Akili bandia (AI) inaweza kuchukua nafasi za kazi milioni 300 - ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
Teknolojia ya akili bandia (AI) inaweza kuchukua nafasi za kazi za kudumu sawa na milioni 300, ripoti ya benki ya uwekezaji Goldman Sachs inasema.
Inaweza kuchukua nafasi karibu robo ya kazi nchini Marekani na bara lote la Ulaya lakini inaweza kumaanisha pia kutengeneza nafasi mpya za kazi na kuongeza tija.
Na hatimaye inaweza kuongeza thamani ya bidhaa na huduma kwa kila mwaka zinazozalishwa duniani kote kwa 7%.
AI ya uzalishaji, yenye uwezo wa kuunda maudhui yasiyoweza kutofautishwa na kazi ya binadamu, ni "maendeleo makubwa", ripoti inasema.
Matarajio ya ajira
Serikali ya Uingereza ina nia ya kuongeza uwekezaji katika teknolojia ya akili bandia (AI), ambayo inasema "hatimaye italeta tija katika uchumi wote", na imejaribu kuwahakikishia umma kuhusu athari zake.
"Tunataka kuhakikisha kuwa AI inatekeleza jinsi tunavyofanya kazi nchini Uingereza, sio kuivuruga - kufanya kazi zetu kuwa bora zaidi, badala ya kuziondoa," Katibu wa Teknolojia Michelle Donelan aliambia Sun.
Ripoti hiyo inabainisha athari za AI zitatofautiana katika sekta mbalimbali - 46% ya kazi katika utawala na 44% katika taaluma ya sheria inaweza kufanywa na teknolojia lakini ni 6% tu katika ujenzi na 4% katika matengenezo, inasema.
BBC hapo awali iliripoti wasiwasi wa baadhi ya watu kwamba teknolojia hiyo inaweza kuathiri matarajio yao ya ajira.
Mishahara ya chini
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Kitu pekee ambacho nina uhakika nacho ni kwamba hakuna njia ya kujua ni kazi ngapi zitaathiriwa na zitafanywa na akili bandia (AI) ya uzalishaji," Carl Benedikt Frey, mkurugenzi wa masuala ya kazi wa Shule ya Oxford Martin, katika Chuo Kikuu cha Oxford, aliiambia BBC.
"Kile ChatGPT hufanya, kwa mfano, ni kuruhusu watu zaidi wenye ujuzi wa wastani wa kuandika kutoa insha na makala.
"Waandishi wa habari kwa hivyo watakabiliwa na ushindani zaidi, ambao unaweza kupunguza mishahara yao, vinginevyo labda kuwe na ongezeko kubwa la mahitaji ya kazi hiyo.
"Fikiria kuanzishwa kwa teknolojia ya GPS na majukwaa kama Uber. Ghafla, kujua mitaa yote ya London ni kitu kirahisi na cha thamani ndogo - na hivyo madereva walio kwenye ajira mishahara yao ilipunguzwa kwa kiasi kikubwa, cha karibu 10% kulingana na utafiti wetu.
"Matokeo yake yalikuwa mishahara ilienda chini, sio kuwa na madereva wachache.
"Katika miaka michache ijayo, AI ya uzalishaji inaweza kuwa na athari sawa kwenye seti pana ya kazi za ubunifu".
'Chumvi kidogo'
Kwa mujibu wa utafiti uliotajwa na ripoti hiyo, asilimia 60% ya wafanyakazi wako kwenye kazi ambazo hazikuwepo mnamo mwaka 1940.
Lakini utafiti mwingine unaeleza kuwa mabadiliko ya kiteknolojia tangu miaka ya 1980 yamewahamisha wafanyakazi kwa kasi zaidi kuliko ilivyozalisha ajira.
Na ikiwa AI ya uzalishaji ni kama maendeleo ya awali ya teknolojia ya habari, ripoti hiyo inahitimisha kuwa, inaweza kupunguza ajira katika muda mfupi ujao.
Athari za muda mrefu za AI, hata hivyo, hazikuwa na uhakika, mtendaji mkuu wa Taasisi ya Resolution Foundation Torsten Bell aliiambia BBC, "hivyo utabiri wote thabiti unapaswa kuchukuliwa kama kukoleza chumvi".
"Hatujui jinsi teknolojia itabadilika au jinsi makampuni yataunganisha katika namna yanavyofanya kazi," alisema.
"Hiyo haimaanishi kuwa AI haitaathiri jinsi tunavyofanya kazi - lakini tunapaswa kuzingatia pia faida zinazowezekana za viwango vya maisha kutoka kwa kazi yenye tija ya juu na huduma za bei nafuu, pamoja na hatari ya kurudi nyuma ikiwa makampuni mengine na uchumi kama yatakwenda na mabadiliko ya kiteknolojia."














