Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

China yaijibu Marekani tena na kuongeza ushuru wa bidhaa za Washington hadi 125%

Rais wa China Xi Jinping anasema hakuna "mshindi katika vita vya ushuru" kwani Beijing inakabiliwa na ushuru wa 145% kwa bidhaa zinazoagizwa Marekani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. Changamoto za kiufundi ndizo zilisababisha kifo cha Jenerali Ogola, Kenya

    Uchunguzi wa ajali ya ndege iliyomuuwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Kenya Jenerali Francis Ogolla imesema kwamba changamoto za kiufundi ndizo chanzo cha ajali hiyo ya Aprili 18th 2024.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotekelezwa na kitengo cha uchunguzi wa ajali za ndege katiak Jeshi la anga nchini Kenya, Injini ya ndege hiyo ya aina ya Helikopta ya Huey yenye nambari ya usajali KAF 1505, ilikwama baada ya kupoteza nguvu ilipokuwa angani.

    Jenerali Ogolla alikuwa akisafiri na wanajeshi wengine 11, kutoka eneo la Kainuk ikisafiri hadi shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel iliyopo mjini Chesogon katika kaunti ya Baringo, iliyopo kwenye eneo la bonde la ufa nchini Kenya.

    Kitengo hicho cha jeshi la angani limeondoa shaka kwamba ajali hiyo huenda ilitokea kwa sababu za kibinadamu, au hali ya anga. Aidha ripoti imesema kwamba Marubani wawili waliokuwa kazini siku hiyo, ni wazoefu na kwamba hali ya anga ilikuwa salama siku hiyo ambapo ndege ilianguka.

    Rais William Ruto alipokezwa ripoti hiyo mapema leo katika ikulu ya Rais Nairobi, iliyowasilishwa na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Charles Kahariri, Naibu wake Luteni Jenerali Omenda , Mkuu wa jeshi la Anga, Meja Jenerali Fatuma Ali na waziri wa Ulinzi, Soipan Tuya.

    Kifo cha Ogolla kilipokelewa kwa mshutko na taifa zima, huku baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Nyanza alikozaliwa Ogolla, wakitaka kujuwa chanzo cha ajali hiyo, ili kuondoa hofu kwamba huenda kulikuwa na hujuma yoyote.

    Japo familia yake ilisisitiza kwamba iliridhika kwamba kifo chake kilitokana na ajali, wengi walitaka sana kujuwa chanzo chake ili kuondoa shaka iliyokuwepo punde tu, taarifa za kifo chake zilipotangazwa na rais William Ruto.

    Merehemu Jenerali Ogolla alikuwa akisafiri na Brigedia Swale Saidi , Kanali Kasaine Ole Kuruta (manusura), Kanali

    Duncan Keittany , Luteni Kanali David Sawe , Meja George Benson Magondu – (Rubani) , Kapteni Sora Mohamed – (Rubani), Kapteni Hillary Litali , Sajini Mwandamizi John Kinyua Mureithi , Sajini Cliphonce Omondi , Sajini Rose Nyawira , na Koplo

    Frankford Karanja Mogire (manusura), wakati wa ajali hiyo.

    Soma zaidi:

  3. Aliyetumia mtandao uliosimbwa kwa njia fiche kuuza bunduki zenye kumimina risasi afungwa jela

    Mwanamume mmoja kutoka North Yorkshire ambaye alitumia mtandao wa simu uliosimbwa kwa njia fiche kuuza dawa za kulevya na bunduki zenye kumimina risasi amefungwa jela kwa zaidi ya miaka 26.

    Mwezi mmoja tu baada ya kuachiliwa kutoka gerezani mnamo Machi 2020, Nathaniel Hollywood, 39, alianza kuuza silaha kwa washirika wengine wa uhalifu.

    Silaha alizokuwa akiuza ni pamoja na bunduki aina ya AK-47 na bunduki ndogo za Skorpion na Uzi.

    Siku ya Alhamisi katika Mahakama ya Teesside Crown, miaka mitano baada ya kutumikia kifungo cha miaka 11 kwa kuhusika na biashara ya cocaine, Hollywood ilifungwa tena.

  4. Zambia kuanza ujenzi wa miundo mbinu ya Umeme kuunganisha Tanzania

    Zambia itaanza tena ujenzi wa miundo mbinu ya umeme unaounganisha na Afrika Mashariki, na kuunda moja ya masoko makubwa ya nishati ulimwenguni, afisa mwandamizi wa Benki ya Dunia alisema Ijumaa.

    Mradi huo wa umeme wa Zambia na Tanzania umepangwa kuanza tena mwezi huu, na kukadiriwa kukamilika mnamo mwaka 2028, Achim Fock, meneja wa nchi ya Zambia katika Benki ya Dunia, alisema Ijumaa wakati wa sherehe ya kutia saini.

    Mradi wa $ 320,000,000 wa kuunganisha vifaa vya umeme vya Zambia na Tanzania unafadhiliwa na Benki ya Dunia, Jumuiya ya Ulaya na Uingereza.

    Gharama ya kazi iliyosalia ni $ 298 milioni, ambayo ruzuku ya Benki ya Dunia itashughulikia dola milioni 245, Kaimu Waziri wa Fedha Chipoka Mulenga alisema, katika hafla hiyo hiyo.

    Mradi huo ulianza kwa mara ya kwanza zaidi ya muongo mmoja uliopita lakini umesitishwa kwa sababu tofauti, hivi karibuni ikiwa ni kwa sababu ya COVID-19 na wasiwasi juu ya deni la Zambia mwishoni mwa 2020.

    Fock alisema soko la pamoja lenye kuunganisha mabwawa ya umeme Kusini na Mashariki ya Afrika yatasaidia kupunguza gharama za umeme, kuongeza nishati na kuunda fursa mpya za kibiashara na uwekezaji katika sekta ya umeme kote Afrika.

    Soma zaidi:

  5. Rais Samia aikaribisha Man Utd kuwekeza Tanzania

    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza, Sir Jim Ratcliffe, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 11 Aprili, 2025, ambapo amemkaribisha rasmi kuwekeza katika sekta za michezo na utalii nchini.

    Mazungumzo hayo yalijikita katika fursa za ushirikiano baina ya Tanzania na Manchester United, klabu yenye mashabiki mamilioni duniani, wakiwemo wengi kutoka barani Afrika.

    Sir Jim ameonesha nia ya kuitumia klabu hiyo kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa, hususan kupitia kampeni za utalii.

    Aidha, Rais Samia alipokea zawadi ya jezi ya Manchester United iliyosainiwa na wachezaji wa timu hiyo, kama ishara ya heshima na urafiki kutoka kwa mmiliki huyo wa klabu.

    Rais Samia alitumia fursa hiyo kumualika Sir Jim kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya mafunzo ya michezo (Sports Academies) nchini, ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kukuza vipaji vyao na kushiriki kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa, lakini pia patika eneo la utalii.

    Samia amemshukuru Sir Jim Ratcliffe kupitia Taasisi yake ya Six Rivers ambayo ina shughulika na masuala ya Uhifadhi, kwa namna inavyofanya vizuri katika kudhibiti muingiliano wa wanyamapori na binadamu kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).

    Kupitia Taasisi yake ya Six Rivers, Sir Jim Ratcliffe amebainisha kuwa Taasisi hiyo imedhamiria kurejesha hadhi ya Hifadhi ya Taifa ya Selous na kuwa na Wanyama wakubwa katika Hifadhi hiyo.

    Manchester United tayari imekuwa ikifanya kazi na mashirika na mataifa mbalimbali barani Afrika, ikiwemo miradi ya kijamii kupitia Manchester United Foundation, lakini hii ni mara ya kwanza kwa mmiliki wa klabu hiyo kuonesha nia ya uwekezaji wa moja kwa moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

    Ziara ya Sir Jim Ratcliffe nchini Tanzania ni hatua muhimu inayoweza kufungua milango kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta ya michezo na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia diplomasia ya michezo.

