Mauaji ya Kimbari Rwanda: Jinsi mauaji yalivyozaa mapenzi

- Author, Yves Bucyana
- Nafasi, BBC Africa, Kigali
Rwanda inaadhimisha kumbukizi ya miaka 28 ya mauaji ya kimbari ambayo yalidumu kwa muda wa siku 100 mnamo mwaka 1994.
Watu karibu 800,000 waliuawa pale waasi wa Kihutu wenye msimamo mkali walipowauwa Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa kati.
Kadri miaka ilivyojiri kumekuwa na jitihada nyingi za kuidhinisha maridhiano.
Miradi kadhaa ya kuzipatanisha jamii na kuendeleza maridhiano na uponyaji imeidhinishwa ikiwemo yale ya madhehebu mbalimbali kutoka makanisa nchini Rwanda.
Na hilo limeonekana kusaidia pakubwa wakati jamii ya Watutsi kadhaa wameamua kuyazika madhila na kuwasamehe wahusika wa mauaji ya baadhi ya jamaa zao - na hivi leo wanaishi pamoja kwa amani.
Katika parokia ya Mushaka magharibi mwa Rwanda, wananchi wanaimba.
Wamemaliza kazi ya kujitolea ya kulisafisha shamba la manusura wa mauaji ya kimbari.
Baada ya kazi, ibada inafuata. Ni kipindi cha kuzisafisha nyoyo.
Kundi linalojumuisha wahusika na waathiriwa wa mauaji ya kimbari wamekusanyika kuhimizana umoja na maridhiano. Mafunzo yanatolewa katika shamba la manusura wa mauaji ya kimbari karibu na parokia ya Mushaka
Somo lake leo kwa jamii iliokusanyika ni umuhimu wa kubadilika, kuomba na kutoa msamaha.
'Nini maana ya kubadilika? kubadilika haina maana ya kubadilika rangi ya ngozi bali kubadilika kiroho' anaeleza mwalimu nani? Apiane Nangwahabo
'Ni kuepuka tabia mbaya na kufuata mienendo safi. Ni kuachana na tabia mbaya zilizokunasa na kuchukua uamuzi wa kufuata njia njema.'
Kuomba radhi na msamaha

Chanzo cha picha, BBC
Bernadette Mukakabera na mkwewe Yankurije Donata ni miongoni mwa watu waliopokea mafunzo haya.
Wawili hawa wana hadithi nzito ya uhusiano uliozaliwa kutokana na umwagikaji damu.
Mume wake Mukakabera aliuawa na babake Donata - Gratien Nyaminani.
Miaka minne baada ya kuomba msamaha kwa mauaji aliyotenda - Gratien alifariki mwezi mmoja uliopita.
Bernadette anasema - msamaha huo ulipelekea watoto wa familia hizi mbili kutangamana katika ndoa.
'Babaake mkwe wangu huyu alihusika katika mauaji ya mume wangu. Aliiomba serikali msamaha na mimi mwenyewe nikaridhia kumsamehe.
'Kijana wangu alimpenda binti yake na akatoa posa na kufunga ndoa naye. Sikuweza kuwa kikwazo cha mapenzi ya watoto, kwani hawana kosa walilofanya' anaeleza Bernadette.
'Siwezi kuwa na kinyongo na mkwe wangu huyu kwa kosa alilotenda mzazi wake'.
Padre Ngoboka Theogene wa Dayosizi ya Cyangugu anasema kuwa mafunzo yanayotolewa ya uponyaji wa katika kanisa katoliki huwa ni kwa miezi misita.

Baada ya hapo ndipo hufanyika shughuli kuu ya wahusika wa mauaji kuomba msamaha, na waathiriwa kutoa msamaha.
Ni shughuli inayofanyika mbele ya halaiki ya waumini.
'Aliyefanya kosa la mauaji ya kimbari hufungiwa huduma za sakramenti. Ili aweze kurejea mbele ya jamii, hana budi kwanza kufunguliwa sakramenti. Jambo linalohitaji kwanza maridhiano na wale aliowakosea.'Anafafanua Padre Ngoboka.
'Muathiriwa husimama nyuma ya aliyehusika na mauaji na kunyosha mikono na viganja juu yake kama ishara ya kumsamehe'.
Donata anasema kwamba mara baada ya kupawa habari za pendekezo la uposo kutoka familia ambayo waliitendea vibaya, alishtuka na anasema hata familia yake haikuamini.
'Nilimwambia baba kwamba, kijana kutoka familia hiyo anataka tufunge ndoa. Baba alishtuka na kuonekana mwenye tatizo'.
Anasema marehemu babaake alimueleza kwamba haiwezekani kutokana na yaliotukia baina ya jamii hizo mbili katika mauaji ya kimbari.
'Ninafikiri alijiuliza... inawezekanaje familia niliyoifanyia vibaya iwe na nia ya kumposa binti yangu?' asema Donata.
Mwishowe Baba yake Donata aliridhia baada ya kuomba msamaha na kufuata njia ya masomo ya umoja na maridhiano.
Ndoa yao ilifanyika miaka minne iliyopita. Baba yake Donata alifariki mapema mwaka huu.
Mwanzoni jamii haikuwa inaelewa kabisa lakini baada ya maridhiano hayo kufanyika sasa wao wenyewe huenda sehemu mbali mbali kufundisha watu wengine kwamba umoja na maridhiano ni suala linalowezekana katika jamii iliyotendeana uhalifu.
Hivi sasa wenza hao wanasema wanaishi raha mstarehe kwani licha ya shida iliyotokea ndani ya familia zao, wao walikuwa marafiki wa tangu utotoni'' kwa mujibu wa Donata.
Unaweza pia kusoma:













