Mapinduzi Niger: Historia ya mapinduzi manne Niger tangu uhuru

Kiongozi wa mapinduzi ya Kijeshi ya Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani ametangaza mpango wa mpito wa miaka mitatu; katika hotuba yake kupitia kituo cha runinga cha serikali. Mkuu wa jeshi lililompindua Rais Mohammed Bazoum mwezi uliopita amesema nchi yake haitaki vita lakini itajilinda dhidi ya uingiliaji kati wa kigeni.

Ni baada ya wapatanishi wa Afrika Magharibi, ECOWAS kuingia Niger kwa mazungumzo ya amani katika juhudi za mwisho za suluhu ya kidiplomasia. ECOWAS imetoa dokezo kwamba inaweka tayari vikosi vya kikanda.

Ujumbe wa ECOWAS pia ulifanya mkutano mfupi na rais aliyepinduliwa, Mohammed Bazoum, ambaye bado yuko kizuizini tangu mapinduzi.

Tangazo la Tchiani linakuja wakati mamia ya watu hasa vijana, wakiandikishwa kujiunga na kikosi cha kujitolea ikiwa Niger itaingiliwa kijeshi.

Urusi imetoa onyo kwamba uingiliaji kati wa kijeshi kwa Niger utasababisha hasara ya muda mrefu. Kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Urusi, uingiliaji kati kama huo ungevuruga eneo la Sahel kwa ujumla.

Urusi haiungi mkono mapinduzi hayo lakini Marekani inasema kundi la Wagner limekuwa likitumia fursa ya kukosekana kwa utulivu kujiimarisha. Ufaransa na Marekani zina kambi za kijeshi nchini Niger ambazo huendesha operesheni dhidi ya makundi ya wanajihadi katika eneo hilo kubwa.

Historia ya Mapinduzi Niger

1974

Aprili 1974, Luteni Kanali Seyni Kountche aliongoza mapinduzi ya kijeshi, na kumaliza utawala wa miaka 14 wa Hamani Diori, alisimamisha katiba ya nchi na kuvunja Bunge la Kitaifa. Kountche aliunda Baraza Kuu la Kijeshi (SMC) lenye wanachama 12 ambalo lilidhibiti masuala ya serikali.

Baadhi ya ripoti, zinaeleza takriban watu 20 waliuwawa katika mapinduzi hayo.

1996

Maafisa wa jeshi walifanya mapinduzi ya kuwapindua Rais Mahamane Ousmane na Waziri Mkuu Hama Amadou mwezi Januari, 1996 wakisema mkwamo wa kisiasa ulitishia mageuzi ya kiuchumi. Mapinduzi hayo yalisababisha hasira ya mkoloni wa zamani Ufaransa.

Luteni Kanali Ibrahim Bare Mainassara, mkuu wa majeshi, akawa kiongozi wa nchi na kusema lengo la mapinduzi ni kuruhusu mwanzo mpya na sio kumaliza demokrasia ya vyama vingi.

1999

Mainassara aliuawa mwezi Aprili na wanajeshi walioasi katika shambulizi la kuvizia katika uwanja wa ndege wa Niamey, na kufungua njia ya mapinduzi ya tatu katika historia ya nchi hiyo yenye misukosuko.

Daouda Malam Wanke, kamanda wa kikosi cha ulinzi wa rais, alichukua mamlaka kabla ya kutangaza kuwa kutakuwa na rais aliyechaguliwa na kurejea kwa utawala wa kiraia ifikapo 2000.

Mamadou Tandja alishinda uchaguzi wa rais wa Niger, akimshinda Mahamadou Issoufou, waziri mkuu wa zamani. Waangalizi wa kimataifa waliuita uchaguzi uliofuata baada mapinduzi ya 1999 kwa ujumla ulikuwa huru na wa haki.

2010

Kundi la viongozi wa kijeshi wanaojiita Baraza Kuu la Kurejesha Demokrasia (CSDR), wakiongozwa na Jenerali Salou Djibo, walimkamata Tandja na mawaziri wake baada ya mapigano ya risasi.

Katiba ilisimamishwa na vyombo vyote vya dola kufutwa. Serikali ya kijeshi iliahidi kuigeuza Niger kuwa "mfano wa demokrasia na utawala bora" baada ya kumshutumu Tandja kwa kuifanyia katiba marekebisho.