Mwaka mmoja tangu kifo cha Magufuli:Kupanda na kushuka kwa wandani wa aliyekuwa rais John Pombe Magufuli serikalini

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi wa siasa Tanzania

Ni mwaka mmoja sasa tangu kutokea kifo cha rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani hayati John Pombe Magufuli.Wiki hii tutakuletea makala maalum kuhusu mambo mbali mbali ya utawala wake hadi nyakati zake za mwisho kama rais.

BABA wa Taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alipata kusimulia kisa kimoja kuhusu watu wake wa karibu katika siku zake za mwisho madarakani. Alieleza namna walivyokuwa wanamshawishi asiachie madaraka kwa vile hakuna mtu mwingine atakayeweza kuvaa 'viatu' vyake.
Hata hivyo, Mwalimu hakuwasikiliza na badala yake aliachia ngazi. Busara, kwa mujibu wa maelezo yake, ilikuwa kwamba waliotaka abaki madarakani, haikuwa kwa sababu walimpenda sana bali walikuwa wanajiwazia maisha yao wenyewe. Bila shaka, hilo ni kundi la watu waliokuwa wakifaidika na utawala wake.
Kufaidika na utawala wa kiongozi mmoja ni mojawapo ya tabia za kipekee za siasa za Tanzania - kwamba kubadilishana uongozi humaanisha kwamba watu wengine tofauti watapata nafasi ya kushika hatamu ya uongozi hata kama chama kilicho madarakani ni kilekile.
Wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, kuna kundi la Watanzania lilipata fursa ya kufaidi ukaribu na kiongozi huyo aliyefariki Machi 17,2021. Ingawa mara zote makundi ya watawala huwa na tabia zisizo za kawaida, kuna sifa za kipekee za kundi lililokuwa likihusishwa na Rais huyo wa tano wa Tanzania.
Wamagufuli ni akina nani?
Jina Wamagufuli lilikuwa likihusishwa na kundi la viongozi, wafanyabiashara na wanasiasa ambao kupanda kwao madarakani, ukubwa au utajiri wao ulihusishwa moja kwa moja na utawala wa Rais Magufuli. Watu hao pia walikuwa na sifa za kitabia zinazoelekeana na za Magufuli kuliko viongozi wengine wa Tanzania waliotangulia.
Serikalini, hawa walikuwa ni viongozi waliokuwa wakijulikana kwa kutoa amri na makaripio - wakati mwingine kwa njia za udhalilishaji, kutojali masuala ya haki na demokrasia, kujipatia ukwasi wa fedha na mali usio na maelezo yakini na ya kuridhisha na utekelezaji wa maagizo ya Magufuli haraka na pasipo kuhoji.

Chanzo cha picha, Ikulu tanzania
Kuna wanasiasa waliokuwa kielelezo kikubwa cha utawala wa Magufuli - Paul Makonda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya pamoja na wengine .
Makonda na wenzake hao walikuwa na sifa mbili za kipekee - ukwasi wa kifedha usio wa kawaida na uwezo wa kufanya mambo ambayo katika hali ya kawaida mtu angeweza kufikiri mara mbili. Wiki iliyopita, Makonda alitawala kwenye vyombo vya habari kwa habari za mgogoro wa mali inayodaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Jumamosi Machi 12, 2021 Makonda aliweka katika ukurasa wa wake wa instagram video ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka ambayo pamoja na mengine alieleza haja ya kutaka Jeshi la Polisi kuchunguzwa, kisha akaweka ujumbe:
"Naunga mkono hoja ya Kamati Kuu, ya kuchunguza mwenendo wa baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi, wanaolipaka tope Jeshi la Polisi kwa kuwalinda wafanyabiashara MATAPELI wanaodhulumu mali za watu. Naomba tuanze na Dar es Salaam na mimi Paul Makonda niko tayari kutoa ushirikiano."
Hii ni kuhusiana na mgogoro wa ardhi kati yake na kampuni ya GSM ambapo anadai ardhi inayobishaniwa ni mali yake halali
Februari 9, 2022 mahakama ya hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es Salaam ilitoa amri ya kutangazwa magazetini na taarifa kupelekwa alikokuwa akiishi Masaki Dar es Salaam na Kijiji kwao Kolomije ilia apate taarifa za kuhitajika mahakamani katika kesi ya jinai iliyofunguliwa na mwandishi wa Habari, Saed Kubenea.
Kubenea anamtuhumu Makonda kwa matumizi mabaya ya madaraka ya umma alipokuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds Machi 17, 2017 na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Kwa upande wa Sabaya, yeye alikuwa akijulikana kwa makosa ambayo sasa yamemfikisha mahakamani. Kuna wakati, Sabaya alikuwa akionekana anaweza kufanya jambo lolote kwa mtu yeyote na asichukuliwa hatua ya aina yoyote na mamlaka za juu za utawala. Wakati wa kujitetea kwenye shauri la kwanza ambalo mwishowe alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela alisema alikuwa akitekeleza maagizo ya rais.
Kuibuka kwa 'Chato Gang'
Kabla ya Magufuli, Tanzania ilikuwa na sifa ya kipekee ya kutoa marais kutoka katika makabila madogo yaliyopo nchini. Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete walitoka miongoni mwa makabila madogo. Magufuli alitoka katika kabila la Wasukuma ambalo linatajwa kuwa kubwa zaidi nchini humo.
Na ingawa yeye anatoka katika eneo la Chato mkoani Geita, wanasiasa na viongozi wanaotoka katika eneo hilo na kwa ujumla katika eneo zima la Kanda ya Ziwa ambako kabila lake limetamalaki, walipachikwa lakabu ya Chato Gang.
Mtawala hakosi wapambe
Utawala wa Magufuli ulikuwa ukifahamika pia kwa aina ya watu waliokuwa wakifanya propaganda za kumsifu. Kwa miaka mingi, CCM na Serikali zimekuwa na wapiga propaganda kwenye vyombo vya habari na miongoni mwa wanachama wake. Chama tawala kinafahamika kwa kuwa na magazeti na vyombo vyake vya habari lakini wakati mwingine vikitumia waandishi walio nje ya mfumo wa chama lakini wenye imani na chama hicho.
Wamagufuli wa propaganda walikuwa wakijulikana kwa sifa mbili kubwa; moja ni kusifu kila kinachofanywa na serikali, pili ni kutumia vyombo hivyo kudhalilisha, kuzushia na kukashifu watu waliokuwa wakionekana kukosoa au kuwa na msimamo tofauti na Rais Magufuli.
Mwisho wa zama
Kifo cha Magufuli mwaka jana ni kama kilimaliza zama za Wamagufuli kutamba. Isivyo bahati ni kwamba nguvu na ushawishi wao ulikuwa unabebwa na mtu mmoja tu - Magufuli mwenyewe. Msiba wake umekuwa kama mporomoko wa mzigo wa karata (House of Cards).
Kundi la Wamagufuli lilikuwa kubwa kiasi cha kuhusisha wale waliokuwa wakipinga jitihada za kupambana na ugonjwa wa Corona kisayansi, wasioamini kwenye siasa za ushindani, wasioamini kwenye usawa wa kijinsia, kidini, kikanda na wanaoamini kwamba watoto wa kike waliopata ujauzito hawastahili kuendelea na masomo kupitia mfumo wa kawaida wa elimu.
Baada ya kifo cha Magufuli, kuna ambao wameondolewa kwenye vyeo vyao na Rais Samia na kuna waliofikishwa mahakamani. Wengine kama Musiba wameamua kukaa kimya huku wakisubiri hatma yao kutokana na kesi walizofunguliwa mahakamani na watu walioumizwa kisheria na vitendo vyao.
Wengine wamebaki serikalini na wanaendelea na kazi - lakini sasa kwa mujibu wa maelekezo ya rais mpya. Waliopinga Corona, sasa wanahubiri sayansi, waliopinga mimba shuleni sasa wanashawishi walioacha shule warudi na wale waliokuwa wakiamini kwamba kusafiri kwenda nje ya nchi ni matumizi mabaya ya fedha za umma, majuzi walikuwa Dubai na kwingine wakila mema ya nchi.
Rais wa tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa aliwahi kushauri siku moja kwamba iwapo mwanasiasa akikwambia nje kuna jua, inabidi utoke kwanza kuangalia kama jua lipo kweli au la. Hao ndiyo wanasiasa lakini kama kuna jambo moja la uhakika katika siasa za Tanzania mwaka mmoja baada ya kifo cha Rais Magufuli ni kwamba Wamagufuli sasa wamepoteza nuru na nguvu yao.
Maoni;Makala hii imeandikwa na mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania Ezekiel Kamwaga