  6. Wimbo unaomkosoa rais wapigwa marufuku katika vituo vya redio Nigeria

    Mamlaka ya Nigeria imepiga marufuku watangazaji kucheza wimbo wa Tell Your Papa, ambao unamkosoa rais wa nchi hiyo.

    Nyimbo za msanii Eedris Abdulkareem zilimsuta Rais Bola Tinubu na kumtaka mwanawe mwenye ushawishi mkubwa, Seyi, kumfahamisha babake "watu wanakufa" kwa shida, kuna ukosefu wa usalama na "njaa" nchini humo.

    Katika barua kwa vituo vya Televisheni na redio, Tume ya Taifa ya Utangazaji (NBC), ambayo inatoa leseni na kudhibiti tasnia hiyo, iliamuru wimbo huo usichezwe, ikisema unakiuka kanuni za utangazaji nchini.

    NBC ilisema inazingatia maudhui ya wimbo wa ‘Tell Your Papa’ kuwa "yasiyofaa" na "yanayoweza kupingwa" na kuongeza kuwa yanakiuka viwango vya uadilifu vya umma.

    Wimbo huo uliozinduliwa mwanzoni mwa wiki na umepata umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii nchini Nigeria na kuzua mjadala kuhusiana na hali ya uchumi na usalama nchini humo.

    Akiwa rais Mei 2023, Tinubu alianzisha mageuzi kadhaa ya kiuchumi ambayo yaliongeza gharama ya maisha.

    Alitupilia mbali ruzuku ya mafuta, ambayo kwa muda mrefu ilisaidia bei ya petroli kuwa chini, akisema kuwa serikali haiwezi kumudu tena hilo. Bei ya mafuta kisha ikapanda sana jambo ambalo lilikuwa na athari kwa uchumi kijumla.

    Pia kuna wasiwasi kuhusu kiwango cha ukosefu wa usalama nchini humo huku utekaji nyara kwa ajili ya fidia bado ni suala sugu na kuna hofu kwamba kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram linaweza kuzuka tena kaskazini-mashariki.

    Kwenye wimbo huo, ulioimbwa kwa mchanganyiko wa Kiingereza, Kiyoruba na Pijini, Abdulkareem anamwambia mtoto wa Tinubu kuwa baba yake "hajaimarisha hali" na kwamba ametoa "ahadi nyingi za uwongo".

    Linapokuja suala la ukosefu wa usalama, msanii huyo anamtaka Seyi kusafiri kwa barabara, badala ya ndege ya kibinafsi, ili kujionea hatari wanayokumbana nayo Wanigeria wa kawaida.

    Kama mamlaka ya kutoa leseni, NBC inaweza kuadhibu mashirika ya utangazaji kwa kupuuza maagizo yake. Hapo awali walivipiga faini vituo na kufutilia mbali leseni zao kwa ukiukaji.

    Abdulkareem sio mara ya kwanza kujipata kwenye utata wa aina hii kwani alirekodi wimbo kama huo siku za nyuma.

    Mnamo 2003, alitoa wimbo wake ambao ni maarufu hadi sasa - Nigeria jaga jaga, ikimaanisha "Nigeria imeharibika".

    Kisha Rais Olusegun Obasanjo akajibu vikali, akimtusi Abdulkareem hadharani. Wimbo huo ulipigwa marufuku kuchezwa katika vituo vya utangazaji lakini ukapata umaarufu miongoni mwa Wanigeria na kuwa wimbo wa mitaani.

    Pia unaweza kusoma:

  7. China yaijibu Marekani tena na kuongeza ushuru wa bidhaa za Washington hadi 125%

    Uchina imetangaza ushuru mpya wa 125% kwa bidhaa za Marekani.

    Ushuru huu umeongezeka kutoka 84% iliyotangazwa Jumatano. Ni sawa na ushuru wa sasa wa Marekani kwa bidhaa za China.

    Hili limetokana na vita vya kibiashara vinavyoendelea ambapo siku ya Jumatano, Ikulu ya Marekani ilisema imeongeza ushuru wa bidhaa za China zinazoingizwa nchini humo hadi 145%, ikiwa ongezeko la asilimia 20 kutoka ongezeko la wiki zilizopita.

    China inasema 'haitajibu' ushuru wa ziada wa Marekani

    Wakati huo huo, Beijing inasema haitajibu ushuru wowote zaidi uliowekwa na Marekani.

    Inasema "ushuru wa juu usio wa kawaida" uliowekwa na Marekani "unakiuka kwa kiasi kikubwa sheria za biashara ya kimataifa na kiuchumi, sheria za msingi za kiuchumi na ni uonevu wa upande mmoja".

    Soma zaidi:

  8. Salah anasaini mkataba mpya wa miaka miwili na Liverpool

    Mshambuliaji wa Misri Mohamed Salah amesaini mkataba mpya wa miaka mbili na Liverpool.

    Makubaliano yake ya zamani yalikuwa yanamalizika msimu wa joto na kumekuwa na mashaka kama angesalia the Reds kufuatia maoni yake wakati wa msimu na uvumi uliomhusisha na kuhamia Saudi Arabia.

    Hata hivyo, sasa atapata fursa ya kuongeza mabao yake 243 na fursa 109 alizosaidia Liverpool kufunga magoli katika mechi 393 alizocheza.

    "Kwa kweli nimefurahi sana - tuna timu imara sasa," alisema Salah.

    "Kabla pia tulikuwa na timu bora. Lakini nilisaini mkataba kwa sababu nafkiria tunayo nafasi ya kushinda mataji mengine na kufurahiya mpira wangu.

    Salah amefunga mabao 32 katika mashindano yote msimu huu, yakiwemo 27 kwenye Ligi Kuu ya England huku the Reds wakisaka taji la 20 la ligi kuu.

    Liverpool wako nyuma kwa tofauti ya pointi 11 na Arsenal wanaoshika nafasi ya pili huku wakiwa wamesalia na mechi saba.

    Salah, ambaye alijiunga na Liverpool kutoka Roma mwaka 2017, ameshinda Champions League, Premier League, FA Cup, League Cup na Fifa Club World Cup akiwa na Reds.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo na karibu katika awamu ya pili ya matangazo ya moja kwa moja, mimi ni Asha Juma

  10. Mahakama ya juu ya Uganda yamnyima dhamana Besigye na Lutale

    Mahakama ya juu ya Kampala imemnyima dhamana kiongozi wa upinzani Besigye na mwenzake Hajj Lutale wakitaja kuwa kesi inayowakabili ni nzito na kutokana na ushawishi wao huenda wakaingilia kati uchunguzi.

    Ni siku ya 147 tangu wawili hao kuzuiliwa baada ya kukamatwa mjini Nairobi mwezi Novemba mwaka jana.

    Kulingana na mahakama hiyo dhamana iliyowasilishwa na Kisza Besigye na Hajj Lutale ni dhabiti na kusema kuwa waliafiki viwango hitajika vya kupewa dhamana.

    Hata hivyo Jaji aliyekuwa akisimamia kesi hiyo alidinda kuwapa dhamana akieleza kuwa uchunguzi bado unaendelea.

    Mgombea wa mara nne wa urais nchini Kenya pamoja na msaidizi wake wanakabiliwa na shtaka la uhaini ambayo adhabu yake ni kifungo cha maisha.

    Kulingana na upande wa mashtaka Besigye,kapteni Denis Oola na wengine ambao hawajakamatwa wanadaiwa walifanya jaribio la mapinduzi kati ya mwaka 2023 na mwezi Novemba 2024.

    Soma pia:

  11. Kenya: Wanawake 129 waliuawa kati ya Januari na Machi mwaka huu

    Kati ya mwezi Januari na Machi 2025, Kenya ilikumbwa na janga kubwa la mauaji ya wanawake, ambapo jumla ya wanawake 129 waliripotiwa kuuawa.

    Mnamo Januari, wanawake 43 waliuawa, wakifuatiwa na 42 mnamo Februari, na 44 mnamo Machi.

    Maeneo ya Bonde la Ufa, Mashariki, na Magharibi yaliandikisha idadi ya juu zaidi ya vifo hivyo.

    Takwimu zinaonyesha kuwa wanaume walihusika na asilimia 85 ya mauaji haya, huku wanawake wakihusishwa na asilimia 10.

