Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hatimaye Marekani na China zazungumza, Kwa nini sasa?
- Author, Koh Ewe & Laura Bicker
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinaweza kuisha, huku mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani yakianza mazungumzo nchini Switzerland.
Maafisa wakuu wa biashara kutoka pande zote mbili walikutana siku ya Jumamosi katika mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu tangu Rais wa Marekani Donald Trump aiwekee China ushuru mwezi Januari.
Beijing ililipiza kisasi mara moja na mvutano mkali ukatokea huku nchi hizo mbili zikirundikiana ushuru. Ushuru mpya wa Marekani kwa uagizaji wa bidhaa kutoka China umefikia 145%, na baadhi ya bidhaa zinazouzwa nje ya Marekani kwenda China zinakabiliwa na ushuru wa 125%.
Nani kaanzisha mazungumzo?
Licha ya duru nyingi za ushuru wa kulipiziana kisasi, pande zote mbili zilikuwa zikituma ishara kwamba zinataka kuvunja mkwamo huo. Ila haikuwa wazi ni nani angeanza kuzungumza na mwenzake kwanza.
"Hakuna upande unaotaka kuonekana umesalimu amri," anasema Stephen Olson, mtaalamu wa uchumi katika Taasisi ya ISEAS-Yusof Ishak ya Singapore na msuluhishi wa zamani wa biashara wa Marekani.
"Mazungumzo yanafanyika sasa kwa sababu nchi zote mbili zinaona zinaweza kusonga mbele bila kuonekana zinapigia goti upande mwingine."
Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian alisisitiza siku ya Jumatano kwamba "mazungumzo yanafanyika kwa ombi la Marekani."
Na wizara ya biashara ililiweka jambo hilo kama neema kwa Washington, ikisema inajibu "wito wa Marekani na watumiaji bidhaa."
Utawala wa Trump, hata hivyo, unadai ni maafisa wa China ndio ambao "wanataka kufanya biashara" kwa sababu "uchumi wao unaanguka."
"Wanasema tulianzisha mazungumzo? Nadhani wanapaswa kurejea kusoma faili zao," Trump alisema katika Ikulu ya White House Jumatano.
Lakini wakati mazungumzo yalipokuwa yakikaribia, rais wa Marekani alizungumza lugha ya kidiplomasia zaidi, akisema: "Sote tunaweza kucheza michezo. Nani alitoa wito kwanza, nani hakutoa wito kwanza - haijalishi," aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi. "Kile kinachotokea katika chumba cha mazungumzo ndio cha muhimu."
Muda pia ni muhimu kwa Beijing kwa sababu ni wakati wa ziara ya Xi huko Moscow. Alikuwa mgeni wa heshima siku ya Ijumaa katika gwaride la Siku ya Ushindi ya Moscow kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 ya ushindi katika Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Ujerumani ya Nazi.
Xi alisimama pamoja na viongozi kutoka Kusini mwa Ulimwengu – huo ulikuwa ni ukumbusho kwa utawala wa Trump kwamba China sio tu kwamba ina chaguzi zingine za biashara, pia inajionyesha kuwa ni kiongozi mbadala wa kimataifa.
Hilo limeipa Beijing nguvu inapoelekea kwenye meza ya mazungumzo.
Athari za kiuchumi
Trump anasisitiza kwamba ushuru utaifanya Marekani kuwa na nguvu zaidi, na Beijing imeapa "kupigana hadi mwisho"- lakini ukweli ni kwamba ushuru huo unaziumiza nchi zote mbili.
Viwanda nchini China vimepata pigo, kulingana na taarifa ya serikali. Shughuli ya uzalishaji kwa mwezi Aprili zilishuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu Desemba 2023.
BBC iligundua kuwa wauzaji wa nje wa bidhaa wa China wamekuwa wakiyumba kutokana na ushuru mkubwa, huku bidhaa zikirundikana kwenye maghala, hata wanapojaribu kutafuta masoko mbali na Marekani.
"Nadhani [China] inatambua kuwa mazungumzo ni bora kuliko kutokuwa na mazungumzo," anasema Bert Hofman, profesa katika Taasisi ya East Asia ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Singapore.
"Kwa hivyo wamechukua msimamo na kusema, 'Sawa, tunahitaji kufanya mazungumzo haya."
Na kwa hivyo baada ya likizo ya Mei Mosi nchini China, maafisa huko Beijing wameamua ni wakati mwafaka sasa kuzungumza.
Kwa upande mwingine, mashaka yaliyosababishwa na ushuru yamepelekea uchumi wa Marekani kudorora kwa mara ya kwanza katika miaka mitatu.
Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea bidhaa zilizotengenezwa China. Mmiliki wa kampuni ya toi ya Los Angeles ameiambia BBC "kuna kukatika kwa mnyororo wa ugavi."
Trump mwenyewe amekiri kwamba watumiaji wa bidhaa wa Marekani wataathirika.
Watoto wa Marekani huenda wakawa "na wanasesere wawili badala ya wanasesere 30," alisema katika mkutano wa baraza la mawaziri mwezi huu, "na huenda wanasesere hao wawili watagharimu pesa nyingi zaidi kuliko kawaida.”
Kukubalika kwa Trump pia kumeshuka kutokana na hofu ya mfumuko wa bei na uwezekano wa kushuka kwa uchumi, zaidi ya 60% ya Wamarekani wanaisema amewekeza macho yake sana katika ushuru.
"Nchi zote mbili ziko katika shinikizo la kutoa hakikisho kwa masoko, biashara, na majimbo yao yanayozidi kuwa na wasiwasi," anasema Bw Olson.
Nini kitatokea?
Ingawa mazungumzo hayo yanaleta matumaini, makubaliano yanaweza kuchukua muda kutekelezwa.
Mazungumzo kwa ujumla yanatarajiwa kuchukua miezi, sawa na yale yaliyotokea wakati wa muhula wa kwanza wa Trump.
Baada ya karibu miaka miwili ya ushuru wa nipe nikupe, Marekani na China zilitia saini makubaliano ya "awamu ya kwanza" mapema 2020 kusimamisha au kupunguza baadhi ya ushuru.
Hata wakati huo makubaliano hayo, hayakujumuisha masuala magumu, kama vile ruzuku ya serikali ya China kwa viwanda muhimu au muda wa kufuta ushuru uliosalia.
Kinachoweza kujitokeza wakati huu ni "makubaliano ya awamu kwa awamu" anasema Olson.
"Misuguano ya kimfumo ambayo inaharibu uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na China haitatatuliwa hivi karibuni," Olson anaongeza.
"Geneva itatoa tu taarifa ya awali ya matumaini' kwa mazungumzo ya kweli' na hamu ya kuendelea kuzungumza."