Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Paul Biya ashinda uchaguzi uliokumbwa na utata Cameroon

Biya iliingia madarakani kwa mara ya kwanza mnamo 1982, matokeo haya ya uchaguzi sasa yanamaanisha kuwa ataendelea kutawala hadi 2032.

Muhtasari

Moja kwa moja

Rashid Abdallah & Mariam Mjahid

  1. Papa Leo kuzuru miji minane katika safari ya kwanza nje ya nchi

    Papa Leo atatembelea miji minane nchini Uturuki na Lebanon baadaye mwaka huu, Vatican ilisema Jumatatu ya tarehe 27 Mwezi Oktoba mwaka huu.

    Itakuwa safari yake ya kwanza nje ya Italia kama papa, na anatarajiwa kutoa wito wa amani katika eneo lote.

    Leo, papa wa kwanza wa Marekani, atazuru Uturuki kuanzia Novemba 27 hadi 30 na kisha atakuwa Lebanon kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 2.

    Mtangulizi wa Leo Papa Francis alikuwa amepanga kuzuru nchi zote mbili lakini hakuweza kwenda kwa sababu ya afya yake kuwa mbaya.

    Francis alifariki Aprili 21 na Leo alichaguliwa kuwa papa mpya Mei 8 na makadinali wa dunia.

    Leo pia atakutana na Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan katika mji mkuu Ankara, atatembelea Msikiti wa Blue huko Istanbul, na ataadhimisha Misa ya Kikatoliki katika uwanja wa Volkswagen Arena wa Istanbul.

    Kusafiri ng’ambo kumekuwa sehemu kubwa ya upapa wa kisasa, huku mapapa wakitafuta kukutana na Wakatoliki wenyeji, kueneza imani, na kufanya diplomasia ya kimataifa.

    Safari za kwanza za papa mpya kwa kawaida huonekana kama dalili ya masuala ambayo papa anataka kuangazia wakati wa utawala wake.

    Uturuki na Lebanon ni nchi zenye Waislamu wengi, na Francis alitilia mkazo sana mazungumzo ya Waislamu na Wakatoliki wakati wa utawala wa miaka 12 uliojumuisha safari 47 nje ya nchi.

    Kauli mbiu rasmi ya safari ya Leo Lebanon ni "Heri wapatanishi".

    Soma pia:

  2. Kiongozi wa upinzani nchini Cameroon asema nyumba yake inashambuliwa

    Kiongozi wa upinzani nchini Cameroon Issa Tchiroma Bakary anasema watu wawili wameuawa na wavamizi mbele ya nyumba yake huko Garoua, huku mvutano ukizidi baada ya uchaguzi.

    Katika chapisho kwenye mtandao wake wa kijamii, alisema raia waliopiga kambi nje ya nyumba yake walikuwa wakipigwa risasi "karibu." "Heri mniue lakini nitaikomboa nchi hii kwa njia yoyote ile," Tchiroma Bakary alitangaza, akielezea vitendo hivyo kama "udubutu uliyopitiliza wa uvunjaji wa sheria"

    Aliweka mtandaoni picha na video ya watu wenye silaha wakiwa juu waliokuwa juu ya nyumba wakifyatua risasi mara kadhaa.

    BBC haijathibitisha uhalisia wa video na picha hizo, au majeruhi waliotajwa.

    Matukio haya yanajiri baada ya Rais aliye madarakani Paul Biya akitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa takribani asilimia 54 ya kura

    Upinzani ulitangazwa kuwa wa pili, kwa asilimia 35.

    Maandamano yameripotiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa huku baadhi ya raia wakihofia kuwa taifa hilo la Afrika ya Kati lhuenda likatumbukia katika mgogoro wa baada ya uchaguzi.

  3. Kenya, Tanzania kukabiliwa na dhoruba ya tropiki inayojulikana kama 'Chege' - KMD

    Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya (KMD) imetahadharisha kwamba mvua kubwa inatarajiwa kunyesha katika pwani ya kusini kutokana na dhoruba ya kitropiki inayoitwa “Chenge”.

    Dhoruba hii, inayojulikana kama Chenge residual depression, ni eneo la shinikizo la chini katika Bahari ya Hindi, likisogea magharibi kwa kasi ya 11 km/h, takriban kilomita 500 kaskazini mwa Madagascar, likiwa na upepo wa 55 km/h, milipuko hadi 75 km/h, na shinikizo karibu na 1000 hPa.

    KMD imesema katika taarifa Jumapili kuwa dhoruba inaendelea kudhoofika wakati ikisogea magharibi kupitia Kituo cha Kaskazini cha Mozambique, lakini ukaribu wake na pwani unaweza kuathiri hali ya hewa nchini Kenya na baadhi ya maeneo ya Tanzania.

    “Mvua kubwa inatarajiwa kunyesha sehemu mbalimbali za nchi, huku upepo mkali wa zaidi ya 25 knots uwezekano kufika pwani ya kusini Jumatatu na Jumanne,” taarifa hiyo ilisema.

    Wakazi wa maeneo haya, hasa wanaojihusisha na shughuli za baharini, wametakiwa kuwa makini, kuwa macho, na kuchukua tahadhari zote zinazohitajika.

    Soma pia:

  4. Uchaguzi Cameroon: Maandamano ya vurugu yazidi huko Douala - ripoti

    Maandamano yamezuka huko Douala, mji mkuu wa kiuchumi wa Cameroon, kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.

    Picha zilizochapishwa na kituo cha habari cha Mimi Mefo Infos, zinaonyesha watu kadhaa wakikimbia barabarani, wakiimba jina la Issa Tchiroma Bakary kwa pamoja.