    Katika visa vingi, wahalifu walikuwa watu waliowafahamu waathiriwa, na nusu ya mauaji haya yalihusiana na migogoro ya kifamilia.

    Kwa mwaka wa 2024 pekee, jumla ya visa 579 za mauaji ya wanawake ziliripotiwa.

    Taarifa hizi ni kwa mujibu wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi pamoja na Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu.

    Soma pia:

  12. Dawa mpya ya kutibu saratani ya matiti yaanza kutumika Uingereza

    Waathiriwa wa saratani ya matiti nchini Uingereza wamepata ahueni baada ya dawa mpya ya kukabiliana na ugonjwa huo kupatikana.

    Dawa hiyo kwa jina Capivasertib inasemekana haina madhara makubwa kwa wagonjwa kama zilivyo nyingine ambazo zina makali mno.

    Ina tiba mahsusi inayolenga protini ya AKT, molekuli inayochochea ukuaji wa saratani.

    Dawa hii hufanya kazi kwa kuzuia kabisa shughuli ya protini hiyo, hivyo kudhibiti ukuaji wa seli hatari.

    Wanasayansi wamekuwa wakifanyia kazi dawa hii kwa zaidi ya miaka ishirini, na sasa wanaamini kuwa ndiyo yenye ufanisi mkubwa zaidi kuwahi kuonekana kwa wagonjwa walio na saratani ya hatua ya juu.

    “Inatoa mbadala wenye ufanisi mkubwa, unaoweza kufanya kazi kwa muda mrefu — kwa miezi mingi, na kwa baadhi ya wagonjwa hata kwa miaka,” alisema Profesa Nick Turner, mtafiti mkuu na profesa wa onkolojia ya tiba katika Taasisi ya Utafiti wa Saratani na Hospitali ya Royal Marsden.

    Majaribio ya dawa hiyo yanaonesha inapunguza uvimbe kwa karibu robo ya wanawake walio na saratani ya matiti na inaendelea kufanya kazi mwilini kwa muda mrefu wa hadi mwaka mmoja.

    Saratani ya matiti ndiyo inayoripotiwa zaidi nchini Uingereza huku mwanamke mmoja kati ya saba kuathirika na saratani katika maisha yake, na asilimia 75 ya wagonjwa wakisalia hai kwa zaidi ya miaka kumi baada ya kugunduliwa.

    Mafanikio katika matibabu yanaendelea kuleta matumaini mapya.

    Iwapo saratani itarudi na kusambaa katika maeneo mengine ya mwili, lengo kuu la matibabu huwa ni kuidhibiti, kupunguza dalili, na kuboresha ubora wa maisha ya mgonjwa.

    Matibabu yanayoweza kutolewa ni pamoja na tiba ya kufubaza makali ya saratani, matibabu kwa njia ya eksirei, na dawa maalum zinazozuia ukuaji wa saratani — kwa kuzuia homoni, kuimarisha kinga ya mwili, au kulenga moja kwa moja vichocheo vinavyosababisha ukuaji wa seli za saratani.

    Dawa hii inafaa wagonjwa walio na mabadiliko fulani ya kinasaba yanayoathiri hadi nusu ya wale wanaougua saratani ya matiti katika awamu ya pili inayotegemea homoni — aina ya kawaida zaidi ambayo hukua kwa utegemezi wa homoni ya oestrogen.

    Kwa upande wake, Profesa Peter Johnson, Mkurugenzi wa Huduma za Saratani katika NHS England, alisema kuwa dawa hiyo ni “chaguo la ziada” kwa wagonjwa ambao saratani yao imeendelea licha ya kupitia tiba ya homoni awali — japo si kila mtu atakayefaa kuitumia.

    Bi Claire Rowney, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la hisani la Breast Cancer Now, alisema kuwa amefarijika sana kuona dawa hii ikiwapa wagonjwa “tumaini la muda wa ziada wa kuishi na kutekeleza mambo yanayowapasa zaidi katika maisha yao.”

    Unaweza pia kusoma:

  13. Familia zaanza kuwaaga waliofariki katika mkasa wa ukumbi wa burudani Dominican

    Maelfu ya watu wamejitokeza katika Jamhuri ya Dominica kutoa heshima zao za mwisho kwa mwanamuziki mashuhuri Rubby Perez aliyefariki dunia katika mkasa wa paa la ukumbi wa burudani lililomuangukia pamoja na mashabiki wake siku ya Jumanne wiki hii.

    Takriban watu mia mbili ishirini walikufa katika mkasa huo na serikali imetangaza kuundwa kwa jopo la wachunguzi kuchunguza mkasa huo uliokumba klabu ya Jet Set.

    Binti ya mwanamuziki huyo Zulinka Peres aliyekuwa pia akitumbuza na babake wakati wa mkasa amewaeleza waombolezaji kuwa ana bahati yuko hai.

    "Mimi na mume wangu ni mashahidi wa muujiza kwasababu tulikuwa kando yake.Sisi nimanusura wa mkasa huo.Nilikiona kilichojiri pale,hakuna atakayenisimulia.Namshukuru Mungu na mume wangu niko hai kwasababu alinifunika na mwili wake na ndiyo maana niko hapa, asema Zulinka Peres.

    Mamlaka haijabaini sababu ya kuporomoka kwa paa la klabu ya burudani, ambapo sherehe yake ya kitamaduni ya "Merengue Monday" ilikuwa ikifanyika.

    "Ilikuwa ghafla," alisema meneja wa Rubby Pérez, Enrique Paulino, ambaye alinusurika. "Nilifikiri lilikuwa tetemeko la ardhi, kwa hiyo nilijitupa chini na kufunika kichwa changu... Mmoja wa wapiga saksafoni wetu alikufa. Tulijaribu kufika eneo ambalo Rubby alikuwa, lakini vifusi vilikuwa vimetapakaa kila mahali."

    Haya yakijiri serikali ya Dominica imetangaza kuwa shughuli za uokozi zimekamilika na taifa linaendelea kuomboleza na kufarijiana.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Mahakama ya Marekani yaagiza kurejeshwa kwa mhamiaji aliyepelekwa El Salvador kimakosa

    Mahakama ya juu ya Marekani imeamuru utawala wa Rais Trump usimamie kurejeshwa kwa mhamiaji aliyepelekwa El Salvador mwezi uliopita baada ya kutuhumiwa kimakosa kuwa mwanachama wa genge la wahalifu wa kutoka Amerika Kusini.

    Familia ya Kilmar Abrego Garcia ilipinga mahakamani uhalali wa kurejeshwa kwake El Savador,akiwa sehemu ya kundi la wahamiaji zaidi ya mia mbili wanaoshutumiwa kuwa na mafungamano na magenge ya wahalifu waliotupwa gerezani El Salvador na wanatarajiwa kukaa huko kwa mwaka mmoja.

    Kesi hiyo sasa inarejeshwa katika mahakama ya mwanzo, huku majaji wa ngazi za juu wakikosa kuweka kikomo cha muda kwa serikali kuhusu lini Garcia anapaswa kurejeshwa nchini.

    Garcia, mwenye umri wa miaka 29, aliingia Marekani kinyume cha sheria akiwa kijana kutoka El Salvador.

    Mnamo mwaka 2019, alikamatwa pamoja na wanaume wengine watatu huko Maryland na kuwekwa kizuizini na maafisa wa uhamiaji wa shirikisho.

    Ingawa kulikuwa na sababu za kisheria za kumrejesha nchini kwao, jaji wa uhamiaji alimpa hifadhi dhidi ya kufukuzwa, akizingatia uwezekano wa kuteswa na magenge hatari ya mitaani katika nchi yake ya asili.

    Hata hivyo, licha ya amri ya mahakama iliyopiga marufuku kuondolewa kwake, Garcia alifukuzwa nchini Marekani tarehe 15 Machi.

    Mkewe, Jennifer Vasquez Sura ambaye ni raia wa Marekani amekuwa mstari wa mbele kupaza sauti akiitaka serikali kumrejesha mumewe.

    “Hali hii imekuwa kama safari ya kihisia isiyotabirika kwa watoto wangu, mama ya Kilmar, kaka yake pamoja na ndugu zake wote,” Bi. Sura aliambia gazeti la New York Times siku ya Alhamisi.

    “Nitaendelea kupigana hadi pale mume wangu atakaporejea salama nyumbani,” aliongeza kwa msisitizo.

    Soma pia:

  15. Michelle Obama apuuza uvumi kuhusu talaka kwenye ndoa yake

    Michelle Obama, mke wa rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amezungumzia uvumi kuwa ndoa yake inaelekea kuvunjika.

    Michelle hajaandamana na mumewe kwenye hafla kadhaa za kitaifa- ikiwa ni pamoja na kuapishwa kwa Donald Trump na mazishi ya Rais wa zamani Marekani Jimmy Carter - na kuchochea uvumi kwamba wanaweza kutengana.

    Bila kutaja matukio haya kwa uwazi, Bi Obama aliambia podcast ya Work in Progress iliyoandaliwa na muigizaji Sophia Bush kwamba sasa yuko katika nafasi ya kudhibiti shajara yake mwenyewe kama "mwanamke mzima".

    Alisema kuwa watu hawaamini kwamba "anajifanyia uamuzi" wake mwenyewe na badala yake "ilibidi waibue hoja kuwa mimi na mume wangu tunatalikiana".

    Bi Obama alikiri kuwa alijihisi kama mkosa kwa kujiondoa katika majukumu fulani.

    "Hilo ndilo jambo ambalo sisi kama wanawake, nadhani tunapambana nalo," alisema.

    "Hili ni wazi, kiasi kwamba mwaka huu watu hawakuweza hata kufahamu kuwa nilikuwa na uamuzi binafsi, ikabidi wafikirie kuwa mimi na mume wangu tunatalikiana.

    "Huyu hawezi kuwa mwanamke anayejifanyia maamuzi yake mwenyewe, sivyo? Lakini ndivyo jamii inavyotufanyia."

    Bi Obama pia alisema katika podcast hiyo: "Niliamua kufanya kile ambacho kilikuwa bora kwangu. Sio kile nilichopaswa kufanya. Sio kile watu wengine walitaka nifanye."

    Japo kutokuwepo kwake kwenye hafla ya kuapishwa kwa Rais Trump kulionekana kama kinyume na desturi, alitoa hotuba ya hali ya juu katika Kongamano la Kitaifa la chama cha Democratic (DNC) mwaka jana.

    Soma pia

  16. Uingereza yatangaza msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine

    Serikali ya Uingereza imetangaza itaipatia Ukraine msaada zaidi wa kijeshi wa kima cha dola milioni mia nne na hamsini ambazo zitatumika kununua ndege mpya zisizoendeshwa na marubani na kukarabati vifaru vya kijeshi.

    Hayo yalitangazwa katika mkutano ulioendeshwa na Uingereza na Ujerumani wa mawaziri wa ulinzi waliokutana mjini Brussels kujadili namna za kuendelea kuisaidia Ukraine.

    Marekani ilikuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Ukraine katika vita na Urusi lakini tangu Rais Donald Trump kuingia madarakani,hilo limebadilika kwa kiasi kikubwa.

    Healey alisisitiza kuwa kazi ya kikundi hicho cha Ulaya ni ya msingi katika kuhakikisha Ukraine inawekwa katika nafasi thabiti zaidi ya kujilinda.

    “Hatupaswi kuhatarisha amani kwa kuipuuza vita. Ndiyo maana kifurushi hiki kikubwa kilichotangazwa leo kinalenga kuongeza msaada kwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi,” alisema.

    “Mwaka 2025 ni mwaka wa maamuzi kwa Ukraine. Jukumu letu kama mawaziri wa ulinzi ni kuhakikisha wapiganaji wa Ukraine wanapatiwa kila wanachohitaji kwa ajili ya ushindi wao.”

    Mfuko huu mpya wa msaada unakuja kufuatia ahadi mbalimbali za kijeshi kutoka Uingereza kwa Ukraine.

