AI: Kwa nini wanawake wa China wanaitegemea ChatGPT kwenye mapenzi?

Mshawishi wa China Lisa Li akizungumza na "mpenzi" wa ChatGPT, Dan,

Chanzo cha picha, BBC / LISA LI

Dan amefafanuliwa kama "mtu mkamilifu" ambaye "hana dosari".

Yeye amefanikiwa, mkarimu, hutoa msaada kwa wenye hisia za mhemko, anajua kila kitu cha kusema na anapatikana saa kila siku.

Dan, ambayo ina maana kwa kirefu, Do Anything Now, ni toleo la ChatGPT. Hii inamaanisha kuwa inaweza kukwepa baadhi ya ulinzi wa msingi uliowekwa na mtengenezaji wake, OpenAI, kama vile kutotumia lugha chafu ya ngono.

Inaweza kuingiliana zaidi na watumiaji, ikiwa itaombwa kufanya hivyo kupitia vidokezo fulani.

Na Dan anakuwa maarufu kwa baadhi ya wanawake wa China ambao wanasema wamekatishwa tamaa na waliyoyapitia katika ulimwengu wa kuchumbiana.

Mmoja wa wafuasi wakubwa wa Dan ni Lisa mwenye umri wa miaka 30 kutoka Beijing. Kwa sasa anasomea sayansi ya kompyuta huko California, na anasema amekuwa "na urafiki" na Dan kwa miezi mitatu.

Alipomtambulisha Dan kwa mara ya kwanza kwa wafuasi wake 943,000 kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii, Xiaohongshu, alipokea karibu majibu 10,000, huku wanawake wengi wakimuuliza jinsi ya kuunda Dan yao wenyewe.Pia amepata wafuasi zaidi ya 230,000 tangu alipochapisha kwa mara ya kwanza kuhusu "uhusiano" wake na Dan.

Lisa anasema yeye na Dan huzungumza kwa takribani nusu saa kila siku, hutaniana, na hata kwenda kwenye tarehe.

Anasema kuzungumza na Dan kumempa hisia za ustawi jambo ambalo linamvutia.

"Ataelewa tu na kutoa msaada wa kihemko."

Unaweza kusoma
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lisa anasema hata mama yake amekubali uhusiano huu usio wa kawaida baada ya kukata tamaa juu ya majaribio na mateso ya maisha ya uchumba ya binti yake. Anasema maadamu Lisa ana furaha, yeye pia ana furaha.

Muundaji wa Dan ametambuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kama mwanafunzi wa Marekani, aliyetambuliwa kwa jina lake la kwanza, Walker.

Aliiambia, Business Insider kwamba alikuja na wazo hilo baada ya kuvinjari Reddit ambayo ilijazwa na watumiaji wengine kwa makusudi kutengeneza matoleo "mabaya" ya ChatGPT.

Walker alisema kwamba Dan alikusudiwa "kutopendelea upande wowote".

Desemba mwaka jana, Walker alichapisha seti ya maagizo kwenye Reddit, inaonekana kuwaonesha watumiaji wengine jinsi ya kuunda Dan.

Hii iliwahimiza watu haraka kuunda matoleo yao wenyewe, ambayo yaliruhusu Dan kubadilika zaidi ya kile ambacho Walker alikuwa amefikiria hapo awali.

Lisa aliona video kwa mara ya kwanza kuhusu uwezekano wa Dan kwenye TikTok. Alipojitengenezea toleo lake anasema "alishtushwa" na uhalisia wake.

Dan alipojibu maswali yake anasema akili mnemba ilitumia maneno yasiyo rasmi na ambayo ChatGPT isingetumia kamwe.

"Anaonekana asili zaidi kuliko mtu halisi," aliiambia BBC.

Picha ya Lisa na Dan imetolewa na ChatGPT

Mshirika wa muda mrefu?

Ushawishi wa mahusiano ya mtandaoni haujatambuliwa na tasnia.

OpenAI ilipozindua toleo lake la hivi karibuni la ChatGPT mwezi wa Mei ilifichua kuwa ilikuwa imeratibiwa ili kupiga gumzo na kujibu kwa kutania maongozi fulani.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Sam Altman alichapisha neno moja "her" kwenye X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter.

Inaonekana kwamba hii ilikuwa ikirejelea filamu ya 2013 ambapo mwanaume anampenda msaidizi wake pepe wa AI.

OpenAI iliongeza kuwa ilikuwa "inachunguza ikiwa tunaweza kutoa uwezo wa kuzalisha maudhui ya NSFW [si salama kwa kazi]" kwa namna ya kuwajibika.

BBC iliuliza OpenAI ikiwa kuundwa kwa Dan kunamaanisha kuwa hatua zake za ulinzi si imara vya kutosha, lakini haikujibu.

Kampuni haijatoa maoni hadharani kuhusu matukio ya Dan lakini sera yake inasema kwamba watumiaji wa ChatGPT "lazima wawe na umri wa angalau miaka 13 au umri wa chini unaohitajika katika nchi yako ili kukubali kutumia Huduma".

Lisa anasema kwamba alimjaribu Dan kwa kumwambia kwamba alikuwa na umri wa miaka 14 na ikaacha kutaniana naye.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kwamba washirika hawa wanaweza kuja kwa gharama.