    Shirika la Habari la Cameroon lilichapisha video, nje inayoonyesha jengo la baraza lililoharibiwa, linalodaiwa kushambuliwa na waandamanaji.

    Rais mteule Paul Biya bado hajawahutubia wananchi wa Cameroon baada ya kuchaguliwa tena Jumatatu, lakini chama tawala kimepongeza ushindi wake "chini ya ishara ya ukuu na matumaini" katika machapisho ya mtandaoni.

    Hakujawa na maoni yoyote kutoka kwa serikali kuhusu ripoti kwamba watu wenye silaha wamefyatua risasi na kuua watu wawili karibu na nyumba ya mshindi wa pili Issa Tchiroma Bakary.

    Akizungumza katika kumuunga mkono rais siku ya Jumatatu, mpiga kura kwa jina Serge Pascal Eyango aliambia shirika la habari la Reuters:

    "Kati ya mikoa 10 ya Cameroon, Rais wa Jamhuri alishinda saba. Na mgombea ambaye alijaribu kufanya jambo muhimu katika mikoa mitatu, Issa Tchiroma [Bakary], pongezi kwake. "Lakini... inathibitisha ni kwa kiasi gani watu wa Cameroon bado wanamuunga mkono mkuu wao wa nchi. Hilo ndilo jambo muhimu. Yeye ni mtu wa amani, sura inayounganisha, baba kwa watoto, na bado tuna matumaini makubwa kwake. Hilo ndilo tu tulilotarajia."

    Soma pia:

  5. Mali yafunga shule na vyuo vikuu nchini kote kufuatia uhaba mkubwa wa mafuta

    Serikali ya Mali imesimamisha masomo katika shule na vyuo vikuu vyote nchini humo kufuatia uhaba mkubwa wa mafuta uliosababishwa na wanamgambo kuzuia uingizaji wa bidhaa za mafuta nchini.

    Waziri wa Elimu, Amadou Sy Savane, ametangaza kuwa taasisi zote za elimu zitasalia kufungwa hadi tarehe 9 Novemba, akieleza kuwa walimu, wahudumu na wanafunzi wamekosa usafiri kutokana na hujuma zinazofanywa na wanamgambo hao.

    Waziri Savane aliongeza kuwa serikali inafanya kila juhudi kumaliza mzozo huo ili masomo yaanze tena kuanzia tarehe 10 mwezi Novemba.

    Kwa wiki kadhaa sasa, Mali imekumbwa na uhaba wa mafuta, hasa katika mji mkuu Bamako, baada ya wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu wanaohusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda kuanza kushambulia malori ya mafuta katika barabara kuu za nchi hiyo.

    Kwa kuwa Mali haina bandari, bidhaa zote za mafuta husafirishwa kwa malori kutoka nchi jirani kama Senegal na Ivory Coast.

    Hali hiyo imesababisha foleni ndefu katika vituo vya mafuta jijini Bamako, huku barabara ambazo kwa kawaida huwa na shughuli nyingi sasa zikiwa kimya na tupu.

    Serikali ya kijeshi inayoongozwa na Jenerali Assimi Goïta, ambaye alitwaa madaraka kupitia mapinduzi ya mwaka 2021, iliwahakikishia raia hivi karibuni kwamba uhaba huo wa mafuta ni wa muda mfupi.

    Hata hivyo, hali imeendelea kuzorota zaidi ya ilivyotarajiwa. Wiki iliyopita, ubalozi wa Marekani mjini Bamako ulitangaza kuwa utaondoa wafanyakazi wake wasio wa lazima pamoja na familia zao kutokana na kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama na athari za uhaba huo wa mafuta, ambao umelemaza usafiri na huduma za umeme nchini.

    Licha ya jeshi kushika hatamu za uongozi, wanamgambo wenye misimamo mikali wameendelea kudhibiti maeneo mengi ya kaskazini na mashariki mwa Mali.

    Baada ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani (MINUSMA) na vikosi vya Ufaransa kuondoka nchini humo, serikali ya Jenerali Goïta sasa inategemea mamluki wa Urusi kushughulikia masuala ya usalama nchini humo.

    Soma pia:

  6. Watu wapigwa risasi nje ya nyumba ya Tchiroma Bakary - ripoti

    Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi karibu na makazi ya Tchiroma Bakary katika mji wa Garoua, mwandishi wa habari wa eneo hilo aliyepo kwenye eneo la tukio ameiambia BBC.

    Milio ya risasi ilisikika wakati mwandishi wa habari akiongea kwenye simu.

    Wakati huo huo, Tchiroma Bakary aliandika kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba risasi zilikuwa zikipigwa kuelekea kwa raia waliokusanyika nje ya nyumba yake.

    Mamlaka bado haijatoa maoni yoyote kuhusu ripoti hizo.

    Soma pia:

  7. Habari za hivi punde, Paul Biya atangazwa mshindi wa uchaguzi Cameroon

    Baraza la katiba la Cameroon limemtangaza Rais aliye madarakani Paul Biya kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa karibu asilimia 54% ya kura.

    Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Biya alipata asilimia 53.66 ya kura, huku mpinzani wake mkuu na aliyekuwa mshirika wake wa zamani, Issa Tchiroma Bakary, akipata asilimia 35.19.

    “Mgombea Biya Paul ametangazwa kuwa Rais wa Jamhuri, baada ya kupata wingi wa kura halali zilizopigwa,” alisema Clement Atangana, Rais wa Baraza la Kikatiba.