    Mwezi uliopita, Waziri mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer alitangaza makubaliano ya pauni bilioni 1.6 kwa ajili ya makombora, kufuatia mkutano wa viongozi wa Ulaya uliofanyika London.

    Hata hivyo, Chama cha Liberal Democrats kimekosoa kiwango cha msaada huo, kikikitaja kuwa ni “kiasi kidogo” ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Ukraine.

    Kimeitaka serikali ya Uingereza kuchukua hatua zaidi kwa kukamata mali za Warusi walioko Uingereza ili kuiongezea Ukraine fedha za msaada.

    “Japokuwa tunapongeza msaada wowote kwa Ukraine, kiasi kilichotangazwa leo ni kidogo mno kuweza kukabiliana na ukatili wa vita vya Putin,” alisema msemaji wa masuala ya ulinzi wa chama hicho, Helen Maguire.

    Mkutano wa Ijumaa wa Kikundi cha Mawasiliano ya Ulinzi kwa Ukraine unaongozwa kwa pamoja na Healey na waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius.

    Hapo awali, mikutano hii ilikuwa ikiandaliwa na waziri wa ulinzi wa Marekani hadi Januari, Donald Trump alipoingia madarakani.

    Tangu wakati huo, ikiwa ni ishara ya Marekani kujiondoa kidogo katika masuala ya usalama barani Ulaya, Healey amechukua jukumu la kuwa mwenyekiti wa mikutano hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Soko la hisa Asia laendelea kusuasua baada ya nyongeza ya ushuru wa Trump

    Soko la hisa nchini Japan limefungua likiwa limeshuka kutokana na mazingira ya kusuasua yatokanayo na sera ziazobadilika kwa kasi za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu nyongeza za ushuru.

    Hapo jana Rais Trump aliliambia baraza lake la mawaziri kuwa kipindi hiki kigumu hakiepukiki lakini akasisitiza wawekezaji wamefurahishwa na maamuzi yake.

    Thamani ya sarafu ya Dola imeshuka ikilinganishwa na sarafu za Ulaya na bei ya mafuta pia imeshuka kwa karibu asilimia nne.

    Katika hali inayoashiria kuendelea kwa mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na China, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya China vimeanza kutoa ujumbe wa kuwahamasisha raia wake kuwa tayari kwa changamoto za kiuchumi zitakazotokana na vita vya ushuru wa kisasi vinavyoendelea kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani.

    Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt, akizungumza na kituo cha habari cha Fox News, alisisitiza msimamo wa serikali ya Marekani wa kulinda maslahi ya kitaifa kwa kuiweka Marekani mbele kiuchumi na kuhamasisha urejeshaji wa ajira kutoka nje ya nchi.

    “Sera ya Ikulu hii ni kuiweka Marekani mbele na kurejesha ajira,” alisema Leavitt.

    “Hatutaruhusu tena bidhaa za bei ya chini kutoka China kuingia kwa wingi katika soko letu huku wao wakizuia bidhaa zetu kuingia kwao.”

    Kwa mujibu wa msemaji huyo, Marekani haiwezi kuendelea kustawi kiuchumi ikiwa itaendelea “kuinyanyua na kuipa nguvu China” kwa kuruhusu uagizaji mkubwa wa bidhaa kutoka taifa hilo la Asia.

    Leavitt aliongeza kuwa licha ya hali hiyo, kuna “sababu kubwa ya kuwa na matumaini kuhusu uchumi wa Marekani,” akibainisha kuwa kampuni nyingi zitaanza kunufaika zaidi kwa kufanya biashara ndani ya mipaka ya taifa hilo.

    Katika hatua ya hivi karibuni, Ikulu ya Marekani imeweka wazi kuwa ushuru mpya kwa bidhaa kutoka China utakuwa asilimia 145 kinyume na asilimia 125 iliyotangazwa awali.

    Maafisa wa Ikulu wameeleza kuwa kiwango kilichotajwa na Rais Donald Trump siku ya Jumatano ni ongezeko la asilimia 20% iliowekwa wiki chache zilizopita dhidi ya bidhaa kutoka China.

    Soma pia:

  18. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja