Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa UKraine: Je Urusi inatawala vipi maeneo iliyovamia?
Urusi inatambulisha sarafu yake, huduma ya vyombo vya habari na mtandao katika baadhi ya maeneo nchini Ukraine ambayo jeshi lake limeyachukua - hasa katika mji wa kusini wa Kherson.
Ukraine inasema kuwa huenda Urusi inapanga kufanya kura ya maoni katika mji huo - ili kuona kama wakazi wake wanataka kuanzisha "jamhuri ya watu" waliojitenga inayounga mkono Urusi lakini kura hiyo itakuwa kinyume cha sheria na udanganyifu.
Kwa nini Urusi imeweka mkazo Kherson?
Vikosi vya Urusi viliutwaa mji wa Kherson mapema mwezi Machi, wiki moja baada ya uvamizi wa Ukraine kuanza.
Ulikuwa mji muhimu wa kwanza kuanguka.
Kabla ya uvamizi huo, kulikuwa na idadi ya watu 290,000.
Lakini, kulingana na meya wake wa zamani, baadhi ya 40% ya wakazi wamekimbia jiji hilo.
Ikiwa Urusi inalenga kuchukua kusini mwa Ukraine na kuanzisha daraja la ardhini hadi Crimea, Kherson, kwenye mlango wa Mto Dnieper katika pwani ya Bahari Nyeusi, itakuwa muhimu, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza inasema.
Ni mabadiliko gani ambayo Urusi imefanya Kherson?
Mamlaka za kijeshi za Urusi zilimfukuza meya aliyechaguliwa kutoka kwenye wadhifa wake.
Ihor Kolykhaiev "hakuwa akishirikiana" na vikosi vinavyotawala, shirika la habari la serikali ya Urusi Ria lilisema.
Katika nafasi yake, utawala unaounga mkono Urusi katika mji huo na eneo jirani umewekwa.
Upatikanaji wa chaneli za televisheni za Kiukreni umezuiwa na watoa huduma za mtandao zimebadilishwa na kuwekwa za Kirusi.
Wakaazi wa Kherson wamehimizwa kusikiliza vituo vya redio vinavyounga mkono Urusi ili kupata habari zao.
Ukraine inasema lengo la Urusi ni "kufanya propaganda zao za uongo kuwa chanzo chga habari kisichopingwa".
Serikali mpya ya katika mji huo pia imeondoa sarafu ya Ukraine, hryvnia, na kuanzisha sarafu ya rouble ya Urusi.
Kipindi cha mpito cha miezi minne kilianza tarehe 1 Mei, huku mamlaka ikipiga marufuku uwasilishaji wa pesa za Kiukreni kwenye benki.
Wakaazi wa Kherson wameiambia BBC kuwa mamlaka ya kijeshi imeanza kulipa pensheni za watu kwa sarafu ya Urusi rouble.
Lakini wengi wanajaribu kutafuta njia ndogo za kukaidi majeshi ya Kirusi, ikiwa ni pamoja na kubadilishana pesa ya urusi rouble yoyote wanayopokea tena kwenye hryvnia.
Je, Urusi inapanga kufanya kura ya maoni?
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaonya wakazi kuwa Urusi inalenga kufanya "kinachojulikana kura ya maoni" katika eneo la Kherson, juu ya kujitenga na Ukraine na kuwa "jamhuri ya watu".
Amewashauri watu kutozipa mamlaka za Urusi taarifa zozote binafsi, kama vile nambari za pasipoti, kwa kuwa zinaweza kutumiwa kughushi kura.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema, katika taarifa za kiinteligensia za mwezi Aprili, kura ya maoni itakuwa njia ya Urusi kuhalalisha uvamizi wake wa Ukraine.
Lakini Bw Kolykhaiev alisema itakuwa kinyume cha sheria kwa vile Kherson inabakia kuwa sehemu ya Ukraine.
Na Rais Zelensky amesema inalingana na mipango ya Urusi ya kuivunja Ukraine kwa kuunda "jamhuri bandia" kote nchini.
Je, Urusi imebadilisha vipi maisha katika maeneo yaliyojitenga ya Ukraine?
Mtazamo wa Urusi kwa Kherson umefuata muundo wake walioutumia Crimea, ambayo ilitwaa mwaka wa 2014, baada ya kura ya maoni kutangazwa kuwa batili na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Ilijenga daraja kati ya Crimea na kusini mwa Urusi na kuhamisha silaha, ilianzisha ruble na kuondokana na hryvnia.
Na vyombo vya habari vinavyounga mkono Urusi sasa vinatawala katika eneo hilo
Lakini hali ya Kherson inafanana na ile ya miji miwili ya mashariki mwa Ukraine iliyotekwa na vikosi vinavyotumiwa na Urusi muda mfupi baada ya Crimea kutwaliwa.
Viongozi ambao ni vibaraka wa mashariki waliunda kinachojulikana kama jamhuri za watu, huko Luhansk na Donetsk, ambapo pia wanatumia ruble na wamewapa idadi ya watu pasipoti za Kirusi.
Urusi inalipa pensheni na mishahara ya serikali huko.
Katika shule, watoto hufundishwa kwa mtaala wa Kirusi.
Na Ukraine ililalamika kwa Moscow juu ya kile kinachoitwa "Russification" ya mashariki mwa Ukraine.
Bado hakuna pendekezo la kuitawala Kherson, la kuunda jamhuri ya watu.
Kura sawa kama hiyo huko Luhansk na Donetsk, Mei 2014, zimekataliwa kwa kiasi kikubwa kuwa zimeibiwa na si halali.
Lakini kuna mazungumzo juu ya Urusi kupanga kura ya maoni zaidi katika kanda hizo mbili, juu ya kuziunganisha na Urusi.
Ukraine imeweka wazi kura zote ni bandia zitakuwa batili na kuepukwa
Unaweza pia kusoma
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Vita Ukraine : Marekani inataka kuidhoofisha Urusi
- UCHAMBUZI:Urusi na Ukraine: Zijue athari za vita ya Ukraine kwa Afrika
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Vita vya Ukraine: Makombora yapiga Kyiv, Umoja wa Mataifa wakiri kushindwa