Matokeo ya Uchaguzi Kenya 2020: Kura za maeneo yanayotiliwa shaka zaanza kukaguliwa na kuhesabiwa upya

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchunguzi wa masanduku 45 ya kura za urais kutoka vituo 15 umeanza Jumatano katika eneo moja la Mahakama ya Juu katika Jumba la Forodha huko Milimani.
Zoezi hilo linafanywa chini ya usimamizi wa maafisa wa tume ya uchaguzi IEBC na msajili wa Mahakama ya Juu.
Mawakili wa IEBC, wawawikilishi wa mwenyekiti wake Wafula Chebukati, Makamishna wake, na wawakilishi wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga na wale wa rais mteule William Ruto wanashuhudia shughuli hiyo
Kwa sasa, wanajumlisha na kukagua masanduku ya kura kutoka vituo 15 . Usalama katika eneo hilo umeimarishwa kwa kiwango cha juu ili kuzuia jaribio lolote la kutatiza shughuli hiyo.
Hatua hiyo inajiri baada ya mahakama ya Juu kuiamuru tume ya uchaguzi IEBC kumpa mgombea urais wa Muungano wa Azimio Raila Odinga idhini ya kutazama sava za tume ya Uchaguzi katika Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha kura ambazo huenda zilitumika kuhifadhi na kusambaza taarifa za upigaji kura.
Siku ya Jumanne mahakama pia iliagiza tume hiyo kumpa masanduku ya kura ya vituo mbalimbali vya kupigia kura kwa lengo la ukaguzi, ili kuchunguzwa na kuhesabiwa upya.
Vituo hivyo ni pamoja na Shule ya Msingi ya Nandi Hills na Sinendeti huko Nandi, Belgut, Kapsuser na Shule ya Msingi ya Chepkutum katika Kaunti ya Kericho; Vituo vya Kupigia Kura vya Jomvi, Mikindani na Wizara ya Maji katika Kaunti ya Mombasa; Shule za Msingi ya Mvita, na Majengo katika Kaunti ya Mombasa; Tinderet CONMO, katika Kaunti ya Nandi; Jarok, Gathanji na Shule ya Msingi ya Kiheo katika Kaunti ya Nyandarua.
Matokeo ya hesabu hiyo yanahitajika kuwasilishwa mbele ya mahakama hiyo hapo siku ya Alhamisi saa nane.
Maagizo hayo yatamwezesha Bw Odinga na walalamishi wengine wa uchaguzi wa Rais kuthibitisha madai kwamba kura ziliibiwa.
Kulingana na agizo hilo, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inahitajika kumpa Bw Odinga ufikiaji unaosimamiwa na seva zozote ambazo zinaweza kuhifadhi habari za kitaalamu zinazotumiwa kunasa nakala ya Fomu 34C ambayo ni jumla ya kura zilizopigwa.
Walalamishi wengine watakaopewa fursa ya kutazama sava hizo ni pamoja na mgombea mwenza wa Bw Odinga Martha Karua, Youth Advocacy for Africa (YAA), Peter Kirika, Khelef Khalifa, George Osewe, Ruth Mumbi na Grace Kamau.
IEBC pia iliamriwa kuwapa nakala za sera yake ya usalama ya mfumo wa teknolojia inayojumuisha sio tu sera ya neno la siri, matrix ya neno la siri na wamiliki wa nywila za usimamizi wa mfumo.
Pia watapewa Habari zozote kuhusu utumiaji wa mfumo huo wa teknolojiana viwango vyake vya kuutumia , mazungumzo yaliofanyika ndani yake kwa utambulisho , ujumlishaji wa kura, upperushaji matokeo na uchapishaji matokeo hayo.

Chanzo cha picha, SIMON MAINA/GETTY IMAGES
Kura 4,463 za Raila zadaiwa kupatiwa Ruto
Wakati huohuo, Julie Soweto, wakili katika timu ya wanasheria wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga, amedai kuwa kura 4,463 zilitolewa kutoka kwa mteja wake na kuongezwa kwa Rais mteule William Ruto katika Kaunti za Bomet, Kiambu, Kakamega, Nairobi na Baringo.
Akizungumza katika mahakama ya Juu siku ya Jumatano bi Soweto pia alilalamika kwamba kulikuwa na tofauti katika fomu 41 za 34A kutoka Bomet, Kiambu na Kakamega zilizopewa maajenti na zile zilizopo kwenye tovuti ya IEBC, ambazo ziliwasilishwa katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura cha Bomas.
"IEBC ilinunua seti mbili za fomu 34A licha ya kutakiwa kununua kijitabu kimoja pekee ambacho kingetumiwa katika vituo vya kupigia kura huku 2/2 kikihifadhiwa kwenye bahasha isiyoweza kuguswa. Hati ya kiapo ya Celestine Anyango inaonyesha ubaya wa kimakusudi katika matumizi ya fomu. Fomu ambazo mawakala wanazo na fomu kwenye tovuti ni sawa katika vipengele vyote (namba za mfululizo, mihuri, sahihi). Hata hivyo, takwimu katika fomu zimebadilishwa na ni tofauti," alisema.
Awali, wakili Mkuu James Orengo, ambaye pia katika timu ya wanasheria wa Bw Odinga, alidai kuwa IEBC haina utendakazi na haiwezi kufanya uchaguzi. Pia alidai kuwa fomu hizo zilibadilishwa.












