'Ufaransa inatuchukulia kama wajinga' - Ndani ya Niger iliyokumbwa na mapinduzi

Na Mayeni Jones

BBC News, Niamey

Nchi ya Afrika Magharibi ya Niger ni miongoni mwa nchi zenye vifo vingi zaidi duniani kwa mashambulizi ya wanajihadi. Kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwezi Julai, kuna hofu kuwa uamuzi wa kuamuru wanajeshi 1,500 wa Ufaransa walioko nchini kuondoka huenda ukawatia moyo zaidi waasi.

Mwandishi wa BBC Mayeni Jones alipata fursa ya nadra kuingia Niger na alizungumza na serikali, wafuasi wake na wale wanaoipinga.

Adama Zourkaleini Maiga anazungumza kwa upole, lakini macho yake yanaashiria uamuzi thabiti

Mama huyo wa watoto wawili anaishi katika eneo tulivu, la watu wa tabaka la kati la mji mkuu wa Niger Niamey, lakini asili yake ni Tillabéry, mojawapo ya maeneo ambayo yamekumbwa na ghasia zaidi.

"Binamu ya mama yangu alikuwa chifu wa kijiji kinachoitwa Téra," ananiambia wakati wa chakula cha mchana. "Aliuawa miezi saba tu iliyopita.

"Magaidi walikuwa wakimtafuta na walipogundua kuwa amekodi gari ili kukimbia, walimkamata na kumuua. Walimkata koo. Ilikuwa mshtuko mkubwa kwa familia yetu yote."

Adama anailaumu Ufaransa - ambayo imekuwa na wanajeshi 1,500 katika eneo hilo kupambana na wanamgambo wa Kiislamu - kwa kushindwa kuzuia ghasia hizo.

"Hawawezi kutuambia kuwa jeshi la Ufaransa lilifanikiwa," anasema. "Sielewi ni jinsi gani wanaweza kusema wako hapa kusaidia watu kupambana na ugaidi, na kila mwaka hali inazidi kuwa mbaya."

Niger ilionekana kama mshirika wa mwisho wa Magharibi katika Sahel, eneo hili lenye ukame ambalo limekuwa kitovu cha ghasia za kijihadi. Ufaransa na Marekani zina vituo vya askari nchini Niger, ambayo pia ni nyumbani kwa kituo kikubwa zaidi cha ndege za Marekani zisizo na rubani.

Lakini Ufaransa ilipokataa kuitambua serikali mpya ya kijeshi hapa, chuki iliyozuka kutokana na uingiliaji kati wa Ufaransa katika masuala ya ndani ya Niger ilichemka.

Wananchi wengi wa Niger wanaamini Ufaransa imekuwa na fursa ya kuwafikia watu wa juu wa kisiasa na maliasili kwa muda mrefu sana. Wanayaona mapinduzi kama fursa ya suluhu safi, njia ya kurudisha uhuru na kuondoa ushawishi wa Ufaransa.

"Jeshi halijawahi kukaa madarakani kwa muda mrefu nchini Niger," Adama anasema, akimaanisha mapinduzi matano ambayo yameitikisa nchi hiyo tangu uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.

"Jeshi hatimaye litarejea katika ngome zao na kukabidhi kwa serikali bora ya kiraia ambayo itaiongoza Niger kwenye hatima yake," anaongeza.

Hasira ya wananchi iliyofuatia Ufaransa kukataa kuukubali uongozi mpya wa Niger iliongezeka wakati utawala wa kijeshi ulipowataka wanajeshi wake na balozi kuondoka nchini humo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron hapo awali alikataa kutii, lakini sasa anasema ameamua kukubaliana na matakwa ya serikali kwa sababu mamlaka ya Niger "haina nia tena ya kupambana na ugaidi".

'Ufaransa inatuchukulia kama wajinga'

Nje ya kambi ya kijeshi huko Niamey inayotumiwa na wanajeshi wa Ufaransa, mamia ya waandamanaji wamepiga kambi kwa wiki kadhaa, wakizuia vifaa kuwafikia wafanyikazi huko.

Siku ya Ijumaa waandamanaji hufanya maombi ya kukaa ndani. Katika joto kali la mchana, Imam Abdoulaziz Abdoulaye Amadou anaushauri umati kuwa na subira.

"Kama vile talaka kati ya mwanamume na mwanamke inavyochukua muda, ndivyo pia talaka ya Niger kutoka Ufaransa itakavyokuwa," anauambia umati.

Baada ya mahubiri yake, ninamuuliza kwa nini, baada ya miaka mingi ya ushirikiano wa karibu, watu wa Niger wanawakasirikia sana Wafaransa.

"Katika eneo lote la Sahel, Niger ni mshirika bora wa Ufaransa." Anasema. "Lakini ni Ufaransa ambayo sasa inakataa kukubali kile tunachotaka na ndio maana kuna mvutano.

"Ufaransa ingeweza kuondoka kimya kimya baada ya mapinduzi na kurejea kufanya mazungumzo na waasi. Kwa nini Emmanuel Macron sasa anasema hatambui mamlaka yetu, wakati amekubali mapinduzi katika nchi nyingine kama vile Gabon na Chad?

"Hilo ndilo limetukasirisha na tunadhani Ufaransa inatuchukulia kama wajinga."

Wakati wa maombi kunakuwa na zogo huku gari kubwa likiwa limepakiwa na walinzi wenye silaha likiingia.

Gavana mpya aliyeteuliwa wa Niamey, Jenerali Abdou Assoumane Harouna - maarufu kama Plaquette - anajitokeza. Yeye ni jitu la futi 6 na inchi 5, amevaa sare za kijeshi na bereti ya kijani kibichi.

Tunapopigania mahojiano naye, anaelekeza kwa mtayarishaji wangu na kuwaambia umati: "Ona, watu wanasema hatupendi wazungu, lakini tunawakaribisha kwa mikono miwili."

Ananiambia watu wa Niger wanataka nchi yenye ustawi, fahari na uhuru na kwamba watu wa nje wanapaswa kuheshimu mapenzi yao. Ninapouliza kama utawala wa kijeshi unaweza kuweka nchi yake salama dhidi ya magaidi, anajibu kwamba vikosi vya Niger vimekuwa vikiwalinda watu wao, na vinaweza kufanya hivyo bila washirika wa kigeni.

Lakini wale wanaopinga utawala huo wanahofia kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa kunaweza kuwa mbaya kwa Niger na eneo zima.

"Katika mapambano dhidi ya magaidi, Ufaransa ni mshirika mkuu ambaye hutoa taarifa nyingi za kijasusi ambazo hutusaidia kuwapiga magaidi," Idrissa Waziri mwenye makazi yake Paris, msemaji wa zamani wa Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum, ananiambia kupitia Zoom.

"Kuondoka kwa haraka kwa Wafaransa kumesababisha kuzorota kwa hali ya usalama nchini Mali na Burkina Faso. Ufaransa siku hizi imekuwa kisingizo cha kuwatoa watu mitaani, ikilaumiwa kwa matatizo yetu yote.

"Ufaransa sio tatizo, tatizo leo ni jaribio hili la mapinduzi ambalo ni hatua muhimu ya kurudi nyuma kwa Niger."

Kwa Fahiraman Rodrigue Koné, meneja wa mradi wa Sahel katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama yenye makao yake makuu Afrika Kusini, ni mapema mno kusema iwapo kuondoka kwa Ufaransa kutasababisha ukosefu wa usalama zaidi nchini Niger na Sahel nzima.

Katika nchi jirani ya Mali, kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni na wa Umoja wa Mataifa kumefuatiwa na kuongezeka kwa ghasia za waasi wa Kiislamu na makundi ya waasi. Lakini Bw Koné anasema kuna tofauti za kimsingi kati ya nchi hizo.

"Tofauti na Mali, jeshi la Ufaransa lilichukua jukumu la kuunga mkono zaidi Niger, kusaidia wanajeshi wa ndani katika nafasi ndogo zaidi," anasema. "Jeshi la Niger tayari lilikuwa na uzoefu mkubwa wa kupambana na makundi ya kigaidi, hasa katika eneo la mashariki dhidi ya Boko Haram."

Anaongeza kuwa vikosi vya jeshi vya Niger vipo zaidi katika eneo lao kuliko vikosi vya Mali. Nchini Mali, makundi ya kigaidi yanaweza kuteka maeneo makubwa ya kaskazini mwa nchi, ambapo serikali na jeshi havikuwepo.

Kufuatia tishio kundi la kanda hiyo Ecowas kwamba lingeivamia Niger ikiwa Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum hatarejeshwa, Mali, Burkina Faso na Niger zilianzisha muungano tarehe 16 Septemba.

Katika muungano wa usalama wa Sahel, walikubaliana kusaidiana dhidi ya uvamizi wa kutumia silaha kutoka nje. Bw Koné anadhani hili linaweza kubadilisha hali.

"Kukosekana kwa ushirikiano kati ya nchi hizo tatu ilikuwa mojawapo ya sababu za makundi ya kigaidi kuvuka kwa urahisi kutoka eneo moja hadi jingine," anasema. "Tayari kumekuwa na operesheni mbili au tatu za pamoja za kijeshi kati ya nchi hizi tatu. Kuongezeka kwa ushirikiano huu kunaweka shinikizo la kweli kwa waasi."

Pia anafikiri muungano huo unaweza kusaidia kushiriki mazoezi bora kutoka Niger hadi nchi nyingine hizo mbili.

Mwaka jana, vifo vinavyotokana na ugaidi nchini Niger vilipungua kwa 79% kulingana na Global Terrorism Index; ilhali nchi jirani za Mali na Burkina Faso zimekuwa sehemu mbili kuu za mashambulizi ya kigaidi. Asilimia 90 ya ghasia za mwaka jana zinazohusiana na itikadi kali za Kiislamu katika Sahel zilitokea katika nchi hizo mbili.

"Sababu ya utawala wa Bazoum kuwa na mafanikio katika kupunguza vifo nchini Niger ni kwa sababu ulianzisha mbinu ya kiujumla zaidi: kuchanganya mkakati wa kijeshi na ushirikishwaji wa jamii na maendeleo ya kijamii na kiuchumi," Bw Koné anasema.

Lakini licha ya mafanikio yake, mchakato huu haukupendwa na kila mtu, huku baadhi ya wanajeshi wakiiona kama serikali kuwa laini kwa magaidi na kuhimiza kutokujali. Haijulikani ikiwa uongozi wa kijeshi utaendelea kwa njia ile ile.

Pia ni vigumu kupima ni kiasi gani cha uungwaji mkono wa Rais Bazoum huko Niamey.

Ukaribu wake na serikali ya Ufaransa umewakasirisha wengi, lakini tulijitahidi kupata wafuasi wake, au yeyote aliyepinga uamuzi wa kuifukuza Ufaransa, kuzungumza nasi kwa rekodi. Watu wengi walionekana kuogopa sana matokeo.

Haikusaidia kwamba jeshi lilifuata kila hatua ya timu ya BBC nchini, na kufahamu kile waliohojiwa walituambia.

Kuondoka kwa Ufaransa haimaanishi mwisho wa ushirikiano wa Niger na mataifa yenye nguvu ya magharibi. Bado kuna wanajeshi wa kigeni nchini Niger, wakiwemo wale kutoka Marekani.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin aliwaambia waandishi wa habari nchini Kenya siku ya Jumatatu kwamba nchi yake bado haijafanya mabadiliko yoyote muhimu kwa vikosi vyake vya kijeshi nchini Niger.

Lakini alisema wataendelea kutathmini hali ya huko na hatua zozote zitakazochukuliwa zitaweka kipaumbele malengo yao ya kidemokrasia na usalama.

Wakati Sahel ikijipata katika mstari wa mbele wa vita dhidi ya ugaidi, maamuzi yatakayotolewa na watawala wa kijeshi huko yatakuwa muhimu kwa kuenea kwa itikadi kali za Kiislamu katika eneo hilo kubwa.