Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mkuu wa majeshi wa Kenya aliyeaga dunia Francis Ogolla alikuwa nani?
Na Yusuf Jumah
BBC Swahili , Nairobi
Kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Kenya Jenerali Francis Ogolla kimeishtua nchi baada ya rais William Ruto kutangaza habari hizo za kusikitisha siku ya Alhamisi .
Ogolla alithibitishwa kufariki katika ajali ya helikopta eneo la Kaben, Marakwet Mashariki siku ya Alhamisi.
Ogolla aliteuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi katika mabadiliko katika jeshi mnamo Aprili 2023.
Alichukua nafasi kutoka kwa Jenerali Robert Kibochi ambaye aliondoka baada ya kutimiza umri miaka 62.
Kabla ya uteuzi huo Jenerali Ogolla alikuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.
Taaluma yake katika jeshi
Mnamo 28 April 2023, rais William Ruto, alimpandisha cheo Lieutenant General Francis Omondi Ogolla hadi kuwa jenerali na kumteua Mkuu wa majeshi ya Kenya .
Jenerali Francis Omondi Ogolla alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Kenya tarehe 24 Aprili 1984 na akateuliwa kuwa Luteni wa Pili tarehe 6 Mei 1985 na kutumwa kwa Jeshi la Wanahewa la Kenya. Alipata mafunzo ya urubani wa ndege na USAF na kama rubani mkufunzi katika Jeshi la Wanahewa la Kenya (KAF).
Pia alipata mafunzo katika nyanja zingine zikiwemo ujasusi wa picha, kukabiliana na ugaidi na uchunguzi wa ajali.
Jenerali Francis O Ogolla ni mhitimu wa ÉcoleMilitaire de Paris na Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi cha Kenya. Ana Diploma katika Masomo ya Kimataifa na Sayansi ya Kijeshi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton, Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa, Migogoro ya Silaha na Mafunzo ya Amani (Heshima za Daraja la Kwanza) na Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Mafunzo ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alipanda vyeo hadi kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Kenya mnamo 15 Julai 2018 wadhifa ambao alihudumu kwa miaka mitatu. Hapo awali amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Mafunzo, Kamandi na Wafanyakazi ikiwa ni pamoja na Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga la Kenya, Kamanda wa Kambi ya Laikipia Air Base, Afisa Mkuu wa kitengo cha Tactical Fighter Wing, Mkufunzi Mkuu wa Usafiri wa Ndege katika Shule ya Mafunzo ya Anga kwa Jeshi la Anga la Kenya na Afisa wa Dawati la Operesheni katika Jeshi la Wanahewa la Kenya.
Pia alihudumu katika iliyokuwa Yugoslavia kama Mwangalizi na Afisa Habari wa Kijeshi kutoka 1992 hadi 1993, kama mwenyekiti wa Ushirika wa Kijeshi wa Kikristo kutoka 1994 hadi 2004 na Mwenyekiti mwenza wa Chama cha Wakuu wa wanajeshi wa angani wa Afrika kati ya 2018-2019.
Alikuwa na mke Aileen, na amebarikiwa na watoto wawili na mjukuu. Alikuwa akipenda kusoma na kucheza gofu.
CDF au Mkuu wa Majeshi ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa kijeshi katika Jeshi la Ulinzi la Kenya na mshauri mkuu wa kijeshi wa Rais wa Kenya na Baraza la Usalama la Kitaifa.
Rais William Ruto alieleza sababu za kumteua Ogolla kama Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi (CDF).
Kulingana na Ruto, tajriba ya Ogolla iliyodumu kwa zaidi ya miaka 39 ilimfanya kupandishwa cheo hadi afisi kuu katika jeshi la nchi kuchukua nafasi ya Robert Kibochi ambaye alistaafu.
"Katika kuzingatia uteuzi wako, nilitathmini historia yako, ulikotoka, umefanya nini, na safari yako ya kijeshi, na nimeridhika kwamba unastahili," Ruto alisema.
"Wito wangu wa wazi ni wa kikosi kimoja, dhamira moja. Tutakuwa kikosi kimoja kilichounganishwa kwa lengo moja la kutoa Ulinzi na kubaki waaminifu kwa kauli mbiu yetu ya Ulinzi Daima," alisema Ogolla wakati akiapishwa .
Kama sehemu ya dhamira yake, alisema ataendelea kufanya kazi kwa karibu na vyombo vingine vya usalama .