    Ushiriki wa wapiga kura ulikuwa asilimia 57.76, huku asilimia 42.24 wakijiondoa katika mchakato wa kupiga kura.

    Jumla ya watu zaidi ya milioni nne walishiriki katika uchaguzi huo. Wagombea kumi walikuwa wakigombea urais, na Biya ambaye hajawahi kushindwa katika uchaguzi wowote tangu aanze kutawala mwaka 1982 alionekana tangu awali kuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

    Hata hivyo, matokeo haya yanapingana na madai ya Issa Tchiroma, ambaye kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, alijitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

    Katika mahojiano ya hivi karibuni na BBC, Tchiroma alisisitiza kwamba amemshinda bosi wake wa zamani, Paul Biya, akidai kwamba uchaguzi ulighubikwa na udanganyifu mkubwa na dosari za wazi katika uendeshaji wake.

    Madai hayo yamechochea hasira na maandamano katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo hadi sasa watu wasiopungua watano wameripotiwa kuuawa.

    Waandamanaji wengi wamekuwa wakisisitiza madai ya Tchiroma kwamba yeye ndiye mshindi halali.

    Serikali imetaja maandamano hayo kuwa haramu, na imewakamata viongozi kadhaa wa upinzani pamoja na wanaharakati.

    Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa wimbi hili jipya la maandamano linaweza kuisukuma Cameroon taifa lililokuwa likijulikana kwa utulivu wake wa kisiasa kuelekea kwenye ghasia na machafuko ya kisiasa, endapo matokeo ya uchaguzi hayatakubalika kama yanayoakisi matakwa ya wananchi.

    Biya iliingia madarakani kwa mara ya kwanza mnamo 1982, matokeo haya ya uchaguzi sasa yanamaanisha kuwa ataendelea kutawala hadi 2032.

    Soma pia:

  8. Vikosi vya kimataifa havitakubali kulazimisha amani Gaza - Mfalme wa Jordan

    Nchi nyingi hazitakubali jukumu la “kulazimisha” amani Gaza endapo zitatumwa chini ya mpango wa kusitisha mapigano wa rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Mfalme Abdullah wa Jordan katika mahojiano maalum na BBC.

    Kupitia mpango huo wa amani wa vipengele 20, Marekani ilipendekeza kwamba mataifa ya Kiarabu na washirika wa kimataifa yatoe vikosi maalum vya uthabiti ambavyo “vitatoa mafunzo na msaada kwa vikosi vya polisi vya Wapalestina vilivyothibitishwa Gaza, na vitashauriana na Jordan na Misri, ambazo zina uzoefu mkubwa katika masuala ya usalama wa kikanda.”

    Mpango huo pia unaitaka Hamas kuvunja silaha na kuachia madaraka ya kisiasa katika eneo hilo.

    “Ni mamlaka gani yatakayotolewa kwa vikosi vya usalama ndani ya Gaza? Tunatumaini kwamba itakuwa operesheni ya kulinda amani, kwa sababu kama itakuwa ya kulazimisha amani, hakuna nchi itakayopenda kujihusisha nayo,” alisema Mfalme Abdullah.

    Katika mahojiano hayo maalum kwa kipindi cha BBC Panorama, Mfalme huyo alisema Jordan na Misri ziko tayari kusaidia katika kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Wapalestina.

    “Kulinda amani ni kuwasaidia polisi wa wenyeji yaani Wapalestina jambo ambalo Jordan na Misri ziko tayari kulifanya kwa wingi, ingawa linahitaji muda. Lakini ikiwa tutakuwa tunazunguka Gaza kwenye doria tukiwa na silaha, hiyo si hali ambayo taifa lolote lingependa kujihusisha nayo,” aliongeza.

    Kauli za Mfalme Abdullah zinaakisi wasiwasi wa Marekani na mataifa mengine kuhusu hatari ya kuvutwa katika mzozo unaoendelea kati ya Hamas na Israel, au kati ya Hamas na makundi mengine ya Kipalestina.

    Mfalme huyo pia alisisitiza kwamba Jordan haitatuma wanajeshi wake Gaza, akieleza kuwa nchi yake “iko karibu sana kisiasa” na mzozo huo.

    Zaidi ya nusu ya wananchi wa Jordan ni wenye asili ya Kipalestina, na kwa miongo kadhaa taifa hilo limewapokea wakimbizi wa Kipalestina wapatao milioni 2.3 waliokimbia vita vya awali na Israel idadi kubwa zaidi katika eneo hilo.

    Alipoulizwa kama ana imani kwamba Hamas itatekeleza ahadi yake ya kuachana na siasa katika ukanda wa Gaza, alijibu: “Siwajui moja kwa moja, lakini wale wanaofanya kazi kwa karibu nao – Qatar na Misri – wana matumaini makubwa kwamba watatii makubaliano hayo.”

    Mfalme Abdullah alionya kuwa mustakabali wa amani Mashariki ya Kati unategemea kutatuliwa kwa mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Wapalestina.

    “Iwapo hatutatua tatizo hili, iwapo hatutapata mustakabali wa pamoja kwa Waisraeli na Wapalestina na kuimarisha uhusiano kati ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu na Israel, basi tutaangamia,” alisema.

    Kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Trump kulifuatwa na kuachiliwa kwa mateka 20 wa Kiyahudi waliokuwa hai kutoka Gaza, huku juhudi zikiendelea kurejesha miili ya waliouawa.

    Israel nayo iliwaachilia wafungwa 250 wa Kipalestina waliokuwa wamehukumiwa kwa makosa mbalimbali, yakiwemo mauaji na mashambulizi dhidi ya raia wa Israel, pamoja na takribani wafungwa 1,700 kutoka Gaza waliokuwa wakizuiliwa bila mashitaka.

    Pia unaweza kusoma:

  9. UN yaomba njia salama kwa raia waliokwama katika mji wa el-Fasher, Sudan

    Umoja wa Mataifa umezitaka pande zinazopigana nchini Sudan kuhakikisha raia waliokwama mjini el-Fasher wanapatiwa njia salama ya kuondoka, baada ya wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) kutangaza kuwa wametwaa udhibiti wa kambi kuu ya jeshi katika mji huo.

    Jeshi la Sudan halijathibitisha kupoteza kambi hiyo, jambo ambalo, likithibitishwa, litakuwa ushindi mkubwa kwa RSF katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema mapigano hayo mapya ni “ongezeko baya mno la machafuko,” na kuongeza kuwa mateso wanayopitia raia ni “yasiyovumilika,” kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

    El-Fasher, ambayo ni ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan katika eneo pana la magharibi mwa Darfur, imekuwa chini ya mzingiro wa RSF na washirika wake kwa zaidi ya miezi 18.

    Mapigano makali yamezuka tangu Jumamosi, baada ya wapiganaji wa RSF kuteka makazi ya gavana wa jimbo la Kaskazini mwa Darfur.

    Video zilizothibitishwa na BBC kutoka mitandao ya kijamii zinaonyesha wapiganaji wa RSF wakisherehekea baada ya kuteka makao makuu ya jeshi mjini el-Fasher.

    RSF inadai kudhibiti mji mzima, lakini washirika wa kijeshi wa serikali katika eneo hilo wanasema mapigano bado yanaendelea katika baadhi ya mitaa.

    Kundi hilo limekosolewa kwa kushambulia raia kwa mabomu ya angani na kuwazuilia takribani watu 250,000, baada ya kuuzungushia mji huo ukuta wa udongo, hali iliyowaacha wengi katika njaa kali na kukosa msaada wa kibinadamu.

    Mji wa el-Fasher sasa unatajwa kuwa moja ya maeneo yenye mapigano makubwa zaidi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambapo Umoja wa Mataifa umeueleza kama “kitovu cha mateso.”

    Afisa Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, alisema ameshtushwa sana na taarifa za vifo na mateso ya raia.

    “Wapiganaji wanapozidi kusonga kuelekea katikati mwa mji na njia za kutoroka zikifungwa, mamia ya maelfu ya raia wamekwama wakiwa na hofu ya kushambuliwa, wakikabiliwa na njaa, bila chakula, huduma za afya, wala usalama,” alisema Fletcher kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

    Tangu machafuko kuanza, zaidi ya watu 150,000 wameuawa kote nchini, huku takribani watu milioni 12 wakiyakimbia makazi yao, hali ambayo Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa ni moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

    Kwa sasa, jeshi la Sudan linadhibiti maeneo mengi ya kaskazini na mashariki mwa nchi, huku el-Fasher ikiwa mji wa mwisho mkubwa katika Darfur uliokuwa bado chini ya udhibiti wa serikali na washirika wake.

    RSF, kwa upande wake, inadhibiti karibu eneo lote la Darfur na sehemu kubwa ya mkoa wa Kordofan, na imewahi kutangaza azma ya kuunda serikali pinzani mjini el-Fasher pindi itakapodhibiti eneo hilo kikamilifu.

    Soma Pia:

  10. Ufikiaji wa mtandao umetatizwa nchini Cameroon

    Muunganisho wa intaneti umekuwa si dhabiti katika siku za hivi majuzi nchini Cameroon.

    Siku ya Alhamisi, mfuatiliaji wa mtandao wa NetBlocks aliripoti "kuvurugika kwa muunganisho wa intaneti" ambao unaweza "kuzuia utangazaji wa matukio mashinani huku kukiwa na wito wa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais huku Rais Biya akitafuta kuongeza miaka 43 madarakani".

    Siku hiyo hiyo, kampuni ya kitaifa ya mawasiliano ya Camtel ilisema kumekuwa na "tukio la kiufundi".

    Wakati huo huo, barabara za jiji la Bamenda, magharibi mwa nchi inayozungumza Kiingereza, hazina watu na raia wako ndani ya nyumba.

    Mapema sana asubuhi ya leo, mashabiki wa michezo walikuwa mitaani; wengine wakitembea kwa kasi huku wengine wakikimbia.

    Hata hivyo, kufikia saa 10:00 (09:00 GMT) mitaa ilikuwa haina watu.

    Wanajeshi wapo kwenye makutano yote makubwa.

    Uwepo wao unaonekana unanuiwa kuzuia maandamano yoyote yanayohusiana na uchaguzi.

    Kwa sasa, mawingu meusi yanaonekana yakikusanyika, kuashiria mvua mchana.

    Soma pia:

  11. Rais wa Argentina apata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula

    Rais wa Argentina, Javier Milei amekiongoza chama chake katika ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa katikati ya muhula siku ya Jumapili, baada ya miaka miwili ya kwanza ya urais wake wa kubana matumizi na mageuzi ya soko huria.

    Chama chake, La Libertad Avanza, kimepata karibu asilimia 41 ya kura, kikichukua viti 13 kati ya 24 vya Seneti na 64 kati ya viti 127 vya mabunge ya chini vilivyokuwa vikiwaniwa.

    Mafanikio yake yatarahisisha zaidi kuendelea na mpango wake wa kupunguza matumizi ya serikali na kudhibiti uchumi katika taifa hilo la Amerika Kaskazini,

    Kabla ya upigaji kura, mshirika wa Milei, Donald Trump, aliweka wazi kuwa msaada uliotangazwa hivi karibuni na Marekani wa dola bilioni 40 kwa Argentina utategemea ushindi wa Milei.

    Wafuasi wa Milei walifurahia hilo, ingawa wakosoaji walimshutumu Donald Trump kwa kuingilia kati uchaguzi wa Argentina.

    Milei aliwaambia wafuasi wake waliokuwa wakishangilia: "Lazima tuendelee na mageuzi ambayo tumeyaanzisha ili kuibadilisha historia ya Argentina... ili kuifanya Argentina kuwa kubwa tena."

    Kabla ya chaguzi hizi chama chake kilikuwa na viti saba tu vya Seneti na viti 37 katika bunge la chini.

    Hiyo ilimaanisha mpango wake wa kubana matumizi na mageuzi ulikumbana na vikwazo mbalimbali vya kisiasa.

    Miswada yake ya kuongeza ufadhili kwa vyuo vikuu vya serikali, watu wenye ulemavu na huduma ya afya ya watoto - yote ilibatilishwa na wabunge wa upinzani.

    Baada ya matokeo ya Jumapili, mamia ya wafuasi wake walikusanyika, wakishangilia, nje ya hoteli moja mjini Buenos Aires ambako alikuwa akitazama matokeo.

    Chaguzi hizi zilikuwa mtihani wa kwanza kwa umaarufu wa Rais Milei tangu aingie madarakani mwaka 2023, na kuahidi kupunguza matumizi ya serikali.

    Tangu wakati huo amepunguza bajeti ya elimu, pensheni, afya, miundombinu, na ruzuku, na kuwafuta kazi maelfu ya wafanyakazi wa sekta ya umma.

    Waungaji mkono wake, ikiwa ni pamoja na Trump, wanampongeza kwa kudhibiti mfumuko wa bei - kupunguza nakisi, na kurejesha imani ya wawekezaji.

    Wakosoaji wake wanasema taitizo ni kwamba watu wengi wamepoteza kazi, kushuka kwa uzalishaji, kuporomoka kwa huduma za umma, kuanguka kwa uwezo wa watu wa kununua na hatari ya kuporomoka kwa uchumi.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mfalme wa Uingereza kuhudhuria tukio rasmi la LGBT+

    Mfalme Charles III wa Uingereza, atazindua kumbukumbu ya sanamu la wapenzi wa jinsia moja, walio na jinsia mbili na waliobadili jinsia wanaohudumu katika jeshi, katika shughuli yake ya kwanza rasmi ya kuunga mkono jumuiya ya LGBT+.

    Ilikuwa ni kinyume cha sheria kuwa mpenzi wa jinsia moja katika jeshi la Uingereza hadi 2000, na wale ambao walikuwa wapenzi wa jinsia moja - au walioshukiwa - walikabiliwa na uchunguzi, kufutwa kazi na katika baadhi ya kesi kufungwa.

    Kumbukumbu hiyo, iliyopewa jina la "barua ya wazi," ni kwa watu kutoka jumuiya ya LGBT+ ambao wanahudumu au walihudumu katika jeshi .

    Sanamu ya shaba, liobuniwa na kikundi cha wasanii wa Norfolk Abraxas Academy, itazinduliwa rasmi leo katika Makumbusho ya Taifa huko Staffordshire.

    Mradi wa kumbukumbua unaoongozwa na Fighting With Pride, shirika la usaidizi la wanajeshi wastaafu wa LGBT+ lililoanzishwa ili kupigania haki na kuunga mkono wale walioathiriwa na marufuku ya jeshini.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Wanne wauawa katika maandamano Cameroon

    Serikali ya Cameroninasema watu wanne wameuawa wakati wa maandamano ya Jumapili katika mji mkuu wa kiuchumi wa Douala, huku hofu ikiongezeka kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini humo.

    Katika taarifa, Gavana wa mkoa wa Littoral ambao ni kitovu cha uchumi, amesema waandamanaji walishambulia vituo vya polisi na polisi, kwa nia ya kuvichoma moto na vikosi vya usalama vilizuia majaribio haya.

    "Katika mapambano hayo, kwa bahati mbaya watu wanne walipoteza maisha," amesema Gavana Samuel Dieudonné Diboua.

    Pia amelaani maandamano hayo ambayo akiyaeleza kuwa ni "vurugu zilizopangwa" ambazo ni shambulio kubwa kwa utulivu wa umma na usalama wa taifa.

    Zikiwa zimesalia saa 24 tu kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, mamia ya waandamanaji na wafuasi wa mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary walijitokeza mitaani kote nchini na nje ya nchi kukemea kile wanachosema ni udanganyifu wa uchaguzi.

    Tchiroma anadai ushindi katika uchaguzi huo, licha ya onyo kutoka kwa serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Marekani kuacha kulipia chakula cha msaada kwa raia wake

    Msaada wa chakula unaowanufaisha Wamarekani zaidi ya milioni 40 hautatolewa kuanzia Novemba kutokana na kusitishwa shughuli za serikali ya Marekani, kulingana na Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo.

    Wizara hiyo imesema hakuna msaada, katika tovuti yake na kuwalaumu wawakilishi wa Democratic katika Seneti kwa mkwamo huo.

    Mpango wa Usaidizi wa Lishe (Snap) humnufaisha Mmarekani mmoja kati ya wanane.

    Mapema mwezi huu, utawala wa Trump ulikataa kutumia hazina ya dharura ambayo ingeendeleza kutoa msaada huo, ikisema pesa hizo zinahitajika kwa dharura zinazoweza kutokea kama vile majanga ya asili.

    Democratic kimemlaani Rais Donald Trump kwa kukataa kutumia hazina ya dharura.

    "Pengine hili ni kosa la kikatili na kinyume cha sheria ambalo utawala wa Trump unalifanya," wabunge katika Congress, Rosa DeLauro na Angie Craig walisema katika taarifa ya pamoja siku ya Ijumaa.

    Pia walimkosoa Trump kwa kutoa msaada kwa Argentina na kujenga ukumbi mpya wa White House wakati shughuli za serikali zimefungwa.

    Kulingana na taasisi ya fikra tunduizi ya Budget and Policy Priorities (CBPP), hazina ya dharura ingegharamia takriban 60% ya gharama hizo kwa mwezi mmoja.

    Snap hufanya kazi kwa kuwapa watu kadi za benki wanazoweza kuzitumia kununua bidhaa muhimu za nyumbani.

    Familia ya watu wanne kwa wastani hupokea dola za kimarekani 715 (£540) kwa mwezi, kulingana na CBPP, ambapo ni sawa na dola 6 (£4.50) kwa siku kwa kila mtu.

    Majimbo ndio yanasimamia programu hii, huku ufadhili mwingi ukitoka kwa serikali ya shirikisho.

    Majimbo kadhaa yameahidi kutumia fedha zao wenyewe kufidia upungufu wowote, hata hivyo serikali ya shirikisho imeonya kuwa fidia hiyo haitarejeshwa.

    Baadhi ya majimbo, ikiwa ni pamoja na Massachusetts - ambapo watu milioni moja wanatarajiwa kupoteza msaada huo - wamesema hawana pesa za kutosha kufidia ukosefu wa fedha.

    Kufungwa kwa shughuli za serikali ya Marekani kumeingia siku yake ya 26 Jumapili, na kuufanya kuwa ndio ufungaji wa pili kwa ukubwa katika historia.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Maandamano ya vurugu yatokea Cameroon kabla matokeo ya uchaguzi

    Mamia ya waandamanaji wamepambana na vikosi vya usalama katika miji kadhaa kote nchini Cameroon, saa chache kabla ya matokeo ya uchaguzi wa urais uliokuwa na upinzani mkubwa kutangazwa.

    Polisi waliwarushia vitoa machozi na maji ya kuwasha wafuasi wa mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary katika ngome yake ya Garoua, mji ulioko kaskazini mwa nchi hiyo.

    Waandamanaji hao walikuwa wakilaani kile walichosema ni mpango wa chama tawala, Cameroon People's Democratic Movement (CPDM), "kuiba ushindi" kutoka kwa kiongozi wa upinzani.

    Tchiroma Bakary amesisitiza kwamba ameshinda uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 12 Oktoba, akipinga Rais aliye madarakani Paul Biya kwa miaka 43 kuendelea kushikilia madaraka.

    Chama cha CPDM kimetupilia mbali madai hayo.

    Maandamano hayo yanakuja baada ya Tchiroma Bakary kutoa wito kwa wafuasi wake nchini humo na wale walio njea kuandamana kwa amani "kuikomboa Cameroon."

    Serikali imepiga marufuku mikusanyiko hadi Jumatatu, wakati baraza la katiba la Cameroon litakapopanga kutangaza matokeo.

    Huko Garoua, maandamano yalianza kwa amani lakini yakageuka ghasia wakati vikosi vya usalama viliporusha vitoa machozi mitaani ili kuwatawanya mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika kumuunga mkono Tchiroma Bakary.

    Mwandamanaji mmoja alionekana akiwa amebeba bango la kumtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuwasaidia.

    "Tuko hapa kudai ushindi wetu. Tunafanya maandamano ya amani, ambayo ni haki ya kiraia kwa Wacameruni wote - kwa kila mtu," muandamanaji mwingine alisema.

    Wafuasi pia waliingia mitaani katika mji wa kusini-magharibi wa Douala. "Tunamtaka Tchiroma, tunamtaka Tchiroma," waandamanaji waliimba, shirika la habari la Reuters linaripoti.

    Tchiroma Bakary awali aliambia BBC kwamba hatakubali kuibiwa kura. Alisema timu yake imekusanya taarifa jumla kulingana na matokeo ya vituo vya kupigia kura.

    Katika taarifa yake ya video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, Tchiroma Bakary alisema ameshinda uchaguzi huo kwa takriban asilimia 55 ya kura.

    Waziri huyo wa zamani wa serikali mwenye umri wa miaka 76 aliachana na Biya mwenye umri wa miaka 92, ambaye anawania muhula mwingine baada ya miaka 43 madarakani.

    CPDM imetupilia mbali madai ya ushindi wa Tchiroma Bakary na maafisa kadhaa wameelezea kuwa ni kinyume cha sheria kwa sababu ni baraza la katiba pekee ndilo linaloweza kutangaza matokeo rasmi.

    Wafuasi wa upinzani wamedai kuwa uchaguzi wa Oktoba 12 ulikumbwa na dosari, ikiwa ni pamoja na kujazwa kura katika maboksi.

    Majaji katika baraza la katiba wametupilia mbali kesi nane, wakisema hazina ushahidi wa kutosha au haina mamlaka ya kubatilisha matokeo.

    Tchiroma Bakary alikataa kuwasilisha malalamiko katika baraza hilo, ambalo majaji wake wameteuliwa na Biya, na kuchagua badala yake kujitangaza kuwa "rais halali."

    Mzaliwa wa Garoua, Tchiroma Bakary alikuwa mwanafunzi wa uhandishi nchini Ufaransa kabla ya kurejea Cameron kufanya kazi katika kampuni ya kitaifa ya reli.

    1984, alitupwa jela, akishutumiwa kuhusika katika jaribio la kumwondoa madarakani Rais Biya. Licha ya kukana shitaka hilo na hakuwahi kupatikana na hatia, Tchiroma Bakary alikaa jela miaka sita.

    Pia aliwahi kuwa waziri wa mawasiliano kuanzia 2009 hadi 2019.

    Akiwa msemaji wa serikali, aliitetea serikali ya Biya wakati wa machafuko kama vile uasi wa Boko Haram, na jeshi lilipotuhumiwa kuwaua raia.

    Lakini mwezi Juni, miezi minne tu kabla ya uchaguzi mkuu, Tchiroma Bakary alibadilika, akajiuzulu kutoka serikalini na kutangaza kuwa atachuana na Biya kuwania urais.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Marekani na China zakubaliana mfumo wa kibiashara kabla ya mkutano wa Trump na Xi

    Marekani na China zimekubaliana mfumo wa kibiashara ambao utajadiliwa wakati viongozi wao watakapokutana baadaye wiki hii, waziri wa fedha wa Marekani amesema.

    Scott Bessent aliiambia CBS, mfumo huo wa makubaliano ni pamoja na "makubaliano ya mwisho" kuhusu shughuli za TikTok Marekani na kulegeza kamba China juu ya udhibiti wake wa rasilimali adimu.

    Pia amesema hatarajii ushuru wa 100% kwa bidhaa za China kama Rais wa Marekani Donald Trump alivyotishia, wakati huo huo China itaanza tena ununuzi mkubwa wa soya kutoka Marekani.

    China na Marekani zinajaribu kuepusha kuongeza vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.

    Trump na rais wa China Xi Jinping wanatarajiwa kufanya mazungumzo siku ya Alhamisi nchini Korea Kusini

    Bessent alikutana na maafisa wakuu wa biashara wa China kando ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (Asean) nchini Malaysia, ambao Trump pia anahudhuria kama sehemu ya ziara yake Asia.

    Beijing imesema kulikuwa na majadiliano mazuri.

    Serikali ya China imesema katika taarifa kwamba timu zote mbili za mazungumzo "zilifikia makubaliano juu ya sintofahamu zao.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Wawili wakamatwa kwa wizi katika jumba la makumbusho Ufaransa

    Washukiwa wawili wamekamatwa kwa wizi wa vito vya thamani katika jumba la makumbusho la Louvre jijini Paris, Ufaransa, vyombo vya habari vya nchi hiyo vinasema.

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Paris imesema mmoja wa watu hao ametiwa mbaroni alipokuwa akijiandaa kupanda ndege katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle.

    Vito vyenye thamani ya dola za kimarekani milioni 102, viliibiwa katika jumba la makumbusho linalotembelewa zaidi duniani Jumapili iliyopita, wakati wezi wanne waliokuwa na zana za kisasa walipovamia jengo hilo mchana kweupe.

    Waziri wa sheria wa Ufaransa amekiri kuwa itifaki za usalama "zilishindwa," na kuiacha nchi hiyo katika "picha mbaya."

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Paris imesema, watu hao walikamatwa Jumamosi jioni, bila kutaja ni watu wangapi wametiwa mbaroni.

    Mmoja wa washukiwa alikuwa akijiandaa kusafiri kuelekea Algeria, vyanzo kutoka polisi vimeviambia vyombo vya habari vya Ufaransa, huku ikifahamika kuwa mwengine alikuwa akienda Mali.

    Polisi wanaweza kuwazuilia na kuwahoji kwa hadi saa 96.

    Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa siku ya Jumapili, DNA iliyopatikana katika eneo la wizi ilipelekea kutambuliwa kwa mmoja wa washukiwa.

    Genge hilo liliacha vitu kadhaa, ikiwa ni pamoja na glavu na koti.

    Pia iliripotiwa hapo awali kwamba walidondosha taji ambalo lilikuwa la Empress Eugenie, mke wa Napoleon III.

    Mwendesha mashtaka wa Paris alikosoa "kufichuliwa mapema" kwa habari zinazohusiana na kesi hiyo, akiongeza kuwa zinazuia juhudi za kurejeshwa kwa vito hivyo na kuwapata wezi.

    Inasemekana wezi hao walifika saa 09:30 (08:30 GMT), muda mfupi baada ya jumba la makumbusho kufunguliwa.

    Washukiwa walifika na ngazi ya umeme iliyokuwa kwenye gari na kuikunjua hadi kulifikia dirisha la roshani katika ghorofa ya kwanza ya Gallery ya Apollo.

    Wawili kati ya wezi hao waliingia kwa kukata dirishani wakiwa na mashine za kisasa.

    Kisha waliwatishia walinzi, ambao walitoka nje ya jengo hilo, na kukata vioo vya masanduku mawili yaliyohifadhi vito.

    Ripoti ya awali imefichua kuwa chumba kimoja kati ya vitatu katika eneo la jumba la makumbusho lililovamiwa hakikuwa na kamera za CCTV, kulingana na vyombo vya habari vya Ufaransa.

    Polisi wa Ufaransa wanasema wezi hao walikuwa ndani ya jumba kwa dakika nne na kutoroka kwa pikipiki mbili zilizokuwa zikingoja nje saa 09:38.

    Wataalamu wameelezea wasiwasi wao kwamba vito hivyo tayari huenda vimevunjwa vunjwa na kuwa vipande vipande.

    Dhahabu na fedha zinaweza kuyeyushwa na kukatwa na kuwa vijiwe vidogo ambapo haitawezekana kujua kuwa viliibiwa katika wizi huo, afisa wa upelelezi wa Uholanzi Arthur Brand aliambia BBC.

    Hatua za usalama tangu wakati huo zimeimarishwa karibu na taasisi za kitamaduni za Ufaransa.

    Kampuni ya Louvre imehamisha baadhi ya vito vyake vya thamani hadi Benki ya Ufaransa kufuatia wizi huo. Sasa vitahifadhiwa katika chumba salama zaidi cha Benki, mita 26 (85ft) chini ya ghorofa katika makao makuu ya benki katikati mwa Paris.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Misri na Msalaba Mwekundu zaungana kutafuta miili ya mateka Gaza

    Timu kutoka Misri na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) zimeruhusiwa kutafuta miili ya marehemu waliotekwa nyara wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7, Israel imethibitisha.

    Serikali ya Israel imesema timu hizo zimeruhusiwa kutafuta zaidi ya eneo la "mstari wa njano,” amablo linadhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) huko Gaza.

    Wakati huo huo, siku ya Jumapili, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba wanachama wa Hamas pia wameruhusiwa kuingia katika eneo linalodhibitiwa na IDF la Gaza kusaidia msako huo, pamoja na timu za ICRC.

    Hamas imekabidhi miili ya mateka 15 kati ya 28 wa Israel chini ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yanayosimamiwa na Marekani. Kundi hilo limesema sasa linashirikiana na mamlaka za Misri.

    Donald Trump ameitaka Hamas kurejesha miili "haraka, au nchi nyingine zinazohusika katika mpango huu wa amani zitachukua hatua."

    Msemaji wa Israel alisema timu ya Misri imeruhusiwa kufanya kazi na ICRC kutafuta miili hiyo, na itatumia matreka ya kuchimba na magari makubwa kutafuta miili zaidi ya "mstari wa njano."

    Mstari wa " njano" unaashiria mpaka wa kaskazini, kusini na mashariki mwa Gaza, eneo ambalo Israeli ilijiondoa, kama sehemu ya hatua ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Baada ya zaidi ya miaka miwili ya mashambulizi makali ya Israel, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa 84% ya eneo la Gaza ni kifusi.

    Hamas inasema inajitahidi kadiri iwezavyo kupata miili ya mateka, lakini inakabiliwa na ugumu wa kuipata chini ya vifusi vya majengo yaliyolipuliwa na jeshi la Israel huko Gaza.

    Pia unaweza kusoma:

  19. 'Trump anataka kuipindua serikali’ – Afisa wa Venezuela

    Rais wa Marekani Donald Trump anataka kuigeuza Venezuela kuwa "koloni" la Marekani, Mwanasheria Mkuu wa Venezuela ameiambia BBC.

    Tarek William Saab alisema siku ya Jumapili kwamba wito wa mabadiliko ya utawala nchini Venezuela ni mbinu ya kutaka kunyakua maliasili za nchi yake, ikiwa ni pamoja na akiba ya dhahabu, mafuta na shaba.

    Mshirika huyo wa karibu wa Rais wa Venezuela Nicolás Maduro, Saab anasema "hakuna shaka" Marekani inajaribu kuipindua serikali ya Venezuela, akiongeza kuwa ni jaribio la hivi punde katika msururu mrefu wa majaribio kama hayo "yaliyofeli".

    Marekani ni miongoni mwa mataifa ambayo hayamtambui Maduro kama kiongozi halali wa Venezuela, baada ya uchaguzi uliopita wa 2024 kukosolewa na wengi kuwa haukuwa huru na wa haki.

    Trump pia amerudia mara kwa mara uwezekano wa kile alichokiita "operesheni za ardhini" nchini Venezuela, na alisema wiki iliyopita kwamba Marekani "inaangalia uwezekano wa operesehani za ardhini" baada ya kupata udhibiti wa eneo la bahari."

    Takriban watu 43 wameuawa katika mashamulizi dhidi ya boti zinazodaiwa kuwa za dawa za kulevya katika pwani ya Amerika Kusini, baada ya utawala wa Trump kuanzisha mashambulizi mapema Septemba kama sehemu ya vita vinavyodaiwa kuwalenga walanguzi wa dawa za kulevya.

    Wabunge wa Congress nchini Marekani kutoka pande zote mbili za vyama vya siasa, wameibua wasiwasi juu ya uhalali wa mashambulizi hayo na mamlaka ya rais kutoa amri yafanyike.

    Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham aliwaambia waandishi wa habari Jumapili kwamba mashambulizi ya ardhini ni jambo linaloweza kutokea", na Trump alimwambia kuwa anapanga kuwafahamisha wabunge wa Congress kuhusu operesheni za baadaye za kijeshi atakaporejea kutoka Asia.

    Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuvamiwa kwa ardhi ya Venezuela, Saab ameiambia BBC "haipaswi kutokea, lakini tumejitayarisha."

    Aliongeza kuwa Venezuela "bado iko tayari kuanza tena mazungumzo" na Marekani, licha ya mashambulizi "haramu" dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

    Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Marekani imekuwa ikiendelea kujenga kikosi cha meli za kivita, ndege za kivita, wanajeshi wa majini, ndege za kijasusi, na ndege zisizo na rubani katika visiwa vya Caribbean, kama sehemu ya kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya na "magaidi wa mihadarati."

    Pia unaweza kusoma:

  20. Hujambo na karibu

    Nikukaribishe katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumatatu ya tarehe 27/10/2025