Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hatua saba za Trump zinazompa ushindi Putin katika mazungumzo ya amani ya Ukraine - Politico
Katika juhudi za kuafikia amani na kusitisha mapigano kati ya Urusi na Ukraine, Rais Donald Trump, ameonekana kubadilisha mkondo wa namna anavyoshirikiana na nchi hizi mbili, huku akidhoofisha mustakabali wa mazungumzo ya maridhiano, yaandika gazeti la Politico.
Chapisho hilo la Amerika limeandika kuwa Rais wa Marekani anashinikiza zaidi Ukraine huku akiwa mwenye subira na Urusi kwasababu anaamini, kama vile alivyoambia Volodymyr Zelensky katika ikulu ya Whitehouse , kuwa Ukraine haina ''ushawishi''.
Ukraine ina unyonge kiasi fulani hasa inavyotegemea usaidizi kutoka Washington na Ulaya, yaandika Politico.
Vile vile, kulingana na chapisho hilo Trump amefanya maamuzi na kuchukua hatua kadhaa ambazo zinaonekana zinapiga makumbo msimamo wa Zelensky.
1.Trump ampigia simu Putin
Hatua ya kwanza ambayo inamfanya Rais wa Ukraine aonekane hana mashiko katika mazungumzo yakusitisha mapigano na Moscow, ni Trump kupigia Putin zaidi ya mara moja, na kumleta karibu katika ngazi za kimataifa.
Hii ni baada ya Putin kukaa gizani katika kipindi cha utawala wa Rais aliyeondoka Joe Biden, gazeti hilo la Marekani laandika.
Trump alizungumza na Putin kwa simu kwa zaidi ya dakika 90 na siku ya Alhamisi- baada ya Rais wa Urusi kukataa mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30 ambayo Ukraine ilikubali, muda wa mazungumzo na Putin ulizidi ukilinganisha na ilivyodhaniwa.
Politico linaona kuwa kama Trump angeendelea kuwa kimya kwa muda mrefu zaidi, angekuwa na nguvu zaidi ya kushinikiza Kremlin kwa masharti mengine.
2. Mazungumzo na Urusi bila Ukraine
Mwezi Februari, Marekani na Urusi walikutana huko Saudi Arabia kwa ajili ya kupanga njia za kurejesha ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kurejesha wafanyakazi katika balozi za Washington na Moscow, ushirikiano wa kiuchumi, na kupunguza vikwazo dhidi ya Urusi kutokana na uvamizi wake wa Ukraine.
Gazeti la Politico inaamini kuwa juhudi hizi zingeweza kuokolewa na kutekelezwa ikiwa Urusi na Ukraine zingefikia makubaliano ya amani.
Hata hivyo, Ukraine haikualikwa mezani wala washirika wake ambao ni viongozi wa Ulaya kama ilivyokuwa ikifanyika hapo awali.
Hii ilionyesha wazi kwamba utawala wa Trump ulikuwa unafanya kazi bila ya kushirikiana na washirika wake wa zamani, na hivyo kupunguza matumaini ya kupata suluhu ya pande zote.
3. Makubaliano ya Ukraine
'' Huku Trump akipuuzilia mbali maswali kuhusu ni kipi Urusi itakubali kuachilia katika makubaliano ya amani, lakini kwa upande mwingine, alisisitiza kuwa Ukraine inahitaji kutoa sehemu ya ardhi yake ambayo sasa inadhibitiwa na Urusi'', nikinukuu gazeti hilo.
Mshauri wake wa usalama wa taifa, Michael Walz, alielezea kuwa hiyo ilikuwa ni "sawa," hasa ukizingatia hali ya vita ilivyo sasa baada ya miaka mitatu ya mapigano.
Katika mazungumzo mengine, Trump alizungumzia jinsi Ukraine inavyoweza kudhibiti mikoa yake, ikiwa ni pamoja na mtambo wa nishati ya nyuklia wa Zaporizhzhia, akisema kuwa kama Ukraine inataka kudumisha udhibiti wa kituo hicho, basi Marekani inaweza kuchukua jukumu la kuwekeza hapo baada ya vita.
Trump ameendelea kusisitiza wito kwa Ukraine kulipa dola bilioni 120 ambayo Marekani imetumia kuwapa ulinzi wakati wa vita.
Ili kujinasua Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alikubali kutia saini makubaliano ya kukabidhi rasilimali na miundombinu kama ishara anaunga mkono mchakato wa amani na udiplomasia wa Trump.
''Lakini Urusi haikushinikizwa kufanya hivyo,'' gazeti hilo lasema.
4. Shinikizo kwa Zelensky
Trump amekuwa akionyesha wazi kutaka kumshinikiza Zelensky.
Hii ilijitokeza wazi katika kikao na Zelensky katika ikulu ya White house ambapo Rais huyo wa Ukraine kuelezea shauku aliyokuwa nayo kuhusu nia ya Urusi kumaliza vita.
Kutokana na msimamo mkali wa Zelensky, Rais wa Marekani Trump alisitisha msaada wa kijeshi na kukata mawasiliano ya Marekani kuwapa Ukraine Ujasusi ambao wanauhitaji wakati wa vita.
Alipiga abautani baada ya Ukraine kulegeza msimamo na kukubali pendekezo la kusitisha mapigano na Urusi kwa siku 30.
Jarida la Politico linakumbusha jinsi Trump alivyokubaliana na maoni ya Putin kuhusu uchaguzi nchini Ukraine, akimuita Zelensky aliyechaguliwa kidemokrasia kuwa "dikteta."
5. Kuahirisha mazungumzo kuhusu dhamana za usalama na NATO
Trump amekataa kutoa dhamana za usalama kwa Ukraine baada ya mapumziko ya vita.
Kwa maoni yake, akisema kuwa makubaliano ya madini ya vyuma adimu, ambayo Marekani itapata faida kubwa, ndio dhamana halisi ya usalama.
Alisema kuwa Putin hatothubutu kufanya mashambulizi mapya iwapo Wamarekani wapo nchini Ukraine haswa wakiendelea na shughuli zao za kuvuna rasilimali.
Kupitia mtandao wake wa kijamii, Trump alimtishia Putin kuwa atamuekea vikwazo, na kisha baadaye kusema Ukraine ilikuwa imeanza kuingililia mazungumzo ya kuleta amani nchini humo.
Hata baada ya Putin kukataa pendekezo la mapumziko ya vita, Trump hakumkosoa, badala yake alielezea kuwa kusimamisha mashambulizi ya miundombinu ya nishati ilikuwa ni "hatua nzuri."
6. Kikomo cha uwajibikaji wa Urusi
Baada ya mazungumzo yake na Putin, Marekani ilijiondoa kutoka kwa kundi la kimataifa linalochunguza viongozi wa Urusi wanaoendekeza vita kama vile Putin.
Pia Marekani ikakata fedha kwa Maabara ya Utafiti ya Sayansi ya Binadamu ya Chuo Kikuu cha Yale, ambayo ilikuwa ikichunguza uhamishaji wa watoto wa Ukraine kwenda Urusi.
Hatua hizo ziliibua hisia mseto miongoni mwa mawakili, huku wabunge wa Republican wakikosoa vikali.
Utawala wa Trump uliwajibu kuwa ilikuwa ikitathmini upya mpango huo.
Hata hivyo, gazeti la Politico lilisema kuwa uamuzi huo unashabihiana na maamuzi ya mamlaka za ulinzi kusitisha juhudi za kukabiliana vikali na mashambulio ya mtandaoni ya Urusi na habari potofu.
7. ''Pande zote mbili zina hatia''
Trump 'alidhihaki' mapendekezo ya kushikilia mipaka ya kimaadili, kama vile yale yaliyofanywa na Marekani na Ulaya wakati wa kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Kwa mtazamo wa Trump, aliona kuwa "huwezi kuwa mchezaji mzuri wa maamuzi iwapo una upendeleo upande mmoja."
Lakini wakati huo, Trump alikubali mtazamo wa Putin kuwa vita hivi vilichochewa na hamu ya Ukraine kujiunga na NATO.
Kwa kufanya hivyo, alihalalisha msimamo wa Kremlin kuwa uhuru wa baadhi ya nchi za zamani za Umoja wa Kisovyeti bado ni suala ambalo halijatatuliwa, yaadika gazeti la Politico.
Mazungumzo yaliyofanyika Saudi Arabia
Marekani imefichua kilichozungumzwa katika mkutano wake na Urusi nchini Saudia siku ya Jumatano, tarehe 25 mwezi Machi mwaka huu.
Urusi na Ukraine zimekubali kusitisha mashambulizi ya kijeshi katika Bahari Nyeusi - Marekani
Ikulu ya White House inasema Urusi na Ukraine zimekubali kuhakikisha kupita kwa usalama kwa meli za kibiashara na kusitisha mashambulizi ya kijeshi katika Bahari Nyeusi.
Marekani inasema Urusi ilikubali kuendeleza hatua za kutekeleza marufuku ya mashambulizi dhidi ya vituo vya nishati nchini Ukraine na Urusi.
Nchi hizo mbili pia zimejitolea kusaidia kufanikisha ubadilishanaji wa wafungwa wa vita, kuachiliwa kwa wafungwa wa kiraia na kurudi kwa watoto wa Ukraine waliohamishwa kwa nguvu.
Marekani na Ukraine zitaendelea kushirikiana kuelekea kufikia "amani ya kudumu", na kukaribisha nchi za tatu kusaidia utekelezaji wa makubaliano ya bahari na nishati
Aidha, Marekani ilisisitiza kwa pande zote mbili katika vita kwamba mauaji yanapaswa kukoma na itaendelea kuwezesha mazungumzo.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid