliopotea, akisema ni ukiukaji wa mpango wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

    Mabaki hayo yalitambulika kuwa ni ya Ofir Tzarfati, ambaye tayari mwili wake ulikutwa mwanzoni mwa vita.

    Hamas ilidai inatekeleza matakwa ya kusitisha mapigano na inajitahidi kupata na kutambua mabaki yote, lakini inakosa vifaa vinavyohitajika kutokana na uharibifu mkubwa katika Gaza.

    Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem, alisema kundi hilo litaendelea na juhudi zake zote kuhakikisha mabaki ya mateka yaliyobaki yote yanarudishwa.

    Wakati huo huo, milipuko bado inaendelea kusikika Gaza huku majeshi ya Israeli yakikaribia kuharibu mahandaki ya Hamas, ambapo Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema takriban 60% ya mahandaki bado ipo.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Tanzania yaongoza uchumi wa kanda, Kenya na Rwanda zikibaki nyuma - ripoti ya AU

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uchumi wa Kenya umeendelea kusuasua ikilinganishwa na ule wa Tanzania katika eneo la Afrika Mashariki, hasa kutokana na utegemezi mkubwa wa mauzo ya bidhaa ghafi nje ya nchi jambo linalokwamisha ukuaji wa uchumi na kuongeza kiwango cha umaskini.

    Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Ujumuishaji wa Bara la Afrika 2025 iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU).

    Ripoti hiyo inaonyesha kuwa ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla unafanya chini ya wastani wa bara katika juhudi za kuimarisha uchumi wake kupitia ubunifu, uongezaji thamani wa bidhaa na upanuzi wa sekta za uzalishaji.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kenya inajipata ikifanya vibaya zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku uchumi wake ukiendelea kutegemea zaidi mauzo ya bidhaa ghafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani.

    Hali hiyo, ripoti inasema, imeathiri maendeleo ya viwanda na sekta ya uzalishaji nchini, jambo linalochangia upungufu wa ajira, kipengele muhimu katika kupunguza ukosefu wa ajira na umaskini.

    Alama ya utofauti wa biashara katika EAC (0.3920) imebaki chini kidogo ya wastani wa bara la Afrika (0.4072).

    Biashara nchini Kenya bado inatawaliwa na mauzo ya bidhaa ghafi (asilimia takribani 68 ya mauzo nje), huku mauzo ya bidhaa za viwandani (0.3420) yakiwa nyuma ya uagizaji wake (0.5986).

    Kwa upande wa utofauti wa biashara, Tanzania inaongoza kwa alama 0.4457, ikifuatiwa na Burundi, kisha Kenya.

    Nchi zinazofanya vibaya zaidi ni Uganda (0.2848), Rwanda (0.2241) na Sudan Kusini (0.2116), hali inayoonyesha pengo kubwa kati ya wingi wa biashara na kiwango cha ubunifu wa uchumi.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa biashara ya bidhaa za kati bado ni dhaifu, huku mitandao ya uzalishaji wa kikanda ikiwa haijakomaa ipasavyo.

    Wataalamu wa Umoja wa Afrika wanapendekeza kuwa jumuiya ya Afrika mashariki EAC ichukue hatua mahsusi za kupunguza pengo la biashara kwa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara ndani ya eneo, kukuza uzalishaji wa viwandani, na kuhamasisha uongezaji thamani wa bidhaa.

    “Kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, hasa katika sekta za usindikaji wa mazao na viwanda vidogo, kunaweza kusaidia kupunguza pengo kati ya uagizaji na uuzaji nje. Uboreshaji wa njia kuu za usafirishaji kama vile Mombasa na Dar es Salaam ni muhimu kwa kuongeza ujumuishaji wa kiuchumi,” inasema ripoti hiyo.

    Aidha, ripoti inabainisha kuwa nchi dhaifu kama Somalia na Sudan Kusini zinahitaji msaada maalumu unaojumuisha uwekezaji katika miundombinu na ushirikiano wa kiusalama, ili kuwezesha ushiriki wao kamili katika ujumuishaji wa kiuchumi wa bara.

    Soma pia:

  7. Habari za hivi punde, 11 wafariki katika ajali ya ndege pwani ya Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Social Media

    Ndege iliyokuwa na watu 11 imeanguka katika eneo la kaunti ya Kwale, pwani ya Kenya.

    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA) Emile Arao amethibitisha kwamba ndege hiyo, nambari ya usajili 5Y-CCA, iliyokuwa na watalii ilikuwa ikielekea Kichwa Tembo eneo la Maasai Mara kutoka Diani kabla ya kuanguka.

    Picha zinazoonekana kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha ndege hiyo ikiwaka moto.

    Kupitia taarifa iliyotumwa na serikali kwa vyombo vya habari,mabaki ya ndege hiyo yalipatikana katika Kijiji cha Tsimba Golini, Kata ya Matuga, Kaunti ya Kwale.

    Kwa mujibu wa serikali ya Kenya ndege hiyo iliharibiwa kutokana na kishindo cha anguko hilo kilichosababisha moto na kuteketeza ndege hiyo.

    Kufuata masharti ya Kiambatisho cha 13 cha Mkataba wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), watafiti kutoka Idara ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege (AAID) wametumwa kwenye eneo la ajali kuanza uchunguzi wa kina wa moja kwa moja kuhusu mazingira yaliyozunguka tukio hili la kusikitisha.

    Akizungumza kuhusu tukio hili, Waziri wa Uchukuzi wa Kenya alisema:

    “Serikali inahuzunika kwa vifo vya wale waliopoteza maisha katika ajali hii. Usalama wa anga unabaki kipaumbele chetu cha juu, na tumejizatiti kuhakikisha uchunguzi huu unafanywa kwa uwazi, kwa kina na kwa uhuru.”

    Serikali ya Kenya inawahakikishia wananchi kuwa hatua zote muhimu zitatumika kudumisha viwango vya juu zaidi vya usalama wa anga, na kuhakikisha kwamba matokeo ya uchunguzi huu yatachochea hatua zinazohitajika za kimaendeleo na kiasili ya usalama wa ndege.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Jeshi la Sudan lapoteza mji muhimu wa el-Fasher kwa wanamgambo wa RSF

    ,

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mkuu wa jeshi la Sudan amethibitisha kujiondoa kwa jeshi kutoka ngome yake ya mwisho ya magharibi ya el-Fasher baada ya Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kutangaza kudhibiti mji huo.

    Katika hotuba ya televisheni, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alisema ameidhinisha kuondoka eneo hilo ili kukabiliana na "uharibifu wa kimfumo na mauaji ya raia".

    Alisema amekubaliana na viongozi wa eneo hilo "kuondoka na kwenda mahali salama ili kuwalinda raia waliosalia na wengine wa jiji kutokana na uharibifu".

    Umoja wa Mataifa umeonyesha wasiwasi kuhusu ripoti za ukatili uliofanywa na RSF katika siku za hivi karibuni, na umetoa wito wa uwepo wa njia salama kwa raia walionaswa.

    Soma zaidi:

  9. Mashambulizi ya Ukraine yalenga Moscow kwa usiku wa pili mfululizo, Urusi inasema

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ukraine iliilenga Moscow kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwa usiku wa pili mfululizo, wizara ya ulinzi ya Urusi na meya wa Moscow walisema Jumanne.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema katika taarifa yake vitengo vyake vya ulinzi wa anga viliharibu ndege 17 za Ukraine usiku kucha, ikiwa ni pamoja na moja iliyokuwa ikielekea Moscow na 13 katika eneo la Kaluga ambalo linapakana na mkoa wa Moscow kaskazini mashariki mwake.

    Meya wa Moscow Sergei Sobyanin alisema kwenye mtandao wa Telegram kwamba huduma za dharura zilitumwa kwenye eneo ambapo ndege isiyo na rubani iliyokuwa ikielekea Moscow ilianguka.

    Hakukuwa na ripoti za uharibifu, lakini Urusi ni mara chache sana imezungumzia athari kamili za mashambulizi ya Ukraine ndani ya eneo lake.

    Vikosi vya ulinzi wa anga vya Russia viliharibu ndege tatu zilizosalia zisizo na rubani katika eneo la Bryansk, ambalo linapakana na Ukraine upande wa magharibi na eneo la Kaluga kaskazini mashariki mwake.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Uchaguzi Mkuu Tanzania 2025: Upigaji kura wa mapema unaendelea Zanzibar

    .

    Upigaji kura wa mapema unafanyika leo 28/10/2025 huko Zanzibar kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa Oktoba 29.

    Zoezi hili maalum la kupiga kura na la kipekee kwa Zanzibar, linaruhusu watendaji wa umma kama polisi na maafisa wa uhamiaji, maafisa wa uchaguzi, na wahusika wachache wa kawaida walio na idhini kutoka kwa tume ya uchaguzi kupiga kura mapema.

    Mpangilio wa kupiga kura ya mapema ulioanzishwa kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi wa 2020, imekuwa chanzo cha ubishani.

    Chama kikuu cha upinzaji, ACT Wazalendo, kinadai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hutumia mchakato huo kushawishi matokeo, kikidai CCM inatumia fursa hiyo kufanya ujanja kwenye uchaguzi.

    "Hakuna haja ya kuweka siku mbili tofauti za kupiga kura; siku moja inatosha kwa kila mtu kupiga kura," alisema Othman Masoud Othman, mgombea wa rais wa chama cha Wazalendo.

    Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetupilia mbali madai haya kwa kusema kuwa hayana msingi na yamekusudia kupotosha umma.

    "Kura hii inafanyika kulingana na sheria na imewekwa kuhakikisha kuwa wafanyikazi muhimu wa uchaguzi - kama maafisa wa usalama na maafisa wa uchaguzi ambao watakuwa kazini wakati wa uchaguzi mkuu – wanapata fursa ya kutekeleza haki yao ya kupiga kura," alisema Thabit Idarous Faina, mkurugenzi wa Zanzibar Tume ya Uchaguzi.

    Vyama kadhaa vya kisiasa vitashiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, na kinyang’anyiro kikali kinatarajiwa kuwa kati ya chama tawala CCM na Upinzani ACT Wazalendo.

    Zanzibar ina historia ya uchaguzi unaokumbwa na msukosuko ambao miaka ya nyuma uligeuka kuwa mbaya na baadaye ukachochea kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ili kupunguza mvutano wa kisiasa.

    Matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar yanatarajiwa kutangazwa ndani ya saa 24 baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Alassane Ouattara wa Ivory Coast ashinda muhula wa nne kwa kishindo

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara amechaguliwa kwa muhula wa nne kwa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa marudio, kulingana na matokeo ya muda yaliyotangazwa Jumatatu, matokeo ambayo yalitarajiwa kwa kiasi kikubwa baada ya wapinzani wake wakuu kuonekana kutokuwa na ushawishi.

    Alassane Ouattara mwenye umri wa miaka 83 alipata asilimia 89.77% ya kura zilizopigwa.

    Mtangulizi wake, Laurent Gbagbo, alikataa kukiri kushindwa katika kinyang'anyiro kilichopita, na kusababisha vita vya miezi minne vilivyoua takriban watu 3,000.

    Waziri wa zamani wa Biashara Jean-Louis Billon, ambaye alikubali kushindwa na Ouattara siku ya Jumapili, alipata asilimia 3.09% ya kura, huku mke wa rais wa zamani Simone Gbagbo akipata asilimia 2.42%, kulingana na matokeo yaliotolewa kwenye televisheni ya serikali na Ibrahime Coulibaly-Kuibiert, rais wa tume ya uchaguzi.

    Simone Gbagbo alimpigia simu Ouattara siku ya Jumatatu kumpongeza kwa ushindi wake, chanzo kiliiambia Reuters.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Kimbunga Melissa: Jamaica inajizatiti kukabili dhoruba kali zaidi duniani ya 2025

    .

    Chanzo cha picha, Octavio Jones/Reuters

    Watu watatu tayari wamefariki nchini Jamaica wakati ikijiandaa na dhoruba kali zaidi duniani mwaka huu - na pengine dhoruba kali zaidi kuwahi kurekodiwa katika kisiwa hicho - huku wataalamu wa hali ya hewa wa Marekani wakionya kuhusu hali "mbaya na ya kutishia maisha".

    Na kasi ya upepo ya hadi 175mph (282km/h), Kimbunga Melissa ni dhoruba ya kitengo cha tano - nguvu ya juu zaidi. Inazidi kuongezeka na inatarajiwa kutua katika kisiwa cha Karibea mapema Jumanne.

    Kimbunga hicho kimesemekana kusababisha vifo vinne nchini Haiti na Jamhuri ya Dominika, pamoja na maisha yaliyopotea huko Jamaica.

    Wataalamu wanaonya kwamba mwendo wa polepole wa kimbunga Melissa unaweza kumaanisha mvua kubwa ya muda mrefu katika baadhi ya maeneo, na hivyo kuongeza hatari ya mafuriko mabaya na maporomoko ya ardhi.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Mwandishi wa habari wa Uingereza Sami Hamdi azuiliwa na mamlaka ya Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

    Mwandishi wa habari wa Uingereza na mchambuzi wa vyombo vya habari Sami Hamdi, mkosoaji mkubwa wa Israeli, amekamatwa na Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha wa Marekani (ICE).

