Kwa nini Afrika haikuweza kupata mpango wa dharura kukabiliana na ukame

Chanzo cha picha, Getty Images
Afrika imekumbwa na ukame uliokithiri mara 14 katika kipindi cha miaka miwili pekee - zaidi ya bara jingine lolote - na Umoja wa Mataifa unaonya kuwa baadhi ya watu milioni 20 wako hatarini katika Afrika Mashariki mwaka huu baada ya mvua kushindwa kwa mara nyingine tena.
Kwa hivyo ilikuwa inafaa kwamba Ivory Coast ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mwezi huu ulioitishwa na Umoja wa Mataifa kuhusu athari mbaya za pande tatu - ukame, jangwa na uharibifu wa ardhi.
Hata hivyo, hakuna mengi yaliyopatikana katika mkutano wa wiki mbili mjini Abidjan ili kukabiliana na migogoro hii.
Nchi nyingi za Kiafrika zilibishana kuhusu makubaliano ya kisheria ya kimataifa ya kukabiliana na ukame - kitu kama itifaki ya Kyoto iliyozinduliwa mwaka 1997 ili kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa, vyanzo viliiambia BBC.
Uganda na Angola zilikuwa miongoni mwa mataifa ya kuongeza mahitaji ya ukanda wa Afrika.
Lakini walikuwa na nia ya kuhakikisha kuwa halionekani kama tatizo kwa Afŕika pekee - walitaka ukame uchukuliwe kama tatizo la kimataifa, ili kuhakikisha linapata uangalizi wa kimataifa.
Walisema kuwa ukame ulikuwa ukichochewa na mabadiliko ya hali ya hewa, na hivyo ni hatua za kimataifa pekee zinazoweza kuleta mabadiliko, ingawa kwa upande wa Afrika uharibifu wa ardhi na kuenea kwa jangwa kumezidisha hali hiyo.
''Ni suala la kimataifa, si lile la Afrika pekee,'' alisem mpatanishi wa Uganda Kabango Freddie.
''Tunaamini ikiwa pande zote za UNCCD [Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa] ziko tayari kushughulikia mgogoro huu chini ya chombo kinachofunga kisheria, tunaweza kusaidia jamii ambazo zimekumbwa na ukame, au ziko hatarini kukabiliwa nazo, kuwa mvumilivu.''
Lakini pendekezo hilo halikupata kuungwa mkono na sehemu nyingine za dunia.
Walisema kwamba tayari kulikuwa na mikataba mingine ya kimataifa na taratibu za kukabiliana na mgogoro huo - kama vile Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa, Malengo ya Maendeleo Endelevu au hata makubaliano ya Hali ya Hewa ya Paris - na kwamba kuunda chombo kingine hakutasaidia.
Argentina na Jamhuri ya Dominika - zinazowakilisha Amerika ya Kusini na Caribbean - zilisema juhudi kubwa zaidi ikiwa ni pamoja na msaada wa kifedha na kiufundi zinahitajika kusaidia nchi kukabiliana na ukame na kuenea kwa jangwa, wakati Umoja wa Ulaya (EU) ulisema mbinu zilizopo zinapaswa kutumika ili kuepuka kurudiwa kwa makosa yale yale.
Mwishowe, kulikuwa na maelewano - makubaliano ya kuahirisha uamuzi kwa miaka miwili na kuunda kikundi kazi cha serikali ambacho kitaangalia njia za kuzingatia udhibiti wa ukame.
Itaripoti ifikapo 2024 - kufikia wakati ambapo mambo matatu tunayoangazia yanatarajiwa kuwa tatizo kubwa zaidi.
Mkutano huo pia ulikubali kurejesha hekta bilioni moja za ardhi iliyoharibiwa duniani kote ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, baadhi wanahofia kwamba lengo hili kubwa linaweza lisifikiwe, kama vile malengo ya awali.
Upotevu wa ardhi wasababisha migogoro
Ripoti iliyozinduliwa katika mkutano huo, Ukame kwa Hesabu, ilionyesha kuwa kati ya nchi 23 ambazo zimekuwa na dharura kwa sababu ya ukame katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, nyingi - 14 - zilikuwa barani Afrika.
''Afrika ilikumbwa na ukame mara nyingi zaidi kuliko bara lolote lile na ukame 134 kati ya 2000 na 2019, ambapo 70 ulitokea Afrika Mashariki,'' ilisema.
Ripoti ya hivi punde zaidi ya Jopo la Serikali mbalimbali kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa ilionyesha kuwa ukame umeongezeka katika sehemu fulani za Afrika, na inatabiri ongezeko zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Theluthi mbili ya Afrika ni jangwa na nchi kavu, kwa hivyo ina ardhi ndogo ya uzalishaji kwa kuanzia.
Kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, 65% ya ardhi yenye tija tayari imeharibiwa, kulingana na UN.
Uzalishaji wa ardhi umeharibiwa kwa kiasi kikubwa hasa kwa sababu ya matumizi yasiyo endelevu kwa madhumuni ya kilimo na kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula.
Tafiti pia zimeonyesha kuwa Afrika inapoteza hekta milioni nne za misitu kila mwaka na uzalishaji wa mkaa unasalia kuwa tishio kubwa kwa misitu katika nchi nyingi.
Zaidi ya hayo, UNCDD inasema asilimia 45 ya eneo la ardhi barani Afrika limeathiriwa na hali ya jangwa na zaidi ya nusu yake iko katika hatari kubwa ya kugeuka jangwa zaidi.
''Tunaona hali ngumu zaidi mwaka baada ya mwaka,'' Patrick Youssef, mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.
Na kuenea kwa jangwa kunamaanisha kuongezeka kwa ushindani wa ardhi bora, na kusababisha migogoro.
''Kuongezeka kwa uharibifu wa ardhi, hali ya jangwa na ukame kumemaanisha ardhi ya malisho na maji yanatoweka katika maeneo kama [kaskazini] ya Mali na wafugaji wanalazimika kuingia katika ardhi ya kilimo ya jamii nyingine,'' alisema Bw Youssef.
Kuwapa wakulima ardhi
Tangu mwaka 1999, nchi nyingi za Afrika zimeandaa mipango ya kikanda ya kukabiliana na uharibifu wa ardhi na kuenea kwa jangwa.
Lakini uchambuzi uliochapishwa mwaka jana na Shiŕika la Chakula na Kilimo na wakala wa maendeleo wa Umoja wa Afŕika uligundua kuwa hakuna maendeleo ya kutosha yalikuwa yamepatikana.
Ripoti nyingine iliyotolewa muda mfupi kabla ya mkutano huo ilisema kwamba ni kati ya 4% na 20% tu ya lengo la awali la mpango wa 'Great Green Wall' ulikuwa umefikiwa ifikapo 2020.
Mpango huo ulizinduliwa kwa shauku kubwa mnamo 2007 kurejesha hekta milioni 100 za ardhi kwa kupanda mamilioni ya miti, kurejesha nyasi, mimea na ardhi oevu katika nchi 11, kuanzia Senegal kwenye pwani ya magharibi ya Afrika hadi Djibouti mashariki kufikia mwaka 2030.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshauri wa masuala ya hali ya hewa wa shirika la World Vision Tony Rinaudo alisema serikali zinahitaji kuongeza kiwango cha ardhi ya kilimo inayomilikiwa na wakulima, lakini hili linapingwa na serikali.
''Haipaswi kustaajabisha kwamba wakazi wa vijijini hawana motisha ya kulinda na kusimamia kwa uendelevu kile ambacho hawamiliki na kile ambacho hawana haki ya kisheria kunufaika nacho,'' alisema.
Lakini umiliki peke yake hautatua tatizo.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanazidi kuchangia ukame.
Ukame wa sasa katika Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika umeweka hadi watu milioni 20 katika hatari ya kukabiliwa na njaa kali.
Moja ya nchi zilizoathiriwa ni Ethiopia, ambayo imeweka juhudi kubwa katika kufanya matayarisho ya kukabiliana na ukame lakini sasa inakabiliana na ukame mbaya zaidi katika takriban nusu karne.
''Ethiopia iliweza kustahimili ukame kwa karibu miaka mitano kwa sababu ya ardhi yake iliyorejeshwa ambayo ilikuwa na inahimili ukame,'' afisa wa UNCDD Louise Baker alisema.
''Lakini ukame katika Pembe ya Afrika sasa umefikia hatua mbaya sana, hivyo kwamba ardhi haina uwezo wa kustahimili. Mnapiga hatua kwa upande mmoja lakini hali ya hewa inaweka shinikizo kubwa katika ardhi ambayo imehuishwa tena, aliongeza.

Pia unaweza kusoma:
Tazama zaidi jinsi ukame ulivyoathiri Afrika:
- TANZANIA:
- SOMALIA:
- AFRIKA:


















