Uchaguzi Ufaransa: Je ni Macron au Le Pen wa mrengo wa kulia?

Raia wa Ufaransa wanashiriki kura ya uchaguzi itakayoamua ikiwa Rais Emmanuel Macron atapewa miaka mingine mitano kuongoza nchi au kumuondoa na kumpatia nafasi hiyo mgombea wa mrengo wa kulia Marine Le Pen.

Baada ya kampeni za uchaguzi zilizokumbwana mgawanyiko, Bi Le Pen anakabiliwa na kibarua kigumu cha kumshinda Rais Macron aliye madarakani.

Ili kushinda wote wawili wanahitaji kuwavutia wapiga kura waliowaunga mkono wagombea wengine katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo.

Lakini viongozi hawa wawili wameibua mgawanyiko mkubwa miongoni mwa Wafaransa na huenda wengine wasipige kura katika uchaguzi wa duru ya pili.

Wapinzani wa Bw. Macron wanamuita mjeuri na rais wa matajiri, huku kiungozi wa mrengo wa kulia naye akituhumiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Bw. Macron aliingia madarakani kwa ahadi ya kuleta mabadiliko, lakini wengi wanalalamika kuwa hawajaona mabadiliko yoyote.

Wakati huohuo Marine Le Pen amejifunza kutokana na makosa aliyoyafanya aliposhindwa kwa kishindo na mpinzani huyo huyo katik aduru ya pili mwaka 2017. Hii ni ni mara ya tatu anagombea kiti cha urais na iwapo atashindwa inaweza kuwa mwisho wake.

Jambo kubwa lisilojulikana katika uchaguzi huu ni wapiga kura wangapi watakataa kumuunga mkono mgombea yeyote, iwe kwa kupiga kura bila kuchagua kiongozi yeyote au kutojitokeza kabisa. Sehemu kubwa ya Ufaransa iko likizoni na waliojitokeza wanaweza kuwa wachache katika kihistoria.

Kampeni imekuwa fupi lakini chaguo la wapiga kura liko wazi, kati ya rais anayeunga mkono Uropa na mgombea mzalendo anayetaka kupiga marufuku vazi la hijabu kwa wanawake wa Kiislamu na kuzuia uhamiaji.

Vituo vya kupiga kura vilifunguliwa saa mbili majira ya Ulaya (06:00 GMT) huku upigaji kura ukitarajiwa kuendelea kwa saa 12.

Vyovyote itakavyokuwa,Jumapili jioni Bw Macron atahutubia wapiga kura kutoka kwenyd jukwaa la chini ya Mnara wa Eiffel.

'Mahali hapa husalia mahame baada ya saa moja usiku'

Suala la kupanda kwa gharama ya maishi - linalotajwa na Wafaransa kama pouvoir d'achat au uwezo wa matumizi - limekuwa namba moja kwa wapiga kura wa Ufaransa na Marine Le Pen amewaahidi wapiga kura kwamba atalipatia kipaumbele mara atakaposhinda na kuingia madarakani.

Alifanya vyema katika miji midogo na maeneo ya vijijini ambako wakazi wamekuwa wakitatizika kiuchumi wakati wa enzi ya Macron.

Umaarufu wake ulipanda wiki mbili zilizopita huko La Ferté-sous-Jouarre, mji mzuri kwenye Mto Marne uliopo mashariki mwa Paris.

Mmoja wa wakazi Cécile anasema janga la corona liliathiri sana eneo hilo: "Kabla ya Covid kulikuwa na baa hapa inayoitwa Avenue de Champagne, lakini ilifungwa na sasa mahali hapo pamesalia mahame baada ya saa moja usiku.""

Atampigia kura Le Pen kama vile Fred, ambaye anafanya kazi kwenye mtandao wa jiji la Paris: "Watu hawana uwezo wa kulipia gesi na umeme. Ninapokuwa Paris baadhi ya vitu ni ghali sana na unapaswa kula." Wahamiaji wa Kiafrika anaowafahamu katika mji mkuu pia wanasema watampigia kura, anaongeza.

Kuna wafuasi wengi wa Le Pen hapa. Ufaransa inahitaji mabadiliko, wanasema hivyo na kukomea hapo.

Ameangazia maoni yake kwa uangalifu, lakini bado anapanga kura ya maoni kuhusu udhibiti mkali wa uhamiaji na wazo lake la "Ulaya ya mataifa" lingesambaratisha EU.

Jean-Claude, 66, huenda asikubaliane na uhasama wake dhidi ya EU, lakini analalamika kuwa watu wengi hutumia mfumo wa ustawi wa Ufaransa na kutumia dawa za kulevya.

Le Pen na Putin

Kote nchini Ufaransa Emmanuel Macron ni maarufu sana miongoni mwa wapiga kura vijana, na hivyo ndivyo hali ilivyo huko La Ferté pia.

Mwanafunzi mhasibu Séréna, 18, ana wasiwasi kuhusu vita nchini Ukraine: "Hatujui kwa hakika Le Pen anahisi nini kuhusu Putin. Kubadilisha rais kunaweza kuyumbisha hali ya sasa."

Nicole, 76, anaendesha maktaba katika kijiji jirani na ameona watu wengi wakigeukia upande wa kulia. "Sina wasiwasi juu yake, zaidi kuhusu watu walio nyuma yake - wakuu wake."

Bi Le Pen anafanya vyema katika miji mikubwa, kama Paris na Lyon, ambapo mpinzani wake aliongoza katika duru ya pili. Lakini kinachoweza kuamua uchaguzi huu ni nani ataungwa mkono na karibu 22% ya wapiga kura waliompigia kura mgombea wa siasa kali za mrengo wa kushoto Jean-Luc Mélenchon.

Alishindwa na Marine Le Pen lakini alishinda katika miji ikiwa ni pamoja na Marseille na Nantes.

Mji wa Trappes, kusini-magharibi mwa Paris, ni ngome ya Mélenchon ambapo kuna uhaba wa wapiga kura wa Le Pen.

Mwanamke aliyevalia hijab analaani sera za mrengo wa kulia akisema ni za kibaguzi. "Nitapiga kura bila kumchagua yeyote," anasema. Ni wazo maarufu ambalo linaonekana kama kura ya ukaidi ambayo haifaidi mgombea yeyote. Baada ya kutafakari anaongeza kuwa anaweza kumuunga mkono Macron, au hata asipige kura kabisa.

Wafuasi wa Mélenchon wanaonekana hawajaamua. Mmoja wao Mura, anasema huenda akapiga kura bila kumchagua mgombea yeyote. "Macron anahusishwa zaidi na matajiri kuliko maskini," anasema, kabla ya kuongeza kuwa bado anaweza kumpigia kura.

Ukosefu wa ajira unaweza kupungua na uwezo wa kununua unaweza kuwa mkubwa zaidi kuliko mwaka wa 2017, lakini wapiga kura wengi walio upande wa kushoto wamekatishwa tamaa na rais aliyepomadarakani kwa kukata misaada ya makazi kwa mamilioni ya watu wa kipato cha chini na kukomesha ushuru wa mali uliolenga mamilionea.

Wakati Emmanuel Macron alipoingia madarakani, iliahidi kuleta mabadiliko. Lakini maoni unayosikia kila mahali ni kwamba hakuna kilichobadilika hata kidogo.

Iwapo kura za maoni zitakuwa sahihi na akashinda, atakabiliwa na kibarua kigumu katika muhula wa pili.