    Akiwa katika ziara ya kuzungumza Marekani mwishoni mwa juma, Hamdi alizuiliwa na maafisa wa ICE na viza yake ikabatilishwa, msemaji wa Idara ya Usalama wa Nchi (DHS), Tricia McLaughlin, alitangaza siku ya X Jumapili.

    Hamdi yuko chini ya ulinzi wa ICE akisubiri kufurushwa nchini humo, aliongeza.

    Wizara ya Mambo ya Nje na DHS wanadai kuwa Hamdi anaunga mkono ugaidi na ni tishio kwa usalama wa taifa, huku kundi la utetezi wa Waislamu likisema analengwa kisiasa kinyume na haki yake ya uhuru wa kujieleza.

    "Tumesema hapo awali, na tutasema tena: Merekani haina jukumu la kuwakaribisha wageni wanaounga mkono ugaidi na kudhoofisha usalama wa Wamarekani," Wizara ya Mambo ya Nje ilisema kwenye X katika chapisho kuhusu kuzuiliwa kwa Hamdi.

    Idara hiyo iliongeza kuwa itaendelea kubatilisha viza za watu wanaojihusisha na shughuli hizo.

  14. Uchaguzi Tanzania 2025: Huduma za usafiri kusitishwa kati ya Dar es Salaam na Zanzibar siku ya uchaguzi mkuu

    .

    Chanzo cha picha, TANZANIA

    Huduma za kivuko kati ya mji wa kibiashara wa Tanzania wa Dar es Salaam na Zanzibar zitasimamishwa Oktoba 29, 2025, wakati nchi hiyo itakapokuwa na uchaguzi mkuu.

    Waendeshaji pekee, Azam Marine na Zan Fast Ferries wametangaza kuwa hakuna feri zitakazoendesha shughuli zake katika mwelekeo wowote hadi Oktoba 30.

    Katika taarifa tofauti, makampuni hayo mawili yamesema uamuzi wa kusimamisha huduma hizo ulifanywa ili kuwezesha ushiriki wa wapiga kura katika uchaguzi.

    Vivuko vinavyoendeshwa na wawili hao, husafirisha karibu abiria 10,000 kila siku kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.

    Mabrouk Hussein, msafiri wa kawaida kati ya maeneo hayo mawili, aliiambia BBC, "Nashangaa. Kwa nini iwe hivyo? Itakuwaje ikiwa mtu anahitaji kusafiri kwa ajili ya mazishi au matibabu?

    Hii si haki, inaonekana ina madhumuni ya kisiasa. Kwa nini sasa? Sio kila mtu anapenda kupiga kura.

    Baadhi ya mabasi kusimamisha huduma

    Baadhi ya makampuni ya mabasi ya umbali mrefu pia yametangaza kuwa huduma za kwenda na kutoka Dar es Salaam zitasitishwa.

    Siku ya uchaguzi, baadhi ya mabasi hayataendesha hadi miji mikubwa kama Mwanza, Tarime, Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Bukoba na Kigoma.

    Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimesema kusimamishwa kwa shughuli za usafiri kunalenga kuwawezesha wafanyakazi wa usafirishaji na abiria kupiga kura zao.

    Hata hivyo, Shirika la Haki za Abiria limekosoa uamuzi huo na kudai kuwa shirika la wamiliki limeshindwa kuzingatia wajibu wa kijamii na familia.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Israel yapokea maiti ambayo Hamas inasema ni mateka aliyeachiliwa Gaza

    ,

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Israel imepokea, kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu, jeneza ambalo Hamas inasema lina mwili wa mateka mwingine aliyeachiliwa huko Gaza.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema wanajeshi wake wamechukua jeneza kutoka Gaza na kurejesha mwili Israel, ambapo uchunguzi wa kitaalamu utatumika kutambua mabaki hayo.

    Iwapo watathibitishwa kuwa ni wa mateka, Hamas itakuwa imewarudisha Waisraeli 16 kati ya 28 waliokufa na raia wa kigeni iliyokuwa ikiwashikilia kabla ya kuanza kwa usitishaji mapigano wiki mbili zilizopita.

    Makabidhiano ya hivi punde yalikuja baada ya serikali ya Israel kusema kuwa imeruhusu mwanachama wa Hamas kuingia katika eneo ndani ya Gaza linalodhibitiwa na IDF kusaidia wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu na wafanyakazi wa Misri kuwatafuta mateka waliobakia waliokufa.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya tarehe 28/10/2025.