Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Kenya 2022: Kwanini kura za Wakikuyu zinapiganiwa katika uchaguzi?
- Author, Na Evelyne Musambi
- Nafasi, BBC News
Wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa urais nchini Kenya wamechagua wagombea wenza kutoka kabila la Wakikuyu ambalo lina kura nyingi ili kuongeza nafasi yao ya kushinda katika uchaguzi wa mwezi Agosti unaosubiriwa kwa hamu.
Naibu wa Rais William Ruto amemteua mfanyabiashara na mbunge Rigathi Gachagua huku Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga akimteua Waziri wa zamani wa Sheria Martha Karua.
"Wawili hao wanatoka ulimwengu mbili tufauti, ijapokuwa wanatoka eneo la mlima Kenya," mchambuzi Javas Bigambo aliambia BBC.
Eneo la Mlima Kenya ni nyumbani kwa jamii ya Wakikuyu, ambayo inaweza kuwa muhimu katika kuamua matokeo ya uchaguzi.
Bw. Gachagua ni mhamasishaji hodari na ana ushawishi mkubwa miongoni mwa Wakikuyu wanaohangaika, ambao wamekuwa wakimuunga mkono Bw Ruto kuhusu mipango yake ya kushughulikia malalamishi ya kiuchumi.
Bi Karua ni gwiji wa kisiasa anayetambuliwa nje ya jamii ya Wakikuyu - na anajulikana kwa shauku yake ya mageuzi ya mahakama na kampeni dhidi ya ufisadi.
Wachambuzi wanasema kwamba wakati wasomi wanaweza kumuunga mkono mwanaharakati wa kupinga ufisadi, uchaguzi huu zaidi unahusu mageuzi ya kiuchumi.
"Pande zote mbili zimegubikwa na tuhuma za ufisadi na ndiyo maana hakuna anayenyooshewa vidole. Ufisadi si suala la msingi tena. Inaonekana kuwa mtindo wetu wa maisha na imekuwa vigumu kuonyesha kiongozi shupavu ambaye hajachafuliwa na ufisadi," mchambuzi Bobby Mkangi aliambia BBC.
Bw. Gachagua anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na utakatishaji fedha za thamani ya dola milioni 65 (£53m). Amepinga mashataka, na kusema kuwa anateswa na serikali kwa kumuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto.
Rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta anamuunga mkono Bw. Odinga, ambaye alisalimiana naye 2018 katika kile kilichofahamika kama ''Hand Shake'' kuashiria maridhiano kati yao baada ya uhasama wa kisiasa wa miaka kadhaa.
Wachambuzi wanasema kuanzia wakati huo, Bw. Odinga, kiongozi mkongwe wa upinzani ambaye amejaribu mara nne kugombea urais wa Kenya na kushindwa, kwa kiasi kikubwa amepuuza uozo wote serikalini.
Uamuzi wake wakumteua Bi Karua kama mgombea mwenza pia ni jaribio la kuvutia kura ya wanawake, lakini Bw. Bigambo hana uhakika atapata ufanisi kiasi gani.
"Anawavutia wananawake kielimu sio kivitendo. Anavutia sehemu ya tabaka la kati na jumuiya ya mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo hayana mchango mkubwa katika matokeo ya uchaguzi," Bw Bigambo anasema.
Bi Karua aligombea urais mwaka wa 2013 na kupata kura 43,881 - au 0.36% ya jumla ya kura ziliyopigwa.
Lakini anafahamika kwa kuwa jasiri na mpigania demokrasia ya vyama vingi.
Ametofautiana na marais wawili wa zamani kiasi cha kuondoka kwa hasira katika mikutano yao.
Mwaka 2001 aliondoka katika mkutano uliokuwa ukuhudhuriwa na rais wa wakati huo hayati Daniel arap Moi, kupinga kauli iliyotolewa dhidi ya aliyekuwa mkuu wa chama chake wakati huo Mwai Kibaki.
Bi Karua alijiuzulu wadhifa wa waziri wa sheria mwaka wa 2009 akitaja hali ya kufadhaika baada ya Bw Kibaki, rais wakati huo kuwateua majaji bila yeye kujua.
"Swali kuu ni iwapo ana uwezo wa kung'atuka kama kinara wa Mlima Kenya kwa sasa Rais Uhuru anapostaafu. Je, atakumbatiwa kikamilifu miongoni mwa nyadhifa za chini za Mlima Kenya?" Bwana Bigambo anauliza.
Bw Gachagua kwa upande mwingine amesifiwa na wachanganuzi kwa uwezo wake wa kuingia katika mtandao wa kisiasa aliokuwa sehemu yake alipokuwa akifanya kazi kama msaidizi wa kibinafsi wa Rais Kenyatta na afisa wa wilaya katika maeneo tofauti.
"Uwezo wake wa kutumia fursa aliyopata kufikia wadhifa huu ukizingatia majina ya watu wengine walijulikana kitaifa ni kitu cha ajabu," Bw Mkangi anasema.
Bw. Gachagua ni Mbunge wa eneo bunge la Mathira kati kati mwa Kenya, ambalo linajivunia kutoa Marais watatu wa Kenya - Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta.
Ni mfanyabiashara ambaye hotuba zake katika majukwaa ya kampeni zinaashiria anaelewa masuala yanayowaathiri Wakikuyu.
"Ni mbwa mwitu wa kisiasa anayeogopwa ambaye Ruto alihitaji ili kuweza kukabiliana na Rais Uhuru katika eneo la kati," Bw Bigambo anasema.
Licha ya masuala ya kiuchumi kujitokeza katika uchaguzi huu kama kigezo kinachowezekana cha jinsi watu watakavyopiga kura, ukabila bado una ushawishi mkubwa kwa wapiga kura.
Hii ni mara ya kwanza tangu Kenya ipate uhuru ambapo Mkikuyu hajajitokeza kuwa mgombeaji mkuu wa urais - Bw Ruto ni Mkalenjin, kabila la tatu kwa ukubwa, na Bw Odinga ni Mjaluo, kabila la nne kwa ukubwa.
Kwa hivyo wawili hao wamependekeza Wakikuyu - kabila kubwa zaidi - kama wagombea wenza katika uchaguzi wa Agosti 9, uamuzi ambao unaweza kuimarisha au kuvunja kampeni zao za urais.
"Chaguo la wagombea wenza kutoka jamii ya Wakikuyu ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuhamasisha jamii hiyo kujitokeza kupiga kura," Bw Mkangi anasema.