Vuta nikuvute kuhusu ‘selfie’ ya tumbili

Slater anasema alitatizika sana kabla ya kufanikiwa kupata picha

Chanzo cha picha, Other

Maelezo ya picha, Slater anasema alitatizika sana kabla ya kufanikiwa kupata picha

Mpigapicha ambaye amekuwa akipigania hakimiliki ya picha ambayo tumbili mmoja anadaiwa kujipiga nchini Indonesia ameambia BBC kwamba atapinga jaribio la majuzi zaidi la kutaka kumpokonya hakimiliki ya picha hiyo.

Jumatatu wiki hii, wanaharakati wa kutetea haki za wanyama waliomba idhini ya kisheria kupokea mapato kutoka kwa picha hizo kwa manufaa ya tumbili huyo.

Lakini David Slater amesema ilimchukua siku tatu za ‘kazi ngumu’ kupata picha hiyo. Alisema pesa zinazotokana na kutumiwa kwa picha hiyo, aliyoipiga katika kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia mwaka 2011, ni zake.

"Ilinichukua siku tatu za kutoa jasho kupata selfie hii kuhakikisha ninakubalika na kundi la kima kabla yao kunikubali kiwakaribie vya kutosha na kuwaonyesha kamera yangu,” Bw Slater ameambia BBC.

"Tatizo ni kwamba, watu wengine wanajaribu kuiba haki zangu za umiliki na nitapinga hilo.”

Selfi hiyo ilisambazwa sana kote duniani na mtandaoni.

Wanaompinga Slater wanasema hawezi kuwa na hakimiliki ya picha hiyo kwa sababu ilipigwa na mnyama.

Mapema wiki hii, watetezi wa haki za wanyama kutoka kwa kundi la People for the Ethical Treatment of Animals (Peta) waliwasilisha ombi kortini San Francisco wakitaka ruhusa ya kupokea pesa zote kutoka kwa matumizi ya picha hizo, kwa manufaa ya tumbili huyo waliyesema jina lake ni Naruto na ana umri wa miaka sita.