Bamenda: Mji wa Cameroon ambapo biashara ya majeneza ndiyo ilioshamiri

Mji wa Bamenda wakati mmoja ulikuwa mji uliostawi lakini sasa umevurugwa na vita vya miaka mitano kati ya watu wanaozungumza kiingereza wanaotaka kujitenga na wale wanaozungumza Kifaransa ambao wanaoongoza serikali.

Mji wa Bamenda ni mji uliokufa. Ni bishara ya majeneza pekee ilioshamiri. Miili hutupwa kila mahali mara kwa mara katika mji ,vyumba vya kuhifadhia maiti , barabarani na kwenye mito.

Wafanyakazi wa baraza la mji huo huokota miili hiyo na kuifanyia maziko.

‘’Ni baraka kuzikwa, sio tu na familia na marafiki’’, anasema mfanyakazi wa maziko wakati anapochukua majeneza 10 ya bei rahisi kutoka kwa chumba cha mzishia.

Mahitaji ya mtindo wa majeneza hayo yaliokuwa na sifa umeshuka – yakiundwa kama biblia, magari au chupa za pombe ili kuonesha hali ya maisha au mahitaji ya mwisho ya mfu.

Majeneza ambayo yalikuwa yakiuzwa kwa $1,500, au £1,270 hayana soko kwasababu hakuna anayeweza kujyanunua. Wengi wao wanaweza kununua majeneza ya ghrama ya faranga 50,000 , kulingana na mfanyakazi wa chumba cha mazishi.

Mazishi ya mara kwa mara ya vijana na wavulana ni ukumbusho wa kikatili wa mzozo katika mikoa inayozungumza Kiingereza ya Cameroon Kaskazini-Magharibi na Kusini-Magharibi.

Katika miaka mitano tu, mzozo huo umegharimu makumi ya maelfu ya maisha, huku ukilazimisha zaidi ya milioni moja kukimbilia maeneo yanayozungumza Kifaransa na wengine 80,000 kukimbilia hifadhi katika taifa jirani la Nigeria

Vita hivyo vina mizizi yake katika malalamiko ambayo yalianza tangu mwisho wa ukoloni, wakati eneo lililotawaliwa na Waingereza liliunganishwa na maeneo ya Ufaransa kuunda kile ambacho sasa kinaitwa Cameroon.

Raia wengi wa Cameroon wanaozungumza Kiingereza wamehisi kutengwa tangu wakati huo na wamepinga kile wanachoona kama majaribio ya serikali - inayotawaliwa na watu wengi wanaozungumza Kifaransa - kuwalazimisha kuacha maisha yao, pamoja na lugha yao, historia na elimu na mifumo ya sheria.

Mvutano uliongezeka mwaka wa 2016 wakati makumi ya maelfu ya watu huko Bamenda na maeneo mengine yanayozungumza Kiingereza walipoanzisha mfululizo wa maandamano dhidi ya matumizi ya Kifaransa katika shule na mahakama zao, pamoja na kushindwa kuchapisha nyaraka za serikali kwa Kiingereza, ingawa ni lugha rasmi.

Huku serikali ikitoa amri kwa vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na maandamano hayo badala ya kuingia katika mazungumzo ya kutatua kero zao, vijana wa kiume walichukua silaha mwaka uliofuata kudai nchi huru ya Ambazonia, kama wanavyoita mikoa miwili inayozungumza Kiingereza.

Sasa, magari ya kijeshi - ikiwa ni pamoja na yale yaliyo na bunduki - mara kwa mara hushambulia Bamenda.

Wakaazi wanasema wanajeshi huvamia nyumba, kukamata, kuchoma moto masoko na hata kuonyesha miili ya wahasiriwa wao, wakiwemo makamanda wa wanamgambo, kwenye makutano makubwa ili kuwaonya wakaazi dhidi ya kujiunga na wapiganaji wanaotaka kujitenga.

Vikosi vya serikali pia vimepata hasara kubwa katika mzozo huo, huku miili ya wanajeshi walioshambuliwa wakiondolewa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha wanajeshi katika mji mkuu, Yaoundé, kila Alhamisi na Ijumaa.

Wajane wakiomboleza mbele ya mistari mirefu ya majeneza yaliyotundikwa kwenye bendera ya Cameroon, kabla ya wanajeshi hao kuzikwa huku kukiwa na sherehe za mazishi ya kijeshi.

Wapiganaji wanaotaka kujitenga pia wamepata sifa mbaya kwa ukatili dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na kuwakata vichwa na kuwatesa wanawake ambao wanawalaani kwa "kusaliti mapambano", wakiwaita "miguu myeusi" - neno ambalo linasambazwa mara kwa mara kuhusu sasa.

Wanasambaza video za ukatili huu ili kuwaonya watu kuhusu adhabu inayowakabili iwapo watashukiwa kushirikiana na vikosi vya usalama.

Siku za Jumatatu, Bamenda unakuwa "mji wa kiroho" huku barabara zikiwa tupu na masoko yakiwa yamefungwa - sehemu ya kampeni ya kutotii uchumi wa raia uliyoanza kabla ya mapambano ya kutumia silaha. Siku hizi, wakaazi wanaothubutu kupuuza agizo la kufunga maduka yao hupigwa risasi au kuona maduka yao yakichomwa moto .

Wanajeshi na polisi pia hutoweka mitaani, ili wasiwe shabaha laini kwa wapiganaji wanaotaka kujitenga ambao wana uwepo mkubwa katika jiji hilo.

Wanaojitenga pia waliamuru kufungwa kwa shule zote miaka minne iliyopita kama sehemu ya kampeni yao. Shule chache zimesalia wazi kwa ujasiri, lakini watoto hawathubutu kuvaa sare.

Wanajeshi hutekeleza amri ya kutotoka nje karibu kila usiku katika jiji hilo, na kusababisha mikahawa yake mingi, baa na vilabu - vilivyojulikana kuwa bora zaidi nchini Cameroon - kufunga biashara.

Mkazi wa muda mrefu, Peter Shang, ambaye wakati fulani alipenda maisha katika jiji hilo, anasema watu sasa wanachukua siku moja baada ya nyingine: "Maisha ni bahati nasibu. Mambo mengi sana yanakukumbusha kuhusu kifo kisichotarajiwa. Unazungumza na mtu leo ​​na kesho hayupo tena. ."

 Kwa Marie Clair Bisu, kuna mpangilio mzuri - anaona zaidi mume wake, anafika nyumbani kabla ya amri ya kutotoka nje.

"Sasa amegundua watoto wake. Huyu ni mtu ambaye alikuwa akichelewa kurudi wakati fulani akiwa amelewa na alikuwa anaelekea kulala tu. Sasa anaweza kucheza na watoto na kuangalia vitabu vyao. Mgogoro huu umetukutanisha," anasema.

"Tatizo pekee ni kwamba milio ya risasi huwa inaharibu usiku wetu."

Na baada ya usiku wa milio ya risasi, wakazi wanapaswa kupiga simu kadhaa na kusikiliza trafiki ili kuangalia hali iko salama kabla ya kujitosa. Hata hivyo, milio ya risasi imekuwa jambo la kawaida sana huko Bamenda wakati wa mchana hivi kwamba watu hawatoroki mara moja wanaposikia sauti hiyo.

"Tungekula nini ikiwa tutaendelea kutoroka? Nina watoto wa kulisha," muuza mboga anasema.

"Tunapiga mbizi kwa urahisi na kurudi kwenye biashara wakati milio ya risasi inaposita."

Mwanamke mwingine anasema mtoto wake amezoea sauti ya risasi hivi kwamba anajua ni nani anayefyatua risasi.

"Binti yangu ana umri wa miaka saba na anaweza kujua kama sauti hizo ni za bunduki za jeshi au bunduki za AK-47 za 'The Boys'," anasema, akimaanisha wapiganaji wanaotaka kujitenga.

Baadhi ya watawa ambao ninakutana nao kando ya barabara katikati ya jiji wanasema wanasubiri teksi kwenda kwenye Kituo cha watoto yatima cha Abangoh.

Vita hivyo vimeshuhudia mlipuko wa mimba za utotoni zisizotarajiwa, wanasema - huku wasichana ambao wamelazimika kukimbia makazi yao wakiwa wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia na kunyanyaswa na pande zote mbili. Mmoja kwa hasira anasema: "Ubakaji kama silaha ya vita ni wa kudharauliwa."