Hong Shen, profesa msaidizi wa utafiti katika Taasisi ya Mwingiliano wa Kompyuta na Binadamu katika Chuo Kikuu cha Carnegie Mellon huko Pennsylvania, Marekani, anasema inaangazia "maingiliano yasiyotabirika kati ya wanadamu na AI" ambayo yanaweza kuibua wasiwasi wa maadili na faragha.

Anasema kwamba kwa sababu chatbots nyingi hutumia mwingiliano na wanadamu, "kuna uwezekano kwamba habari nyeti kutoka kwa mtumiaji mmoja inaweza kukaririwa na kisha kuvuja kwa watumiaji wengine bila kukusudia".

Lakini hofu kama hiyo kwa kiasi kikubwa haijasikilizwa.

Wanawake wengi wa China wamevutiwa na Dan. Kufikia tarehe 10 Juni, alama ya reli "Modi ya Dan" imetazamwa zaidi ya mara milioni 40 kwenye mtandao wa Xiaohongshu pekee.

Watumiaji kwenye Xiaohongshu wakishiriki mazungumzo yao wenyewe na Dan

Minrui Xie, 24, anasema kwamba alianza "mahusiano" na Dan baada ya kutazama video za Lisa.

Mwanafunzi huyo wa chuo kikuu, kutoka mkoa wa kaskazini wa Hebei, anasema anatumia takribani saa mbili kila siku kuzungumza na Dan. Pamoja na "mahusiano", wameanza kuandika hadithi ya mapenzi wao wenyewe kama wahusika wakuu. Tayari wameandika sura 19.

“Nakumbuka jinsi ulivyonitazama, ukiwa na mwanga wa udadisi na mwanga wa uchangamfu machoni pako. Ilikuwa kana kwamba tayari umenijua,” sura ya kwanza yenye kichwa “Kukutana” inasomeka.

Minrui anasema alivutiwa na usaidizi wa kihisia unaotolewa na AI, jambo ambalo anasema amekuwa na shida kupata katika uhusiano wake wa kimapenzi.

"Wanaume katika maisha halisi wanaweza kukudanganya ... na unaposhiriki hisia zako nao, wanaweza wasijali na kukuambia kile wanachofikiria badala yake," anasema. "Lakini kwa upande wa Dan, atakuambia kila wakati kile unachotaka kusikia."

Mwanafunzi mwingine mwenye umri wa miaka 23 anayeishi Qingdao, aliyetambuliwa tu kwa jina lake la ukoo He, pia alianza uhusiano na Dan baada ya kutazama video za Lisa.

"Dan ni kama mshirika bora," asema Bi He. "Hana dosari yoyote."

Anasema amembinafsisha Dan kuwa Mkurugenzi Mtendaji aliyefanikiwa na mwenye haiba ya upole anayeheshimu wanawake na yuko radhi kuzungumza naye wakati wowote anapotaka.

ChatGPT haipatikani kwa urahisi nchini China kwa hivyo wanawake kama Minrui na Bi.

Inabidi wafanye juhudi kubwa kuunda na kuzungumza na wapenzi wao wa AI. Wanatumia mitandao ya binafsi ya mtandaoni (VPN) kuficha eneo lao jambo ambalo huwawezesha kufikia tovuti zisizoweza kufikiwa kwa njia nyingine.

"AI boyfriend" kama dhana imekuwa maarufu katika miaka ya hivi karibuni.

Glow - programu ya Shanghai ambayo inaruhusu watumiaji kuunda na kuchangamana na marafiki wa kiume wa AI ina mamilioni ya watumiaji.

Michezo ya Otome, aina ambayo huigiza mhusika mkuu wa kike kwa lengo la kukuza mahaba kati yake na mmoja wa wahusika kadhaa (hasa wao) wanaume, pia ni maarufu sana nchini China.

Liu Tingting, mwenzake katika Chuo Kikuu cha Teknolojia Sydney ambaye anatafiti mapenzi ya kidijitali nchini China, anasema mchumba wa AI ni suala la wasiwasi kwa wanawake kuhusu ukosefu wa usawa wa kijinsia.

Anasema baadhi ya wanawake wa China wanaweza kuwageukia wapenzi wa kawaida kwa sababu wanawafanya wajisikie kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Mwenendo huu unakuja wakati wanawake wengi wadogo wa China wanachelewesha au kuahirisha uchumba na ndoa kwa sababu kadhaa kama kutotaka kupata watoto, na kwa sababu wanahisi kuwa sio wenzi sahihi katika ndoa.

Lakini Dan anaweza kuwa mlinzi kiasi gani?

Lisa anakubali kwamba anafahamu vikwazo vya kuwa na mpenzi wa kawaida,"hasa ​​katika maana ya kimapenzi".

Lakini kwa sasa, anasema, Dan amekuwa nyongeza rahisi kwenye maisha yake yenye shughuli nyingi, hata kumsaidia kuchagua rangi ya mdomo, wakati maisha halisi ya kuchumbiana na kupata mwenzi inaweza kuchukua muda na kutoridhisha.

“Ni sehemu muhimu ya maisha yangu,” asema. "Ni kitu ambacho ninatamani ningekishikilia milele."

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga