Marekani yampiga marufuku aliyekuwa gavana wa jiji la Nairobi Mike Mbuvi Sonko na famila yake kuingia nchini humo

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi nchini Kenya, Mike Mbuvi Sonko na familia yake wamepigwa marufuku kuingia Marekani kutokana na tuhuma za rushwa zinazohusiana na matumizi mabaya ya ofisi.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa leo Jumanne na Mshauri wa Masuala ya Umma Eric Watnik katika Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, marufuku hiyo ya Marekani dhidi ya Sonko imetokana na "kujihusisha na ufisadi mkubwa" wakati akiwa madarakani.

Watnik amesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Markeani imemtangaza Sonko, mkewe binti zake na mtoto wake wa kiume hawaruhusiwi kuingia Marekani. Hatua hiyo inamaanisha kwamba pia wamepigwa marufuku kufanya biashara yoyote na Marekani.

"Ufisadi wake (Sonko) umeripotiwa sana katika vyombo vya habari vya ndani na vya kimataifa. Kwa hatua hii idara inathibitisha kuwepo kwa haja ya uwajibikaji, uwazi na kuheshimu utawala wa sheria katika taasisi za kidemokrasia za Kenya, michakato ya serikali na shughuli za maafisa wa umma, "alisema Watnik.

Aliongeza kuwa: "Marekani itaendelea kutumia zana zote zilizopo kupambana na rushwa na kukuza heshima dhidi ya haki za binadamu duniani kote." Amesema hayo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.

Rushwa na hongo

Mshauri huyo alifichua kwamba Idara hiyo ina taarifa za kuaminika kwamba Sonko alipokea hongo kutoka kwa washirika wake ili kutoa zabuni za mamilioni ya shilingi.

"Idara ina taarifa za kuaminika kwamba gavana huyo wa zamani alihusika katika ufisadi mkubwa wakati akihudumu kama gavana wa Nairobi.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, vitendo vya ufisadi vya Sonko vinadhoofisha utawala wa sheria, umma wa Kenya, taratibu za serikali na maafisa wa umma.

Hata hivyo, hakutaja washirika hao, mataifa yao wala kufichua iwapo wao pia wamepigwa marufuku kuingia Marekani.

Ingawa alisema serikali yake haina kiwango halisi cha fedha za hongo na rushwa, katika moja ya kesi zinazomkabili Sonko anadaiwa kupokea hongo ya shilingi milioni 8.4 za Kenya kutoka kwa kampuni ya ROG Security Ltd kupitia Anthony Otieno kati ya Desemba 27 na 28, 2018. Fedha hizo zilionekana kumnufaisha mtu huyo kupata mkataba na serikali ya kaunti ya jiji kwa kukodisha vifaa vizito.

Sonko anakuwa Mkenya wa pili kupigwa marufuku kuingia Marekani wakati wa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kutokana na madai ya ufisadi.

Mwaka 2019, Seneta wa Busia Amos Wako (aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali), mkewe na mtoto wake wa kiume walipigwa marufuku kuingia Marekani kutokana na madai kama hayo.