Mamia ya waandamanaji wamepambana na vikosi vya usalama katika miji
kadhaa kote nchini Cameroon, saa chache kabla ya matokeo ya uchaguzi wa urais
uliokuwa na upinzani mkubwa kutangazwa.
Polisi waliwarushia vitoa machozi na maji ya kuwasha wafuasi wa mgombea
wa upinzani Issa Tchiroma Bakary katika ngome yake ya Garoua, mji ulioko
kaskazini mwa nchi hiyo.
Waandamanaji hao walikuwa wakilaani kile walichosema ni mpango wa
chama tawala, Cameroon People's Democratic Movement (CPDM), "kuiba
ushindi" kutoka kwa kiongozi wa upinzani.
Tchiroma Bakary amesisitiza kwamba ameshinda uchaguzi wa urais
uliofanyika tarehe 12 Oktoba, akipinga Rais aliye madarakani Paul Biya kwa miaka 43 kuendelea kushikilia madaraka.
Chama cha CPDM kimetupilia mbali madai hayo.
Maandamano hayo yanakuja baada ya Tchiroma Bakary kutoa wito kwa wafuasi
wake nchini humo na wale walio njea kuandamana kwa amani "kuikomboa
Cameroon."
Serikali imepiga marufuku mikusanyiko hadi Jumatatu, wakati baraza la
katiba la Cameroon litakapopanga kutangaza matokeo.
Huko Garoua, maandamano yalianza kwa amani lakini yakageuka ghasia
wakati vikosi vya usalama viliporusha vitoa machozi mitaani ili kuwatawanya
mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika kumuunga mkono Tchiroma Bakary.
Mwandamanaji mmoja alionekana akiwa amebeba bango la kumtaka Rais wa
Marekani Donald Trump kuwasaidia.
"Tuko hapa kudai ushindi wetu. Tunafanya maandamano ya amani,
ambayo ni haki ya kiraia kwa Wacameruni wote - kwa kila mtu," muandamanaji
mwingine alisema.
Wafuasi pia waliingia mitaani katika mji wa kusini-magharibi wa Douala.
"Tunamtaka Tchiroma, tunamtaka Tchiroma," waandamanaji waliimba,
shirika la habari la Reuters linaripoti.
Tchiroma Bakary awali aliambia BBC kwamba hatakubali kuibiwa kura. Alisema timu yake imekusanya taarifa jumla kulingana na matokeo ya vituo
vya kupigia kura.
Katika taarifa yake ya video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii,
Tchiroma Bakary alisema ameshinda uchaguzi huo kwa takriban asilimia 55 ya kura.
Waziri huyo wa zamani wa serikali mwenye umri wa miaka 76 aliachana na Biya
mwenye umri wa miaka 92, ambaye anawania muhula mwingine baada ya miaka 43
madarakani.
CPDM imetupilia mbali madai ya ushindi wa Tchiroma Bakary na maafisa
kadhaa wameelezea kuwa ni kinyume cha sheria kwa sababu ni baraza la katiba
pekee ndilo linaloweza kutangaza matokeo rasmi.
Wafuasi wa upinzani wamedai kuwa uchaguzi wa Oktoba 12 ulikumbwa na
dosari, ikiwa ni pamoja na kujazwa kura katika maboksi.
Majaji katika baraza la katiba wametupilia mbali kesi nane, wakisema
hazina ushahidi wa kutosha au haina mamlaka ya kubatilisha matokeo.
Tchiroma Bakary alikataa kuwasilisha malalamiko katika baraza hilo,
ambalo majaji wake wameteuliwa na Biya, na kuchagua badala yake kujitangaza
kuwa "rais halali."
Mzaliwa wa Garoua, Tchiroma Bakary alikuwa mwanafunzi wa uhandishi nchini
Ufaransa kabla ya kurejea Cameron kufanya kazi katika kampuni ya kitaifa ya
reli.
1984, alitupwa jela, akishutumiwa kuhusika katika jaribio la kumwondoa
madarakani Rais Biya. Licha ya kukana shitaka hilo na hakuwahi kupatikana na
hatia, Tchiroma Bakary alikaa jela miaka sita.
Pia aliwahi kuwa waziri wa mawasiliano kuanzia 2009 hadi 2019.
Akiwa msemaji wa serikali, aliitetea serikali ya Biya wakati wa
machafuko kama vile uasi wa Boko Haram, na jeshi lilipotuhumiwa kuwaua raia.
Lakini mwezi Juni, miezi minne tu kabla ya uchaguzi mkuu, Tchiroma
Bakary alibadilika, akajiuzulu kutoka serikalini na kutangaza kuwa atachuana na
Biya kuwania urais.