Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gereza la kutisha zaidi duniani: ‘Ukiingia hakuna kutoka’
Gereza la wafungwa 40,000 limejengwa huko El Salvador. Lina ukuta wa kilomia 2. Hata genge maarufu la mafia El Chapo hawakuweza kutoroka kutoka hapo.
Angelica, anayeishi El Salvador, tayari anajua mume wake yuko katika gereza hilo. Picha rasmi za video zilizotolewa na serikali na kupakiwa kwenye mitandao ya kijamii zilithibitisha.
Baada ya kutazama video kwa dakika 25, alimtambua mume wake - anaonekana akipeana mikono na mfungwa mwenzake.
Mumewe hakuwa amevaa chochote zaidi ya kaptula nyeupe. Lakini Angelica hakuwa na shaka kwamba alikuwa Darwin. Hakuwa amemwona tangu kukamatwa kwake miezi 11 iliyopita.
Huu ulikuwa ushahidi wa kwanza wa Angelica kwamba Darwin amefungwa katika gereza kubwa na lenye sifa mbaya huko El Salvador.
Gereza la Secot lilizinduliwa na Rais wa El Salvador, Naib Bukele, Januari mwaka huu. Liko kilomita 74 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, San Salvador. Limekuwa ni 'ishara ya Rais Bukele ya vita vyake dhidi ya magenge'.
Wizara ya Usalama ya El Salvador hivi majuzi ilitangaza takriban watu 68,000 wamezuiliwa tangu Machi 2022. Gereza hili huhifadhi maelfu ya watu ambao hawaruhusiwi kuwasiliana na watu wa nje. Familia nyingi kama ya Angelica zinatafuta jamaa zao kupitia video kama hizi.
Kampeni ya rais Bukele dhidi ya magenge imezua hali ya hatari nchini humo. El Salvador inachukuliwa kuwa moja ya nchi zenye vurugu zaidi ulimwengu.
Vita dhidi ya magenge
Mnamo Januari 2023, watu 1,200 walihojiwa huko El Salvador - asilimia 92 ya waliotoa maoni walimuunga mkono Rais. Mauaji nchini El Salvador yamepungua sana tangu aingie madarakani. Wananchi wa Salvador wanahisi haya ni mabadiliko makubwa.
Mabadiliko haya yanaonekana zaidi katika maeneo ambayo hapo awali yalidhibitiwa na magenge ambapo majambazi yakitishia raia. Walikuwa wakisema, 'angalia, sikiliza lakini funga mdomo wako.' Sasa wananchi wa kawaida wanaweza kupita katika maeneo hayo bila woga au vurugu zozote.
Serikali imesema takriban wafungwa 40,000 wanaweza kuwekwa katika jela ya Sekot. Wanachama wa magenge mawili yanayoshindana wanaweza kuwekwa hapo - genge la Mara Salvatrucha (MS-13) na Barrio 18. Vita kati ya magenge hayo mawili vimeiacha El Salvador na miongo kadhaa ya ugaidi na migogoro ya umwagaji damu.
BBC iliomba mara kadhaa kutembelea gereza hilo, lakini serikali imekuwa ikikataa.
Kabla ya kuzinduliwa kwa gereza hilo, serikali ilitoa baadhi ya video na picha. BBC pia iliwahoji maafisa wa El Salvador na wahandisi waliohusika katika ujenzi wa gereza hilo kwa masharti ya kutotajwa majina.
Jela ya Secot ina jumla ya seli 256. Ina uwezo wa kuhifadhi wafungwa 40,000. Seli moja inaweza kuhifadhi wafungwa 156.
Kuna vyumba vilivyotengenezwa kwa chuma ili wafungwa walale. Kila seli ina beseni mbili za kuogea na kwa ajili ya wafungwa kufulia nguo zao. Pia kuna vyoo viwili. El Salvador ina joto sana lakini hakuna madirisha, feni au viyoyozi katika seli hizi. Kulingana na mamlaka, wafungwa hawa wanaweza tu kutoka nje wakati wa kusikilizwa kesi zao.
Ukosoaji
Kulingana na habari iliyopatikana na BBC, kila seli katika gereza hilo ina upana wa mita 7.4 na urefu wa mita 12.3. Hivyo, kulingana na jumla ya idadi ya wafungwa katika seli, kila mfungwa anaweza kuwa na mita za mraba 0.58 za nafasi. Shirika la Msalaba Mwekundu linapendekeza mita za mraba 3.4 za nafasi kwa kila mfungwa katika seli ya pamoja kama kiwango cha kimataifa.
Kulingana na taarifa zilizotolewa na maafisa wa serikali, hakuna anayeweza kusema ni lini wafungwa wa Sekot wataachiliwa. Haijabainika ni wafungwa wangapi walioko Sekot kwa sasa. Hakuna kitu hata kimoja kinachowekwa Sekot kwa burudani. Hakuna mfungwa anayeruhusiwa kukutana na wanafamilia.
Huu ni ukiukaji wa miongozo ya kimataifa kuhusu haki za wafungwa. Pia, haijabainika iwapo wafungwa hao ni wapya au wamehamishwa kutoka magereza mengine. Kuna uhaba wa taarifa kuhusu jinsi wafungwa wanavyolishwa au kutunzwa.
Hakuna habari au picha za vifaa kama vile jikoni, chumba cha kulia, duka au hospitali. Sekot ina mfumo wa usalama wa hali ya juu.
"Gereza hili ni shimo la saruji na chuma, linalojaribu kuwatupa watu bila adhabu ya kifo," Miguel Sarre, mjumbe wa zamani wa kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mateso, aliiambia BBC.
Antonio Duran, jaji mkuu na mkosoaji mkubwa wa sheria ya dharura ya Rais Bukele, anaonekana kukubaliana na Sarre.
Kumnyima mtu uhuru wake ni kosa linaloweza kuadhibiwa katika nchi inayotawaliwa na sheria, Duran anaamini.
Will Grant wa BBC akiwa na Waziri wa Sheria na Usalama wa Umma wa El Salvador, Gustavo Villatoro, alisema, "tumejitolea kwa watu wa Salvador. Wafungwa huko Cecot hawatatembea tena katika jamii. Tutatayarisha kesi zinazohitajika dhidi yao ili wasirudi."
"Kwetu sisi, Sekot ni mnara mkuu wa haki kuwahi kujengwa. Hakuna cha kuficha," aliongeza.
Ujumbe huo huo pia uliwasilishwa na tweet ya Rais Bukele hapo awali.
"Waambie NGOs zote zinazoshughulikia haki za binadamu kwamba tutawaangamiza wauaji hawa na wamwagaji damu na washirika wao, tutawaweka gerezani na hawatatoka nje," Bukele aliandika kupitia twitter.
Wiki chache zilizopita timu ya BBC ilienda karibu na gereza hilo iwezekanavyo.
'Hata El Chapo asingeweza kutoroka'
Afisa wa polisi katika eneo hilo alitupa habari, "hata mafia wa dawa za kulevya wa Mexico El Chapo hawatoweza kutoroka," afisa wa gereza aliambia BBC. El Chapo ametoroka kutoka magereza kadhaa hapo awali.
Jela imeenea zaidi ya ekari 57. Ina mgawanyiko nane. Kando na hayo, gereza hilo lina kuta mbili za zege. Ina minara 19 ya uchunguzi.
"Vita vya magenge vilipoanza, nilikuwa natumia muda wangu kuwakamata washiriki wa magenge kutoka majumbani mwao. Kwa sasa natumia siku zangu kwenye vituo vya ukaguzi. Wakati mwingine ni wakati wa kunywa kahawa," anasema.
Denis, anayeishi La Campanera, nje ya San Salvador, aliambia BBC: "mji huu haukuwa salama hata kidogo hadi rais alipoanza kampeni hii. Nadhani ulikuwa uamuzi bora zaidi. Bukele ndiye rais bora kuwahi kutokea."
Kwa upande mwingine, Maria mwenye umri wa miaka 23 ana maoni tofauti. Tulikutana naye nyumbani kwake huko El Maniadero. "Ni hatia kuwa kijana huko El Salvador sasa," Maria anasema.
BBC ilizungumza na makumi ya jamaa za wafungwa waliozuiliwa chini ya kile kinachoitwa hali ya hatari. Wanasema - jamaa zao wamechukuliwa kutoka katika makazi yao bila hati yoyote. Wanakamatwa kabla ya kusikilizwa. Utaratibu huu unaweza kuendelea kwa miaka, sio miezi.
Katika mwaka wa kwanza wa kampeni, kulikuwa na mateso na kupigwa katika magereza. Makumi ya wafungwa wamekufa kutokana na ukosefu wa huduma za afya, linadai shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za binadamu Cristosal.
Mnamo Mei 24, kamishna wa haki za binadamu nchini humo, Andres Guzmán Caballero, alikiri wakati wa mkutano na vyombo vya habari kwamba ripoti hiyo ilikuwa "ya kutatanisha".
Alisema, "wakati magenge mawili au matatu yanapohusika katika jela, huwa na mapigano ya wao kwa wao. Inaweza pia kusababisha vifo vya wafungwa. Kila kesi ya kifo kama hicho inapaswa kuangaliwa."
Kulingana na ripoti ya Cristosal, Secot inatia wasiwasi hasa kwa sababu hali ya huko ni mbaya.
"Masharti ya Secot yanaweza kuwa ya kinyama na ya kufedhehesha, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kulifikia gereza hilo," anasema Zaira Navas, inspekta mkuu wa polisi wa zamani wa El Salvador na mkuu wa sheria wa Cristosal.
Hakuna mwanasheria au vyombo vya habari vinavyoweza kwenda huko.