Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Ulaya ina ubavu wa kuisaidia Ukraine kijeshi ikiwa Marekani itakaa pembeni?
- Author, Na Sammy Awami
- Nafasi, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mara baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kufukuzwa Ikulu ya Marekani kufuatia malumbano yake na Rais Donald Trump na Makamu wa Rais JD Vance, viongozi wa Ulaya walituma jumbe nyingi kumuhakikishia kwamba watasimama nae hadi dakika ya mwisho
Siku iliyofuata tu Jumamosi (1 Machi), Zelensky alitua Uingereza, akaonana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kier Starmer na hata kufanya mazungumzo na Mfalme Charles. Siku ya Jumapili akakutana na viongozi wengine wa Ulaya waliokutana London kujadili mustakabali wa usalama wa bara lao
Pamoja na maonyesho yote haya, swali kubwa ni; Ulaya ina ubavu wa kuisaidia Ukraine kijeshi ikiwa Marekani itakaa pembeni?
Jibu la haraka ni; Hapana, haina uwezo huo katika uvamizi huu wa sasa wa Urusi
Uhaba wa bajeti
Kuna vitu vingi Ulaya inahitaji kuweka sawa, muda ni mchache na haina utashi wa kisiasa wa kutosha
Ukianza na bajeti ya kijeshi tu, kwa mujibu wa International Institute of Strategic Studies, bajeti ya kijeshi ya Urusi kama nchi ni kubwa kuliko ile ya bara zima la Ulaya. Wakati Urusi imetenga 6.7% ya pato lake la taifa, wakati Ulaya (wanachama wa Nato ukiondoa Marekani) wanatumia wastani wa 1.6%.
Ili kukabiliana na Urusi, wataalamu wanasema Ulaya itapaswa kuongeza matumizi yake ya kijeshi hadi kufikia wastani wa 3.5% ya pato la taifa la umoja huo, hasa kwa nchi za Mashariki ya Ulaya zilizo karibu na Urusi kama vile.
Tayari tunaona nchi kadhaa za Ulaya zimeanza kuongeza bajeti yao ya kijeshi. Uingereza kwamfano, siku chache zilizopita imetangaza mpango wa kukata pesa inayotuma kwa misaada nje ya nchi na kuielekeza katika bajeti yake ya ulinzi.
Idadi ya wanajeshi na uongozi kwenye uwanja wa vita
Kuhusu wanajeshi walio tayari kupigana, wakati Urusi ina wanajeshi takribani 250,000 walio tayari kupelekwa Ukraine muda wowote, Ulaya haiwezi kutoa wanajeshi 150,000, ambao Zelensky anasema watahitajika kulinda amani na kumzuia Putin asivamie tena.
Viongozi wengi wa Ulaya wamesema wakijitahidi sana, basi wanaweza kupeleka wanajeshi wasiozidi elfu thelathini (30,000).
Ulaya inakabiliwa na ukosefu wa kiongozi mmoja (mtu au ofisi) wa kijeshi. Kwa ujumla Ulaya (wanachama wa Nato) ina wanajeshi wapatao 1.47 ambao wako tayari kupigana, lakini hawana komandi moja ya kuwakusanya na kuwaongoza. Kwasasa Nato inategemea hii kazi kufanywa na Marekani.
Hivyo Marekani akikaa pembeni, Ulaya itakuwa na kazi ya kutafuta kiongozi ambaye anaweza kuvikusanya, kuvijumuisha na kuviongoza vikosi vya nchi zote za Ulaya wanachama wa Nato kuwa kikosi kimoja chenye nguvu, badala ya kila nchi Kwenda kukabiliana na Urusi kama nchi moja moja.
Ulaya ina teknolojia ya kutosha, lakini inahitaji uwekezaji mkubwa kuanza kutengeneza vifaa vikubwa na bora zaidi - hasa vya masafa marefu kama ambavyo Marekani imetoa kwa Ukraine ndani ya miaka hii mitatu
Silaha za anga na utashi wa kisiasa
Nchi za Ulaya pia zinategemea vifaa vya anga vya Marekani na uwezo wake mkubwa wa kukusanya intelijensia, uwezo ambao Ulaya haina.
Hata katika usafirishaji wa silaha, Ulaya imekuwa ikitegemea sana miundombinu na uratibu wa Marekani kufanikisha kusafirisha msaada wa vifaa uliopeleka Ukraine.
Wakati Nato inavamia Libya mwaka 2011, hata kama Ulaya ndio ilikuwa inaongoza mapambapo, walitegema zaidi vituo vya mafuta vya Marekani kujaza vifaa vyao.
Ulaya inahitaji kiongozi katika masuala ya dunia, kama ambavyo Marekani imekuwa. Aidha Ujerumani au Ufaransa inaweza kuchukua nafasi hii, lakini nchi tatu; Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinahitaji kuwa katika ukurasa mmoja, zikazungumza lugha moja na zikawa na utayari wa pamoja kuongoza nchi zingine 27 za Nato katika kuikabili Urusi.
Mbali na uwezo wa kifedha na kijeshi, nchi nyingi za Ulaya zinakabiliwa na mikingamo na mivutano ya kisiasa ndani ya nchi zao, zingine zikiwa na idadi kubwa ya wananchi wasiotaka nchi zao kujihusisha moja kwa moja na vita kwa ujumla na hasa mapigano na nchi kubwa kama Russia.
Utayari wa serikali nyingi za Ulaya kuingia vitani na Urusi kutategemea utashi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla kutoka nchini mwao, jambo ambalo ni changamoto kwa nchi nyingi za Ulaya.
Hizi ni baadhi ya sababu zinazowafanya nchi nyingi za Ulaya kuendelea kuiangukia Marekani itoe hakikisho la ushiriki wake katika kuisaidia Ukraine kupambana na Urusi na kulinda mkataba wa amani ili Urusi isiukiuke.
Kizungumkuti cha NATO
Tangu awamu ya kwanza, Trump amekuwa akitishia kupunguza mchango wa Marekani au hata kujiondoa kabisa uanachama wa Nato (North Atlantic Treaty Organization). Huu ni umoja wa kijeshi unaoundwa na wanachama 32 – Thelathini kutoka Ulaya na wawili (Canada na Marekani) kutoka Amerika ya Kaskazini.
Umoja huu uliundwa mwaka 1949 ukiwa na lengo la kuzisaidia nchi wanachama kiusalamana, huku ukiongozwa na falsafa ya ikiwa mwanachama mmoja atashambuliwa, basi wanachama wote wataingilia kumtetea.
Lakini Marekani ndio mwanachama mwenye misuli mikubwa kuliko wengine wote; kiuchumi, kijeshi lakini hata kwa ushawishi wa kisiasa. Hivyo, Trump alipokuwa akitishia kujiondoa, wanachama wengine wa Ulaya walikuwa na wasiwasi juu ya mustakabali wa usalama wao
Ni katika awamu hii ya pili ya Trump ambapo swali juu ya uwezo wa Ulaya kujilinda limekuwa la muhimu zaidi, hasa kutokana na Marekani kuonekana wazi kwamba haongozwi ten ana falsafa ya kuwalinda na kuwapigania washirika wake kwa hali na mali bali inajali zaidi maslahi yake ya kiuchumi.
Serikali ya Trump imeonekana wazi kuegemea upande wa Urusi, ambao kwa miaka mingi Ulaya na Marekani wameiona kuwa ni adui.
Malumbano kati ya Trump, makamu wake JD Vance na Zelensky yaliyotokea ikulu ya Marekani yameibua wasiwasi mkubwa zaidi kwamba si tu Marekani haina mpango wa kutoa hakikisho la ulinzi kwa ulaya lakini linapokuja suala la maslahi yake ya kiuchumi, ipo tayari kuendana na misimamo ya Urusi
Hata kama nchi nyingi za Ulaya sasa zimeamka na kuukubali ukweli kwamba hawawezi kuitegemea Marekani kuwalinda, jitihada wanazozifanya sasa- kama vile kuongeza misaada yao kwa Ukraine na kuongeza bajeti zao za Ulinzi – hazitoshi na hazitaweza kuisaidia Ukraine katika msukosuko ilionao sasa.
Ikumbukwe pia kwamba Urusi imeendelea kujifunza na kujiimarisha kupitia mapambano yake na Ukraine ndani ya miaka mitatu hii iliyopita. Hivyo wakati Ulaya inaanza kujiimarisha zaidi, Urusi pia inaendelea kujizatiti zaidi.
Jitihada zozote inazozifanya Ulaya kwa sasa, zitakuwa za manufaa miaka mingi ijayo, lakini miaka kadhaa ijayo, bado itaendelea kutegemea hisani ya Marekani.
Imehaririwa na Yusuph Mazimu