Uchaguzi Kenya 2022: Mfahamu Ida Odinga, Mke Raila Amollo Odinga

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakenya leo wameamkia mitandaoni kumtakila kila la heri Bi Ida Odinga, mke wa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani nchini humo Raila Amollo Odinga katika siku yake ya kuzaliwa. Sherehe ya mwaka huu ya kuzaliwa ya Ida Odinga inafanyika huku mume wake Raila Odinga akiwa tayari amewasilisha pingamizi lake mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe 9 Agosti, yaliyomnyima ushindi na mpinzani wake William Ruto kutangazwa mshindi.

Bw Odinga kupitia ujumbe wake wa Twitter amemtakia Bi Oda siku njema ya kuzawaliwa, ujumbe uliojibiwa na wimbi la jumbe za wakenya za kumtakia heri njema ya siku ya kuzaliwa.

Katika ujumbe wake wa Twitter ulioambatanishwa na picha Bw Odinga ameandika:''Katika kila siku yako ya kumbukumbu ya kuzaliwa kama leo, ninatafakari ni kwa jinsi gani wewe ni kitu bora zadi kilichotokea maishani mwangu. Uwezo wako, uvumilivu, busara, na sala ambavyo vimeweza kuifikisha familia hapa ilipo . Heri ya siku ya kuzaliwa mpendwa wangu Ida Betty''

Lakini je Bi Ida Odinga ni nani hasa?

Kama umewahi kusikia '' kila nyuma ya mwanaume mwenye mafanikio nyuma kuna mwanamke '', basi msemo huu huenda kuhusishwa na Ida Odinga, mke wa mwanasiasa mkongwe wa Kenya Raila Amollo Odinga. Hii ni kutokana na mchango wake binafsi katika maisha ya kibinafsi na ya kisiasa ya Bw Odinga. Hatahivyo Bi Ida binafsi ameshiriki pakubwa katika maendeleo ya kijamii hususan katika jamii. Lakini je Bi Ida Odinga ni nani hasa?

Kabla ya kuwa mke wa Odinga

Akifahamika kwa jina la kuzaliwa kama Ida Anyango Oyoo alizaliwa tarehe 27 Agosti, 1950, katika kaunti ya Migori Magharibi mwa Kenya. Alisomea masomo yake ya shule ya sekondari ya wasichana ya Ogande (Girls High School). Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alitunukiwa shahada ya Elimu, mwaka 1974, akiwa na umri wa miaka 24. Ida alilelewa katika familia ya watoto sita. Baba yake alikuwa daktari huku mama yake akiwa muunguzi. Ida Odinga alifiwa na baba yake mzazi akiwa na umri wa miaka saba.''Tulipofiwa na baba yetu, maisha yalibadilika hayakuwa rahisi, lakini mama yetu alichukua jukumu na akatulea vyema kutujenga kuwa watu tulio sasa'' , alisema Bi Ida.

Alivyokutanana na kuoana na Bw Raila Amollo Odinga

Ida alikutana kwa mara ya kwanza na mume wake Raila Amollo Odinga alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Aliwahi kukiri awali kwamba hakufikiria kuwa wakati mmoja angeolewa na mwanasiasa au mtu yeyote anayejihusisha na siasa. Hatahivyo alipoolewa na Bw Raila alifahamu fika kuwa anaolewa na Mhandisi kwani Odinga alikuwa akisomea uhandisi.

Ndoa na watoto

Ida aliolewa na Bw Raila Amollo Odinga tarehe 1 Septemba 1973 na, katika ndoa yao walijaaliwa watoto wanne, Fidel Odinga , Winnie Odinga, Raila Odinga Jr na Rosemary Odinga. Hata hivyo mtoto wao wa kwanza Fidel Odinga alifariki dunia mwaka 2015.

Kwa Wakenya wengi Bi Ida Odinga, anaonekana kama mwanamke shupavu, na mwenye msimamo, aliyeweza kusimama na mume wake na familia yake katika nyakati ngumu, na hivyo kuwa na sifa ya kuitwa 'mama Ida'. Sifa hii inatokana na kwamba kwamba, Bi Ida alilazimika kuwalea watoto wanne peke yake wakati mume wake alipofungwa na serikali ya zamani ya Rais Moi mwaka 1982.

Ida Odinga kama mke wa Raila Amollo Odinga

Akifahamika na wengi nchini Kenya kama 'Mama' Ida Odinga, ni mwanamke ambaye kila mara amekuwa akionekana hadharani akiambatana na mume wake na kuonyesha uungaji mkono wa hali ya juu kwa mume wake Raila Odinga hususan katika mikutano ya kisiasa, kila mara mume wake anapowania urais wa Kenya.

Mara kwa mara husikika kwenye majukwaa ya kisiasa na kampeni akimpigigia debe Raila kuwa yeye ndiye anayefaa kuwa Rais wa Kenya.''Ninaufahamu upendo alionao Raila kwa nchi hii'', alisika wakati mmoja akisema Bi Ida katika kampeni za hivi karibuni.

Japo kitaaluma Mama Odinga ni mfanyabiashara, mwanaharakati na Mwalimu, lakini umaarufu wake zaidi umetokana na jinsi anavyosimama kidete katika harakati za kumuunga mkono Bwana Raila Amollo Odinga katika siasa na azma yake ya kuongoza taifa la Kenya. Hii imekuwa ikidhihirika katika mikutano ya kisiasa ambapo huambatana na mumewe na kuwarai wapiga kura wamchague mumewe kama Rais wa Kenya.

' Si mke, mama,wala mwanasiasa tu'

Bi Odinga sio mke wa mwanasiasa tu. Binafsi ameonyesha kuwa mwanamke mwenye ushawishi hususan kwa wanawake wenzake na bado ni mhimili imara katika jamii, akiwa mstari wa mbele kutetea nafasi ya wanawake katika maendeleo ya jamii.

Bi Odinga alianzisha vuguvugu lililowahamasisha wanawake kuwachagua wanawake wenzao katika mwaka 1991, na kufahamika kama sura ya ukaidi katika utawala wa chama kimoja nchini Kenya. Pia ni mmoja wa wanawake wa kwanza kuongoza kampuni kubwa ya biashara ya usambazaji wa gesi nchini Kenya.

Bi Ida Odinga ambaye ni mwalimu kitaaluma anaamini mwanamke anapaswa kuelimika: "Ni vizuri kuwa mke mwema, lakini ni vyema kuwa mwanamke aliyeelimika. Kuwa mwanamke sio nafasi tu kuwa katika fursa ya utiifu---ni nafasi ya nguvu ," "Na ninamfanya yeye [Raila Odinga] imara kwa kuwa imara ."aliiambia BBC ilipomtembelea nyumbani kwake kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, wakati Bw Odinga alikuwa mgombea wa

Mwaka 2010, katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti la The Standard ilimtaja miongoni mwa wanawake maarufu zaidi nchini Kenya.

Kwa miaka mingi, amekuwa akijihusisha katika miradi mingi sana, ikiwemo miradi ya kampeni ya uelewa kuhusu saratani ya matiti na fistula. Hali kadhalika amekuwa mshauri wa wanafunzi kadhaa wa kike na pia mdhamini mkubwa katika kujenga maktaba ya kisasa katika shule yake ya zamani ya sekondari. Bi Ida Odinga aliweza kuchangisha shilingi milioni 176.9 kwa ajili ya ujenzi wa maktaba ya wanafunzi 500.

Mwaka 2021, alipewa tuzo ya kutambua uungaji mkono wake mkubwa katika masuala ya afya, elimu, wanawake, amani, pamoja na uwezeshwaji wa watoto wavulana na wasichana. Tuzo hiyo iliandaliwa na taasisi ya Hekima Kaka.

'Haiba na muonekano'

Si ajabu Bi Ida Odinga akaitwa mama kutokana na haiba na muonekano wake hasa anapokuwa hadharani. Kauli zake mara kwa mara zimekuwa zenye mvuto kutokana na uwezo alionao wa kuifanya hadhila yake iamini kile anachokisema sawa na mama anapokuwa nyumbani.

''Ni mama mchangamfu sana unapokutana naye kwa mara ya kwanza utadhani mnafahamiana'', aliiambia makala hii Bi Atieno Omondi, mkazi wa Migori.

Kutokana na ukweli kwamba ameweza kusimama kidete na mume wake Raila Odinga, hasa katika nyakati ngumu za misukosuko ya kisiasa, na kuweza kuitunza familia yake wakati mumewe Odinga alipofungwa miaka mitano na utawala wa rais wa zamani Daniel Arap Moi, baadhi ya Wakenya wanamuona kama mama mwenye msimamo, na anayefaa kuitwa Mama.

''Kusema kweli Mama Ida ana haiba yenye mvuto na akisimama kuongea lazima utamsikiliza…sauti yake kuna vile inavutia kumsikiliza, ni mama mwenye heshima zake'', aliiambia BBC Juliet Mwendwa mkazi wa Nairobi.

'Ni rahisi kubainika ndani ya umati wa watu'

Iwapo umekua ukifuatilia mavazi ya Bi Ida, huenda ukakubalia nami kwamba , Bi Ida Odinga ni mwanamke ambaye bila shaka hutatatizika kumuona na kumbaini kwenye umati wa watu, kutokana na kimo chake pamoja na mavazi nadhifu anayoyavaa yenye rangi unazoweza kuziona hata anapokuwa miongoni mwa umati wa watu.

Mtindo wake wa mavazi ni wa stara, kuanzia mavazi ya Kiafrika ya batiki hadi vitenge hususan pale anapoonekana mbele ya umma kwenye mikutano ya hadhara ya kiasa ambapo mara nyingi huambarana na mumewe Raila Amollo Odinga.

Ni mwanamke anayejali mavazi anayovaa, kutokana na ukweli kwamba kila mara anapojitokeza hadharani huonekana mwanamke nadhifu.

Mbali na mikutano ya kisiasa, akiwa katika shughuli za kawaida katika ofisi yake, Bi Ida huvaa mavazi mbali mbali, kama vile, suti za sketi na koti na mavazi mengine yasiyo rasmi awapo nyumbani kwake.

Akizungumza na BBC Bi Ida Odinga, awali alisema kuwa iwapo mume wake atachaguliwa na hivyo kuwa Mke Rais atahakikisha kuwa watoto wa kike wanapata elimu na maisha bora, na kuhakikisha afya ya wanawake na Wakenya kwa ujumla inazingatiwa.

Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma